Friday, March 16

‘Wakazi wa Dar maji yapo, msilalamike’


Dar es Salaam. Wakazi wa Dar es Salaam wametakiwa kuacha kulalamikia uhaba wa maji kwa kuwa huduma hiyo inapatikana kwa wingi katika sehemu kubwa ya jiji.
Ofisa Mtendaji Mkuu wa Shirika la Majisafi na Majitaka (Dawasco), Mhandisi Cyprian Luhemeja amesema hayo leo wakati wa maadhimisho ya wiki ya maji.
Amesema kuna changamoto kubwa ya watu kutoomba maji licha ya kuwa maji ya Dawasco yanapatikana katika maeneo yao.
Mhandisi Luhemeja amesema kwa sasa Dawasco inazalisha lita milioni 502 kwa siku ambayo ni sawa na asilimia 92 ya maji yanayohitajika. 
"Maji yapo tena mengi sana na tunaendelea na juhudi kuhakikisha tunayafikia maeneo yote, nichukue fursa hii kuwaambia wakazi  Dar na Pwani, maji yapo waje waombe," amesema  Mhandisi Luhemeja na kuwataka viongozi wa Serikali za mitaa kuwawezeshe wananchi kuzifikia huduma za shirika hilo.
"Viongozi wa mitaa wawakusanye wananchi wanaotaka maji, waje kwetu hatulipishi gharama zozote mwanzoni, utapigiwa hesabu kisha utaunganishiwa maji halafu utalipa taratibu," amesema. 
Katika hatua nyingine, Mhandisi Luhemeja amesema shirika hilo linatambua ufinyu wa mtandao wa maji taka na liko mbioni kutatua changamoto hiyo.
Amesema tayari Sh26 bilioni na kazi ya upanuzi wa mtandao huo itaanza. 
"Lengo ni kuwasaidia wananchi hasa katika maeneo yanayokumbwa na magonjwa ya kipindupindu kama Tandale, Mwananyamala Kisiwani na Makumbusho," amesema.
Dawasco pia, imejipanga kuongeza mtandao wa usambazaji maji kwa mwaka wa fedha 2018/19 na kwamba Sh62 bilioni zimetengwa kwa ajili ya kazi hiyo.
Mhandisi Luhemeja amesema upanuzi huo umelenga kuyafikia maeneo ya Tabata,Temeke, Kigamboni, Kimara na kwenye viwanda wilayani Kibaha.

No comments:

Post a Comment