Wednesday, August 30

MBUNGE ULANGA ATOA FEDHA KWA WAHANGA WA AJALI YA BASI


Makamu Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Ulanga Mh. Amina Seif na Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri Ndg. Yusuf Semuguruka wakimsikiliza mmoja wa majeruhi wa ajali ya basi la Mfundo iliyotokea katika Mlima Ndororo hivi karibuni.
Makamu Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Ulanga Mh. Amina Seif akimkabidhi Mganga Mkuu wa Wilaya fedha zilizochangwa na Waheshimiwa Madiwani wa kamati ya Fedha, Utawala na Mipango na Wakuu wa Idara kwa ajili ya kulipia gharama za matibabu yaliyotolewa kwa majeruhi wa ajali ya basi la Mfundo.

Na Sekela Mwasubila – Afisa Habari

Mbunge wa Ulanga Mh. Goodluck Mlinga ametoa kiasi cha shilingi milioni tano na laki tano kwa ajili ya kuwafariji majeruhi  na wafiwa wa ajali ya basi la Mfundo iliyotokea hivi karibuni katika mlima Ndororo.

Fedha hizo zilikabidhiwa kwa Mkuu wa Wilaya ya Ulanga Jacob Kassema ambaye ni mwenyekiti wa kamati ya maafa wilaya ili awasilishe kwa walengwa ikiwa kwa ajili ya kuwapa pole familia za waliopoteza maisha na majeruhi  wa ajali hiyo.

Akipikea fedha hizo Mkuu wa Wilaya Ndugu Kassema alimshukuru mbunge kwa msaada alioutoa kwani utawasaidia sana wafiwa na majeruhi na kuwafariji kutokana na kupoteza mali zao katika eneo la ajali.

Wakati huo huo madiwani wa kamati ya fedha, Utawala na Mipango na Idara nao walitoa mkono wa pole kwa wafiwa na majeruhi ambapo mchango huo ulikabidhiwa kwa Mganga Mkuu na Makamu Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya Ulanga Mh. Amina Seif na kusema kuwa fedha hiyo imetolewa kwaajili ya kugharamia matibabu ya majeruhi waliopo wodini na waliotibiwa na kuruhusiwa.

Aliongeza kuwa waheshimiwa madiwani wameguswa sana na ajali hiyo na kuona kuwa kuna haja ya kuwasaidia kuwalipia matibabu kwani wengi wao wamepoteza vitu sehemu ya ajali hivyo ingewahuia ugumu wa kulipia matibabu na kuamua kuwachangisha madiwani wa kamati ya fedha na wakuu wa Idara na kufanikiwa kukusanya kiasi cha Tshs. 327,000.

Akipokea fedha hizo Mganga Mkuu wa Hospitali ya Wilaya Dkt. Rajabu Risasi amewashukuru waheshimiwa madiwani kwa msaada huo na kueleza kuwa fedha hiyo itawasaidia katika kufidia madawa yaliyotumika siku ya ajari kwani majeruhi wote walitibiwa bila kujali kama wana fedha za matibabu.

Basi la Mfundo lilipata ajali siku ya alhamisi katika mlima Ndororo na kujeruhi watu thelathini na tatu na kusababisha vifo vya watu saba.

WITO UMETOLEWA KWA WANANCHI KUCHANGIA UJENZI VYUMBA VYA MADARASA


Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Mhe.Anthony Mtaka akizungumza na wananchi wa Kata ya Nkololo wilayani Bariadi (hawapo pichani) katika Mkutano wa Hadhara, wakati wa ziara yake aliyofanya kwa lengo la kusikiliza kero mbalimbali za wananchi.
Wajumbe wa Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Mkoa wa Simiyu na viongozi wengine wa Mkoa na Wilaya ya Bariadi wakimsikiliza Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Mhe.Anthony Mtaka (hayupo pichani) wakati wa ziara aliyofanya katika Kata ya Nkololo wilayani Bariadi, kwa lengo la kusikiliza kero mbalimbali za wananchi.
Baadhi ya wananchi wa Kata ya Nkololo wilaya ya Bariadi wakimsikiliza Mkuu wa Mkoa wa Simiyu,Mhe.Anthony Mtaka katika Mkutano wa Hadhara aliofanya katika Kata hiyo wakati wa ziara yake yenye lengo la kusikiliza kero mbalimbali za wananchi.

Na Stella Kalinga, Simiyu

Wananchi wa Kata ya Nkololo katika Halmashauri ya Wilaya ya Bariadi wametakiwa kutambua wajibu wao katika kuchangia ujenzi wa Vyumba vya madarasa ili kupunguza tatizo la upungufu wa vyumba vya madarasa katika shule za msingi na sekondari. Wito huo umetolewa na Mkuu wa Mkoa wa Simiyu Mhe.Anthony Mtaka wakati alipokuwa akijibu kero mbalimbali za wananchi katika Mkutano wa Hadhara uliofanyika katika Kijiji cha Nkololo Kata ya Nkololo Wilayani Bariadi.

Mtaka amesema ni vema wananchi wakahamasika kuchangia katika ujenzi wa vyumba vya madarasa kama wanavyochangia katika masuala mengine ili watoto wao wawe na mazingira mazuri ya kusomea. “Kujenga vyumba vya madarasa siyo wajibu wa walimu wetu ni wajibu wenu wenu wazazi, ni lazima wananchi wa Nkololo mjenge vyumba vya madarasa kama mnavyojitoa katika mambo mengine, najua hamuwezi kushindwa kutoa angalau mfuko mmoja wa saruji kila kaya; Nkololo itajengwa na wana Nkololo wenyewe” amesema Mtaka.

Aidha, Mtaka ametoa wito kwa wananchi hao kuzingatia suala la uzazi wa mpango kwa kuwa ongezeko kubwa la watoto ndio linalopelekea idadi kubwa ya wanafunzi ikilinganishwa na vyumba vya madarasa. “Mhe.Diwani nikuombe tengeneza utaratibu hapa na watu wako, Nkololo ni moja ya centre(kituo) kubwa wachangie, wala wasiseme tumechangia sana ni lazima wachangie; na kama hatutajirekebisha kwenye kuzaana, tutachanga, tutachanga, tutachanga” amesema Mtaka.

Naye Afisa Elimu wa Halmashauri ya Wilaya ya Bariadi, Doreen Rutahanamilwa amesema, Serikali kwa kushirikiana na wadau mbalimbali inaendelea na ujenzi wa miundombinu ya elimu vikiwemo vyumba vya madarasa na matundu ya vyoo, hivyo wananchi wanao wajibu kuunga mkono jitihada hizo ili kuleta maendeleo katika sekta ya elimu.

Kuhusu kero ya uharibifu wa mazao unaofanywa na wanyamapori hususani Tembo, ambayo ilitolewa na Luja Masala Mkazi wa Kijiji cha Bubale, Mkuu huyo wa Mkoa amesema, Serikali kupitia watalaam wake wa Wanyamapori watakabiliana na tatizo hilo, hivyo akawataka wananchi wasiache kulima na wazingatie ushauri wanaopewa na watalaam hao.

Akitoa ufafanuzi wa kitaalam juu ya kero hiyo, Mkuu wa Idara ya Ardhi na Maliasili, Ndg.Mazengo Sabaya amesema, Halmashauri imekuwa ikipeleka askari wa Wanyamapori katika maeneo yanayovamiwa na tembo na akawataka wananchi kuendelea kufuata ushauri wa kutumia uzio wa pilipili katika mashamba yao ili kuwazuia tembo hao.

Katika suala la upatikanaji wa mbegu bora, Mkuu wa Mkoa wa Simiyu Mhe.Anthony Mtaka Serikali kupitia kwa wakala wa mbegu ina mpango wa kuhakikisha wakulima wanapata mbegu bora katika bei wanayoweza kuimudu. Katika hatua nyingine Mtaka ametoa maelekezo kwa Halmashauri ya Wilaya ya Bariadi kuhakikisha inaweka mipango ya ujenzi wa stendi, soko na barabara katika kituo cha Nkololo ambacho ni moja vituo vikubwa vya kibiashara wilayani humo.

Mkuu wa Mkoa ameanza ziara katika Halmashauri ya Wilaya ya Bariadi katika Kata ya Nkololo na baadaye atafanya ziara katika kata za Dutwa na Ngulyati ambapo atafanya mikutano ya hadhara na kusikiliza kero mbalimbali za wananchi.

KIKAO CHA BARAZA LA MAWAZIRI

RAIS DKT MAGUFULI AONGOZA KIKAO CHA BARAZA LA MAWAZIRI, ALIYEKUWA KARANI WA BARAZA MAREHEMU HASSAN RASHID SHEBUGE AKUMBUKWA

 Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli, Makamu wa Rais Mhe Samia Suluhu Hassan na Katibu Mkuu Kiongozi pamoja na mawaziri wakisimama kwa heshima kumkumbuka aliyekuwa Karani wa Baraza la Mawaziri Marehemu Hassan Rashid shebuge aliyefariki mwezi Julai mwaka huu, kabla ya kuanza kwa kikao hicho kilichofanyika Ikulu jijini Dar es salaam leo Agosti 29, 2017.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli akiongoza kikao cha baraza la Mawziri kulu jijini Dar es salaam leo Agosti 29, 2017.

MPANGAJI APEWE NOTISI YA MUDA GANI KUONDOKA KWENYE NYUMBA ?.


Na  Bashir  Yakub.

Kuna  matatizo  sana   kati  ya  wapangaji  na  wenye  nyumba  kuhusu  notisi  ya  kuondoka  au  kuondolewa.  Wako  wanaosema  notisi  ni  mwezi mmoja,  wako  wanaosema  ni  miezi  mitatu  n.k.  Kama  ni kweli  ama  hapana  tutaona hapa   sheria  inasemaje. 

Masuala  ya  pango  yanaongozwa  na  sheria  kuu  mbili.  Moja  sheria  ya  ardhi  namba  4  ya  mwaka  1999  na  pili  sheria  ya  mikataba  sura  ya  345.  Kwa  pamoja  sheria  hizi  mbili  husimamia   jambo  hili.

1.MIKATABA YA  PANGO.                
Mikataba ya pango  inahusisha  makubaliano  ya  upangaji  kati  ya  mwenye  nyumba  na  mpangaji  au  mpangaji  na  mpangaji  mwingine  wa  pili.  Pango  laweza  kuwa   la  nyumba  ya  kuishi,   kwa  ajili ya  biashara,  nyumba  ya  ibada  au  shughuli  nyinginezo.   Yote  haya  yataingia  katika  maana  ya  pango.

2.   AINA   ZA  MIKATABA  YA   PANGO.
Sheria  ya ardhi   vifungu  vya  78  na  79  inatambua   mikataba ya  upangaji  ya  muda  mrefu  na  vipindi  vifupi. Inatambua  pango  la  wiki,  mwezi,  miezi,  mwaka  na  miaka.  Imetoa  uhuru  kwa  wahusika  wenyewe  kuamua  ni  muda  gani  wangependa  kuingia  mkataba. 

3.   NOTISI  YA  KUONDOKA.
Katika  vitu  muhimu  sana  katika  suala  la  pango  ni  notisi ya kuondoka   au  kuondolewa  katika  pango.  Jambo  la  kuzingatia awali  kabisa  ni  kuwa   notisi  hii  ni  muhimu  pande  zote  mbili.  Upande  wa  mwenye  nyumba  na  upande  wa  mpangaji.  Kila  mmoja  kwa  nafasi  yake  anawajibika  kutoa  notisi  kwa  mwenzake  panapo  mahitaji  ya  kuondoka  au  kuondolewa.

Ikumbukwe  notisi  si  kwa  ajili  tu  ya kuondoka  na kuondolewa   bali  pia   hutakiwa  yanapotokea mabadiliko  yoyote  katika  masharti  ya  mkataba. Hii  ina  maana  hata  kuongeza  kodi, kupanga  kukagua  nyumba, kufanya  marekebisho  n.k.  notisi  yafaa  itolewe. 

KUSOMA  ZAIDI  sheriayakub.blogspot.com
 

WAKAZI WA SHINYANGA NA GEITA KUNUFAIKA NA UWEKEZAJI MRADI WA UMEME


Kampuni ya Acacia, kwa ushirikiano na TANESCO, imejenga kituo cha kupozea umeme kilichopo katika mgodi wake wa dhahabu wa Bulyanhulu ambacho kimeweza kuongeza uhakika wa upatikanaji wa umeme katika maeneo ya mgodi huo.

Acacia imewekeza shilingi bilioni 5.5 katika mradi huo ambao utanufaisha maeneo yanayozunguka migodi ya Buzwagi na Bulyanhulu na maeneo mengine ikiwa ni pamoja na Kahama, Shinyanga, Msalala, na sehemu nyingine za Geita.

Ujenzi wa Kituo hicho ulianza Desemba 2016 na unatarajiwa kukamilika hivi karibuni.
Haya ni maendeleo makubwa kwa viwanda na biashara zinazozunguka eneo hilo ambazo zitafaidika na uwepo wa umeme wa uhakika jambo litakalosaidia kuboresha ufanisi na kuongeza uzalishaji.

Mkuu wa kitengo cha miradi ya maendeleo wa mgodi wa Bulyanhulu, Jiten Divecha ameeleza kuwa tatizo la mabadiliko ya nguvu ya umeme limekuwepo kwa muda mrefu na limekua likisababisha uharibifu mkubwa wa mashine.“Ujenzi wa kituo hiki utasaidia kupunguza athari zinazotokana na kuongezeka au kupungua kwa nguvu ya umeme katika migodi yetu hivyo kuboresha shughuli za uzalishaji. Wakazi na viwanda vinavyotumia umeme katika wilaya ya Msalala mkoani Shinyanga na wilaya zingine za mkoa wa Geita zitafaidika na uwekezaji huu pia,” alisema Jiten.

Aliongeza: "Acacia inajitahidi kuleta manufaa ya kiuchumi ya pamoja kwa jamii zinazotuzunguka na wadau wake kupitia miradi endelevu."
Wakati wa ujenzi wa kituo hicho, ajira mbalimbali zilitolewa kwa jamii zinazozunguka mgodi wa dhahabu wa Bulyanhulu.
Akizungumzia fursa hiyo, David Nyanda alisema: “tunathamini sana ujenzi wa mradi huu kwa sababu tumepata fursa za ajira. Japokuwa fursa hizi ni za muda, tunaweza kupata mapato ili kuendesha familia zetu hasa katika kipindi hiki cha ukame.”

WANAFUNZI MSALATO GIRLS WAJIPANGA KUINGIA 10 BORA MATOKEO YA KIDATO CHA SITA.


Wanafunzi wa kidato cha sita katika shule ya sekondari ya wasichana ya Msalato Manispaa ya Dodoma wamemuahidi Naibu Waziri Ofisi ya Rais, Tamisemi Mhe. Selemani Jafo kwamba watapambana ili katika matokeo ya kidato cha sita mwakani shule yao iwe miongoni mwa shule kumi bora nchini. 

Ahadi hiyo ilitolewa na wanafunzi hao katika ziara ya Naibu Waziri Jafo alipotembelea shule hiyo kukagua ujenzi wa miundombinu inayojengwa na serikali ili kuirudisha shule hiyo katika hadhi yake.

Shule hiyo ni miongoni mwa shule kongwe 88 zilizo katika mpango wa ukarabatiwa na serikali ambapo ndani ya miaka 4 shule hizo zitakuwa ni shule zenye ubora wa hali ya juu kwa kuboreshewa mazingira yake yakiwemo mabweni, madarasa, vyoo, mabwalo, mifumo ya maji na umeme, pamoja na nyumba za walimu. 

Katika shule hiyo, serikali hadi sasa imeshakamilisha ukarabati wa mabweni nane, mfumo wa umeme na maji.Aidha Serikali imejipanga kuendelea na ukarabati wa madarasa na ujenzi wa madarasa mengine manne mapya, ukarabati wa bwalo la chakula, majengo ya utawala, na nyumba za walimu. 

Kufuatia uboreshaji huo, Wanafunzi wameishukuru serikali na wamemuahidi Naibu Waziri huyo kwamba watahakikisha wanajitahidi ili mwakani shule yao iwe miongoni mwa shule kumi bora katika matokeo ya kidato cha sita.

Akizungumza na wanafunzi hao, Naibu Waziri Jafo amewahakikishi watanzania kwamba mpango wa serikali ni kuboresha shule za umma ili ziweze kutoa elimu bora hapa nchini.Mwaka jana, Naibu Waziri Jafo alitembelea shule hiyo na kuwataka wanafunzi wa kidato cha sita kuhakikisha wanafanya vizuri katika mitihani yao ili shule hiyo itoke kutoka shule ya 21 katika matokeo ya kidato cha sita mwaka jana ili waingie 10 bora. Jambo ambalo katika matokeo ya mwaka huu shule hiyo imeshika nafasi ya namba 14 kitaifa.
Naibu Waziri Ofisi ya Rais, Tamisemi Selemani Jafo akikagua maeneo ya vyoo na mifumo ya maji iliyokarabatiwa katika shule ya Sekondari ya wasichana Msalato.
Naibu Waziri Ofisi ya Rais, Tamisemi Selemani Jafo akipata maelezo ya ukarabati wa mabwene kutoka kwa mmoja wa wakandarasi wanaofanya ukarabati huo.
Naibu Waziri Ofisi ya Rais, Tamisemi Selemani Jafo akifanya ukaguzi wa mabweni nane yaliyofanyiwa ukarabati katika shule ya Sekondari ya wasichana.
Naibu Waziri Ofisi ya Rais, Tamisemi Selemani Jafo akiwa na Mkuu wa shule hiyo pamoja na maafisa wengine wakifanya ukaguzi wa majengo.
Naibu Waziri Ofisi ya Rais, Tamisemi Selemani Jafo akizungumza na wanafunzi wa shule ya sekondari ya wasichana Msalato Dodoma.
Miongoni mwa mabweni yaliyokarabatiwa na serikali

KESI YA AVEVA, KABURU YAZIDI KUPIGWA KALENDA


Kwa mara nyingine tena upelelezi dhidi kesi ya utakatishaji fedha na kugushi inayomkabili Rais wa  Klabu ya Simba, Evans Aveva na Makamu wake Godfrey Nyange Kaburu umedaiwa kuwa bado kukamilika na kwamba kuna nyaraka mbalimbali zimepelekwa kwa mtaalamu wa maandishi.

Wakili wa serikali, Eatazia Wilson amedai hayo leo mbele ya Hakimu Mkazi Victoria Nongwa, pindi kesi hiyo imekuja kwaajili ya kutajwa na kudai bado wanasubiri ripoti ya polisi.

Kufuatia taarifa hiyo, Hakimu Nongwa aliutaka upande wa jamuhuri kujitahidi kuharakisha upelelezi kwasababu washtakiwa wapo ndani na kwamba
Kesi hiyo imeahirishwa hadi Septemba 8 mwaka huu kwa ajili ya kutajwa.

Aveva na Kaburu  wanakabiliwa na mashtaka matano ya kughushi, kuwasilisha nyaraka ya uongo na kutakatisha fedha USD 300,000.

Mvutano kuhusu kufunguliwa kwa mitambo ya tume Kenya


Kesi ya kupinga matokeo ya uchaguzi wa urais nchini Kenya imeendelea leo kwa siku ya pili katika mahakama ya juu zaidi ya taifa hilo, huku mahakama hiyo ikisikiliza hoja za upande wa washtakiwa.
Mapema Mahakama hiyo ilipokea malalamiko ya mawakili upande wa upinzani NASA kwamba Tume ya uchaguzi (IEBC) ilikataa kuwapatia wataalam wake wa teknolojia ya mawasiliano fursa ya kuchunguza mitambo ya data ya tume hiyo ilizotumiwa kuhesabu kura za urais, kama ilivyoagizwa na mahakama Jumatatu.
Upinzani umedai mitambo ya IEBC iliingiliwa ili kumpatia ushindi rais Uhuru Kenyatta katika uchaguzi uliofanyika tarehe 8 Agosti, tuhuma ambazo tume hiyo imekanusha.

Kim Jong-un: Tutarusha makombora zaidi Pacific

Baraza la usalama la umoja wa mataifa UN limeishutumu Korea Kaskazini.Haki miliki ya pichaBBC SPORT
Image captionBaraza la usalama la umoja wa mataifa UN limeishutumu Korea Kaskazini.
Vyombo vya habari vya taifa hilo pia vilirejelea vitisho katika kisiwa cha Marekani cha Guam katika bahari ya Pacific ambacho imesema kinamiliki kambi ya uvamizi wa kijeshi ya Marekani
Kombora lililorushwa siku ya Jumanne lilipitia juu ya kisiwa cha Japan cha Hokaido na kusababisha hali ya wasiwasi wa kusalama huku raia wakitakiwa kujificha kabla ya kombora hilo kuanguka baharini.
Baraza la usalama la umoja wa mataifa UN limeishutumu Korea Kaskazini.
Likifanya kikao chake siku ya Jumanne usiku mjini New York , baraza hilo lilitaja urushaji huo wa kombora kama ''ukatili'' na kulitaka taifa hilo kusitisha majaribio yake ya makombora.
Lakini matamshi hayo hayakutishia vikwazo vipya dhidi ya Pyongyang.
Korea Kaskazini mara kwa mara imekuwa ikifanyia majaribio makonbora yake katika miezi ya hivi karibuni, licha ya kupigwa marufuku kufanya hivyo chini ya sheria za Umoja wa Matifa.
Kombora la hivi karibuni lililotengezwa ni lile la Hwasong-12 ambalo lilizinduliwa mapema siku ya Jumanne katika kituo kimoja karibu na Pyongyang.
Njia iliotumiwa na kombora hilo la Korea Kaskazini
Image captionNjia iliotumiwa na kombora hilo la Korea Kaskazini
Liliruka kwa umbali wa kilomita 2,700 lakini likaenda chini chini juu ya Hokkaido kabla ya kuanguka baharini yapata kilomita 1,180 mashariki mwa Japan.
Japan ilitoa tahadhari kwa raia wake wa Hokkaido kujificha.
Waziri mkuu Shinzo Abe baadaye alisema kuwa ni hatua ''isiokuwa ya kawaida, hatari na tishio kubwa''.
Kwa mara ya kwanza chombo cha habari cha Korea Kaskazini KCNA kilikiri kurusha kombora la masafa marefu juu ya anga ya Japan.
Vifaa vyengine vilivyoonekana vikipitia juu ya nga ya Japan vilidaiwa kuwa satlaiti.
Korea ksakzini imesema kuwa kombora hilo lililenga kujibu zoezi la pamoja la kijeshi kati ya Marekani na Korea Kusini ambalo linaendelea mbali na kuadhimisha makubaliano ya Japan-Korea 1910 ambalo lilipelekea jeshi la Japan kuondoka katika rasi ya Korea.
KCNA kilimnukuu kiongozi wa taifa hilo Kim Jong Un akisema kuwa kama vita vya ukweli, urushaji wa kombora hilo ni hatua ya kwanza ya kijeshi ya raia wa Korea katika bahari ya Pacific na hatua ya kutaka kudhibiti kisiwa cha Guam.
Bwana Kim ameagiza kurushwa kwa makombora zaidi yanayolenga eneo hio la pacific.
Bwana Kim ameagiza kurushwa kwa makombora zaidi yanayolenga eneo hio la pacific.Haki miliki ya pichaKCNA
Image captionBwana Kim ameagiza kurushwa kwa makombora zaidi yanayolenga eneo hio la pacific.
Korea Kaskazini imetishia kushambulia kisiwa cha Guam, ambacho kinamiliki kambi kubwa ya kijeshi ya Marekani ambapo raia takriban 160,000 wa Marekani wanaishi mapema mwezi huu.
Maafisa wa Marekani walisema kwa kuwa Korea Kaskazini imeshindwa kutekeleza tishio lake kufikia sasa ni wazi kwamba imeanza kuogopa.
Rais wa Marekani katika taarifa yake iliyotolewa na Ikulu ya Whitehouse, amesema kuwa ''ulimwungu umepokea tishio la Korea Kaskazini kwa sauti kubwa na bila tashwishi''.
''Utawala huu umeamua kutojali majirani zake, na wanachama wote wa UN mbali na kufanya vitendo ambavyo havikubaliki kimataifa'', alisema.

Wapinzani Venezuela matatani

Rais Nicolas MaduroHaki miliki ya pichaGETTY IMAGES
Image captionRais Nicolas Maduro
Bunge jipya la Katiba nchini Venezuela limepiga kura kwa kauli moja kuunga mkono viongozi wa upinzani kushtakiwa kwa makosa ya uhaini, kwa tuhuma za kuchochea nchi hiyo ikawekewa vikwazo vya kiuchumi na Marekani.
Agizo hilo linaelezea mashtaka hayo ni ya kihistoria na kusema kuwa wanakusudia kuwashugulikia wale wote wanaokwenda kinyume na matakwa ya raia wa kawaida wa Venezuela.
Rais wa nchi hiyo Nicolas Maduro mara kwa mara amekuwa akiwatuhumu viongozi wa upinzani kuwa upande wa Marekani, nchi ambayo anasema inajiandaa na uvamizi wa kijeshi.
Wiki iliyopita Rais Donald Trump aliamuru vikwazo vipya kwa Venezuela.

Jaji wa mahakama ya juu Kenya augua kesi ya upinzani ikiendelea

Jaji Mkuu David Maraga na Jaji Mohammed IbrahimHaki miliki ya pichaAFP/GETTY
Image captionJaji Mkuu David Maraga na Jaji Mohammed Ibrahim wakati wa kuanza kusikilizwa kwa kesi ya upinzani August 27, 2017
Jaji mmoja wa Mahakama ya Juu nchini Kenya ameugua kesi ya kupinga matokeo ya uchaguzi wa urais ikiendelea kusikizwa.
Kwa mujibu wa Jaji Mkuu David Maraga, ambaye ndiye kiongozi wa mahakama hiyo, Jaji Mohammed Ibrahim, mmoja wa majaji saba ambao wamekuwa wakisikiliza kesi hiyo iliyowasilishwa na kiongozi wa upinzani Raila Odinga alianza kuugua kabla ya vikao vya leo kuanza na alihudumiwa na madaktari.
Kuugua kwake kuliwaacha majaji sita wakisikiliza hoja za pande mbalimbali katika kesi hiyo.
Majaji hao wengine ni Naibu Jaji Mkuu Philomena Mwilu, Prof Jackton Boma Ojwang, Bi Njoki Ndung'u, Isaac Lenaola na Dkt Smokin Wanjala.
Bw Odinga amepinga hatua ya Tume ya Uchaguzi (IEBC) kumtangaza Rais Uhuru Kenyatta kuwa mshindi wa uchaguzi wa urais uliofanyika tarehe 8 Agosti.
Majaji hao wanatarajiwa kutoa uamuzi wao kufikia Ijumaa tarehe 1 Septemba.
Kwa mujibu wa matokeo ya IEBC, Rais Kenyatta alipata kura 8,203,290 huku naye Raila Odinga akipata kura 6,762,224.