JESHI la Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam limewahakikishia hali ya usalama na amani wakazi, wananchi wa jiji la Dar es Salaam katika kipindi chote cha sikukuu ya Eid inayotarajiwa kuwa Jumatatu.
Lucas Mkondya, Kaimu Kamanda wa Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam amesema kuwa askari wa jeshi hilo wamejipanga vyema kuhakikisha wananchi wa jiji la Dar es Salaam wanasherehekea sikukuu hiyo kwa kwa amani na utulivu pasipo bugudha za wahalifu.
“Uzoefu unaonesha kuwa, mara nying kipindi cha sikukuu kama hii watu wenye nia ovu hujiandaa kufanya vitendo vya kihalifu, ndiyo maana tumejipanga kukabiliana na aina yoyote ya uhalifu kwa kuzuia au kuwatia nguvuni wote watakaoshiriki vitendo vya uvunjifu wa sheria,” amesema.
Kamanda Mkondya amesema polisi watafanya doria za masaa 24 katika maeneo yote ya jiji la Dar es Salaam hasa maeneo yenye korofi na yenye rekodi au viashiria vya uhalifu.
“Pia kutakuwa na doria katika maeneo ya misikiti, kumbi za starehe na maeneo yenye mikusanyiko mikubwa ya watu na tutatumia taarifa za kiintelijensia ili kuwabaini wahalifu wanaopanga kufanya matukio ya uhalifu.
“Tutaimarisha vikundi vya ulinzi shirikishi ili kuhakikisha maeneo yote hatarishi yanadhibitiwa,” amesema Kamanda Mkondya.