Kwa ufadhili wa Serikali, Chuo Kikuu cha Ruaha (Rucu) kimeweka mazingira rafiki ya kujifunzia kwa mapacha hao walioungana ambao wamelazimika kuwahi kuwasili chuoni hapo ili waanze masomo ya kompyuta kabla ya kuungana na wenzao ambao bado wapo likizo.
Kabla ya wanafunzi hao kujiunga na chuo kikuu hicho, uongozi ulilazimika kuchukua hatua za haraka kuweka mambo sawa ili kuhakikisha mabinti hao wanafurahia safari yao ya kuwa walimu wenye shahada.
Makamu mkuu wa chuo hicho, fedha na utawala, Padri Kelvin Haule anasema walianza maandalizi ya nyumba watakayoishi kwa kipindi chote cha masomo yao na kuandaa mazingira na mahitaji yote muhimu kwa ajili yao.
“Fahari yetu ni kuona wanafurahi, tunapenda kuona wanatimiza ndoto zao,” alisema Padri Haule na kufafanua:
“Tulianza kuandaa sebule. Hapa ndipo wanaposomea, kupokea wageni na kuna TV kwa ajili ya kupata habari mbalimbali. Sebule hiyo pia wanaitumia kwa ajili ya kusali.” Sebuleni kuna kochi kubwa kidogo lililotengenezwa maalumu kuwawezesha kukaa bila wasiwasi.
Chumbani kwao kuna kitanda kifupi na kipana. Kimetandikwa vizuri kana kwamba hakijawahi kulaliwa na mtu yeyote. Chumba hicho kina nafasi ya kutosha na kila kitu kimewekwa katika mpangilio mzuri.
Choo wanachotumia pacha hao kilijengwa ‘kimahesabu’ tofauti na vingine. Chao ni kifupi ili waweze kupanda na kukaa kwa urahisi. Mabomba ya maji na soketi za umeme pia vipo chini tofauti na ilivyozoeleka ili kuwarahisishia kuvitumia kutokana na maumbile yao.
“Wakitaka kuwasha au kuzima taa hawahitaji msaada wa mtu mwingine kwa kuwa miundombinu inawawezesha,” anasema.
Pamoja na maboresho hayo ya mazingira, hawakukuta kila kitu chuoni hapo, walihama na baadhi ya vifaa vya ndani kutoka Kilolo walikoishi na kusoma kuanzia kidato cha kwanza hadi cha sita.
Japokuwa ni muda mfupi umepita tangu wawasili chuoni hapo kuanza masomo yao ya elimu ya juu, pacha hao wana furaha na tabasamu la upendo wakati wote, hivyo kuwa rafiki wa kila mmoja.
Ukibahatika kupata nafasi ya kukaa na kuzungumza nao, hakika hutapenda kumaliza haraka. Kadri unavyozungumza nao ndivyo ungependa kuendelea. Ukarimu, ucheshi uliochanganyika na upole, hekima na upendo ni sifa za pekee zinazowafanya wapendwe zaidi.
Baada ya kuishangaza dunia walipofaulu kidato cha sita kutoka Sekondari ya Udzungwa iliyopo wilayani Kilolo, pacha hao wanaendelea kuthibitisha kuwa ulemavu si kukosa uwezo.
Maria na Consolata sasa ni wanafunzi wa chuo kikuu wakiishi kwenye nyumba maalumu iliyoandaliwa kwa ajili yao ndani ya chuo hicho.
Mwaka 2010 baada ya kuhitimu darasa la saba waliwahi kusema ndoto yao ni kufika chuo kikuu na sasa imetimia wakitarajia kuanza masomo ya shahada ya kwanza ya ualimu muhula mpya wa masomochuoni hapo utakapoanza hivi karibuni.
Consolata anasema haikuwa rahisi kwao kufika hapo na kwamba hilo limewezekana kwa neema za Mungu. “Tunafurahia maisha mapya, tunamshukuru Mungu kwa hatua hii hakika ni kwa neema tu wala si nguvu na uwezo wetu,” anasema.
Maria na Consolata wana malengo na wanajua wanachopenda kufanya baada ya kuhitimu masomo yao. “Tunapenda kuwa walimu wa Kingereza na Kiswahili,” wanasema.
Kufanikiwa kujiunga chuo kikuu kumewapa ari mpya na sasa wanafikiria kuendelea zaidi mpaka wapate shahada ya uzamivu (PhD).
Unapozungumza nao unagundua ama mmoja wao huanza halafu mwingine hudakia baadaye au wanaanza na kumaliza sentensi pamoja.
Pacha hao huzungumza pamoja na hawawezi kuongea sentensi mbili au tatu bila kutamka baadhi ya maneno kwa pamoja.
‘Tunamshukuru Mungu’ ni neno lililotawala vinywa vyao. Kwao, Mungu ni wa kwanza. Wanaamini mafanikio yao ni kwa neema za Mungu na si kwa akili zao.
Mvuto wa Maria na Consolata ndani na nje ya nchi hautokani na kuungana kwao pekee, bali uwezo wa kitaaluma waliouonyesha katika shule walizosoma.
Siku chache kabla ya wenzao kufika chuoni hapo kuanza muhula mwingine, wao wamewahi ili wapate fursa ya kujifunza masomo ya kompyuta kwa miezi miwili kwa ajili ya kuendana na mahitaji ya ngazi waliyopo.
Padri Haule anasema wamefurahi kupata heshima kwa Maria na Consolata kuwa miongoni mwa wanafunzi wao. “Tunawapenda, tangu wafike wanaendelea vizuri,” anasema.
Nilipowasili chuoni hapo, saa mbili asubuhi, ofisa habari wa Rucu, Mwadharau Matola alinipeleka kwenye nyumba wanayoishi mapacha hao tulikowakuta wameketi kwenye kochi wamejipumzisha baada ya kupata kifungua kinywa.
“Oooh dada Tuma, karibu sana,” walinikaribisha kwa furaha.
Kwa sababu safari yangu ilikuwa ya kikazi, walitaka kujiridhisha kama uongozi wa chuo una taarifa za ujio wangu.
“Father Kelvin anajua umekuja? Walimu wetu je? Father Mgimwa naye anajua?” waliniuliza kwa awamu. Mwadharau aliwaeleza chuo kimetoa baraka za kuongea nao. Tulianza mazungumzo.
Siku walipowasili chuoni hapo, shughuli zilisimama kwa muda kwa kuwa kila mtu alikuwa na shauku ya kuwaona na kujua chochote kuhusu maisha yao.
Jambo la kufurahisha ni kuwa kila mmoja kwenye chuo hicho yupo tayari kuona mapacha hao wanatimiza ndoto zao. “Tulikusanyika kuwasubiri nje ya jengo la utawala na walipowasili tuliwapokea kwa shangwe kubwa,” anasema Padri Haule.
“Tulijiweka sawa kuona ni wenzetu tukistaajabia uumbaji wa Mungu.”
Kabla ya kuwasili kwao, chuo kilifanya maandalizi ya msingi. Padri Haule anasema taarifa za mapacha hao kuchaguliwa kujiunga chuoni hapo ziliwalazimu kujipanga jinsi ya kuwafanya wawe na maisha ya amani na furaha, hivyo walifunga safari kwenda Kilolo katika shule waliyoishi kabla ya kumaliza kidato cha sita ili kujifunza namna nzuri ya kuwalea.
“Kwa hiyo tulikwenda kujifunza ili nasi tunapowapokea tuhakikishe tuna miundombinu wezeshi kwao, wasione tofauti kubwa,” anasema.
Anasema walichozingatia zaidi ni muundo wa chumba cha kulala, bafu, sebule na choo pamoja na maisha yao ya kila siku. Walihakikisha wanajua wanachohitaji tangu wanapoamka hadi muda wa kulala.
Padri Haule anasema baada ya kupata ripoti ya mahitaji yao ya msingi walianza kuandaa mazingira kabla ya kuwapokea.
Anasema ili kufanikisha masomo yao chuoni hapo, Maria na Consolata wameandaliwa mhudumu wa nyumbani, muuguzi pamoja na dereva ambao wanalipwa na Serikali ili kuhakikisha wanahudumiwa kwa kila wanachohitaji.
RC, mhudumu wanavyozungumzia
Mkuu wa Mkoa wa Iringa, Halima Masenza anasema kuna fungu limetengwa kwa ajili ya Maria na Consolata na chuo kimefungua akaunti maalumu kwa ajili yao. “Wapo chini ya uangalizi wetu baada ya kuwapokea kutoka kwa masista, Serikali ndiyo iliyosimamia kuhakikisha wanapata mahitaji yote ya msingi. Chuo kina jukumu la usalama wao,” anasema.
Mhudumu anayewasaidia kazi mbalimbali nyumbani ikiwamo kuwapeleka darasani, Nuru Mfikwa anasema furaha yake imeongezeka tangu alipoanza kuwalea pacha hao. Baada ya vipindi vya darasani, marafiki zao au walimu huwa wanawasindikiza hadi nyumbani. “Najisikia mwenye furaha, nawapenda Maria na Consolata na nitajitahidi kuwahudumia kwa bidii,” anasema Nuru.
Katika kipindi hiki, wanachuo hao wapya hawaamki alfajiri sana, isipokuwa huamka saa moja, na kati ya saa tano hadi saba wanaingia darasani.
Wakiamka, huanza kwa kumshukuru Mungu kisha hutandika kitanda na kusafisha chumba chao.
Kwa siku moja niliyoshinda nao nilishuhudia wakichukua kompyuta yao kisha kupanda baiskeli na Nuru kuisukuma kuelekea darasani ambako kulikuwa na wahadhiri wawili; Robert Manase na Anthony Challu waliowapokea na kuwasaidia kukaa kwenye kiti chao ambacho pia ni maalumu.
Kiti hicho wanakitumika tangu wakiwa sekondari kwa kuwa watawa wa shirika la Maria Consolata waliokuwa wakiwalea awali waliwafungashia vifaa vyao muhimu walipokuwa wakijiandaa kujiunga na chuo hicho.
Katika kipindi cha takriban saa mbili, mwalimu Manase aliwafundishwa namna ya kutengeneza kadi kwa kutumia programu ya microsoft publisher. Kwa saa moja aliwaelekeza kabla hajawapa kadi ya harusi waitengeneze kama ilivyo.
Pia kwa muda mfupi waliitengeneza kadi hiyo na kuitoa kama ilivyokuwa. “Uwezo wao darasani ni mkubwa sana, ni wepesi wa kuelewa,” anasema Robert.
“Tumewatengenezea mouse mbili ingawa wanatumia kompyuta moja.”
Hata hivyo, wanayo kompyuta mpakato (laptop) wanayoitumia wakiwa nyumbani kwa vile hivi sasa wana kipindi kimoja kwa siku na hupewa kazi kwa ajili ya kuzifanya wakiwa kwenye makazi yao.
Kipindi kinapoisha, wanafunzi wenzao huwasaidia kupanda baiskeli na kuwasukuma kurejea kwao huku njiani wakipiga soga za hapa na pale. Wanafunzi chuoni hapo wanasema ni furaha kwao kuwa na Maria na Consolata.
Mmoja wa wanafunzi, Harrison Damas anasema ucheshi wa pacha hao umewafanya wawe marafiki wa kila mmoja wanayekutana naye.
“Ni wakarimu na wameifundisha jamii kwamba, unapowapa nafasi watu wenye ulemavu wanaweza kufanya maajabu ya kushangaza,” anasema.
Ingawa wanaye msaidizi ambaye huhakikisha mambo yako sawa, wakati mwingine wakifika kwenye nyumba yaohupenda kujishughulisha kwa kuandaa chakula cha mchana kisha kupumzika kidogo.
Kwenye ratiba yao ya kila siku upo muda ambao huutumia kusaidia kufanya kazi za nyumbani.
Padri Haule anasema awali hawakuwaandalia jiko wakijua watakuwa wanaandaliwa chakula na msaidizi wao.
Cha ajabu, anasema walipofika walitaka kuingia jikoni kupika. “Tulishangaa, ikabidi tuwaandalie jiko la gesi. Lakini ikashindikana kwa sababu gesi si nzuri kwao kutokana na harufu, waliomba jiko la mkaa,” anasema Padri Haule.
Kwa kawaida hawapendi kubweteka. Wanapenda kufanya kazi zote wanazoweza. “Tunaweza kufanya kazi zote isipokuwa kuanika nguo tu,” anasema Maria.
Wakiwa na muda huwa wanaondoka kwenda kutembea nje ya chuo hicho ili kubadilisha na kujifunza mazingira ya mji wa Iringa. Mara nyingi, kama eneo wanalokwenda wanaweza kufika, hufanya hivyo kwa kutumia baiskeli yao ingawa wanalo gari kwa ajili ya kuwapeleka popote wanapotaka. “Tumeshawahi kwenda sokoni na kurudi. Na tunaweza kwenda popote pale,” anasema Maria.
Padri Haule anasema awali alikuwa na wasiwasi, lakini kwa sababu pacha hao wapo simple na wasimamizi wao wanawalinda, huwaacha watembelee hasa maeneo yaliyopo jirani.
Ofisa elimu wa Mkoa wa Iringa, Majuto Nyaga anasema Serikali imetenga fungu maalumu kwa ajili yao ili pacha hao wasome bure. Anasema wameshawasiliana na Wizara ya Elimu pamoja na Bodi ya Mikopo ya Elimu ya Juu (HESLB) kuhakikisha hawakopeshwi katika gharama za masomo yao.
“Hata wasaidizi akiwamo dereva na muuguzi watakaowahudumia kwa kipindi chote Serikali itagharamia,” anasema.
Anasema mkoa umegharamia mahitaji yote ya awali mpaka sasa huku wakisubiri hatua nyingine kutoka wizarani.
Hata hivyo, Mwadharau anasema Maria na Consolata wamejiunga na chuo hicho kikiwa na kitengo cha elimu maalumu. “Tunacho kitengo kwa ajili ya wenye mahitaji maalumu,” anasema.
Padri Haule anasema awali walipata shida kuhusu miundombinu ya madarasa walipowasili lakini tayari suluhisho limepatikana na mkakati wa chuo ni kuwa na mazingira rafiki zaidi kwa makundi yote. “Kwa hiyo mazingira yaliyopo wanaweza kuja kwa baiskeli yao kutoka nyumbani hadi darasani bila wasiwasi,” anasema.
Maria na Consolata wanatoa somo kuhusu watu wenye ulemavu nchini.
Mkuu wa Mkoa wa Iringa, Masenza anasema wameonyesha kuwa inawezekana. “Licha ya kwamba ni walemavu wanaonyesha bidii, maana yake ni kwamba jamii isiwafungie watu wa aina hii ndani. Wawatoe na kuwapeleka shule wanaweza kufanya maajabu kama Maria na Consolata,” anasema.
Njia wanazopita kwenda kanisani
Chuo kinajua pacha hao wanapenda kuabudu, hivyo kimewaandalia mazingira yatakayowawezesha kwenda na kurudi kanisani.
“Kanisa lipo hapa chuoni lakini awali njia zilikuwa na ngazi ili kulifikia, kwa hiyo walikuwa wanapata shida, tukaamua kuandaa mazingira rafiki ili wakati wa ibada waende bila wasiwasi,” anasema Padri Haule.
Anasema waliandaa njia mbadala za wao kupita waendapo na kurudi kutoka kanisani bila wasiwasi. “Wanapita geti la kutokea chuo, wanaenda hadi ilipo benki ya NMB kisha wananyoosha hadi kwenye ATM ya CRDB, hapo tumejenga daraja dogo ambalo wanavuka na kuingia mlango utakaowapeleka moja kwa moja kanisani,” anasema.
Maria na Consolata wanaamini kusali ndiko kulikowafanya wafikie ndoto ya maisha yao.
Maria na Consolata wanajua kutumia fursa. Pia wanaamini bidii pekee ndiyo inayoweza kuwafanikisha kwenye maisha yao. Wanafanya biashara ya vitenge na ukienda kuwatembelea watakuonyesha bidhaa zao ili uwaungishe.
“Tulikuwa na mtaji mdogo ila sasa umefika zaidi ya laki moja,” anasema Maria. Wanasema biashara hiyo haitawafanya washindwe kutimiza ndoto yao.
Mkuu wa Wilaya ya Iringa, Richard Kasesela anasema mapacha hao ni funzo kwa Watanzania wasiopenda kufanya kazi. “Nitawasaidia kwenye hii biashara yao kwa sababu wanaonyesha moyo wa kujituma licha ya uhakika wa Serikali na chuo kufanikisha kila kitu,” anasema.
Siyo vitenge tu, pacha hao wanapenda kufuma vitambaa huku mmoja akitumia mkono wa kushoto na mwingine wa kulia, wanaweza kushona vitambaa vizuri wanavyoviuza.