Sunday, October 22

Msigwa aeleza anavyosuka mpango wa kumuondoa Spika


Mbunge wa Iringa Mjini (Chadema), Mchungaji Peter Msigwa ameelezea jinsi anavyosuka mpango wa kumng’oa Spika wa Bunge, Job Ndugai.
Msigwa ametangaza nia yake ya kupeleka hoja ya kumuondoa Spika Ndugai katika mkutano unaotarajiwa kuanza Novemba 7.
Msigwa ametangaza nia yake hiyo kupitia ukurasa wake wa Twitter akisema amezingatia kanuni ya 137 ya Kanuni za Kudumu za Bunge.
“Ninakusudia kupeleka hoja ya kumuondoa Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano Tanzania Mhe. Job Ndungai, kwa kuzingatia Kanuni ya 137 ya Kanuni za Kudumu za Bunge ina complement Ibara ya 84 (7) (d) ya Katiba,” ameandika Msigwa katika ukurasa wake wa Twitter.
Akizungumza kwa simu na Mwananchi jana, Msigwa ambaye ni miongoni mwa wabunge wanaomlalamikia Ndugai wakidai anaendesha Bunge kwa shinikizo na upendeleo, alisema Spika huyo ameshindwa kuiongoza Tume ya Bunge na Bunge kwa ujumla. “Yeye ni kamishna wa Bunge amekuwa akipokea maelekezo kutoka kwenye mhimili wa utawala ili kuliongoza Bunge. Tume ya Bunge haiendeshwi ipasavyo,” alisema Msigwa.
Msigwa alimkosoa Spika Ndugai akidai amekuwa dhaifu kuliko maspika wote waliomtangulia na kwamba katika kipindi chake Bunge limekuwa dhaifu mbele ya Serikali.
Alipoulizwa kama ataungwa mkono katika hoja yake, Msigwa alisema hiyo haijalishi ilimradi tu hoja zake ni za msingi na ni za ukweli.
“Kupata support hilo ni jambo jingine, tutajenga daraja tutakapofika kwenye mto. Kitu cha msingi ni hoja ninazoeleza ni za msingi,” alisema.
Alipotafutwa kwa njia ya simu, Ndugai hakupokea licha ya simu yake kuita kwa muda mrefu. Hata hivyo aliwahi kujibu shutuma hizo siku za nyuma kupitia gazeti hili akisema Bunge linaongozwa na Tume ambamo Msigwa naye ni kamishna.
“Kitendo ambacho yeye anataka kuonyesha kuwa kiongozi mmojawapo ana upungufu, sioni kwa nini na yeye asiwe nao upungufu. Hilo ndilo jibu langu,” alisema Ndugai na kuongeza:
“Decision making yoyote za juu kuliko zote zinafanywa na tume na huyo ni mjumbe. Hapaswi kuwa mlalamikaji kama watu wengine.”
Kanuni za kumtoa Spika
Sehemu ya kwanza ya kifungu anachosimamia Msigwa kipo katika sehemu ya nne ya Kanuni za Bunge inayohusu kumuondoa Spika au naibu wake madarakani na kinasomeka:
“(1) Mbunge yeyote anayetaka kuwasilisha hoja ya kumuondoa Spika madarakani chini ya Ibara ya 84(7)(d) ya Katiba atawasilisha taarifa ya maandishi ya kusudio hilo kwa katibu (wa Bunge) akieleza sababu kamili ya kutaka kuleta hoja hiyo.”
Sehemu ya pili ya kifunmgu hicho inasema mara tu baada ya kupokea taarifa ya maandishi ya kusudio la kumuondoa Spika kwenye madaraka, katibu ataipeleka taarifa hiyo kwenye Kamati ya Haki, Maadili na Madaraka ya Bunge kwa ajili ya kuijadili.
Inaendelea kusema, endapo Kamati ya Haki, Maadili na Madaraka ya Bunge itaridhika kuwa zipo tuhuma mahsusi dhidi ya Spika zinazohusu uvunjaji wa masharti ya Ibara ya 84(7)(a), (b), (e), (f), (g) na (h) ya Katiba, Sheria au Kanuni zinazoongoza shughuli za Bunge, basi kamati hiyo itaidhinisha kuwa hoja hiyo ipelekwe Bungeni ili iamuliwe.
Kifungu hicho kinaendelea kufafanua kuwa, naibu Spika atakalia kiti cha Spika wakati wa kujadili hoja ya kutaka kumuondoa Spika madarakani na Spika atakuwa na haki ya kujitetea wakati wa mjadala.

No comments:

Post a Comment