Saturday, July 22

ELIMU SAHIHI ITUMIKE KWANZA KABLA YA MATUMIZI YA SHERIA KWA WAKEKETAJI.

Mzee maarufu na mwenyeji wa Msange Bi Greta Musa Nyonyi akichangia hoja katika semina ya kupinga Ukeketaji iliyofanyika katika Kata ya Msange Wilayani Singida.
2..
Mratibu wa Mradi wa Kupinga Ukeketaji (WOWAP) Nasra Suleiman akizungumza na washiriki wa semina ya kupinga Ukeketaji iliyofanyika katika Kata ya Msange Wilayani Singida.
3
Afisa Maendeleo ya Jamii kata ya Msange Magni Oisso akichangia hoja katika semina ya kupinga Ukeketaji iliyofanyika katika Kata ya Msange Wilayani Singida.
4
Washiriki wa semiana ya kupinga ukeketaji iliyoandaliwa na Mradi wa WOWAP wakifuatilia kwa umakini filamu fupi ya Ukeketaji iliyofanyika katika Kata ya Msange Wilayani Singida.
5
Mzee wa Kimila Hosea Mnyambi akichangia hoja katika semina ya kupinga Ukeketaji iliyofanyika katika Kata ya Msange Wilayani Singida.
………………………………………………………………..
Elimu sahihi juu ya madhara ya ukeketaji ya muda mfupi na mrefu inatakiwa itolewe kwa jamii kabla ya kuwachukulia hatua baadhi yao wanaoendelea kufanya vitendo vya ukeketaji licha ya uwepo wa sheria kali.
Rai hiyo imetolewa mapema leo na Mratibu wa Mradi wa Kupinga Ukeketaji (WOWAP) Nasra Suleiman katika semina ya kupinga Ukeketaji iliyofanyika katika Kata ya Msange Wilayani Singida, kwa ushirikiano wa Ofisi ya Ustawi wa Jamii Mkoa wa Singida na mradi huo kwa ufadhili wa shirika la WAAF-Japan.
Mratibu huyo amesema nguvu ya sheria itasaidia kuondoa ukeketaji endapo wananchi wengi watakuwa na uelewa wa kutosha juu ya madhara ya ukeketaji na kuamua kwa hiyari kuachana na mila hiyo.
“Sheria isiwe nguvu pekee ya kupambana na ukeketaji, tukifanya hivyo itafikia kipindi tutakwama kwa kiasi kikubwa kwa kuwa watu wataendelea kukeketa kwa kificho ili wasikamatwe, lakini kila mwana jamii akiwa na elimu ya kutosha ya madhara hayo, nguvu ya sheria itatumika tu kwa wachache watao kaidi”, amesisitiza Nasra.
Ameongeza kuwa Watendaji wa kata na vijiji wana uwezo mkubwa wa kubadilisha mtazamo na mila ya ukeketaji kwa kuelimisha wananchi wao hasa baada ya semina zinazoandaliwa na miradi au mashirika Fulani kwakuwa zinawajengea uwezo ili waweze kutoa elimu sahihi na mbinu za kuelimisha.
Nasra amesisitiza kuwa jukumu la elimu lisiachwe kwa sekta binafsi kama mradi wake wa WOWAP pekee bali liwe jukumu la jamii nzima huku akifafanua kuwa elimu inayotakiwa kutolewa ni ile inayoelezea madhara ya ukeketaji na sio kuwakataza kwa kigezo cha kutii sheria pekee.
Naye Afisa Maendeleo ya Jamii kata ya Msange Magni Oisso amesema katika kata hiyo ukeketaji umekufanyika kwa siri sana kwa kuogopa mkono wa sheria huku wahanga wakiwa watoto wachanga na wale waliomaliza kliniki.
Oisso amesema kumekuwa na usiri mkubwa huku wakeketaji wakibadili mbinu namna za kujificha wasigundulike kwa jamii ambayo elimu imeanza kuwafikia baadhi yao.
Aidha amependekeza kuwa ili kukomesha ukeketaji moja ya njia ni kutoa elimu katika vituo vya kutolea huduma za uzazi na mtoto ili mtoto aweze kunusurika pia elimu itolewe shuleni kwa ngazi zote kuanzia darasa la awali hadi la saba.
Akichangia mada katika semina hiyo mzee maarufu na mwenyeji wa Msange Bi Greta Musa Nyonyi amesema elimu ni bora zaidi kuliko kuwaogopesha wanajamii kwa kutumia sheria kwakuwa watatafuta namna ya kutekeleza azma yao kwa usiri ili kukwepa mkono wa sheria na sio kuacha.
Greta ameongeza kuwa kwa sasa kutokana na kuwa wakeketaji wamebainika kuwa wanakeketa watoto wachanga na hugundulika wakienda kliniki baadhi yao wanabadili mbinu na kusubiri mtoto amalize kliniki ndipo anakeketwa.
Naye Mzee wa Kimila Hosea Mnyambi amesema yeye amekulia katika familia ya wakeketaji na wamekuwa wakirithishwa mbinu za ukeketaji kizazi hadi kizazi ila kutokana na kuwepo kwa sheria, dini kuhubiri madhara ya ukeketaji, mila hiyo wameiacha.
Amesema wachache wanaoendelea kufanya vitendo hivy o ha wanawake wamekuwa wakifanya kwa usiri mkubwa huku akina baba wakiwa hawana taarifa ya kinachoendelea na endapo mtoto anafariki hudanganywa ugonjwa uliopelekea kifo cha mtoto.
Mzee Mnyambi amesema elimu iendelee kutolewa hasa kwa kutumia vyombo vinavyoaminika mfano vyama vya siasa, dini na vikundi vya kuweka na kukopa pamoja na kuiweka agenda ya ukeketaji kwa vikao vya Kata na vijiji.
Semina ya kupinga ukeketaji Kata ya Msange imefanywa na mradi wa WOWAP kwa ushirikiano wa maafisa ustawi wa jamii mkoa wa Singia kwa watendaji wa kata na vijiji, watoa huduma za afya, polisi, waalimu, wawakilishi wa viongozi wa dini, maafisa ustawi wa jamii na maendeleo ya jamii, wazee maarufu na wa kimila ili wawe mabalozi wa kusambaza elimu hiyo kwa jamii inayo wazunguka.

Museveni:Sifuatilii mjadala wa kuondoa kikomo cha umri wa kuwania urais

media
Rais wa Uganda Yoweri Museveni amesema hafuatilii mjadala unaendelea kuhusu mpango wa chama chake cha NRM kuwasilisha mswada bungeni kuondoa kifungo cha katiba, kinachozuia mtu mwenye umri wa miaka 75 kuwania urais nchini humo.
Museveni ambaye atakuwa na umri wa miaka 76 wakati wa Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2021, amesema wanaozua mjadala huo wanajaribu kuwapotosha wananchi wa Uganda na kumharibia kazi anayoifanya.
Baadhi ya wabunge wa NRM wamekuwa wakinukuliwa wakisema wanamtaka rais Museveni aendelee kuongoza nchi hiyo katika siku zijazo kwa sababu hawajaona mtu mwingine wa kufanya hivyo.
Rais Museveni ambaye aliingia Madarakani mwaka 1986, amekuwa akisema kuwa tatizo la nchi yake na mataifa mengi ya Afrika sio kiongozi anayekataa madarakani muda mrefu bali ni kazi gani anayowafanyia.
Wanasiasa wa upinzani nchini humo wakiongozwa na mwanasiasa mkongwe Kizza Besigye, amesema jaribio la kuibadilisha kifungu cha katiba kumruhusu rais Museveni kuendelea kukaa madarakani ni kinyume cha katiba ya nchi hiyo na haikubaliki.
Licha ya chama tawala cha NRM kuunga mkono pendekezo hilo la kuondoa umri wa kuwania urais, kumeonekana upingamizi kutoka kwa vijana ndani ya chama hicho.
Ripoti zinasema kuwa tayari marekebisho hayo yamewasilishwa kwenye Gazeti la serikali tayari kupelekwa bungeni ili kujadiliwa.
Wachambuzi wa siasa wanasema kuwa marekebisho hayo yatapita kwa sababu wabunge wa NRM ni wengi ikilinganishwa na wale wa upinzani.

SHEIKH Khalifa Khamis Akamatwa na Jeshi la Polisi

Mwenyekiti  wa Taasisi ya Imamu Bukhary, Sheikh Khalifa Khamis, amekamatwa na Jeshi la Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam na kuhojiwa kwa saa tisa.

Kwa mujibu wa Gazeti la Mtanzania, Sheikh Khalifa alifika Kituo Kikuu cha Polisi Dar es Salaam jana saa nne asubuhi na kuhojiwa kwa muda mrefu, huku ikiwa haifahamiki hasa sababu za kushikiliwa kwake.

Taarifa zilizopatikana  jana jioni zilidai kuwa polisi walikuwa wamepanga kumchukua sheikh huyo kwa ajili ya kwenda kupekua nyumbani kwake. Hata hivyo hadi  saa mbili usiku alikua bado anashikiliwa polisi.

Kwa nyakati tofauti jana Sheikh Khalifa mwenyewe aliliambia gazeti la Mtanzania  kuwa alipofika kituoni alielezwa na polisi kwamba ameitwa kuhojiwa kuhusu tuhuma za uchochezi.

Alisema kwamba alihojiwa kuhusu kuunga mkono kauli ya Waziri Mkuu wa zamani, Edward Lowassa, juu ya masheikh wa uamsho na hatua yake ya kuwataka waumini wa dini ya kiislamu kuungana kutetea haki za Waislamu waliopo katika magereza mbalimbali nchini.

“Wameniuliza mambo ya kumuunga mkono Lowassa na pia waliniuliza kwanini niliwataka Waislamu nchini kuungana kuwatetea Waislamu waliopo kizuizini kwa makosa ya kubambikwa.

“Hadi sasa niko hapa polisi bado nasubiri ni nini kitaendela kama wataniachia au watanibakisha hapa hatujajua,” alisema.

Alichosema Sheikh Khalifa
Baadhi ya mambo aliyoyasema Sheikh Khalifa katika mkutano wake na waandishi wa habari jumapili ya wiki hii.

“Tunaiomba Serikali iweke wazi kwa nini hairuhusiwi kwa sheikh au mtu yeyote aliyewekwa ndani gerezani  kuonwa na zaidi ya mtu mmoja hadi siku 14 zipite, yaani akija mkewe au ndugu yake leo kuonana naye  ipite siku 14 ndio aje ndugu yake mwingine kumuona hayo mambo hayapo na hayamo katika sheria.

“Tunampongeza Lowassa kwa kuona kwamba jamii miongoni mwa Watanzania inadhalilika  na haitendewi haki na kama yeye aliyasema maneno haya kwa kutafuta faida za kisiasa hayo ni maneno yake lakini aliyoyasema ni haki na kweli,” alisema sheikh Khalifa.

Kauli ya Lowassa
Akiwa katika futari iliyoandaliwa na Mbunge wa Ukonga, Mwita Waitara, Lowassa alitaka serikali iharakishe kesi za masheikh wa uamsho na kama baadhi yao hawana makosa waachiwe huru.

Alisema wakati wa kampeni za mwaka 2015, alitoa ahadi nyingi ikiwa ni pamoja na kupitia upya mikataba ya madini, pamoja na kuwaachia masheikh wa uamsho hivyo kama Rais John Dk. Magufuli amefanyia kazi la madini, afanye hivyo pia kwa masheikh hao.

Walichochukua polisi nyumbani kwa Lissu

Tundu Lissu

 Baada ya jeshi la polisi kumkamata Tundu Lissu siku ya Alhamsi uwanja wa ndege akiwa anaelekea nchini Rwanda. Jana jeshi hilo lilikwenda kufanya upekuzi nyumbani kwa Mbunge wa Singida Mashariki (CHADEMA) ambaye pia ni Mwanasheria Mkuu wa chama hicho.

Siku ya jana Ijumaa ya tarehe 21/07/2017  jeshi la polisi walimchukua Tundu Lissu na kwenda naye mpaka kwa Mkemia Mkuu wakiwa na lengo la kutaka kumpima mkojo kabla ya kuelekea nyumbani kwake kufanya ukaguzi. Lakini kiongozi huyo aligoma kufanya kipimo hicho kwa madai kuwa tuhuma anazotuhiwa haziendani na vipimo hivyo.

Kwa mujibu wa Tumaini Makene ambaye ni Afisa habari wa (CHADEMA) anasema kuwa jana polisi baada ya kufanya ukaguzi nyumbani kwa Tundu Lissu waliweza kuchukua CD 6 na kuondoka nazo.

"Jeshi la Polisi bado linamshikilia, Mhe. Tundu Lissu, Kwenye upekuzi jana nyumbani kwake walichukua CD 6 za 1996 zinazohusu masuala ya mgodi wa Bulyag'hulu, Shinyanga" ilisema taarifa ya CHADEMA

Leo ni siku ya pili toka kiongozi huyo anashikiliwa na jeshi la polisi Dar es Salaam lakini Wakili Peter Kibatala pamoja na Wakili Fatma Karume wa IMMA Advocates kwa upande wao wanasema wanaendelea na juhudi za kisheria kuhakikisha kiongozi huyo anapatiwa dhamana au kufikishwa mahakamani mapema iwezekanavyo.

Tajiri wa Mererani ahukumiwa vifungo vya maisha

Moshi. Mahakama ya Hakimu Mkazi Mkoa Kilimanjaro, imemhukumu vifungo vya maisha jela, mfanyabiashara mashuhuri wa madini wa Mererani, Benedict Kimario (43), kwa makosa mawili ya ubakaji na ulawiti.

Mahakama hiyo ilimhukumu mfanyabiashara huyo vifungo vya maisha mara mbili kwa makosa hayo mawili.

Hukumu ya kesi hiyo ambayo ilikuwa ikifuatiliwa na mamia ya wananchi wa Kijiji cha Mrau wilayani Rombo mkoani Kilimanjaro, ilitolewa mjini Moshi na Hakimu Mkazi, Idan Mwilapo.

Katika kesi hiyo iliyoendeshwa na Wakili Mwandamizi wa Serikali, Tamari Mndeme, mshitakiwa alikuwa akikabiliwa na mashitaka mawili ya ulawiti na kubaka mtoto mwenye umri wa miaka minane.

Akisoma hukumu hiyo, Hakimu Mwilapo alisema ushahidi uliotolewa na mashahidi watano wa upande wa mashitaka, umeweza kuithibitishia Mahakama pasipo kuacha shaka kuwa alitenda makosa hayo.

Hakimu Mwilapo alisema kitendo kilichofanywa na mshitakiwa huyo ni kibaya na kwa vile vitendo hivyo vinaongezeka katika jamii, Mahakama inalazimika kutoa adhabu kali ya kifungo cha maisha.

“Kwa hiyo kwa kosa la kwanza la kubaka utatumikia kifungo cha maisha jela na pia shitaka la pili la kulawiti nalo utatumikia kifungo cha maisha jela,” alisema Hakimu Mwilapo katika hukumu yake.

Awali Wakili Mndeme alidai mahakamani kuwa, mshitakiwa alitenda makosa hayo Mei 10 mwaka jana katika kijiji cha Mrau katika Wilaya ya Rombo mkoani Kilimanjaro, kitendo ambacho ni kosa kisheria.

 Tangu siku ya kwanza ya kesi, Novemba 30, 2016, mshitakiwa alikuwa akitetewa na Wakili Joseph Peter.

Wakili huyo alimtetea mshitakiwa kuanzia mwanzo wa kesi hadi shahidi wa nne wa upande wa mashitaka alipowasilisha ushahidi wake.

Hata hivyo, ilipofika shahidi wa tano, mtuhumiwa alibadili wakili na kuanza kumtumia Wakili Mussa Mziray.

TAZAMA Picha Mama Zari Alivyozikwa Uganda

Mama mzazi wa Zarina Hassan ‘Zari The Boss Lady’, Halima Hassan aliyefariki dunia Alhamisi hii asubuhi, baada ya kuugua kwa wiki kadhaa na kulazwa hospitali amezikwa Ijumaa hii katika Kitongoji cha Munyonyo, Kampala.

 Kifo cha mama Zari ambaye alizaliwa Mei 15, 1959, kimekuja ikiwa ni takribani miezi miwili tu tangu mkwe wake, Ivan Semwanga, aliyeaga dunia Mei 25 mwaka huu huko Steve Biko Academic Hospital nchini Pretoria, Afrika Kusini.

Diamond ambaye ni mpenzi wa Zari, alisafiri na team yake ya WCB kwaajili ya kushiriki mazishi hayo. Angalia picha za mazishi.


MUGABE Apania Kuwafunga Wabakaji Miaka 60 Jela

Serikali ya Zimbabwe imependekeza adhabu ya kifungo cha miaka 60 jela kwa watu watakaopatikana na makosa ya ubakaji watoto chini ya umri wa miaka 12 na walemavu nchini humo.

Kwa mujibu wa gazeti la 'The Herald'  la nchini Zimbabwe linasema kuwa adhabu ya kifungo kisichopungua miaka 40 jela kitawahusu wale wote watakaokabiliwa na kesi za ubakaji kama hatua ya kukomesha unyama huo.

Rasimu ya mapendekezo ya kurekebisha Sheria ya Uhalifu, imefanyika baada ya kilio cha wananchi kufuatia kuongezeka kwa visa vya ubakaji nchini humo.

Takwimu za Kipolisi zinaonyesha kwamba, takribani wasichana 325 walibakwa kwa mwezi mwaka jana na wengi wao wakiwa na umri wa kati ya miaka 11 na 15 hali hiyo ikimaanisha kila siku matukio zaidi ya 11 ya ubakaji hutokea.

RAIS Magufuli: Wawekezaji Wakichelewa Kufanya Mazungumzo na Serikali Nitafunga Migodi yote nchini

Akizungumza na wananchi akiwa eneo la Kakonko,Kigoma,maghiribi mwa Tanzania,Rais Magufuli ameonya kufunga migodi yote iwapo wawekezaji wataendelea kuchelewa kwa ajili ya mazungumzo.

Rais Magufuli ameyasema hayo leo katika mkutano wa hadhara katika wilaya ya Kakonko mkoani Kigoma ambapo yupo kwa ziara ya siku tatu. Amesema haiwezekani makampuni hayo yanaendelea kuwa kimya wakati wameshakubaliana kuanzisha mazungumzo haraka.

"Makampuni ya madini yaliyoahidi kukaa na serikali kuzungumza, wafanye haraka wakiendelea kuchelewa nitafunga migodi yote wanayomiliki" Rais John Pombe Magufuli

Wakati huo huo, Wizara ya Nishati na Madini ya Tanzania imesimamisha shughuli za utoaji leseni za utafutaji na uchimbaji madini, mpaka tume ya madini itakapoundwa na kuanza kufanya kazi rasmi.

OFISI YA MAKAMU WA RAIS YAKABIDHI VIFAA VYA KUTAMBUA GESI ZINAZOHARIBU NA ZISIZOHARIBU TABAKA LA OZONI (REFRIGERANT IDENTIFIERS) KWA CHUO CHA VETA NA SHIRIKA LA VIWANGO TBS

Mkurugenzi wa Idara ya Mazingira Ofisi ya Makamu wa Rais Bwana Richard Muyungi (kushoto) akikabidhi kifaa kinachotumika kutambua gesi zinazoharibu na zisizoharibu tabaka la ozoni (Refrigerant Identifier) kwa Mkufunzi wa Chuo cha Ufundi stadi (VETA) Bwana Daudi Kadinda wakati wa makabidhiano Ofisini kwa Mkurugenzi huyo.
Mkurugenzi wa Idara ya Mazingira Ofisi ya Makamu wa Rais Bwana Richard Muyungi (kushoto) akikabidhi kifaa kinachotumika kutambua gesi zinazoharibu na zisizo haribu tabaka la ozoni(Refrigerant Identifier ) kwa Afisa toka Shirika la Viwango Tanzania (TBS) Bwana Arnold Mato, wakati wa makabidhiano Ofisini kwa Mkurugenzi huyo.
Mkurugenzi wa Idara ya Mazingira Ofisi ya Makamu wa Rais Bwana Richard Muyungi akipeana mkono na Wataalamu kutoka Shirika la Viwango Tanzania (TBS) na Chuo cha ufundi Stadi VETA-Chang'ombe mara baada ya kuwakabidhi vifaa vya vinavyotumika kutambua gesi zinazoharibu na zisizoharibu tabaka la ozoni.

Polisi wamemfikisha Tundu Lissu kwenye ofisi ya mkemia mkuu kupima Mkojo



Dar es Salaam. Mkurugenzi wa Itifaki, Mawasiliano na Mambo ya Nje wa Chadema, John Mrema amesema baada ya Tundu Lissu kutolewa Kituo cha Polisi cha Kati leo mchana, amefikishwa kwa Mkemia Mkuu wa Serikali na kupimwa mkojo.

Mapema asubuhi, mawakili akiwamo Fatma Karume walizuiliwa kuonana naye huku Jeshi la Polisi likisema litaendelea kumshikilia hadi uchunguzi utakapokamilika.

Mbunge huyo wa Singida Mashariki amekamatwa Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNIA), akielekea Kigali, Rwanda kwenye kikao cha Halmashauri ya EALS kilichoanza jana.

"Kabla ya kuelekea nyumbani kwake Tegeta, wamempeleka kwa mkemia mkuu na ameshapimwa mkojo, sasa sijui ni kitu gani wanachunguza, kwa sasa wameshaelekea nyumbani kwake kwa ajili ya kumpekua,"amesema Mrema.

Licha ya kulala rumande hakuna aliyeruhusiwa kuingia na kumuona Tundu Lissu wakiwamo wanasheria wake. Mbali na Fatma, wengine waliokuwapo ni Peter Kibatala na Frederick Kihwelo.

RAIS MAGUFULI AZINDUA MIRADI MBALIMBALI YA MAENDELEO NA KUHUTUBIA WANANCHI KWENYE MIKUTANO MBALIMBALI YA HADHARA


 Rais wa jamhuri ya muungano wa Tanzania,  Dkt. John Pombe Magufuli akiwahutubia wananchi wa Kakonko kabla ya kuzindua Ujenzi wa barabara ya Kibondo -Nyakanazi yenye urefu wa kilometa 54, katika mkoa wa Kigoma.
 Wananchi wa Wilaya ya Kakonko mkoani Kigoma wakisikiliza hotuba ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli wakati wa Uzinduzi wa  Ujenzi wa Barabara  ya Kibondo -Nyakanazi yenye urefu wa kilometa 54, kwenye Sherehe zilizofanyika katika uwanja wa Standi Mpya ya Mabasi Kakonko katika mkoa wa Kigoma Rais yupo mkoani Kigoma kwa ziara ya siku Tatu
Baaadhi ya Viongozi wa vyama vya siasa na wananchi wa Wilaya ya Kakonko Mkoani Kigoma wakisikiliza Hotuba ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli wakati wa Uzinduzi wa  Ujenzi  wa Barabara  ya Kibondo -Nyakanazi.
 Rais wa jamhuri ya muungano wa tanzania Dkt. John Pombe Magufuli  pamoja na viongozi mbalimbali wakifungua kitambaa kuashiria kuweka jiwe la msingi la ufunguzi wa Barabara  ya Kibondo -Nyakanazi kiwango cha lami.
 Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli  pamoja na viongozi mbalimbali serikali wakikata Utepe  kuashiria kuweka jiwe la Msingi la Uzinduzi wa Ujenzi wa  Barabara  ya Kibondo -Nyakanazi 
 
 Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli  akiwasalimia wananchi wa mji wa Kibondo wakati akiwa safarini kutoka Ngara kuelekea Mkoani Kigoma.
 Rais wa jamhuri ya muungano wa tanzania Dkt. John Pombe Magufuli  akisalimiana na kijana mwenye ulemavu amabye ni fundi wa kushona nguo ndugu Aron Michael Kapililo mkazi wa Kibondo ambaye alisimiana na Rais Magufuli 
 Rais wa jamhuri ya muungano wa tanzania Dkt. John Pombe Magufuli akisalimiana na mamia ya wananchi wa kijiji cha Kifura,  Kibondo Mkoani kigoma waliokuwa wamesimama njiani ili kusalimiana na mh Rais akiwa njiani  safarini kutoka Ngara kuelekea Mkoani Kigoma
 Mamia ya wakazi wa Kasulu Mkoani Kigoma waliojitokeza kumsikiliza Rais wa jamhuri ya muungano wa tanzania Dkt. John Pombe Magufuli wakati wa uzinduzi wa ujenzi wa barabara kwa kiwango cha lami yenye urefu wa kilometa 63 Kidawe - Kasulu. 
 Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli  akisalimiana na mamia ya wananchi wa Mamia ya wakazi wa Kasulu Mkoani Kigoma waliojitokeza kumsikiliza wakati wa uzinduzi wa ujenzi wa barabara kwa kiwango cha lami yenye urefu wa kilometa 63 Kidawe - Kasulu.
 Mke wa Rais Mama Janeth Magufuli akiwapungia mikono mamia ya wakazi wa Kasulu, Mkoani Kigoma.

Mamia ya wakazi wa Kasulu Mkoani Kigoma waliojitokeza kumsikiliza Rais wa Jamhuri ya muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli wakati wa uzinduzi wa ujenzi wa barabara kwa kiwango cha lami yenye urefu wa kilometa 63 Kidawe - Kasulu.
 Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli akisalimiana na baadhi ya viongozi walioshiriki uzinduzi wa uzinduzi wa ujenzi wa barabara kwa kiwango cha lami yenye urefu wa kilometa 63 Kidawe - Kasulu
  Rais wa Jamhuri ya Muungano waTanzania Dkt. John Pombe Magufuli akisalimiana na Mbunge Kigoma Mjini Mheshimiwa Zitto Zuberi Kabwe mara baada ya kuzindua  ujenzi wa barabara kwa kiwango cha lami yenye urefu wa kilometa 63 Kidawe - Kasulu
 Rais wa Jamhuri ya Muungano waTanzania Dkt. John Pombe Magufuli akiwa na viongozi mbalimbali wa mkoa wa Kigoma akikata utepe kuashiria Uzinduzi wa  ujenzi wa barabara kwa kiwango cha lami yenye urefu wa kilometa 63 Kidawe - Kasulu Mkoani Kigoma,
 Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli akiwapungia mkono wananchi waliokuwa wamefurika njiani mara baada ya  Uzinduzi wa  ujenzi wa barabara kwa kiwango cha lami yenye urefu wa kilometa 63 Kidawe - Kasulu Mkoani Kigoma.

WAJASIRIAMALI WAKIWA KAZINI


 .Kamera imenasa wakazi wa jiji Dar es Salaam wajasiliamali maarufu kama machinga wakiandaa biashara zao leo katika soko la Karume Ilala.
Machinga akisafisha viatu ili kwa kuingiza sokoni katika soko la Karume Ilala jijini Dar es Salaam.
Watembea kwa miguu wakikwepa shimo lililopo katika barabara ya Kilwa jijini Dar s Salaam.

Picha na Emmanuel Massaka,Globu ya jamii.

Dk. Kigwangalla afanya ziara mikoa ya Rukwa, Katavi na Tabora


Naibu Waziri wa Afya Maendeleo ya Jamii, Jinsia Wazee na Watoto, Mh. Dk.Hamisi Kigwangalla ameendelea na ziara yake ya kikazi ya kukagua huduma za Afya ‘Imarisha Afya’ katika Zahanati, Vituo vya Afya na Hospitali mbalimbali kwenye mikoa ya Rukwa, Katavi pamoja na Tabora.  

Akiwa katika mkoa wa Rukwa, Dk. Kigwangalla aliweza kutembelea Hospitali ya Sumbawanga ambayp ni ya Mkoa wa Rukwa na kujionea mambo mbalimbali huku akiwapongeza kwa namna walivyoboresha huduma zao ikiwemo ile ya Maabara, Chumba cha upasuaji na huduma zingine ambapo aliwaagiza kuhakikisha wanakuwa na hakiba ya kutosha ya damu salama kwa ajili ya dharura kwa wagonjwa wa ukanda huo. 

 Mbali na Hospitali ya Mkoa wa Rukwa, pia aliweza kutembelea kituo ca Laela ambapo pia mbali ya kujionea utendaji kazi wa kituo hicho alipongeza juhudi za Mbunge wa jimbo la Kwera, Mh. Ignas Alloyce Malocha kwa kushirikiana na wananchi wake katika masuala ya huduma za Afya. Ziara hiyo katika mkoa wa Rukwa, aliweza kumalizia katika Kituo cha Afya Wampembe kilichopo Wilayani Nkasi ambapo alijionea shughuli mbalimbali ikiwemo huduma za Upasuaji hata hivyo aliutaka uongozi wa kituo hicho ambacho kipo mwambao wa Ziwa Tanganyika kuhakikisha wanakamilisha mifum ya maji safi na salama ndani ya kituo pamoja na kuboresha huduma za Maabara na usafi kwa ajumla.  

Akiwa katika Mkoa wa Katavi, Dk. Kigwangalla aliweza kufanya ziara ya kushtukiza kituo cha Afya Inyonga,kilichopo Mlele majira ya Saa Sita mchana na kuweza kukagua maeneo mbalimbali ikiwemo Chumba cha Maabara, Chumba cha Upasuaji na wodi ya akina mama wanaosubiria kujifungua.  

Hata hivyo, Dk. Kigwangalla amemtaka Kaimu Mganga Mkuu wa Kituo hicho kumuandikia maelezo juu ya kutokuwepo kwa watoa huduma kwenye jingo la chumba cha upasuaji na eneo la wodi ya akina mama wanaosubiria kujifungua kwani licha ya kufika hapo hakukuta mtoa huduma hata mmoja kwa wakati huo hali ambayo inaweza kuleta hatari.  

“Nataka kupata maelezo kwa maandishi. Kwa nini hakukua na watoa huduma ndani ya Chumba cha upasuaji na kule kwa wodi ya wamama wajawazito. Nilifika kuwakagua kwa upande wa Maabara nimekuta safi mumeweza kuboresha huduma na mumezingatia maelezo yangu niliyoyatoa kipindi nilichofika kukagua mwaka jana. Lakini pia hali niliyoikuta katika maeneo hayo niliyotembelea bila kuwakuta wahusika hii ni hatari nitahitaji maelezo ya kimaandishi” alieleza Dk. Kigwangalla wakati akitoa maagizo kwa Kaimu Mganga Mkuu wa kituo hicho. 

 Aidha, akiwa katika mkoa wa Tabora, aliweza kutembelea eneo la jengo linalojengwa Hospitali ya Wilaya ya Uyui na baadae aliweza kumalizia ziara yake katika Zahanati ya Isikizya ambapo aliagiza Mkurugenzi wa Wilaya ya Uyui kuhakikisha wanatenga bajeti pamoja na kushirikiana na nguvu za wananchi na mbunge wa jimbo hilo wanajenga majengo ya kulazwa wagonjwa, chumba cha upasuaji, maabara na miundombinu mingine ili Zahanati hiyo ije kupanda na kuwa Kituo cha Afya kwani kinahudumia eneo kubwa katika mji huo wa Isikizya ambayo hipo ndani ya Makao makuu ya Wilaya hiyo.
Naibu Waziri wa Afya Maendeleo ya Jamii, Jinsia Wazee na Watoto, Mh. Dk.Hamisi Kigwangalla akikaguachumba cha upasuaji Hospitali ya Mkoa wa Rukwa
Naibu Waziri wa Afya Maendeleo ya Jamii, Jinsia Wazee na Watoto, Mh. Dk.Hamisi Kigwangalla akikagua Maabara ya Mkoa wa Rukwa
Naibu Waziri wa Afya Maendeleo ya Jamii, Jinsia Wazee na Watoto, Mh. Dk.Hamisi Kigwangalla akikaguachumba cha upasuaji Hospitali ya Mkoa wa Rukwa
Naibu Waziri wa Afya Maendeleo ya Jamii, Jinsia Wazee na Watoto, Mh. Dk.Hamisi Kigwangalla akitoa maagizo kwa viongozi wa Hospitali ya Mkoa wa Rukwa
Naibu Waziri wa Afya Maendeleo ya Jamii, Jinsia Wazee na Watoto, Mh. Dk.Hamisi Kigwangalla akiingia chumba cha Wodi ya wanawake kituo cha Afya Laela Mkoa wa Rukwa
Naibu Waziri wa Afya Maendeleo ya Jamii, Jinsia Wazee na Watoto, Mh. Dk.Hamisi Kigwangalla akielekea kukagua Maabara ya Kituo cha Afya Laela Mkoa wa Rukwa
Mkuu wa Wilaya ya Nkasi Mh. Saidi Mtanda akihutubia wakati Naibu Waziri wa Afya Maendeleo ya Jamii, Jinsia Wazee na Watoto, Mh. Dk.Hamisi Kigwangalla alipotembelea kituo cha Afya Wampembe Mkoa wa Rukwa
Naibu Waziri wa Afya Maendeleo ya Jamii, Jinsia Wazee na Watoto, Mh. Dk.Hamisi Kigwangalla akikagua kitanda ndani ya chumba cha kujifungulia katika kituo cha Afya Wampembe Mkoa wa Rukwa
Naibu Waziri wa Afya Maendeleo ya Jamii, Jinsia Wazee na Watoto, Mh. Dk.Hamisi Kigwangalla akitembelea kituo cha Afya Wampembe, Mkoa wa Rukwa. kulia ni Mkuu wa Wilaya ya Nkasi, Mh. Said Mtanda
Naibu Waziri wa Afya Maendeleo ya Jamii, Jinsia Wazee na Watoto, Mh. Dk.Hamisi Kigwangalla akikagua mfumo wa maji unaoingia kituo cha Afya Wampembe, kutokea Ziwa Tanganyika, Mkoa wa Rukwa
Naibu Waziri wa Afya Maendeleo ya Jamii, Jinsia Wazee na Watoto, Mh. Dk.Hamisi Kigwangalla akikagua chumba cha upasuaji mdogo cha Kituo cha Afya Nkasi alipotembelea hapo majira ya saa mbili usiku, Mkoa wa Rukwa
Naibu Waziri wa Afya Maendeleo ya Jamii, Jinsia Wazee na Watoto, Mh. Dk.Hamisi Kigwangalla akikagua eneo litakalojengwa majengo ya utanuzi wa kituo hicho cha Afya ambapo kikikamilika kinatarajia kuwa Hospitali ya Wilaya ya Nkasi Mkoa wa Rukwa
Naibu Waziri wa Afya Maendeleo ya Jamii, Jinsia Wazee na Watoto, Mh. Dk.Hamisi Kigwangalla akipatiwa maelezo ya maendeleo ya jengo linalojengwa kwa ajili ya Hospitali ya Wilaya ya Uyui, Mkoani Tabora, kutoka kwa Mbunge wa Jimbo la Tabora Kaskazini Mh. Almasi Maige
Naibu Waziri wa Afya Maendeleo ya Jamii, Jinsia Wazee na Watoto, Mh. Dk.Hamisi Kigwangalla akikagua jengo litakalojengwa Hospitali ya Wilaya ya Uyui, Mkoani Tabora.
Jengo linaloendelea kujengwa kwa ajili ya Hospitali ya Wilaya ya Uyui
 
Naibu Waziri wa Afya Maendeleo ya Jamii, Jinsia Wazee na Watoto, Mh. Dk.Hamisi Kigwangalla akikagua ndani ya Maabara ya Kituo cha Afya Inyonga, Mlele, Mkoani Katavi
Naibu Waziri wa Afya Maendeleo ya Jamii, Jinsia Wazee na Watoto, Mh. Dk.Hamisi Kigwangalla akisaini kitabu cha wageni Kituo cha Afya Inyonga, Mlele, Mkoani Katavi