Rais wa Uganda Yoweri Museveni amesema hafuatilii mjadala unaendelea kuhusu mpango wa chama chake cha NRM kuwasilisha mswada bungeni kuondoa kifungo cha katiba, kinachozuia mtu mwenye umri wa miaka 75 kuwania urais nchini humo.
Museveni ambaye atakuwa na umri wa miaka 76 wakati wa Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2021, amesema wanaozua mjadala huo wanajaribu kuwapotosha wananchi wa Uganda na kumharibia kazi anayoifanya.
Baadhi ya wabunge wa NRM wamekuwa wakinukuliwa wakisema wanamtaka rais Museveni aendelee kuongoza nchi hiyo katika siku zijazo kwa sababu hawajaona mtu mwingine wa kufanya hivyo.
Rais Museveni ambaye aliingia Madarakani mwaka 1986, amekuwa akisema kuwa tatizo la nchi yake na mataifa mengi ya Afrika sio kiongozi anayekataa madarakani muda mrefu bali ni kazi gani anayowafanyia.
Wanasiasa wa upinzani nchini humo wakiongozwa na mwanasiasa mkongwe Kizza Besigye, amesema jaribio la kuibadilisha kifungu cha katiba kumruhusu rais Museveni kuendelea kukaa madarakani ni kinyume cha katiba ya nchi hiyo na haikubaliki.
Licha ya chama tawala cha NRM kuunga mkono pendekezo hilo la kuondoa umri wa kuwania urais, kumeonekana upingamizi kutoka kwa vijana ndani ya chama hicho.
Ripoti zinasema kuwa tayari marekebisho hayo yamewasilishwa kwenye Gazeti la serikali tayari kupelekwa bungeni ili kujadiliwa.
Wachambuzi wa siasa wanasema kuwa marekebisho hayo yatapita kwa sababu wabunge wa NRM ni wengi ikilinganishwa na wale wa upinzani.
No comments:
Post a Comment