Saturday, February 18

Kiama posho serikalini chaja


POSHO za vikao ambazo mjadala wake umechukua takriban mwaka mmoja sasa, huenda zikafikia ukomo mwaka huu kutokana na kuwapo kwa taarifa kwamba wabunge wamepania kuzifuta katika Bajeti ya mwaka ujao wa fedha.

Habari ambazo zimelifikia gazeti hili kutoka bungeni na serikalini zinasema Tume ya Huduma za Bunge tayari imeanza kujadili suala hilo na kwamba uamuzi ni kuanza kufuta posho za vikao kwa wabunge ambazo ni Sh70,000 kwa siku.
Taarifa za kuwapo kwa mpango huo zimekuja siku chache tangu Rais Jakaya Kikwete alipokataa kuidhinisha mapendekezo mapya ya posho za vikao kwa wabunge kutoka kiasi hicho cha Sh70,000 hadi Sh200,000 kwa siku.

Ikiwa uamuzi huo utatekelezwa, utakuwa ni ‘ushindi’ kwa wabunge ambao waliasisi vita dhidi ya posho za vikao kiasi cha kusababisha tofauti za wazi na wabunge wenzao ambao wamekuwa wakiwatuhumu kwamba wanatafuta umaarufu wa kisiasa.

Miongoni mwa wabunge hao ni Mbunge wa Bumbuli (CCM), ambaye pia ni Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Nishati na Madini, January Makamba na Mbunge wa Kigoma Kaskazini (Chadema) ambaye pia ni Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Hesabu za Mashirika ya Umma, Zitto Kabwe.

Mwingine ni Kiongozi wa Upinzani Bungeni, Freeman Mbowe ambaye aliwahi kuziita posho za vikao kuwa ni wizi wa kitaasisi ulioasisiwa hali ukiwa hauna tija kwa Taifa na badala yake kupoteza fedha nyingi za Serikali.
Mmoja wa viongozi waandamizi wa Bunge ambaye hakutaka jina lake liandikwe gazetini alisema suala la wabunge kufuta posho za vikao tayari limeanza kujadiliwa na Tume ya Huduma za Bunge ambayo Mwenyekiti wake ni Spika Anne Makinda.
“Kuanzia mwaka ujao wa fedha tunataka kuacha kabisa kulipwa posho za vikao (sitting allowance), kwa hiyo hata hiyo Sh70,000 hatutachukua itakuwa ni ziro kabisa maana tumechoka kuandamwa,” alisema kiongozi huyo na kuongeza:
“Lakini wakati tukifanya uamuzi huo, serikalini, mahakamani na katika mashirika mengine ya umma nako wajiandae, hakuna bajeti yoyote ya posho za vikao itakayopitishwa na hili tutaanza kuwapa maelekezo rasmi wakati wa vikao vya mipango ya bajeti mwezi Aprili mwaka huu.”

Spika wa Bunge, Makinda alipotafutwa juzi na jana kuzungumzia taarifa za taasisi yake kuweka mkakati wa kufuta posho hizo, simu yake ya kiganjani ilikuwa ikiita kwa muda mrefu bila majibu.
Kwa upande wake Naibu Spika, Job Ndugai alipoulizwa iwapo kuna mpango wa wabunge kusimamia kufutwa kwa posho zote za vikao ndani ya Bunge, serikalini na katika Idara ya Mahakama hakukanusha wala kuthibitisha suala hilo, badala yake akashauri kwamba: “usubiriwe wakati mwafaka.”

Alipoulizwa wakati mwafaka ni upi alisema: “Mimi nadhani suala la posho linachosha, hakuna jambo jingine la kuzungumza ina maana ni posho tu? Tumesema sana kama ni kuhusu kufutwa basi mimi nadhani tusubiri wakati mwafaka, wakati wa bajeti maana mchakato wake unaanza Aprili, tusubiri tutapata majibu mwafaka,” alisema Ndugai ambaye amekuwa msemaji wa suala hilo kwa muda mrefu sasa.

Serikalini nako
Wakati wabunge wakiwa wameanza mchakato huo wa kufuta posho, Serikali nayo inatajwa kwamba iko katika mchakato wa kufuta malipo hayo ambayo yamekuwa yakitajwa kwamba hayana tija kwa nchi.
Katibu Mkuu Wizara ya Fedha, Ramadhani Kijja alisema juzi kuwa: “Ninachofahamu mimi ni kwamba posho ziko nyingi siyo posho za vikao tu, kwa hiyo ni kweli kwamba Serikali inazipitia zote ili kuzihuisha na baadaye kufanya uamuzi sahihi, lakini sasa si rahisi kujua ni uamuzi gani utakaofikiwa.”

Kijja alisema mapitio yatakayofanywa na wataalamu serikalini yatalenga kubaini aina za posho zilizopo, tija yake katika utekelezaji wa kazi za umma na hatimaye kuamua ni zipi zibaki, zifutwe au kuongezwa kwa kuzingatia mapendekezo ya wataalamu.

Katibu Mkuu huyo aliongeza: “Hata kama zipo zitakazobaki mapendekezo ya wataalamu yatatuambia iwapo zinahitaji kuongezwa au la, tusubiri wataalamu wakimaliza kazi basi tutafahamu uamuzi wa Serikali utakuwa ni upi.”

Wakati wa Bunge la Bajeti la Juni mwaka jana, Waziri wa Fedha na Uchumi, Mustafa Mkulo alisema: “Suala la kupunguzwa kwa posho zisizokuwa na tija ni sehemu ya mpango wa Serikali kupunguza matumizi.”
Licha ya kutoa kauli hiyo, Mkulo pamoja na wabunge kadhaa, walisikika wakiwabeza wenzao waliokuwa wakipinga kuwapo kwa posho za vikao kwa maelezo kwamba wanajitafutia umaarufu wa kisiasa.

Miongoni mwa mabishano yaliyowahi kutokea baina ya pande zinazopingana kuhusu suala hilo yalihusu fedha za posho katika bajeti ya 2011/12 pale Zitto aliposema kuwa Serikali ilitenga kiasi cha Sh987 bilioni kwa ajili ya malipo ya posho mbalimbali na kati ya hizo Sh360 bilioni ni malipo ya posho za vikao (sitting allowance), huku wabunge wakitengewa kiasi cha Sh11 bilioni.

Kiasi cha Sh360 bilioni kinachodaiwa kutengwa kwa ajili ya fedha za vikao kinatosheleza kujenga vyumba 30,000 vya madarasa ikiwa chumba kimoja kinagharimu Sh12 milioni. Pia kiasi hicho cha fedha kinatosheleza kugharamia barabara ya lami yenye urefu wa kilometa zipatazo 400.

Hata hivyo, Mkulo alikanusha madai ya kutengwa kwa kiwango hicho cha fedha kwa ajili ya posho pale aliposema kwamba posho zote kwa ujumla wake katika bajeti ya mwaka 2011/12 ni Sh352.75 bilioni na kwamba kati ya hizo posho za vikao ni Sh25.68 bilioni huku wabunge wakipata Sh4.92 bilioni.

Mbowe, Makamba na Zitto
Mbowe na January kwa nyakati tofauti wiki hii walisema hawafahamu kuwapo kwa mpango wa kufutwa kabisa kwa posho za vikao, isipokuwa Zitto ambaye alisema amesikia tetesi kwamba Tume ya Huduma za Bunge inalifanyia kazi suala hilo.
Alisema utoaji wa fedha za vikao uliasisiwa na Bunge umesambaa katika taasisi nyingine za umma na kusababisha watendaji kutunga semina na vikao vingi ilimradi wanapata posho huku kazi nyingine zikiendelea kulala.
“Huu ni wizi wa fedha za umma ambao umeasisiwa na sasa unaathiri utendaji katika mfumo mzima wa Serikali, si fedha tu kwani hata kazi zinalala kwani watendaji wote wanakimbilia kwenye vikao vya kutunga kwa sababu kuna posho na si vinginevyo,” alisema Mbowe.

Mbowe aliongeza kuwa kama suala ni mishahara midogo hilo ni jambo linalozungumzika na kwamba Serikali inaweza kujenga hoja na kupandisha mishahara kwa kiwango kinachowezesha watumishi wa umma wakiwamo wabunge kujikimu, lakini si kuweka posho ambazo zinawanufaisha watu wachache na kujenga matabaka miongoni mwa watumishi wa umma.
“Mimi ninaamini watumishi wote wa umma wakiwamo wabunge tunapaswa kulipwa vizuri, kwa hiyo tujenge hoja za malipo mazuri kwa watumishi wote wa ujumla, lakini si kuanzisha posho za vikao kwa kisingizio cha malipo kuwa kidogo halafu hao wengine wadogo wanahudhuria kikao gani?”

Kwa upande wake Zitto alisema: “Nimesikia kwamba kuna mpango huo wa kufuta posho, kama upo ni hatua kubwa sana tutakuwa tumepiga. Msimamo wangu uko palepale kwamba posho za vikao siyo tatizo kwa wabunge tu hata kwa watumishi wengine wa umma na mashirika ya umma.”

Alisema hatua ya Rais Jakaya Kikwete kutoidhinisha nyongeza ya posho za wabunge kama walivyokuwa wamependekeza, ni ushindi wa awali ambao hauna budi kusambazwa katika maeneo mengine kwa kufuta malipo hayo katika mfumo mzima wa Serikali Kuu, Serikali za Mitaa na mashirika yote ya umma.

Naye Makamba alisisitiza kwamba msimamo wake kwamba posho ni tatizo katika mfumo wa utumishi wa umma upo palepale na kwamba ikiwa Bunge litaamua kwamba zifutwe litakuwa ni jambo jema.

“Sifahamu kuhusu mpango wa kufutwa kwake, ila sisi wengine mnatufahamu. Msimamo wangu hauwezi kubadilika katika hili kwa hiyo kama wenzetu wanaungana na sisi kwamba posho hizi za viko zifutwe litakuwa ni jambo jema sana mimi nitakuwa wa kwanza kuliunga mkono,” alisema na kuongeza:

“Nadhani kama kweli hilo lipo na likifanyika kwa nia ya dhati nina hakika tunaweza kusonga mbele kwa ajili ya masuala mengine muhimu badala ya kila siku kubishana kwa mambo ambayo yako wazi”.

Ardhi ya Tanzania yazidi kuumiza wanachama EAC Send to a friend Friday, 17 February 2012 21:13 0 digg Keneth Goliama MVUTANO kuhusu suala la ardhi umeibuka jana katika mkutano wa wataalamu wa kamati za Serikali Kanda ya Afrika Mashariki uliojadili madini, baadhi ya nchi zimepinga kuingiza ardhi kwenye mambo yanayoshughulikiwa na Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC). Wakichangia katika mkutano huo kwa nyakati tofauti, wajumbe walisema itakuwa ngumu kwa baadhi ya nchi kuingia kuingiza suala hilo kwenye mambo ya EAC, kwa sababu bado ndani ya nchi hizo kuna migogoro ya ardhi. Wakati baadhi ya wajumbe wakipinga hilo, wengine kutoka Uganda walisema haiwezekani nchi wanachama kuogopa kuingiza suala hilo kutokana na kuonyesha maendeleo mazuri. Hata hivyo, wajumbe kutoka nchi ya Kenya walionyesha wasiwasi wa uharaka wa kuingia kuingiza ardhi kwenye masuala ya EAC kutokana na mapigano yanayotokea ndani ya baadhi ya nchi wanachama. “Itakuwa ajabu kuingiza shirikisho la ardhi katika jumuiya wakati nchi za Rwanda Burundi na Tanzania zikionyesha kuwa na ugomvi wa ardhi na wawekezaji,” alisema Mkuu wa Sera ya Mipango na Ardhi kutoka Ethiopia, Dk John Kangwanja. Dk Kangwanja alisema kama hatua hiyo itafikia, kuna nchi zinaweza kuathirika kwa kiasi kikubwa kutokana na migogoro ambayo inaendelea kujitokeza baina ya wazawa na wawekezaji. Wakati suala hilo lilipokuwa likizidi kuzua mvutano kwenye ukumbi, wawakilishi wa Tanzania wakiongozwa na Naibu Waziri wa Fedha, Gregory Teu, walionekana kutochangia chochote huku waziri akiulizwa suala hilo kutoa maelezo alijibu kuwa hana maelezo. Wachiangiaji hao walisema Sheria ya mwaka 1995 na Sera ya Ardhi ya Tanzania, inapishana kwa kiasi kikubwa kutokana na kupitwa na wakati.Mhadhiri kutoka Chuo Kikuu cha Ardhi (ARU), Profesa Lucugga Kironde, alisema Tanzania ikikubali kuingiza suala hilo, itarajie kukumbwa na migogoro mikubwa kutokana na nchi nyingi za jumuiya hiyo zinanyemelea baada ya kwao kukumbwa na uhaba. Profesa Kironde alisema haiwezekani Tanzania ikiingia kwenye shirikisho bila kufanya marekebisho ya sheria ya ardhi, Watanzania wataendelea kuonekana maskini huku wachache kutoka EAC wakinufaika. “Afrika ina rasilimali za kutosha kila mahali hasa madini,umefika wakati kufuatilia kwa makini sheria ya ardhi ili mikataba ya nchi iweze kunufaisha wazawa kutokana na kumiliki ardhi,” alisema Profesa Kironde.


MVUTANO kuhusu suala la ardhi umeibuka jana katika mkutano wa wataalamu wa kamati za Serikali Kanda ya Afrika Mashariki uliojadili madini, baadhi ya nchi zimepinga kuingiza ardhi kwenye mambo yanayoshughulikiwa na Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC).

Wakichangia katika mkutano huo kwa nyakati tofauti, wajumbe walisema itakuwa ngumu kwa baadhi ya nchi kuingia kuingiza suala hilo kwenye mambo ya EAC, kwa sababu bado ndani ya nchi hizo kuna migogoro ya ardhi.
Wakati baadhi ya wajumbe wakipinga hilo, wengine kutoka Uganda walisema haiwezekani nchi wanachama kuogopa kuingiza suala hilo kutokana na kuonyesha maendeleo mazuri.

Hata hivyo, wajumbe kutoka nchi ya Kenya walionyesha wasiwasi wa uharaka wa kuingia kuingiza ardhi kwenye masuala ya EAC kutokana na mapigano yanayotokea ndani ya baadhi ya nchi wanachama.

“Itakuwa ajabu kuingiza shirikisho la ardhi katika jumuiya wakati nchi za Rwanda Burundi na Tanzania zikionyesha kuwa na ugomvi wa ardhi na wawekezaji,” alisema Mkuu wa Sera ya Mipango na Ardhi kutoka Ethiopia, Dk John Kangwanja.

Dk Kangwanja alisema kama hatua hiyo itafikia, kuna nchi zinaweza kuathirika kwa kiasi kikubwa kutokana na migogoro ambayo inaendelea kujitokeza baina ya wazawa na wawekezaji.

Wakati suala hilo lilipokuwa likizidi kuzua mvutano kwenye ukumbi, wawakilishi wa Tanzania wakiongozwa na Naibu Waziri wa Fedha, Gregory Teu, walionekana kutochangia chochote huku waziri akiulizwa suala hilo kutoa maelezo alijibu kuwa hana maelezo.

Wachiangiaji hao walisema Sheria ya mwaka 1995 na Sera ya Ardhi ya Tanzania, inapishana kwa kiasi kikubwa kutokana na kupitwa na wakati.Mhadhiri kutoka Chuo Kikuu cha Ardhi (ARU), Profesa Lucugga Kironde, alisema Tanzania ikikubali kuingiza suala hilo, itarajie kukumbwa na migogoro mikubwa kutokana na nchi nyingi za jumuiya hiyo zinanyemelea baada ya kwao kukumbwa na uhaba.

Profesa Kironde alisema haiwezekani Tanzania ikiingia kwenye shirikisho bila kufanya marekebisho ya sheria ya ardhi, Watanzania wataendelea kuonekana maskini huku wachache kutoka EAC wakinufaika.

“Afrika ina rasilimali za kutosha kila mahali hasa madini,umefika wakati kufuatilia kwa makini sheria ya ardhi ili mikataba ya nchi iweze kunufaisha wazawa kutokana na kumiliki ardhi,” alisema Profesa Kironde.