Saturday, March 3

WAZIRI LUKUVI ATANGAZA KIAMA WADAIWA SUGU ARDHI


WAZIRI wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, William Lukuvi, amesema ifikapo Aprili 30, mwaka huu ndiyo siku ya mwisho wa ulipaji kodi ya pango la ardhi kwa halmashauri zote nchini na wamiliki wa ardhi.
Lukuvi alisema wale wote watakaoshindwa kufanya hivyo watatangazwa kwenye magazeti ya umma na kuwasilisha taarifa zao kwa Rais Dk. John Magufuli ili awashughulikie.
Waziri Lukuvi alitoa agizo hilo wilayani Ilemela Mkoa wa Mwanza jana wakati akizungumza na wafanyakazi wa idara ya ardhi na watumishi wa manispaa hiyo katika ziara yake ya siku tatu ya kutatua migogoro baina ya wananchi na taasisi za Serikali.
Akizungumzia juu ya makusanyo ya kodi ya pango, Lukuvi, alizitaka halmashauri zote nchini kuhakikisha kuwa inalifanya zoezi la ukusanyaji wa kodi hiyo kuwa ya msingi na wajibu kwao na zifikie lengo la asilimia 100 za makusanyo ya mwaka wa fedha 2017/18 ifikapo Aprili 30, mwaka huu.
“Wasiofikia lengo hilo nitawatangaza kwenye magazeti ya umma na kupeleka taarifa zao kwa Rais aone wanavyomhujumu, tunafanya hii yote kwa sababu hii ni kodi pekee inayokusanywa na halmashauri kwa niaba ya Serikali kuu.
“Wale wote ambao hawajalipa (wadaiwa sugu), nataka kusikia mpaka kufikia mwezi wa tano wawe wamesekwa rumande kwa sababu tunataka mpaka kufikia mwisho wa mwaka wale wote waliotakiwa kulipa wawe wamelipa na mabaraza yote ya ardhi yawe bize kusikiliza mashauri haya ya ardhi, tutawaburuza mahakamani bila kujali jina na heshima zao,” alisema Lukuvi.
Hata hivyo, akizungumzia zoezi la urasimishaji katika wilaya za Ilemela na Nyamagana mkoani Mwanza, Waziri Lukuvi, aliwasifu kwa kazi nzuri waliyofanya huku akiwataka kuongeza kasi katika umilikishwaji wa ardhi.

SERIKALI YATOA TAMKO KUIJIBU MAREKANI, UE


SERIKALI imeutaka Umoja wa Nchi za Ulaya (EU) na nchi ya Marekani kutotoa matamko pasipo kuwa na taarifa za kutosha juu ya matukio ya watu kuuawa, kupigwa risasi na kutekwa.
Kauli hiyo ya serikali imekuja ikiwa ni takribani wiki moja tangu EU na kabla ya hapo ubalozi wa Marekani kutoa tamko kukemea na kutaka uchunguzi wa kina juu ya matukio yenye viashiria vya ukatili na vitisho hapa nchini ikiwamo watu kuuawa, kupigwa risasi na kutekwa.
Katika tamko lake lililotolewa jana na Waziri wa Mambo ya Nje,Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Kikanda na Kimataifa, Dk. Augustine Mahiga, ambalo liligusia shutuma zinazoelekezwa Tanzania kushirikiana kibiashara na Korea Kaskazini na hivyo kudaiwa kuvuja mkataba Umoja wa Kimataifa ambayo imeiwekea vikwazo nchi hiyo, serikali pia ilieleza kushangazwa na haraka ya nchi hizo kutoa matamko katika wakati ambao vyombo vya dola vinaendelea na uchunguzi wake.
Zaidi serikali ilikwenda mbali na kuhoji EU pamoja na Marekani kutoa matamko hayo sasa na ikishindwa kufanya hivyo wakati yalipotokea mauaji yaliyokuwa yakitekelezwa na watu wasiojulikana katika maeneo ya Kibiti, Mkuranga na Rufiji Mkoani Pwani tena yakiwagusa viongozi wa chama tawala.
“Matamko mbalimbali yanaonesha ukosefu wa uelewa wa usalama na changamoto ambazo serikali imekuwa ikikumbana nazo katika miezi 18 iliyopita, taarifa hizo zilizotolewa hazikuzingatia ukweli wa mwenendo wa kisiasa na usalama nchini” lilieleza tamko hilo la serikali.
Serikali pia ilieleza udhaifu iliouona katika matamko hayo kushindwa kutambua hatua kubwa na muhimu zilizochukuliwa na Rais Dk. John Magufuli katika kapambana na rushwa, dawa ya kulevya, ukwepaji kodi, ujangili  na uwajibikiaji wa mamlaka za ulinzi na usalama.
“Wageni wetu washirika wanapaswa kujitahidi kuelewa mazingira haya magumu ambayo nchi inakabiliana nayo kabla ya kutoa taarifa zenye hisia zisizothibitishwa ambazo zinaweza kuleta ushawishi mkubwa kwa umma…kwa upande wetu tunakaribisha mazungumzo ya wazi kutoka kwa marafiki zetu na washirika juu ya masuala ambayo yanahitaji ufafanuzi ili waweze kupatiwa taarifa bora zaidi” lilieleza tamko hilo
Wiki iliyopita EU kupitia ofisi zake hapa nchini ilitoa tamko kukemea matukio yenye viashiria vya ukatili na vitisho hapa nchini ikiwamo kuuawa kwa Katibu wa Chadema, Kata ya Hananasif, Daniel John,  kifo cha mwanafunzi aliyepigwa risasi, Akwilina Akwilini na mengine.
Tamko hilo la EU lilitolewa kwa ushirikiano na mabalozi wa nchi wanachama wenye uwakilishi hapa nchini na kuungwa mkono na mabalozi wa nchi za Norway, Canada na Uswisi.

CHADEMA YAIANDIKIA BARUA MAREKANI, UJERUMANI


CHAMA cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), kimeziandikia barua Marekani na Ujerumani kuzitaka kuziangalia tuhuma zilizoelekezwa dhidi yao za kukihusisha na chama hicho katika kile kinachodaiwa kuwa ni mipango ya kuhatarisha usalama wa Tanzania.
Barua mbili za Chadema ambazo zimeandikwa Machi mosi mwaka huu na kusainiwa na Mkuu wa Kitengo cha Habari cha chama hicho, Tumaini Makene, zimetaka balozi za nchi hizo nchini kujibu tuhuma hizo ambazo zilielekezwa na Cyprian Musiba aliyejitambulisha kama Mkurugenzi wa Kampuni ya CZI.
Gazeti hili ambalo limefanikiwa kuona barua hizo jana, Chadema kimesema kimeona umuhimu wa kuchukua hatua hiyo ili kupata mwitikio wa nchi hizo juu ya tuhuma hizo nzito ambazo zinatakiwa kuangaliwa zaidi.
Katika barua yenye kumbukumbu No. C/HQ/ADM/KS/24/02  ambayo imeelekezwa kwa John Espinos ambaye ni Mkuu wa Kitengo cha Siasa na Uchumi, Ubalozi wa Marekani, Chadema imeeleza kwamba Februari 25, mwaka huu mtu aliyejulikana kwa jina la Cyprian Musiba, aliituhumu Marekani kwa kufanya mipango na mikakati mbalimbali ya kuhatarisha usalama wa Taifa la Tanzania.
Barua hiyo ilielezea kwa urefu kwamba Musiba kwa kupitia majukwaa mbalimbali ya kubadilishana taarifa na mawasiliano vikiwamo vipande vya video vilivyosambazwa kwenye mitandao ya kijamii alisema Marekani inadaiwa kupanga watu au kuendesha mikakati inayohatarisha usalama wa Tanzania.
“Musiba alikwenda mbali zaidi kwa  kutuhumu kuwa nchi yako imekuwa ikishirikiana na Chadema kupanga uhatarishaji wa usalama wa nchi. “Alituhumu FBI (Federal Bureau of Investgation) kuwa inajihusisha na baadhi ya Watanzania katika mipango hiyo.”
Pia barua hiyo ilisema kuwa Musiba alitaka dunia na Afrika yote kutambua uwapo wa hiyo mipango hatari dhidi ya Tanzania ambayo Marekani inahusishwa kwa namna moja au nyingine kufanya mipango hiyo.
“Kutokana na mapenzi na uwajibikaji wetu kwa nchi yetu ya Tanzania na kama taasisi  ikiwa ni sehemu ya wadau kwa maisha yajayo ya nchi yetu pendwa, kwa kuweka mbele masilahi ya nchi na wakazi wake ndani na nje ya nchi, katikati ya kila kitu na kwa kuguswa na tuhuma kama mdau, tunahisi msukumo na kuona umuhimu wa kukuandikia, hivyo tunaweza kupata mwitikio wako kwa tuhuma hizi nzito na tunafikiri kuziangalia zaidi.
“Katika barua hii tumeambatanisha CD zenye vipande vya video vinavyomwonyesha Cyprian Musiba akiviambia vyombo vya habari siku tajwa hapo juu.”
Kwa kupitia hoja kama hizo barua ya pili yenye kumbukumbu No C/HQ/ADM/KS/24/01 ambayo ilielekezwa kwenda kwa Joerg Hererra ambaye ni Mkuu wa Kitengo cha Siasa na Uchumi cha Ubalozi wa Ujerumani, Chadema ilisema Musiba alikaririwa akikituhumu chama tawala cha nchi hiyo cha Christian Democratic Union (CDU) kushiriki mipango ya kuhatarisha usalama wa Tanzania.
Jumapili iliyopita Musiba alizungumza na baadhi ya waandishi wa habari na kutoa tuhuma nzito kwa nchi hizo mbili huku akitoa orodha ya watu ambao aliwaita ni hatari kwa usalama wa Taifa.
Watu hao ni Mange Kimambi ambaye alimtuhumu kuwa anatumiwa na FBI kuchochea machafuko nchini.
Wengine ni Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe, Maria Sarungi, Zitto Kabwe, Tundu Lissu, John Heche, John Marwa, Evarist Chahari, Julius Mtatiro pamoja na kikundi cha Janja weed alichodai kinaratibiwa na wafuasi wa CUF.

MAOFISA TBS WAFANYA UKAGUZI WA KUSHTUKIZA

MAOFISA wa Shirika la Viwango Tanzania (TBS), wamefanya ukaguzi wa kushtukiza kwa wasambazaji wa bidhaa za viwandani na kuchukua sampuli na kuzihakiki ili kujiridhisha kama zinakidhi matakwa ya leseni walizopewa kwa ajili ya kutumia alama ya ubora.
Maofisa wa TBS walifanya ukaguzi Dar es Salaam juzi na kuchukua sampuli za nondo na mabati kutoka kwa Wakala wa bidhaa hizo, FMJ Hardware Ltd.
Akizungumza baada ya ukaguzi huo, Ofisa Viwango wa TBS, Joseph Ismail, alisema ukaguzi huo ni kwa mujibu wa taratibu za shirika hilo ili kuhakikisha wazalishaji waliopewa leseni ya kutumia alama ya ubora wanaendelea kufuata viwango vya ubora.
“Mojawapo ya kazi zetu ni kutoa leseni kwa wazalishaji, kwa hiyo tunafanya ukaguzi wa kushtukiza kwa wasambazaji wakubwa (mawakala) ili kuchukua sampuli na kuzipima katika maabara zetu kuona kama zinakidhi ubora tuliohakiki,” alisema.
Pia alisema wakitoa leseni ya ubora kwa wazalishaji viwandani, bidhaa zinazozalishwa hupelekwa kwa mawakala wanaowauzia wananchi, hivyo na wao wanafanya ukaguzi huo kujiridhisha kama waliopewa leseni hizo wanaendelea kufuata taratibu walizopewa.
Alisema wale wanaokiuka matakwa ya leseni wanapewa taarifa na kuchukuliwa
hatua za kisheria ikiwamo kuteketezwa kwa bidhaa hizo na ili kuepukana na usumbufu huo aliwataka wazalishaji kote nchini kuhakikisha wanazalisha bidhaa zinazokidhi matakwa ya leseni zao.
“Kwa hiyo lengo la ukaguzi huu ni kuzuia wazalishaji wasiingize sokoni bidhaa ambazo hazina ubora na mwisho kabisa kuwaepusha wasipate hasara kwa kulinda mitaji yao,” alisema.
Kwa upande wake, Ofisa Uhusiano wa TBS, Rhoida Andusamile, alisema ukaguzi huo unakusudia kuhakikisha bidhaa zinazozalishwa viwandani zinakidhi matakwa ya leseni wanazopewa.
“Shirika letu lipo kwa ajili ya kuwalinda walaji, ndiyo maana tunapita kwa wasambazaji wakubwa (mawakala) kuchukua sampuli ili kuzipima upya  kujiridhisha kama zina ubora ule ule wa kwanza tulioupima katika maabara wakati tunawapa leseni ya kutumia alama ya ubora ya shirika letu,” alisema.

Baraza la Usalama lalaani mashambulizi ya Ougadougou

Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa limelaani kile ilichokiita "mashambulizi ya kikatili na woga" dhidi ya makao makuu ya jeshi la ubalozi wa Ufaransa katiika mji mkuu wa Burkina Faso, Ougadougou. 

Burkina Faso Ouagadougou Attacken in Innenstadt (Getty Images/AFP/A. Ouoba)
Taarifa ya Baraza hilo imetaka waliohusika na mashambulizi hayo ya Ijumaa (2 Februari) yaliyouwa wanajeshi wanane, kukamatwa na kufikishwa kwenye mikono ya sheria.
Katika mashambulizi hayo pia washambuliaji wanane waliuawa, wanne kwenye makao makuu ya jeshi na wengine wanne karibu na ofisi za ubalozi wa Ufaransa, kwa mujibu wa wizara ya mawasiliano ya Burkina Faso.
Serikali pia ilisema idadi hiyo ya waliouawa haijumuishi raia ambao nao wanahofiwa kupoteza maisha kwenye mkasa huo unaohusishwa na kundi la al-Qaida magharibi mwa Afrika.
Waziri wa Ulinzi, Clement Sawadogo, alikiambia kituo kimoja cha redio kwamba kiasi cha watu 80 walijeruhiwa, baadhi yao wakiwa na hali mbaya sana.
Mapema hapo Ijumaa, msemaji wa serikali, Remis Dandjinou, aliyaita mashambulizi hayo kuwa ni ya "kigaidi", bila ya kutaja washambuliaji waliohusika. 
Rais Emmanuel Macron wa Ufaransa aliyalaani mashambuliz hayo na alizungumza na mwenzake wa Burkina Faso, Roch Marc Christian Kabore, siku ya Ijumaa, kwa mujibu wa Ikulu ya Ufaransa.
"Ufaransa imedhamiiria kupambana na makundi ya kigaidi kwa kushirikiana na mataifa ya Sahel," ilisema taarifa ya Kasri la Eylsee. 
Meya wa Ougadougou, Armand Beouinde, aliliambia gazeti la Le Monde la Ufaransa kwamba mashambulizi hayo yanawezakana sana kufanywa na wapiganaji wa siasa kali. Hata hivyo, hakuna kundi lililodai kuhusika nayo kwa haraka.
Jinsi mashambulizi yalivyotokea
Watu wenye silaha na wasiofahamika walianza kurusha risasi majira ya saa 4:00 asubuhi siku ya Ijumaa, wakiilenga ofisi ya waziri mkuu, jengo la mkuu wa jeshi na ubalozi wa Ufaransa mjini Ougadougou.
Moshi ukifuka kutoka jengo la makao makuu ya jeshi la Burkina Faso kufuatia mashambulizi mjini Ougadougou.
Moshi ukifuka kutoka jengo la makao makuu ya jeshi la Burkina Faso kufuatia mashambulizi mjini Ougadougou.
Wanajeshi na maafisa wa kikosi maalum baadaye waliyazingira majengo hayo na kuanza msako, kwa mujibu wa mwandishi wa shirika la habari la Ujerumani, dpa, ambaye alikuwepo kwenye eneo la tukio. 
Wizaya ya Masuala ya Ulaya na Mambo ya Nje ya Ufaransa iliwataka raia wake wanaoishi Ougadougou kubakia kwenye maeneo salama, kufuta safari zao kwenye mji huo na kufuata maelekezo kutoka mamlaka za Burkina Faso.
Mwandishi huyo wa dpa aliripoti kuona moshi mkubwa ukifuka kwenye ofisi ya mnadhimu mkuu wa jeshi, huku magari kadhaa ya wagonjwa yakielekea kwenye jengo hilo.
Shahidi mmoja aliiambia dpa kwamba aliona washambuliaji watano wakishuka kwenye gari na kuwarushia watu risasi kabla ya kuelekekea kwenye ubalozi wa Ufaransa.
Wakati huo huo, wanajeshi waliweka ulinzi maalum kwenye majengo ya ofisi ya mnadhimu mkuu wa jeshi, waziri mkuu na ubalozi wa Ufaransa.
Taifa hilo la Afrika Magharibi limekuwa likikumbwa na ghasia za washambuliaji wa itikadi kali kutokea Mali katika miaka ya hivi karibuni. Mnamo mwezi Agosti 2017, mashambulizi kwenye mkahawa mmoja mjini Ougadougou yaliuwa watu 18.
Mwaka 2916, kiasi watu 30 waliuawa wakati wapiganaji hao wa siasa kali walipouvamia mkahawa mwengine kwenye mji huo mkuu.

Berlusconi amuunga mkono Tajani

Waziri Mkuu wa Zamani wa Italia Silvio Berlusconi amempigia chapuo Rais wa Bunge la Umoja wa Ulaya Antonio Tajani,ikiwa imesalia siku moja kabla ya uchaguzi mkuu nchini Italia.

Frankreich ehem. Ministerpräsident von Italien Silvio Berlusconi und Präsident des EU-Parlaments Antonio Tajani (picture-alliance/dpa/Sputnik/A. Vitvitsky)
Berlusconi, ambaye alizuiwa kuwa mgombea kutokana na kukutwa na hatia za udanganyifu, amejiweka katika nafasi ya kuwa mfanya mipango muhimu kupitia uongozi wake wa kundi lenye kufuata siasa za mrengo wa kulia nchini Italia lijulikanalo kama Forza Italia na akiongoza tena vyama vinne vilivyojiunga pamoja, ambavyo vinatarajiwa kujizolea wingi wa kura katika uchaguzi wa taifa hilo siku ya Jumapili.
Sababu za Tajani kuwa waziri mkuu
EU Antonio Tajani (picture alliance/ZUMAPRESS/C. Mahjoub)
Mgombea wa uwaziri mkuu wa Italia Antonio Tajani
Tajiri mkubwa, katika tasnia ya vyombo vya habari mwenye umri wa miaka 81, ambaye anazidhibiti siasa za Italia kwa karibu miongo miwili sasa, anasema Tajani anaonesha ishara ya kuwa tayari kuongoza muungano wao, kama ataibuka na ushindi katika mchakato huo wa upigaji kura. Akizungumza kupitia kituo cha televisheni cha Canale 5, kimoja kati ya mtandao wa vituo vyake amesema "Huyu ni mtu ambaye anaijua vyema Ulaya yote."
Duru zinaeleza kuwa, chaguo hilo linaweza kumwingiza Berlusconi katika mikwaruzano na washirika wake wenye wasiwasi na Umoja wa Ulaya, na hasa kiongozi wao Matteo Salvini, ambaye hata yeye anaonesha hamasa ya kuutaka uwaziri mkuu wa Italia. Lakini awali, waziri mkuu huyo wa zamani alifanya jaribio la kujenga dhana ya uwepo wa mgawanyiko mkubwa kati yake na Salvini, pamoja na Giorgia Meloni wa kundi lenye kujiita "Brothers of Italy" - Ndugu wa Italia (Fdl).
Sauti ya mpiga kura
Kufuatia heka heka za uchaguzi huo dereva wa teksi, Giancarlo Paolini anatoa maoni yake "Nitalipigia kura kundi la "5 Star" kwa sababu katika maisha lazima nikabiliane na changamoto tofauti na nipate mawazo. Nataka kubadili jambo na nataka kuliweka kundi hilo katika majaribio. Nataka kuona kama wanatenda wanachosema, endapo watatatua hizi changamoto mpya na kuleta mafanikio."
Lakini safari hii Berlusconi amejitokeza mbele ya vyombo vya habari mjini Roma akisema hakuna tofauti yoyote kati yao na kama kungekuwa na tofauti miongoni mwao, wasingekuwa na muungano, wasingekuwa na chama kimoja. Na kuongeza kwamba wagombea wa muungano huo wote kwa pamoja wanawasiliana kwa njia ya simu karibu kila siku.
Shirika la habari la Ufaransa AFP limesema Berlusconi aliwafunika washirika wake watatu katika tukio hilo kwa kufika mwishoni na kuibuka msisimko na kuimbwa kwa nyimbo zenye kutaja jina lake " Silvio, Silvio" kulikofanywa na wanaharakati wa vyama walikuwepo mkutanoni. Kwa mujibu wa uchambuzi wa mwisho wa maoni kwa uchaguzi huo wa Jumapili, tawi lenye kufauta siasa za mrengo wa kulia ndio pekee lenye nafasi ya kushinda kwa wingi wa kura katika bunge.

Baraza la Maaskofu : Majadiliano ndio nyenzo ya kupambana na ubinafsi


Serikali ya Tanzania imeshauriwa kuheshimu matakwa ya wananchi na kuonyesha dhamira yake ya dhati kwa kuendeleza maongezi ya mchakato wa Katiba Mpya nchini, na kuwa majadiliano ndio nyenzo ya kupambana na ubinafsi.
Naibu Katibu Mkuu wa Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania (TEC), Padri Daniel Dulle, alisema hayo Ijumaa wakati akifungua kongamano la kujadili Katiba na ujenzi wa amani wakati wa uchaguzi lililoandaliwa na Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC) mjini Dar es Salaam.
Hii ni mara ya pili katika kipindi kisichopungua mwezi mmoja kwa TEC kutoa kauli kama hiyo, kwani kumbukumbu zinaonyesha kuwa Februari 11 mwaka huu, Baraza hilo katika ujumbe wake wa Kwaresma lilitoa msimamo katika masuala matatu kisiasa, kiuchumi na kijamii ambapo lilionya madhara ya kutozingatia matakwa ya Katiba katika kuendeleza shughuli za kisiasa.
Amesema ili imani iendelee kuwepo nchini ni lazima majadiliano yawe ndio nyenzo kuu itakayosaidia kuhuisha mchakato wa Katiba mpya.
Historia ya mchakato wa katiba mpya
Kwa mujibu wa wachambuzi wa siasa nchini Tanzania marekebisho ya Katiba 2011, yanalalamikiwa sana kwa kutungwa bila kuwapa watanzania nafasi ya kushiriki na pia kumrundikia Rais madaraka yote bila hata kuwashirikisha wapiga kura wake.
Wanadai kuwa katika jamii tuliyo nayo hivi leo demokrasia na utawala wa kidemokrasia ni moja ya dhana muhimu sana zinazoleta mchango mkubwa katika maendeleo ya nchi yoyote.
Pia wanasema kuwa demokrasia na utawala wakidemokrasia sio tu vichochezi vya maendeleo bali ni mihimili mikubwa yakupambana na umaskini hasa katika nchi kama Tanzania na nyinginezo.
TEC yahimiza kuwepo majadiliano
Gazeti la Mtanzania limeripoti kuwa Padri Dulle, akizungumza kwa niaba ya Katibu Mkuu wa TEC Padri Raymond Saba , alisema baada ya mchakato wa Katiba Mpya kukwama sasa ni fursa kuendeleza majadiliano juu ya suala hilo ili kudumisha amani nchini.
“Majadiliano ni nyenzo ya kupambana na tabia ya ubinafsi, ili kujenga umoja huo lazima kuwepo na upendo, mshikamano na maridhiano ya watu na kila mtu kupewa nafasi ya kutoa maoni hata kama yanapingana na mtu mwingine na ukiwa unapatanisha kwa njia hiyo unaitwa mwana wa Mungu.
“Ndilo lengo la kukaa hapa na kujadiliana ili kujenga Taifa letu kwa lengo la kupata Katiba Mpya ambayo kila mmoja anaitamani. Kunapotokea mtafaruku ndipo kunakuwa na chuki kama kikundi kingine hakishirikishwi. Haki na amani ni matunda tu, kwani ukosefu wa haki ni chanzo cha vita inayoacha makovu na chuki za kisiasa kwenye chaguzi. Kama tunataka kukwepa haya makovu lazima watu tujenge tabia ya kujadiliana,” alisema.
Historia ya Kanisa Katoliki
Alisema tangu miaka ya 1800, Kanisa Katoliki limekuwa likitoa miongozo kuhusu masuala ya utawala ili kudumisha amani.
“Suala la Katiba ni nia ya watu wote si ya mtu mmoja, ni sauti ya watu na kadiri watu wanavyohitaji sheria na miongozo. Pengine kikundi kikubwa kinahitaji kidogo hakihitaji cha msingi ni kuangalia wananchi wanahitaji nini kwani kwa mujibu wa ibara ya nane ya Katiba ya sasa, Katiba ni mali ya wananchi,” alisema.
Kituo cha Demokrasia (TCD)
Wakati huohuo Profesa Mwesiga Baregu kwa niaba ya Mwenyekiti wa Kituo cha Demokrasia nchini (TCD), James Mbatia, aliitaka Serikali kuhakikisha kabla ya kuingia kwenye uchaguzi mkuu mwaka 2020, Katiba Mpya inapatikana.
Baregu ambaye pia alikuwa Mjumbe wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba, alisema ni vema kukamilisha kiporo hicho cha Katiba.
Ameongeza kuwa kuna ishara za viashiria vya hatari zimekwisha onekana katika chaguzi ndogo zilizofanyika hivi karibuni hususani Jimbo la Kinondoni, na ni vema tukaanza mchakato huo.
Njia Tatu zakuendeleza mchakato
Aidha, Profesa Baregu, alipendekeza njia tatu za kuendeleza mchakato wa Katiba Mpya kwa kuwa hali iliyopo lazima kuwepo na njia ya kuishawishi Serikali.
“Kwanza twende kwenye kura ya maoni, tunaweza kutangaza kura ya maoni kuhusu Katiba pendekezwa ila sijui kura ya maoni kama itaendeshwa kwa uhuru au haki. Kwa sababu hata katika Katiba pendekezwa tumeona asilimia 85 ya maoni ya wananchi yamenyofolewa.
“Pili kuundwe Bunge la Katiba lenye wajumbe wasiokuwa wabunge kwani hawa waliopo bungeni watatengeneza Katiba ya kuwalinda na tatu kuundwe tume ya wataalamu wa Katiba kama walivyofanya wenzetu Kenya, kwani mahali tulipofika lazima tutoke kwenye ujumla ujumla tuwe na mashinikizo ya kuitaka Serikali ifanye nini kabla ya uchaguzi mkuu ujao,” alisema.
Pamoja na mambo mengine alieleza kushangazwa na baadhi ya mawaziri wanaodai kuwa rasimu ya pili ya Katiba Mpya iliwalisha wananchi maoni jambo ambalo si kweli.
“Baadhi ya mawaziri wanasema mambo ya kipumbavu eti watu wamelishwa maneno na tume, kusema kweli hiyo ni dharau kwa watu kuwa hawawezi kusema Rais apunguziwe madaraka na mambo mengine,” alisema.
Chama cha ACT- Wazalendo
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Chama cha ACT – Wazalendo, Yeremia Maganja, alisema hitaji la Katiba ni tangu vizazi na vizazi hivyo Serikali haitakiwi kupuuza takwa la wananchi.
“Pia tunaona tatizo linaloikabili nchi yetu ni taasisi ya rais kutokuwa na mamlaka inayoisimamia, ndiyo maana rais anaonekana kuwa amegeuka Mungu mtu,” alisema.
Aidha, Rais mstaafu wa Chama cha Mawakili Tanganyika (TLS), John Seka, alisema ili kuwepo na chaguzi za kidemokrasia lazima kuwepo na mfumo wa kisheria unaozingatia kutibu vidonda vya chaguzi zilizopita.
“Pia kuwe na miundombinu za kuwezesha vyama vyote ikiwamo kupatiwa gharama za uchaguzi pamoja na mambo mengine,” alisema.

Mwanafunzi auwawa kikatili Afrika Kusini



Mwanafunzi wa Tanzania aliyekuwa akisoma nchini Afrika Kusini ameuwawa kikatili Ijumaa nchini humo.
Gazeti la Habari Leo limeripoti kuwa msemaji wa Wizara ya Mambo na Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mindi Kasiga amesema wizara inafanya mawasilianao na ubalozi wa Tanzania nchini Afrika Kusini ili kubaini undani wa suala hilo.
Alisema wizara inafuatilia kujua chuo alichokuwa akisoma, siku ya tukio hilo na masuala yote muhimu kuhusiana na kifo hicho.
Gazeti hilo limeripoti kuwa jana kulikuwa na taarifa iliyokuwa ikizunguka kwenye mitandao ya kijamii ikielezea kuwa kuna Mtanzania ameuawa kikatili nchini Afrika Kusini.
Taarifa hizo zilidai kuwa mwanafunzi aliyejulikana kwa jina la Baraka Nafari aliyekuwa akichukua Shahada ya Uzamivu (PHD) katika Chuo Kikuu cha Johannesburg (UJ) aliuawa mapema Ijumaa Februari 23, mwaka huu kwa kugongwa na gari mara mbili na kubamizwa kwenye ukuta na baadaye kushambuliwa kwa visu.
Kwa mujibu wa habari hizo za mtandao kamera za usalama za CCTV za chuo hicho zilionesha Baraka na mwanafunzi mwenzake wakikimbia kujiokoa wakati wanaume wawili kwenye teksi wakiwaandama.
Pia kamera hiyo iliendelea kumuonesha dereva wa teksi akimgonga kwa makusudi mwanafunzi huyo kwenye uzio wa makazi ya chuo hicho yaliyoko Auckland Park na kumuua.
Taarifa hizo zimeongeza kuwa dereva wa gari hilo alikamatwa na polisi kwa kuendesha bila leseni, lakini baadaye aliachiwa huru bila kufunguliwa mashtaka yoyote.

Nani wa kulaumiwa iwapo siasa zitachomoza sherehe za Oscar 2018?



Iwapo yoyote katika washindi wa tuzo ya Oscar mwaka 2018 kesho Jumapili huko Hollywood, California atatumia hotuba yake ya kupokea tuzo hiyo kuendeleza ajenda ya kisiasa, mtu pekee wa kumshukuru - au kumlaumu – Marlon Brando.
Muigizaji huyo akimwakilisha Vito Corleone mwaka 1972 katika filamu The Godfather bado ni mashuhuri sana na mwenye kukonga nyoyo za wengi katika tasnia ya filamu.
Lakini kitendo chake cha kuingiza siasa mwaka 1973 wakati wa kupokea tuzo ya Academy Awards kilibadilisha mwenendo mzima wa Oscar.
Utamaduni uliokuwepo wakati huo ni washindi wa Oscar walipokea tuzo zao na kutoa hotuba wakiishukuru taasisi hiyo na sekta ya filamu.
Lakini Brando alileta mabadiliko. Yeye hata hakuhudhuria tafrija hiyo ya Oscar. Alimtuma mwigizaji Sacheen Littlefeather kumwakilisha. Alizungumza kupinga namna Hollywood ilivyokuwa inawafanyia watu ambao ni Wazawa wa Marekani (Native Americans).
.Kufuatia mwaka huo, washindi wa Oscar wameleta kila aina ya masuala ukianzia mabadiliko ya tabia nchi hadi vita na mpaka haki ya malipo sawa kwa wanawake.
Hotuba zao kwa muda mrefu zilikuwa zina ukimya wa namna fulani kwa sababu ya kudhibitiwa na mifumo ya studio,” amesema James Piazza.
Yeye aliandika kitabu mwaka 2002, kinachoitwa The Academy Awards: The Complete History of Oscar kwa kushirikiana na Gail Kinn. Kitabu hicho kina elezea histori kamili ya Oscar.
Mwandishi huyo alisema, “kumekuwa na malumbano kidogo, kwa mfano pale George C. Scott alipokataa kupokea tuzo kwa niaba ya Patton (ambayo ilitolewa mwaka 1970). Lakini hotuba ya Brando ilikuwa ya kipekee kwa hakika.
Wazalishaji wa filamu wa tuzo za onyesho la Oscar mwaka 2018 wanataka hafla hiyo kujikita katika filamu zenyewe. Hata hivyo kunauwezekano mkubwa kuwepo hotuba zenye hamasa za kisiasa.
Kwa mfano #MeToo movement, ambayo ni hashtag inayopinga unyanyasaji wa ngono, ulichangia kwa kiasi kikubwa katika tuzo za Golden awards mwezi Januari 2018.
Tuzo ya heshima ya Honorary Globe Oprah Winfrey pia alizungumza juu ya suala la kisiasa katika hotuba yake ambalo lilipelekea baadhi ya watu kumtaka agombanie urais wa Marekani.
Kabla ya Brando kuingiza siasa katika hotuba yake, washindi wengi wa tuzo hiyo walijiepusha na hotuba zenye siasa, hata kama masuala hayo yalifungamana na filamu yenyewe.

Watoto wanne waliofariki kwa kuungua ndani ya nyumba, wazikwa

Sengerema. Mamia ya wakazi wa mji wa Sengerema jana wamejitokeza kwa wingi kushiriki mazishi ya watoto wanne wa familia moja waliofariki dunia kwa kuungua kwa moto.
Akizungumza wakati wa mazishi hayo leo Machi, 3 Diwani wa Kata ya Nyatukala, Salehe Msaba amesema tukio hilo limeleta simanzi na majonzi kwa familia na jamii nzima hivyo ni vema jamii kushikama pamoja na kuisaidia familia hiyo.
“Tunapaswa kumshukuru Mungu kwa mapenzi yake kwani kila jambo hupangwa na yeye, lakini pia tunapaswa kuwa wamoja na kuondoa makundi yanayoweza kutugawa,” amesema Msaba.
Amesema kutokana na tatizo hilo, mbunge wa jimbo la Sengerema, William Ngeleja ametuma rambirambi ya Sh100, 000 kwa familia iliyopatwa na msiba huo.
Mkazi wa Kata ya Nyatukala, Juma Kalunde amesema wazazi wote tunapaswa kuwa makini katika kutumia nishati yoyote na wakati wa kulala tunapaswa kuzima kila kitu kisha kupumzika.
Amesema vifo vya watoto hawa vimetokea kwa uzembe uliofanywa na dada yao aliyewafungia mlango kwa nje kuondoka na baada ya hapo mshumaa ulishika kwenye neti na kusababisha moto huo.
Mwenyekiti wa CCM Wilaya ya Sengerema, Marco Makoye amezitaka jamii kuwa makini wakati wakitumia nishati  yoyote ya umeme au kuni .
Tukio hilo lilitokea Februari 28, Saa 5:00 usiku, watoto wanne Lydia Elias (10), Modesta Elias (9), Steven Deogratias (9) na Kizengele Elias (8) waliungulia ndani na wamezikwa katika makaburi ya Twitange wilayani Sengerema.

UNAIDS yaeleza namna ya kupambana na VVU

Mkurugenzi mkazi wa Shirika la Umoja wa Mataifa
Mkurugenzi mkazi wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Ukimwi (UNAIDS), Leopold Zekeng.  
Dar es Salaam. Tanzania inaweza kukomesha maambukizi ya Virusi vya Ukimwi (VVU) kama tishio la afya ya jamii ifikapo mwaka 2030 ikiwa kutakuwa na ushiriki wa viongozi wa juu wa siasa, wanaharakati na wataalamu kutoka mitandao ya wanaoishi na virusi hivyo.
Ili kufikia huko, lazima kuwe na mikakati mizuri ya kuzuia maambukizi na kupambana na unyanyasaji kwa watu ambao wameathirika na ugonjwa huo.
Hayo yameelezwa jana Machi 2, 2018 na Mkurugenzi mkazi wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Ukimwi (UNAIDS), Leopold Zekeng.
“Tunatakiwa kuhakikisha kwamba kila mmoja anapata haki ya matibabu ya afya ya mwili na akili,” amesema.
Zekeng ameyasema hayo katika taarifa kwa vyombo vya habari kuhusu siku ya kupinga unyanyasaji kwa waathirika wa VVU  ambayo inafanyika Machi Mosi kila mwaka ulimwenguni kote.
Mkurugenzi Mtendaji wa UNAIDS, Michel Sidibe amesema: “Hatuwezi kuifikia dira yetu ya afya au kufikia Malengo Endelevu ya Maendeleo kama hatutapambana na unyanyasaji kwa waathirika.”
Ripoti ya Tume ya Afrika ya Haki za Binadamu inatoa mwongozo juu ya namna ya kukabiliana na vitendo vya ukiukwaji wa haki za binadamu hasa unyanyasaji.
Baadhi ya mambo hayo ni unyanyapaa dhidi ya waathirika kwa  kutopata matibabu na kupimwa kwa lazima.
Siku ya kupinga unyanyasaji duniani inaongozwa na dira ya UNAIDS ya kupinga aina zote za unyanyasaji wa hali ya maambukizi ya virusi vya Ukimwi, jinsia, umri, dini, kabila, ukanda, hali ya uhamiaji au sababu yoyote ile.

Wabunge wanawake wawakumbuka yatima


Babati. Katika kusherehekea wiki ya siku ya wanawake duniani, wabunge wa viti maalum CCM mkoani Manyara, Martha Umbullah na Ester Mahawe, wametoa msaada wa sare za shule na vifaa vya kuandikia kwa watoto yatima 43 wa shule ya msingi Bonga ya Mjini Babati.
Akizungumza wakati wa makabidhiano hayo, Mahawe alisema kwamba wametumia Sh Sh1.6 milioni kwa ajili ya vitu walivyowanunulia watoto hao.
Alifafanua kuwa wamewanunulia watoto hao sare za shule ambazo ni  kaptula, mashati, sketi, blauzi, masweta, viatu pamoja na maboksi mawili ya kalamu, madaftari na majaladio.
Mahawe alisema wametoa msaada kwa yatima hao kwani jambo lililo bora hapa duniani ni kusaidia wahitaji ndiyo sababu na wao wakashirikiana kufanya hivyo. 
"Ibada nzuri ni kusaidia wahitaji hata sisi wakristo na waislamu tunaambiwa kuwa tuwe tunawasaidia wenzetu na ndivyo tulivyofanya," alisema Mahawe. 
Mwalimu mkuu wa shule hiyo Januari Barnabas alisema kati ya wanafunzi hao yatima 43, wavulana ni 19 na wasichana 24.
Barnabas alisema wanakabiliwa na changamoto nyingi ikiwamo wanafunzi kutokula chakula cha mchana kwani nusu ya wanafunzi wa shule hiyo wanakaa umbali wa zaidi ya kilometa mbili. 
Alisema pia wanakabiliwa na changamoto ya madarasa kwani yapo 15 na nyumba za walimu ni chache, wapo walimu 22 na nyumba zilizopo ni tano ambazo zimechakaa. 
Hata hivyo, Martha Umbullah alisema changamoto ya wanafunzi kutokula shuleni inatakiwa ipatiwe ufumbuzi kwa kuwekewa mikakati kwani si jambo zuri wanafunzi kurudi nyumbani mchana kwa ajili ya kula. 
Umbullah alisema viongozi wa eneo hilo akiwemo diwani na kamati ya shule wanapaswa kukaa pamoja na wazazi ili kufanikisha wanafunzi wapate chakula cha mchana shuleni. 
"Japo sisi si wabunge wa jimbo hili, lakini ni wabunge wa viti maalum wa mkoa tunafanya kazi kwenye wilaya zote tano na halmashauri saba zilizopo," alisema Umbullah. 
Pia, msafara wa wabunge hao uliongozana na viongozi wa UWT wa mkoa huo, ulitoa msaada wa vyakula kwa wanafunzi wa shule hiyo. 
Msaada huo ni magunia 12 ya mahindi, madebe 13 na nusu ya maharage, lita 60 za mafuta ya kupikia na mwanafunzi mmoja wa darasa la pili kushonewa sare hadi atakapohitimu darasa la saba. 

Mkurugenzi NEC ajibu hoja za LHRC

Mkurugenzi wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC),
Mkurugenzi wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC), Kailima Ramadhani  
Dar es Salaam. Baada ya Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC) kutaja hadharani dosari kumi zilizojitokeza katika uchaguzi mdogo uliofanyika kwenye majimbo ya Kinondoni na Siha, Mkurugenzi wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC), Kailima Ramadhani amedai kuwa kituo hicho kimefanya makosa.
Alisema kituo hicho kimetangaza dosari hizo za uchaguzi uliofanyika Februari 17, bila kufuata sheria na kanuni za uchaguzi.
Uchaguzi huo ulifanyika baada ya waliokuwa wabunge wa majimbo hayo, Maulid Mtulia (CUF-Kinondoni) na Dk Godwin Mollel (Chadema-Siha) kujitoa kwenye vyama vyao na kuhamia CCM.
Wabunge hao wawili waliopitishwa tena kwenye uchaguzi huo kupitia CCM walishinda nafasi hizo.
Kutokana na uchaguzi huo, LHRC ilitoa dosari zilizofanana na zile zilizotolewa na vyama vya upinzani hasa Chadema.
Akizungumza wakati wa mahojiano na kituo cha Magic FM, Kailima alisema LHRC imefanya kosa la kisheria na kanuni kwa kutoa taarifa hiyo.
Alisema kifungu namba 4 cha Sheria ya Taifa ya Uchaguzi kimeielekeza tume hiyo kutunga kanuni wakati kifungu namba 64(4) cha Sheria ya Taifa ya Uchaguzi kinasema Tume itatoa muongozo kwa watazamaji wa uchaguzi.
Alieleza kwamba hata katika uchaguzi wa mwaka 2015, tume hiyo ilitoa muongozo kwa watazamaji wa uchaguzi.
“Kipengele cha 12(d) kinasema mtazamaji hatatakiwa kutoa taarifa kwa umma juu ya mchakato wa uchaguzi hadi taarifa ya awali itakapokuwa imekabidhiwa na tume kukiri kupokewa kwa taarifa hiyo,” alisema Kailima.
Alifafanua kuwa kituo hicho kiliandika barua kwa tume na kuiwasilisha Februari 26 ambayo iliifikia tume Februari 28 jioni wakati ofisini kukiwa hakuna viongozi.
“Kutozingatia sheria ni kama wembe, utakukata tu,” alisema.
Mkurugenzi huyo alisema tume hiyo inatafakari iwapo itawapa kibali kingine cha utazamaji wa uchaguzi.
Kuhusu hoja zilizo kwenye taarifa hiyo ikiwamo ya matumizi ya watoto kwenye kampeni za chama kimojawapo, Kailima alisema wao si Wizara ya Afya, Jinsia, Wazee na Watoto na kwamba hoja hizo ilipaswa zipelekwe huko.

Vigogo Maliasili watoa kauli kinzani kifo cha faru

Katibu Mkuu wa Wizara ya Maliasili na Utalii,
Katibu Mkuu wa Wizara ya Maliasili na Utalii, Meja Jenerali Gaudence Milanzi. 
Dar es Salaam. Licha ya mauaji ya faru mmoja katika Hifadhi ya Taifa Serengeti kutokea Desemba mwaka jana, hadi sasa hakuna taarifa kamili iliyotolewa huku watendaji waandamizi wa Wizara ya Maliasili na Utalii wakitoa kauli zinazokinzana.
Wakati katibu mkuu, Meja Jenerali Gaudence Milanzi akisema kunafanyika uchunguzi wa kawaida, Naibu Waziri Japhet Hasunga amekaririwa akisema unafanyika uchunguzi wa kina ukihusisha kuundwa kwa kamati maalumu.
Licha ya kusema kuna uchunguzi wa kawaida, Meja Jenerali Milanzi amekanusha pia madai ya kuhojiwa viongozi wa Shirika la Hifadhi za Taifa (Tanapa).
Chanzo cha taarifa kimelieleza Mwananchi kuwa baada ya wizara kupata taarifa iliundwa kamati ya kuchunguza tukio hilo ambayo pia iliwahoji maofisa wa Tanapa na kwamba kazi hiyo imekamilika.
Alipopigiwa simu na kuulizwa kuhusu suala hilo juzi, mkurugenzi mkuu wa Tanapa, Allan Kijazi alimtaka mwandishi ampigie baada ya saa moja kwa maelezo hakuwa sehemu nzuri.
Baada ya muda huo kupita, meneja mawasiliano wa Tanapa, Pascal Shelutete alimpigia simu mwandishi akisema ametumwa na bosi wake kumsikiliza.
Alipoulizwa taarifa za mauaji ya faru huyo katika Hifadhi ya Serengeti na kwamba kuna maofisa wa Tanapa wamehojiwa na wizara, Shelutete alikiri kutokea kwa mauaji lakini alikanusha maofisa kuhojiwa.
“Taarifa hizo ni za kweli na ziko mikononi mwa vyombo vya dola zinashughulikiwa. Si kweli kwamba tulichelewesha taarifa, tulitoa mapema tu,” alisema Shelutete alipoulizwa ni kwa nini taarifa za kuuawa kwa faru huyo hazikutolewa mapema.
Shelutete alimwahidi mwandishi kuwa atampigia tena baadaye. Baada ya saa tano kupita bila simu kupigiwa, mwandishi alimpigia tena lakini hakupokea bali alituma ujumbe wa maandishi akiandika, ‘Nakupigia’.
Meneja huyo hakupiga simu badala yake alitoa taarifa kwa vyombo vya habari juzi kuhusu tukio hilo ikisema Tanapa inawashikilia watuhumiwa wanne wanaodaiwa kuwa miongoni mwa mtandao wa ujangili na mauaji ya faru katika Hifadhi ya Taifa ya Serengeti, Desemba mwaka jana.
“Pamoja nao, shirika pia limefanikiwa kukamata bunduki aina ya rifle inayoaminika kutumika katika tukio hilo. Shirika linaendelea kushirikiana kwa karibu na vyombo vingine vya dola kukamilisha uchunguzi utakaopelekea kuchukuliwa hatua za kisheria kwa wahusika,” imesema taarifa ya Tanapa.
Jana alipopigiwa simu, Shelutete alisema lengo la kutotoa taarifa hiyo mapema ilikuwa ni kulinda uchunguzi unaoendelea.
“Hata hiyo taarifa unaiona tumeitoa kwa ufupi kwa sababu the more you reveal to the public, (kadri unavyotoa taarifa kwa umma) the more unapoteza chance (nafasi) za kuwakamata hao majangili, kwa sababu ni mtandao mkubwa. Naomba muwe wavumilivu, uchunguzi ukikamilika tutawapa taarifa,” alisema Shelutete.
Ufafanuzi wa wizara
Akizungumza kwa simu, Meja Jenerali Milanzi alikiri kutokea kwa mauaji akisema ni ya kawaida na kwamba kuna uchunguzi wa kawaida unaendelea kuhusu hilo.
“Ni kweli. Mara nyingi huwa ni ‘routine investigation’ inafanyika lakini si kuwahoji viongozi wa Tanapa. Ikitokea ‘incident’ (tukio) yoyote kama mnyama amekufa au ameuawa kunakuwa na ‘routine investigation’. Huwa ni kwenda field pale wanapotupa taarifa. It’s a normal investigation (ni uchunguzi wa kawaida).
Meja Jenerali Milanzi alisema Tanapa waliwapa taarifa mapema na walishaanza kufuatilia.
Alisema licha ya mauaji ya mnyama huyo, bado faru wapo wengi ijapokuwa hakutaja idadi.
“Faru bado wapo hawawezi kwisha. Hata tembo wanapokufa huwa tunachunguza ametoka familia gani. Mnyama akifa ni kawaida mzoga wake kuliwa, lakini hawa wakubwa tunawalinda hata wasiliwe na ‘predators’ (wanyama wanaokula nyama)”.
Alipoulizwa sababu ya Tanapa kuchelewesha taarifa kwa vyombo vya habari alisema, “Kwani ulitaka tufanyeje? Huo ukimya mimi sifahamu kwa nini, labda nitazungumza na Tanapa, lakini naona wametoa taarifa yao jana (juzi).”
Lakini Naibu Waziri Hasunga alisema baada ya kupata taarifa kutoka Tanapa waliunda kamati kwa ajili ya kufanya uchunguzi wa kina.
“Tuliunda kamati kupata taarifa za kina baada ya kupata taarifa ya Tanapa. Hawakuchelewesha taarifa, ila tuliona kuna haja ya kujiridhisha zaidi,” alisema Hasunga.

Mbinu za kuwaepuka madalali wa mazao


Wiki iliyopita jarida hili lilichapisha makala kuhusu kilio cha wakulima, wakiwalalamikia madalali wa mazao kuwa ni kikwazo cha maendeleo yao.
Katika makala haya, wakulima wanaeleza jinsi ambavyo baadhi ya nyakati, wanavyoweza kuwaepuka madalali hao ambao uwepo wao katika masoko unaonekana kuwa kama mfumo rasmi wa uendeshaji wa masoko nchini.
Mkulima wa matunda kutoka wilayani Bagamoyo, Lucy Salema anasema : “Hawa mbona kuwaepuka ni kazi rahisi tu ilimradi tu kuwepo na utaratibu maalum kwenye haya masoko makubwa mfano Kariakoo ili madalali wasiwepo kabisa.”
Anasema kuwa kinachotakiwa kwa mkulima ni kutoa taarifa mapema kwa kiongozi wa soko kabla hajapeleka mazao sokoni, ili kiongozi huyo ajue kwamba ni wakulima wangapi wataingiza mazao sokoni na taarifa hiyo itolewe mwezi mmoja kabla.
Utaratibu huo utampa nafasi kiongozi wa soko kujua ni wakulima wangapi wataleta mazao ya aina moja na wangapi wataleta aina nyingine. Ni utaratibu ambao utasaidia kuondoa msongamano wa wingi wa watu wanaopeleka mazao.
“Wakulima tukienda sokoni wengi, madalali wanapata nafasi nzuri ya kutuumiza, kwa sababu wanajua mkulima hawezi kumkataa maana matunda ukikaa nayo sana yanaharibika, lakini kiongozi wa soko akisimama imara hatuwezi kunyanyaswa na watu hawa,” anasema.
Kwa mkulima, Salim Magege anayeishi mkoani Mwanza, anasema kinachotakiwa kufanywa ni ushirikiano kati ya mkulima, kiongozi wa soko na mnunuzi bila hivyo hawawezi kumaliza tatizo hilo la madalali sokoni wanaokandamiza haki za wakulima.
“Uwezekano wa kutotumia madalali sokoni upo tena mkubwa tu, yaani ni bora kama kuna ushuru mkulima nilipe moja kwa moja kwa uongozi wa soko na uongozi wa soko unikutanishe moja kwa moja na mnunuzi,” anasema.
Anasema kinachofanyika sasa ni kwamba madalali wanachukua fedha, uongozi wa soko nao wanachukua fedha kwa hiyo kuna mlolongo mkubwa ambao mkulima anapitia.
“Ukiangalia kiashiria kikubwa kuwa madalali wanatudhulumu ni kushusha bei. Kwa mfano, mkulima anaenda soko kuu la Kariakoo kwa lengo la kuuza vitunguu Sh 150,000 kwa gunia, lakini ukikutana na dalali unaambiwa uuze kwa 130,000,”anaeleza.
Anasema kuwa madalali wakipanga bei, hawataki mabishano kwani ukifanya hivyo huwezi kupata mteja na bidhaa yako itaoza.
Viongozi wa masoko wawazungumzia madalali
Saidi Mzuzure ni mjumbe wa kamati ya soko la Sterio wilayani Temeke anasema: “Sio kweli kuwa tunawabeba madalali kwa sababu kiongozi wa soko ni kiongozi wa mteja na mkulima kwani bila wao hakuna soko.’’
Akielezea taratibu za soko lao, anasema madalali nao ni wakusanya kodi, kwa kuwa mkulima anapouza bila ya kumtumia dalali Serikali ya wilaya inakosa mapato.
“Tukisema pia hawa wakulima wauze bila kupitia kwa dalali hatuwezi kukusanya ushuru, kwa sababu mkulima anapokuja hapa na kuuza mazao yake bila dalali akipata tu mtu akamuuzia utakuta mkulima yule anaondoka na yule mnunuzi anaondoka na mwishowe Manispaa haipati mapato,”anasema.
Isihaka Ofiole ambaye ni Kaimu Katibu wa soko la Buguruni, anasema wanatambua uwepo wa madalali katika soko hilo ila kuhusu wakulima kudhulumiwa hawalitambui hilo kwani makubaliano hufanywa kati ya wakulima wenyewe na madalali.
“Hilo la kudhulumiwa sijapata malalamiko, lakini kwa kucheleweshewa malipo inatokea mara kwa mara na hii ni kutokana na wakulima na madalali kutotoa taarifa kwa uongozi wa soko pindi wanapokabidhiana mazao yao,” anasema.
Ofiole hata hivyo, anasema madalali wanatokana na wakulima wenyewe kwa kuwa ndio wanaowapa mzigo. Anasema kilichozoeleka ni ule utamaduni waliojiwekea wakulima wa kuuza kupitia kwa dalali hasa kwa wale wanaoleata mzigo mkubwa.
“Lakini pia wakati mwingine mkulima ni mgeni, labda ametokea mkoani kwa hiyo huyu huwezi tu ukamwachia auze vinginevyo watu watamzunguka huko nje na hatimaye matapeli watamuibia, ndiyo maana tunamkabidhi kwa dalali,” anasema.
Anasema dalali anapokabidhiwa mzigo na mkulima na kuuhifadhi anabeba jukumu la kuulinda, kuuhifadhi na hata kulipia ushuru. Ni jukumu lake kwa kuwa yeye ndiye muuzaji.
Ofiole anawashauri wakulima kuwaona viongozi wa masoko kabla ya kuwapa mzigo madalali. Anasema kosa wanalolifanya wakulima ni kukabidhi mzigo kwa dalali bila kuwa na hati ya maandishi, hivyo uongozi unashindwa kuingilia kati kwa sababu hakuna uthibitisho unao onyesha kuwa wawili hao walikabidhiana mzigo.
Wenyewe wajitetea
Dalali wa mbogamboga katika soko la Temeke Sterio, Amosi Kimbute, anasema wanachakifanya wao ni utekelezaji wa majukumu yao, kwani hata kama wasingekwepo bado wakulima wangelalamika.
‘’Ukweli ni kwamba bila sisi hawawezi kuuza mazao yao. Nasema hivyo kwa sababu madalali tuna mtandao mkubwa na tunajua wapi kuna wanunuzi na yupi mnunuuzi wa kweli,”anasema.
Kuhusu bei anasema ni suala la makubaliano kati yao na wakulima na hata wanapopanga wao madalali, lazima wawaulize wenyewe wakulima kama wameridhia au hawajaridhia.
“Sawa tunapanga bei lakini huwa hatulazimishi mtu kukubaliana na bei ile kama akikataa basi na mara nyingi wakikataa tukiwaacha wanaanza kulalamika na ku tubembeleza,”anaongeza.
Anasema kwa mkulima anayelalamika kutapeliwa basi amekutana na dalali ambaye hatambuliki katika soko, kwa sababu madalali wanajuana na wanahakikisha hakuna mkulima anayedhulumiwa.
‘’Unakuta mkulima analeta tikiti zaidi ya 2000 na unapomtafutia mteja dalali anachukua Sh200 pekee sasa hapo namdhulumu vipi?anahoji.
Naye Omari Othman ambaye ni dalali wa matunda katika soko la Buguruni, anasema madalali hawapangi bei ila wanapanga pamoja kati yao na mkulima.
“Kwa wale wanaokwenda shamba sawa lakini sisi wa sokoni inategemea ila mara nyingi bei tunapanga pamoja na mkulima na tunauza pamoja hadi pale matunda yatakapokwisha,”anasema Othman na kuongeza:
“Changamoto iliyopo ni kwamba wanunuzi wanachelewa kulipa fedha, lakini pia hata matunda yanayokuja mengine hayana viwango hivyo unakuta tunayagawanya katika madaraja. Sasa lawama zinakuja unapomweleza kuwa matunda yako yapo daraja la mwisho, hivyo unatakiwa kuuza kwa bei hii. Sisi huwa tunayagawa katika madaraja matatu yaani la kwanza la pili na la tatu”

Maofisa utamaduni mnafanya kazi yenu au anawafanyia waziri?



Anko Kitime
Anko Kitime 
Wiki imemalizika kwa amri ya kuzuia nyimbo kadhaa za ‘Bongo Fleva’ kurushwa kwenye vyombo vya utangazaji nchini. Kwa wengi hili halikuwa jambo la kushangaza, kuna wengine walikuwa wanashangaa kwanini baadhi ya nyimbo zinaendelea kusikika hewani. Na hakika kuna wengi wametetea kuwa nyimbo hizo hazina tatizo ziendelee tu kurushwa watu wafurahi.
Tatizo liko wapi? Binafsi naona kuwa hatua ya kufungia nyimbo hizi haitamaliza tatizo kwani hatua iliyofanyika ni kubandika tu bandeji kwenye kidonda kilichooza. Pengine tujiulize kwanini nyimbo ambazo zinasemekana ‘hazina maadili’ ziliweza kutungwa na kurekodiwa? Kwanini ziliweza kurushwa kwenye vyombo vya utangazaji bila kuonekana shida yoyote mpaka Baraza la Sanaa la Taifa (Basata) na TCRA waingilie kati? Kwanini vijana wengi hawaoni tatizo la nyimbo hizo?
Kuna usemi maarufu usemao ‘Sanaa ni kioo cha jamii’. Ukiangalia kwenye kioo na kukuta sura mbaya inakuangalia basi ujue hivyo ndivyo ulivyo, kuvunja kioo au kubadili kioo hakutabadili sura yako.
Unaweza ukaikubali sura hiyo au ukaanza mkakati wa kutumia vipodozi kujipa mvuto unaoutaka. Kazi za wasanii zinaonyesha tu jamii ilivyo.
Mtoto aliyelelewa na wazazi wenye mdomo mchafu haiwi taabu kwake kuwa na mdomo mchafu, tena anashangaa sana akianza kukatazwa kutoa maneno machafu, anaona anaonewa kwa kuzibwa mdomo bila sababu za msingi. Hivyo kutunga wimbo uliojaa matusi au dalili za matusi kwake si tatizo, ndivyo jamii yake ilivyomlea.
Na wimbo huo utapokelewa vizuri tu na jamii yake kwani hayo ndio maisha yao ya kila siku. Niliwahi kuongea na mzazi wa mwanamuziki mmoja ambaye wimbo wake umeingia katika orodha ya kupigwa marufuku, mama yule alikuwa anajisifu kuwa yeye ndiye aliyeutunga wimbo anaoimba mwanae.
Turudi nyuma miaka 23 iliyopita. Uongozi wa awamu ya tatu ulipoingia madarakani, Wizara ya Utamaduni ilipata pigo ambalo matokeo yake yanaonekana sasa. Katika awamu hii maofisa utamaduni, mkoa na wilaya walifutika. Na baadaye kufufuka kinyemela wakiwa chini ya Idara ya Elimu katika halmashauri mbalimbali.
Hata huko walifufuliwa baada ya kuonekana kunahitajika mtu atakayekuwa akishughulikia kuratibu shughuli kama za Mwenge na sherehe mbalimbali.
Ofisa Elimu alimteua mwalimu aliyemuona anapenda sanaa na kumpa cheo cha uofisa utamaduni.
Maafisa hawa hadi leo bado ni utata, hawana bajeti, hawahusishwi kwenye vikao mbalimbali vya halmashauri, kila wilaya au halmashauri ikiwa na utaratibu wake. Mfano hapa Dar es Salaam kuna halmashauri za Ubungo, Kinondoni, Ilala na Temeke, ni halmashauri ya Kinondoni tu yenye sheria ndogo zinazohusu mambo ya sanaa na burudani, na sheria hizo zinahusiana zaidi na utoaji vibali tu kwa shughuli mbalimbali. Ukiona mkanganyiko huu kwa maofisa utamaduni wa jiji hili tu, je hali ikoje katika halmashauri za nchi nzima?
Waziri anayehusika na Utamaduni hawaongelei maofisa utamaduni hawa kwani hawako katika wizara yake na Waziri wa Tamisemi hawaongelei kwani hawana umuhimu huo kwake. Lakini hawa watu ndio kiungo muhimu sana katika kulinda na kuelekeza ‘maadili’ ya Kitanzania.
Awali walikuwa chini ya Wizara ya Utamaduni walikuwa ndio watekelezaji wa Sera ya Utamaduni, kwa sasa hawawajibiki kwa hilo, hivyo sera ya Utamaduni ni kitabu kiko katika makabati ya Wizara ya Utamaduni tu. Katika miaka hiyo ya nyuma nchi ilikuwa japo na maono kuwa inataka kwenda wapi kimaadili, na ikawa na utekelezaji wa pamoja wa maono hayo.
Kupotea kwa maofisa hawa kulikuja wakati mmoja na kuongezeka kwa vyombo vya utangazaji, luninga na redio.
Vyombo hivyo ndivyo vikaanza kubeba pengine bila kujua au kwa makusudi nafasi ya kulea maadili ya watoto wa Kitanzania. Malezi ya miaka mingi sasa yanatoa matunda, vijana waliokuwa na umri wa miaka 10 au chini zaidi mwaka 1995 na waliozaliwa baada ya hapo, ndio hao watunzi wa nyimbo ambazo zinaonekana hazina maadili, ni vigumu kwao kueleza au kujua maadili ya Kitanzania ni yepi.
Wanamuziki, watangazaji, waandishi, maproducer, mameneja wa wanamuziki na kadhalika wengi ndio waliozaliwa katika kipindi hiki.
Teknolojia imewezesha kazi ya muziki kuwa rahisi sana, ukiwa na kompyuta na microphone moja unaweza kujifungia chumbani kwako ukarekodi wimbo na kuutuma kwa barua pepe mpaka kwa mtangazaji na wimbo ukaanza kurushwa hewani katika kipindi cha masaa kadhaa.
Hivyo kama hakuna aliyelelewa kuona ukakasi katika wimbo basi umma bila kujali umri au uhusiano unajikuta ukisikiliza maneno ambayo kwa kawaida huwa faragha na kwa watu wazima wenye aina fulani ya mahusiano tu, maneno hayo yanatamkwa hadharani bila kumumunya.
Kuna haja kubwa ya Wizara inayohusika na Utamaduni kujiangalia upya na kujipanga upya ili kukabiliana na hali hii na si kuishia kufanya kazi rahisi ya kufungia nyimbo tu.