Saturday, March 3

UNAIDS yaeleza namna ya kupambana na VVU

Mkurugenzi mkazi wa Shirika la Umoja wa Mataifa
Mkurugenzi mkazi wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Ukimwi (UNAIDS), Leopold Zekeng.  
Dar es Salaam. Tanzania inaweza kukomesha maambukizi ya Virusi vya Ukimwi (VVU) kama tishio la afya ya jamii ifikapo mwaka 2030 ikiwa kutakuwa na ushiriki wa viongozi wa juu wa siasa, wanaharakati na wataalamu kutoka mitandao ya wanaoishi na virusi hivyo.
Ili kufikia huko, lazima kuwe na mikakati mizuri ya kuzuia maambukizi na kupambana na unyanyasaji kwa watu ambao wameathirika na ugonjwa huo.
Hayo yameelezwa jana Machi 2, 2018 na Mkurugenzi mkazi wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Ukimwi (UNAIDS), Leopold Zekeng.
“Tunatakiwa kuhakikisha kwamba kila mmoja anapata haki ya matibabu ya afya ya mwili na akili,” amesema.
Zekeng ameyasema hayo katika taarifa kwa vyombo vya habari kuhusu siku ya kupinga unyanyasaji kwa waathirika wa VVU  ambayo inafanyika Machi Mosi kila mwaka ulimwenguni kote.
Mkurugenzi Mtendaji wa UNAIDS, Michel Sidibe amesema: “Hatuwezi kuifikia dira yetu ya afya au kufikia Malengo Endelevu ya Maendeleo kama hatutapambana na unyanyasaji kwa waathirika.”
Ripoti ya Tume ya Afrika ya Haki za Binadamu inatoa mwongozo juu ya namna ya kukabiliana na vitendo vya ukiukwaji wa haki za binadamu hasa unyanyasaji.
Baadhi ya mambo hayo ni unyanyapaa dhidi ya waathirika kwa  kutopata matibabu na kupimwa kwa lazima.
Siku ya kupinga unyanyasaji duniani inaongozwa na dira ya UNAIDS ya kupinga aina zote za unyanyasaji wa hali ya maambukizi ya virusi vya Ukimwi, jinsia, umri, dini, kabila, ukanda, hali ya uhamiaji au sababu yoyote ile.

No comments:

Post a Comment