Saturday, March 3

Wabunge wanawake wawakumbuka yatima


Babati. Katika kusherehekea wiki ya siku ya wanawake duniani, wabunge wa viti maalum CCM mkoani Manyara, Martha Umbullah na Ester Mahawe, wametoa msaada wa sare za shule na vifaa vya kuandikia kwa watoto yatima 43 wa shule ya msingi Bonga ya Mjini Babati.
Akizungumza wakati wa makabidhiano hayo, Mahawe alisema kwamba wametumia Sh Sh1.6 milioni kwa ajili ya vitu walivyowanunulia watoto hao.
Alifafanua kuwa wamewanunulia watoto hao sare za shule ambazo ni  kaptula, mashati, sketi, blauzi, masweta, viatu pamoja na maboksi mawili ya kalamu, madaftari na majaladio.
Mahawe alisema wametoa msaada kwa yatima hao kwani jambo lililo bora hapa duniani ni kusaidia wahitaji ndiyo sababu na wao wakashirikiana kufanya hivyo. 
"Ibada nzuri ni kusaidia wahitaji hata sisi wakristo na waislamu tunaambiwa kuwa tuwe tunawasaidia wenzetu na ndivyo tulivyofanya," alisema Mahawe. 
Mwalimu mkuu wa shule hiyo Januari Barnabas alisema kati ya wanafunzi hao yatima 43, wavulana ni 19 na wasichana 24.
Barnabas alisema wanakabiliwa na changamoto nyingi ikiwamo wanafunzi kutokula chakula cha mchana kwani nusu ya wanafunzi wa shule hiyo wanakaa umbali wa zaidi ya kilometa mbili. 
Alisema pia wanakabiliwa na changamoto ya madarasa kwani yapo 15 na nyumba za walimu ni chache, wapo walimu 22 na nyumba zilizopo ni tano ambazo zimechakaa. 
Hata hivyo, Martha Umbullah alisema changamoto ya wanafunzi kutokula shuleni inatakiwa ipatiwe ufumbuzi kwa kuwekewa mikakati kwani si jambo zuri wanafunzi kurudi nyumbani mchana kwa ajili ya kula. 
Umbullah alisema viongozi wa eneo hilo akiwemo diwani na kamati ya shule wanapaswa kukaa pamoja na wazazi ili kufanikisha wanafunzi wapate chakula cha mchana shuleni. 
"Japo sisi si wabunge wa jimbo hili, lakini ni wabunge wa viti maalum wa mkoa tunafanya kazi kwenye wilaya zote tano na halmashauri saba zilizopo," alisema Umbullah. 
Pia, msafara wa wabunge hao uliongozana na viongozi wa UWT wa mkoa huo, ulitoa msaada wa vyakula kwa wanafunzi wa shule hiyo. 
Msaada huo ni magunia 12 ya mahindi, madebe 13 na nusu ya maharage, lita 60 za mafuta ya kupikia na mwanafunzi mmoja wa darasa la pili kushonewa sare hadi atakapohitimu darasa la saba. 

No comments:

Post a Comment