Friday, May 24

HAKUNA JAMII ITAKAYOACHWA NYUMA KIMAENDELEO: TANZANIA

Naibu Mwakilishi wa Kudumu wa Tanzania katika Umoja wa Mataifa,
Balozi Ramadhan Mwinyi, akizungumza wakati wa
Mkutano wa 12 wa Masuala ya Wazawa,
kuhusu mada ya utafiti uliofanywa kuhusu Ujasiri,
Maarifa ya Jadi na Kujenga uwezo Jamii ya Wafugaji katika Afrika.
Nyuma ya Balozi ni Bi. Ellen Maduhu Afisa wa Ubalozi .


Tanzania imesisitiza kwamba inajukumu kubwa la kuhakikisha kuwa mipango yake ya maendeleo endelevu inamfikia kila mwananchi na kwamba hakuna jamii itakayo achwa nyuma.

Na kwa sababu hiyo, Tanzania imeitaka Jumuiya ya Kimataifa na wadau wengine kushirikiana na Serikali katika kufanikisha azma yake hiyo, lakini pia kutambua kuwa maamuzi mbalimbali inayoyachukua yanafanyika kwa nia njema.

Hayo yameelezwa na Balozi Ramadhan Mwinyi, Naibu Mwakilishi wa Kudumu wa Tanzania katika Umoja wa Mataifa, alipokuwa akichangia majadiliano ya mada ya utafiti kuhusu Ujasiri, Maarifa ya Jadi na Kujenga Uwezo wa Jamii ya Wafugaji katika Afrika.

Mada hiyo ni sehemu ya mada kadhaa zikiwa zao afya, elimu, haki za binadamu, ujasiliamali, vijana mila na tamadu ambazo zimekuwa zikijadiliwa kwa nyakati tofauti katika Mkutano wa Kudumu wa 12 Kuhusu Masuala ya Wazawa. ( Forum on Indigenous Issues) Mkutano huu ambao ulianza mapema wiki hii unafanyika chini ya usimamizi wa Baraza la Uchumi na Maendeleo ya Jamii la Umoja wa Mataifa ( ECOSOC).

Washiriki wa mkutano huu wapatao 2000 wanatoka katika Asasi zisizo za kiserikali wakiwamo wawakilishi kutoka baadhi ya taasisi za kifedha kama Banki ya Dunia, Banki ya Maendeleo ya Afrika na Banki ya Maendeleo ya Asia.

“Tunaendelea na jitihada za kuwaletea maendeleo wananchi wetu ili kuhakikisha kwamba hakuna jamii inayoachwa nyuma kama ambavyo imeainishwa katika Malengo ya Maendeleo ya Millenia ( MDGs) na kutafsriwa katika Mpango wa Maendeleo ya Taifa na mipango migineyo” akasisitiza Balozi Mwinyi.

Hata hivyo akasema licha ya jitihada hizo za serikali , bado kuna baadhi ya jamii chache ambazo zenyewe zimeamua kudumisha mila, tamaduni na maisha yao ya jadi .

Akasema jamii hizo ni zile ambazo hazifahamiki sana katika Jumuiya ya Kimataifa kama ilivyo kwa jamii ya wamasaai.

Akizungumzia masuala ya upatikanaji na ugawaji wa ardhi kwa wananchi zikiwamo jamii ambazo mfumo wa maisha yao unategemea zaidi ardhi na mali asili nyingine. Balozi Mwinyi amewaeleza washiriki wa mkutano huo wakiwamo washiriki kutoka Tanzania, kwamba serikali imejiwekea sheria na taratibu zinazosimamia ugawaji wa ardhi.

Akafafanua kwa kueleza kwamba kwa sheria na taratibu za Tanzania, Hati ya umiliki wa Ardhi katika ngazi ya kijiji hutolewa kwa wanajamii ambao wanaishi au wamekusanyika katika muundo wa kijiji ambao unatambuliwa rasmi.

“ Kwa mujibu wa sheria zetu, ni kijiji ndicho kinatambuliwa kisheria kama chombo huru kinachosimamia masuala ya ardhi ambapo cheti cha ardhi hutolewa kwaajili ya matumizi ya jamii nzima”. Akasema

Na kuongea “ Hata hivyo kuna baadhi ya maeneo hasa yale ya wawindaji ambapo kama idadi ya jamii ile haikukidhi matakwa ya kisheria ya kuwa na hadhi ya kijiji kutokana na uchache wao, bado kwa mfano, mwaka 2011, serikali ilitoa hati ya kumiliki ardhi kwa ya Wahdzabe ingawa walikosa sifa zinazotakiwa kisheria.

Akizungumza kuhusu Loliondo ambako Serikali imetangaza kutenga eneo la kiasi cha kilomita za mraba 2,500 za ardhi kwaajili ya makazi ya jamii ya wamasaai na ambao wengi wao hawakuwa na ardhi na hivyo kuwa katika mazingira magumu. Balozi amesisitiza kwamba uamuzi huo ulikuwa ni wa manufaa kwa jamii hiyo na taifa kwa ujumla.

Akasema kuwa eneo lililotengwa ni kubwa kuliko nchi ya Luxeburg au mara nne ya eneo la nchi ya Singapore ambayo ina kilomita za mraba 624.

Akasema eneo lililobaki la kilomita za mraba 1,500 Serikali imelitenga kwaajili ya hifadhi ya wanyama pori na mazalia yake ikiwa ni pamoja na uhifadhi wa uoto wa asili, utunzaji wa vyanzo vya maji kwa maendeleo endelevu ya uwepo wa wanyama na kwa manufaa ya vizazi vya sasa na vijavyo.

Naibu Mwakilishi wa Kudumu akafafanua Zaidi kwa kueleza kwamba, uamuzi huu wa Serikali wa kutenga ardhi kwaajili ya matumizi ya binadamu na mengine kwa hifadhi ya maliasili ni uamuzi halali na wala haukuanza sasa bali umekuwa ukitekelezwa katika maeneo mengi ya nchi tangu uhuru.

HALI BADO NI MBAYA MTWARA....WANAFUNZI WAWILI WAMETANDIKWA RISASI, MMOJA AMEFARIKI HAPOHAPO

Hivi sasa baadhi ya wananchi wa eneo la magomeni mkoani mtwara wamekimbilia katika Hospitali ya Mkoa wa Mtwara Lugula wakihofia usalama wao kutokana na vurugu za kuchomwa kwa nyumba zao pamoja na vibanda vya biashara zilizotokea leo asubuhi katika eneo hilo..

Maduka maeneo ya Magomeni yamechomwa moto ikiwamo pia mali za Askari magereza . Mwanafunzi wa CHUNO amefikishwa hospitali Ligula na majeraha ya risasi mguuni.
Mwanamke mwingine anayekadiriwa kuwa na miaka 25 mjamzito ameuawa kwa kupigwa risasi maiti ipo Ligula.

Inaelezwa kuwa katika baadhi ya mitaa hali imetulia na ni idadi ndogo ya wananchi ndiyo inayoonekana wakitembea mitaani isipokua eneo la magomeni ambako mbomu yanaendelea kusikika huku huduma za kijamii katika mji huo zikiwa zimesimama zikiwemo usafiri, huduma za kibenki na shule








MTWARA: ASKARI WATUHUMIWA KUBAKA NA KUMUUA MJAMZITO......INASEMEKANA WANAFANYA MAKUSUDI ILI KULIPIZA KISASI

Askari wakiwa lindoni/doriani, Mtwara

Hali ya usalama katika Manispaa ya Mtwara Mikindani mkoani Mtwara imezidi kuwa mbaya baada ya askari polisi kudaiwa kufanya unyama kwa kuwabaka wanawake na kumpiga risasi mjamzito

Mbali na unyama huo polisi pia wanadaiwa kuchoma moto nyumba tatu za wananchi katika mtaa wa Magomeni na vibanda vya maduka kadhaa na kupora vitu vilivyomo ndani.

Hata hivyo Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Mtwara, Linus Sinzumwa anasema hali ni shwari na kwamba wananchi watoke nje kuendelea na shughuli zao kama kawaida.

Kaimu Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Rufaa ya Ligula, Mohamedi Kodi amethibitisha kupokea mwili wa mjamzito ukiwa na tundu tumboni, zinazoaminika kuwa za risasi na hivyo kufanya idadi ya maiti zilizopokelewa hospitalini hapo kufikia mbili na majeruhi 18:

“Ni kweli kwa leo( jana) tumepokea maiti moja ya mwanamke ambaye ni mjamzito wa miezi saba, amepigwa risasi tumboni.pia tumepokea mwanafunzi wa shule ya sekondari ya Chuno, amevunjwa miguu yote kwa risasi.”

Habari zinadai kuwa mjamzito huyo ameuawa akiwa nyumbani kwake baada ya polisi kuvamia makazi yake.

Huduma za kijamii zimesimama, hakuna maduka yaliyo wazi, hakuna usafiri wa daladala wala pikipiki, mji upo kimya, sauti za milio ya mabomu na bunduki zimetawala, wanajeshi waliovalia sare wameuzingira mji wakiwa katika magari na pikipiki.

Wakizungumza na Waandishi wa Habari kwa nyakati tofauti wakazi hao wamelalamikia kitendo cha askari wa jeshi la polisi kuingia katika makazi yao, kuwapiga, kuwabaka na kuwapora mali zao:

“Magomeni A hatuna amani askari wanaingia majumbani mwetu wanatupiga na kutunyang’anya simu, yani huku Magomeni hatuna amani kabisa, tumepoteza watoto na hatujui hata waume zetu wako wapi” alisema Paulina Idd na kuongeza:

“Majumba yetu yamechomwa moto , wanaofanya fujo ni polisi wenyewe halafu wanakuja wanatubaka na kuiba mali zetu halafu tunateseka sisi yaani tumechoka kabisa na serikali yenyewe,” alisema Paulina.

Kamanda Sinzumwa alipoulizwa kuhusiana na tuhuma hizo alisema hawezi kuzungumzia suala hilo kwa madai kuwa atapingana na Waziri wa Mambo ya Ndani, Dk Emmanuel Mchimbi aliyewasili Mtwara leo: “Kuhusiana na suala hilo siwezi kulizungumzia kwa sasa kwani nitapingana na Waziri wangu kwani leo ametoa tamko bungeni na leo atawasili,” alieleza Sinzumwa

Wananchi wazungumzia bajeti

Wakizungumzia uwasilishwaji wa hotuba ya Wizara ya Nishati na Madini wakazi wa hapa wamesema kuwa hawakubaliani na ujenzi wa bomba la kusafirisha gesi kwani mpango huo utawaletea dhuluma:

“Mpango wa kusafirishwa kwa gesi asilia hatuna mpango nao kwa wakazi wote wa Mtwara kwa kifupi akina mama wa mtwara hatutaki itoke,” alisema Fatuma Abdallah.