NI wazi kwamba sasa kila mmoja wetu anapaswa kuwa makini na kuzingatia jinsi anavyokula chakula tangu asubuhi hadi anapokwenda kulala usiku.
Ingawa wataalamu wa lishe wanaeleza kiuhalisia hakuna chakula, ambacho binadamu anazuiwa kula katika maisha yake hapa duniani lakini ni lazima azingatie kiasi na aina ya chakula anachokula kila siku.
Kwa sababu ili aweze kuishi akiwa na afya njema duniani anahitaji kula chakula. Hata hivyo wanashauri kwamba ni vema azingatie kula chakula bora na si bora chakula.
Wanasisitiza iwapo binadamu hatazingatia ulaji unaofaa huwa anajiweka kwenye hatari ya kupata magonjwa mengi hasa yale yasiyo kuwa ya kuambukiza.
Magonjwa hayo ni pamoja na ya moyo, kisukari, shinikizo la damu, saratani na mengineyo ambayo kasi yake ya maambukizi inaonekana kuongezeka ikilinganishwa na kasi ya magonjwa ya kuambukiza.
Kulingana na takwimu zilizotolewa hivi karibuni na Shirika la Afya Duniani (WHO), inakadiriwa kila mwaka takribani watu milioni 17 hufariki dunia, kutokana na kuugua magonjwa ya moyo.
WHO inaeleza kila mwaka zaidi ya watu milioni 75 hugundulika kuwa na magonjwa hayo duniani huku likibainisha kwamba hali ni mbaya zaidi katika nchi zinazoendelea, Tanzania ikiwamo.
Mafuta ya nazi/mawese
Mtaalamu wa Lishe wa Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete (JKCI), Louiza Shem, anasema matumizi ya mafuta ya nazi na mawese katika maandilizi ya chakula yanaweza kumsababishia mtu kupata magonjwa ya moyo.
“Mafuta haya na yale yatokanayo na wanyama yanapaswa kutumiwa kwa kiasi na si kwa wingi kwa sababu huwa yana kiwango kikubwa cha lehemu.
“Yanapoingia mwilini huenda kuganda kwenye mishipa ya damu na inapotokea hali hiyo moja kwa moja mtu huwa kwenye hatari ya kupata magonjwa ya moyo hasa shinikizo la damu,” anasema.
Nyama zilizonona
“Ni vizuri pia kuzingatia ulaji wa nyama, nyama ya kuku na zilizonona huwa na mafuta mengi ambayo yakiingia mwilini huweza kuleta madhara.
“Unywaji wa vinywaji vyenye sukari nyingi huchangia ongezeko la mafuta kwa wingi na uzito mkubwa kwenye mwili wa binadamu.
Unavyopaswa kula
“Kwa bahati nzuri hakuna chakula ambacho mtu hatakiwi kutumia ili kujiepusha na magonjwa ya moyo lakini tunashauri jinsi gani na kwa kiasi gani uvitumie ili kuepuka kupata magonjwa.
“Mfano ukiangalia vyakula vya wanga (ugali, wali viazi na vinginevyo) unakuta mtu anakula kupita kiasi, anajaza sahani… wakati mtu anapaswa kula chakula kulingana na aina yake ya kazi anayoifanya.
“Wengi tunaofanya kazi ofisini hatutumii nguvu nyingi kulinganisha na wale wanaobeba mizigo, wengi tunakula nyama kwa kiwango kikubwa, ni vema kupunguza kiasi.
“Mafuta yanayopatikana kwenye nyama yanaongeza uzito kupita kiasi na huenda kuziba mishipa ya damu, ikiwa ni ya kichwani utapooza mwili na ikiwa ni kwenye moyo utapata ‘heart attack’,” anafafanua.
Anashauri kwamba ni vema jamii ikajenga tabia ya kupunguza kiwango cha matumizi ya chumvi wakati wa maandilizi ya chakula.
“Waepuke na waache kabisa tabia ya kuongeza chumvi mezani wakati wa kula kwani ni hatari kwa afya ya moyo,” anasema.
Anasema kundi linaloathirika ni la vijana ambao wengi wapo katika umri wa uzalishaji mali.
“Tunaona jinsi umri unavyokwenda ndivyo ambavyo mtu anakuwa kwenye hatari zaidi ya kupoteza maisha kutokana na magonjwa haya kwa sababu wengi huchelewa kupata matibabu,” anasema.
Wanawake
Daktari Bingwa wa Magonjwa ya Moyo wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete, Bashir Nyangasa, anasema wanawake ni kundi ambalo pia lipo kwenye hatari ya kupata magonjwa hayo.
“Maumbile yao jinsi yalivyo ni rahisi kupata maambukizi kwa mfano ya njia ya mkojo (U.T.I), anapokuwa kwenye kipindi cha hedhi ni muhimu kuzingatia usafi.
“Ikiwa atatumia pedi moja kwa muda mrefu anakuwa anajiweka kwenye hatari zaidi kwa sababu ile damu ikajaa kwenye pedi hutengeneza bacteria (wadudu) ambao husababisha maambukizi kwenye kizazi.
“Wadudu hao huweza kusafiri na kufika hadi kwenye moyo na kuuathiri pamoja na viungo vingine ikiwamo figo.
“Hivyo ni muhimu kuzingatia suala la usafi wa mwili wakati wote na hasa mwanamke anapokuwa katika kipindi cha hedhi,” anasisitiza.
Watoto
Dk. Nyangasa anasema wakati mwingine hutokea mtoto akazaliwa na magonjwa ya moyo ambayo kitaalamu huitwa ‘congenital heart disease’.
“Wengi huzaliwa na matundu kwenye moyo au unaweza kukuta mishipa yao ya damu haijakaa sawasawa, au wakati mwingine kama mama aliugua magonjwa mbalimbali wakati wa ujauzito kwa mfano kaswende huweza kusababisha mtoto wake kuzaliwa na magonjwa haya.
“Kuna magonjwa ya kurithi pia kwenye familia, kuna magonjwa ya surua, rubella ambayo huweza kusababisha mtoto kuzaliwa na magonjwa ya moyo,” anasema.
Daktari huyo anasema mtoto akizaliwa njiti huwa kwenye uwezekano mkubwa wa kupata tatizo kwenye moyo wake.
“Kunakuwa na mambo mawili, vile ambavyo havijatimia kwa rehema za Mwenyezi Mungu vitaendelea kutimia au vinaweza visiendelee kutimia, ndiyo utakuta wale ambao ukiuliza historia ya mtoto ujagundua ana tatizo,” anaeleza.
Jinsi ya kubaini tatizo
Anasema mzazi anaweza kubaini tatizo la moyo kwa mtoto hata kabla ya kumfikisha hospitalini.
“Unakuta hawezi kushika chuchu ya mama yake kwa dakika mbili au tatu ili anyonye kama inavyotakiwa, utaona anashika kwa dakika kadhaa na kuachia chuchu, akiachia utaona anapumua kwa shida kwa kutumia mdomo wake,” anabainisha.
Hali ilivyo JKCI
Daktari Bingwa wa Magonjwa ya Moyo wa JKCI, Tulizo Sanga, anasema katika taasisi hiyo kila siku wanapokea na kuhudumia wagonjwa zaidi ya 300 wanaosumbuliwa na magonjwa hayo.
Dk. Sanga ambaye pia ni Mkurugenzi wa Huduma Bora za Afya wa Taasisi hiyo, anasema wengi hufika wakiwa wamechelewa.
“Ni kwa sababu hatuna utamaduni wa kupima afya mara kwa mara, ni vema jamii ikabadilika na kuanza kupima afya,” anashauri.
Matibabu
Dk. Nyangasa anasema ili kuzibua mishipa iliyoziba kwenye moyo huwa wanatumia chuma maalumu ambacho kimetengenezwa kwa uwezo wa hali ya juu.
“Kile huwa ni ‘stain- less steel’ ni mfano wa vile vinavyotumika kutengeneza ndege huwa havishiki kutu,” anabainisha.
Anasema mtu aliyewekewa chuma anaruhusiwa kufanya kazi zote isipokuwa zile za kutumia nguvu nyingi.
“Kwa mfano kina mama tukiweka kile chuma lazima tumfuatilie sana kuhusu suala la kubeba ujauzito, msichana ambaye hajawahi kuzaa akiwekewa kile chuma ni lazima atumie dawa za kuyeyusha damu maisha yake yote.
“Akishika ujauzito badala ya kutumia vidonge, miezi mitatu ya awali tutampa dawa kwa njia ya sindano kila siku,” anasema.
“Wagonjwa wangu huwa wananiuliza… watatumia dawa maisha yote, na mimi nawatania mbona wanakula kila siku, jambo la msingi mama akifikia kipindi cha kujifungua lazima ajitahidi aende kwenye hospitali kubwa ili wamsaidie inapotokea tatizo.
Changamoto
Dk. Nyangasa anasema changamoto kubwa inayowakabili ni upatikanaji wa vifaa ambavyo vingi hununuliwa kutoka nje ya nchi.
“Vifaa vyote ambavyo vinatumika katika matibabu ya moyo, vingi havitengenezwi Afrika, vinatengenezwa Ulaya na Marekani. Kwa mfano Kampuni ya St. Jude wale wameshika soko kwa ajili ya kutengeneza ‘valve’ na ukitaka kuwa wakala hapa lazima upate kibali maalumu kutoka kwao.
“Na si vifaa vya moyo tu bali vifaa vingi vya hospitalini vinakuja kutoka huko, sasa changamoto ni kwamba kile kifaa unaweza kukuta kule kinauzwa Dola 1000 (zaidi ya Sh milioni mbili).
“Yule wakala hadi akilete hapa Tanzania akilipie Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), mnunuzi wa mwisho unakuta gharama imeongezeka hadi kufikia Sh milioni tano, ni changamoto kubwa,” anasema.