Thursday, October 12

Wizara ya Madini kufanya mnada wa Tanzanite Mirerani


Dar es Salaam. Wizara ya Madini kwa mara ya kwanza itafanya mnada wa madini ya Tanzanite kutoka kampuni nne za uchimbaji na biashara ya madini eneo la Mirerani wilayani Simanjiro mkoani Manyara.
Kaimu Kamishna Msaidizi (Uchumi na Biashara ya Madini), Godleader Shoo amesema mnada huo utafanyika Oktoba 15.
Shoo amesema utaratibu wa kufanya mnada huo ni jitihada za Serikali za kudhibiti utoroshwaji wa madini hayo nje ya nchi na pia kuwasaidia wachimbaji kuuza madini yao kwa bei ya ushindani inayoendana na soko la dunia.
Taarifa ya Wizara ya Nishati na Madini imemkariri Shoo akisema mnada huo utashirikisha wanunuzi kutoka ndani na nje ya nchi.
Amesema atakayenunua madini hayo katika mnada ni atakayeshinda bei iliyowekwa.
Amezitaja kampuni zitakazouza madini katika mnada huo kuwa ni TanzaniteOne, Franone, Glitter Germs na Classic Gems. Amesema zitauza madini ghafi na yaliyokatwa.
Shoo amesema mnada utafanyika kwa uwazi kwa kushirikisha wachimbaji, wanunuzi, Shirika la Madini la Taifa (Stamico), vikosi vya ulinzi na usalama, Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Halmashauri ya Wilaya ya Simanjiro na Wizara ya Madini.
“Mnada huu utaendeshwa kwa usalama mkubwa kwa kuwa madini ya Tanzanite yana thamani kubwa. Serikali imeimarisha ulinzi ili kujihadhari na watu wasio waaminifu,” amesema Shoo.
Amesema mnada utaiwezesha Serikali kupata mrabaha stahiki na kodi kwa uwazi ili kuchangia pato la Taifa na kuimarisha ulinzi na usalama kwa wauzaji, wanunuzi na mali zao.
Shoo amesema minada kama hiyo pia hufanyika kwa nchi za Afrika zenye madini ya vito kama vile Zambia (emerald), Zimbabwe (almasi) na Afrika Kusini (almasi).

No comments:

Post a Comment