Sunday, July 30

NEC imeteua Wabunge 8 kuziba nafasi ya waliotimuliwa CUF

Ni siku moja baada ya Spika wa Bunge Job Ndugai kumuandikia barua Mwenyekiti wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi kuendelea na hatua zinazostahili kujaza nafasi za Wabunge waliofutwa uanachama na CUF kwa mujibu wa Sheria.
Leo July 27, 2017 Tume ya Taifa ya Uchaguzi ‘NEC’ imefanya uteuzi wa Wabunge 8 wa Viti Maalum ambao wataziba nafasi za Wabunge ambao wamevuliwa uanachama na Mwenyekiti wa CUF Prof. Ibrahim Lipumba.
Taarifa ya Tume ya Taifa ya Uchaguzi imesema kwa mujibu wa Ibara ya 78(4) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya Mwaka 1977, ikisomwa pamoja na Kifungu cha 86A (8) cha Sheria ya Taifa ya Uchaguzi, Sura ya 343, Tume ya Taifa ya Uchaguzi katika kikao chake cha July 27, 2017 imewateua wafuatao kuwa Wabunge wa Viti Maalum katika Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia Chama cha Wananchi CUF.

View image on Twitter

NCHI ya Uturuki Yaomba MSAADA Tanzania

Tanzania imeombwa kuisaidia Uturuki kiwango cha Tani 20 ya Korosho kufuatia nchi hiyo kuwa na uhaba mkubwa wa bidhaa hiyo yenye uhitaji zaidi nchini Uturuki.

Mwenyekiti wa Jumuiya ya wafanyabiashara kutoka Uturuki ijulikanayo kama 'Turkish Exportetrs Assembly' (TIM) Bwana Kemal Batuhan Yazici amesema kuwa, kiwango cha korosho kilichopo nchini kimeshuka wakati mahitaji ya nchi ni Tani 20, hivyo wanaitegemea Tanzania kuondoa uhaba huo nchini mwao.

Kemal Batuhan Yazici amesema, Korosho inayohitajika nchini Uturuki ni ile ambayo tayari imechakatwa na kufungwashwa vyema kwa viwango vya kimataifa na sio malighafi hivyo ni vyema wafanyabiashara hiyo wakaandaa utaratibu wa haraka kuhakikisha Korosho zinasafirishwa kutoka Tanzania kwenda nchini Uturuki.

Kwa muda wa miezi sita, kiwango cha biashara kati ya Tanzania na Uturuki kimeongezeka kwa asilimia 9 kwa bidhaa za Tanzania zinazosafirishwa kutoka nchini Tanzania kwenda nchini Uturuki hivyo ongezeko hilo linaashiria Tanzania kupata soko lenye tija nchini Uturuki.

Katika siku za hivi karibuni nchi ya Uturuki imeongeza ushirikiano wake wa kibiashara na nchi ya Tanzania ambapo nchi hizo zimepata fursa mara kadhaa kuonesha maeneo yao ya uwekezaji baina yao ili kuongeza faida na kuleta maendeleo.

TAMKO TOKA IDARA YA UHAMIAJI


Idara ya Uhamiaji   imesema jukumu la Udhibiti  wa Uingiaji na Utokaji  wa raia  wa kigeni nchini, linatekelezwa kwa mujibu wa Sheria ya Uhamiaji  Sura ya 54 (Rejeo la 2016) na wala  haiwalengi  wafanyakazi  wa  Kampuni ya Madini ya Acacia  peke yake.

Ni hitajio la kisheria  kwa kila raia wa kigeni  anayeingia na kutoka nchini  kukaguliwa  ili kujiridhisha  iwapo  hakuna  dosari zozote za Uhamiaji, Ulinzi na Usalama.

Sheria ya Uhamiaji inaitaka Idara ya Uhamiaji  kumhoji  mtu yeyote awe raia wa Tanzania au kigeni  bila kujali anafanya  kazi  kwenye Kampuni au Shirika  gani, pale  inapotaka kujiridhisha  juu ya  uhalali  wa ukaazi wake hapa nchini na ikijiridhisha kuwa mtu huyu  hana dosari zozote inamwachia huru kama ilivyofanyika  kwa wafanyakazi wa Kampuni ya Madini ya Acacia  waliohojiwa  na kuruhusiwa kuendelea na safari yao hivi karibuni.

Idara ya Uhamiaji  inapenda kuuarifu Umma kuwa hakuna sababu zozote  nje ya matakwa ya  Sheria  ya Uhamiaji zinazopelekea  Idara ya Uhamiaji   kuweka kizuizi  cha kuja au kutoka kwa wafanyakazi wa kigeni wa Acacia.

Tunapenda kuujulisha Umma kuwa  ni muhimu  kwa watanzania na raia wa kigeni wanaokusudia kuingia na kutoka nchini kuhakikisha wanafuata  Sheria za Uhamiaji  ili  kutimiza hitajio la kisheria.

Imetolewa na
Ally M. Mtanda
Msemaji wa Idara ya Uhamiaji

29 Julai 2017

MBUNGE ROSE TWEVE WATENDAJI FANYENI KAZI ACHENI MAJUNGU




Mbunge wa viti Maalum mkoa wa Iringa kupitia chama cha mapinduzi CCM Rose Tweve akizungumza na madiwani na wananchi wa halmashauri ya Mafinga Mjini wakati wa baraza la madiwani
Mwenyekiti wa halmashauri ya Mafinga Mjini Charles Makoga akizungumza wakati wa baraza la madiwani lilofanyika katika ukumbi wa halmashauri hiyo
Baadhi ya madiwani,viongozi pamoja na wananchi waliohudhuria baraza la madiwani lilofanyika katika ukumbi wa halmashauri ya Mafinga Mjini.
 
Na fredy Mgunda, Mafinga.
 
Mbunge wa viti Maalum mkoa wa Iringa kupitia chama cha mapinduzi CCM Rose Tweve amewata watendaji wa halmashauri ya Mafinga Mjini kufanya kazi kwa kujituma na kuwa tumikia wananchi wa Jimbo la Mafinga Mjini ambalo linaongozwa na mbunge Cosato Chumi.
 
Akizungumza wakati wa baraza la madiwani wa halmashauri ya Mafinga Mjini alisema kuwa watendaji wengi wamekuwa wakilalamikiwa kutokana na kufanya kazi chini ya kiwango na kuwapelekea wananchi kuwa na changamoto ambazo hazina sababu.
 
“Hivi watendaji kitu gani kinachosababisha msifanye kazi kwa weledi kama ambavyo mlivyokuwa mnaomba kazi,jamani serikali ya awamu ya tano haitaki mfanye kazi kwa mazoea kama zamani saizi mnatakiwa kufanya kazi kutokana na kasi ya kimaendeleo ya serikali ya awamu ya tano”alisema Tweve
 
Tweve alisema kuwa watendaji wanaohusika na sekta ya maji katika halmashauri ya Mafinga Mjini wamekuwa hawafanyi kazi kwa weledi kwani tatizo kuwabambikia bili wananchi limekuwa Sugu na kuongeza malalamiko mengi huko mitaani hivyo lazima mbadilike maana swala la bili limekuwa kero sana hapa Mafinga Mjini lazima mlitafutie ufumbuzi.
 
“Toka nimerudi nimekuwa nikipokea malalamiko mengi yanayohusu bili za maji naombeni tembeleeni nyumba kwa nyumba kuandika bili sahihi na sio kutoa bili kwa kukisia hii inaalibu sura nzima ya viongozi wa halmashauri ya Mafinga Mjini, narudia tena watendaji fanyeni kazi kwa kujituma acheni mazoea kazini”alisema Tweve
 
Aidha Tweve alimuomba Mwenyekiti wa halmashauri hiyo kuhakikisha wanafanya kazi za wananchi na sio kukaa tu ofisini kitu kinachosababisha kuongezeka kwa matatizo kwa wananchi, hivyo mtalazimika kuwafuata wananchi kujua changamoto zinazowakabili wananchi na kuzitafutia ufumbuzi.
 
Kwa upande wake Mwenyekiti wa halmashauri ya Mafinga Mjini Charles Makoga alisema kuwa ahakikisha watendaji wote wanaenda kufanya kazi kwa wananchi na kuacha kufanya kazi kwa mazoea kama ilivyokuwa miaka ya huko nyuma na kuendelea kutekeleza Sera za chama cha mapinduzi CCM na kuendena na kasi ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dr John pombe Magufuli na kuwaletea maendeleo wananchi.
 
“Watendaji wangu mmekisikia alichosema mbunge Rose Tweve kuhusu wajibu kwa kweli hii ni aibu kubwa inatupaswa kujilekebisha ili kuendelea kutekeleza Sera za serikali ya awamu ya tano la sivyo nitaanza kuwatumbua mmoja baada ya mmoja ili kuendelea kutoa huduma bora kwa wananchi wa halmashauri ya Mafinga Mjini”alisema Makoga
 
Lakini Makoga aliwasifu wabunge Wawili ambao ni mbunge Cosato Chumi na Rose Tweve kwa kufanya kazi kwa nguvu na kuleta maendeleo ya wananchi wa wilaya ya Mufindi kwa ujumla maana kila siku tunapata mambo mapya ya kimaendeleo kupitia migongo yao na kuwaomba waendelee kutafuta njia nyingine za kuiletea maendeleo Mufindi.
 
“Miaka yote tungekuwa na wabunge kama hawa wawili leo hii Mufindi ingekuwa mbali sana kimaendeleo kutokana na Juhudi zao tunaziona maana saizi kila secta wameigusa kwa kuleta maendeleo au mikakati ya kutatua changamoto za maeneo husika” alisema Makoga
 
Nao baadhi ya watendaji wa halmashauri hiyo wasema kuwa bado wazitafutia ufumbuzi changamoto za Mji wa Mafinga licha ya kuwa na ufinyu wa bajeti za kimaendeleo kwenye miradi waliyoiomba hivyo wakipewa bajeti na kuajiri baadhi ya watumishi kila kitu kitaenda vizuri na changamoto za wananchi zitatuliwa kwa wakati.

Neno La Leo: Ni Heri Kuwa Na Adui Mwerevu Kuliko Rafiki Mjinga....!

Image may contain: 1 person, sitting and outdoor


Ndugu zangu, 

Katika dunia hii tunayoishi, wakati mwingine ni heri mwanadamu ukawa na adui mwerevu kuliko kuwa na rafiki mjinga. 

Rafiki yako akitokea kuwa ni mtu mjinga, basi, naye atakushauri mambo ya kijinga. Na pengine asiwe na hata la kukushauri. 

Mwanadamu usikimbilie kumchukia adui yako, na hususan akiwa ni mwerevu. Yumkini kuna ya kujifunza kutoka kwa adui mwerevu.

Angalizo: Mwanadamu unapaswa pia kuusikiliza kwa makini ujinga wa rafiki yako mjinga. Yumkini katika ujinga wake anaokueleza, waweza ukaambulia moja au mawili ya kujifunza. Hivyo, usimdharau rafiki yako mjinga.

Ni Neno La Leo.

Maggid Mjengwa.

MWANAUME AUZIWA SKETI BADALA YA SURUALI!



Unaweza ukacheka kama mazuri, lakini siku yakikutokea na wewe usije ukachanganyikiwa, amini kuingizwa mjini kunauma sana, labda kama hauja wahi kukutana na hali kama hiyo.
Zilikuwa ni dakika chache tu baada ya mfanyabiashara ambaye hutembeza nguo maeneo ya Dar es salaam – Buguruni. Alipokutana na kijana mmoja akiwa katika mizunguko yake.
Kisha akanza kumshawishi ili amuuzie nguo.
Utata uliibuka kidogo kwenye mapatano ya bei coz kila mmoja alikuwa anataka kumlalia mwenzie hakukua na ugomvi, Ila kilicho endelea hupaswi kusimuliwa Itazame video inayoonyesha tukio zimaa hapa…..

Moto wazua taharuki Uwanja wa Ndege Songwe



Taharuki imewakumba wafanyakazi wa Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Songwe (Sia) mkoani Mbeya na wananchi wanaofanya shughuli kando mwa barabara kuu ya Tanzania -Zambia baada ya moto kuwaka ndani ya eneo la uwanja huo.
Moto ambao chanzo chake bado hakijafahamika ulitokea jana mchana na kaimu meneja wa uwanja huo, Jordan Mchami alisema iliwachukua takriban nusu saa kuuzima.
Alisema moto huo ulianzia katika eneo la barabara kuu ya Tanzania - Zambia umbali wa mita 600 kutoka maeneo yalipo majengo na eneo la kurukia ndege.
“Tumefanikiwa kuuzima, hakuna madhara yoyote katika eneo letu na si sahihi kusema uwanja umeungua. Ifahamike kwamba uwanja huu una eneo kubwa ambalo ni kama vile pori tu. Moto umetokea barabara kuu ya Tanzania -Zambia umbali wa mita 600 hivi hadi tulipo sisi,” alisema baada ya kuenea taarifa katika mitandao ya kijamii na maeneo ya jirani kwamba uwanja huo umewaka moto.
Alipoulizwa kuhusu cha moto huo Mchami alisema ulionekana kuanzia barabarani na walipofuatilia kwa kuwauliza kina mama wanaofanya biashara ndogondogo kando mwa barabara hiyo waliambiwa kuwa waliona lori lililokuwa limeegeshwa eneo ulikoanzia hivyo wanahisi huenda mtu au watu waliokuwa katika gari hilo walirusha kipande cha sigara na kusababisha nyasi kuwaka.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mbeya, Mohamed Mpinga alipotafutwa kuzungumzia suala hilo, simu yake ilipokewa na msaidizi wake aliyesema kamanda yupo kwenye msafara wa Waziri Mkuu Kassim Majaliwa.
Hata hivyo, taarifa za ofisa mmoja wa polisi aliyekuwapo eneo la tukio ambaye aliomba jina lake lisiandikwe gazetini kwa kuwa si msemaji alisema, “Tumefanikiwa kuuzima moto ambao ulienea eneo kubwa. Tunashukuru haukuweza kufika maeneo ya kurukia ndege au kuharibu mali za uwanja huu.”
Uwanja huo umeongeza wigo wa fursa za kibiashara na kurahisisha huduma za usafiri wa anga kwa wakazi wa Mbeya, huku ukianza kuunganisha Kanda ya Nyanda za Juu Kusini na maeneo mengine duniani.
Kadri siku zinavyokwenda, watu kutoka nchi jirani za Zambia, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC) na Malawi wamekuwa wakiutumia uwanja huo.
Wageni hao ambao huingia nchini kwa ajili ya shughuli za biashara na utalii, wamezidi kuifungua kibiashara mikoa ya Songwe na Mbeya na kuonyesha ishara chanya kuwa uwanja huo unaelekea kuwa kitovu cha biashara kati ya Tanzania na nchi za kusini mwa Afrika.

Mkuu wa mkoa amzuia waziri kuzindua filamu



Mkuu wa Mkoa wa Geita amemzuia Naibu Waziri wa Habari, Sanaa, Utamaduni na Michezo, Anastazia Wambura kuzindua Filamu ya Magwangala kwa madai ya kuwa na maudhui yanayodaiwa kuutia doa Mgodi wa Dhahabu wa Geita (GGM).
Mkuu wa Wilaya ya Geita, Herman Kapufi alisema uamuzi wa kuagiza kuahirishwa kwa uzinduzi huo ulichukuliwa na mkuu wa mkoa, Ezekiel Kyunga ili kutoa fursa ya kusikiliza hoja na malalamiko kutoka GGM baada ya kubainika kuwa sehemu ya maudhui ya filamu inaigusa kampuni hiyo kwa taswira hasi.
Wambura alifika Geita mchana wa Julai 27 tayari kwa ajili ya uzinduzi wa filamu hiyo iliyochezwa na wasanii wa mkoani hapa wakiwamo Mbunge wa Geita Mjini, Constantine Kanyasu na Mwenyekiti wa Halmashauri ya Mji wa Geita, Leonard Bugomola ambao ulipangwa kufanyika saa moja usiku katika ukumbi wa Desire Park.
Filamu hiyo inaelezea maisha ya wachimbaji wadogo wanavyotegemea magwangala.
“Nilifika kwa mkuu wa mkoa kama mwenyeji wangu ndipo nikapata taarifa kuwa GGM wamelalamikia picha (filamu) kuwa si nzuri kwao. Tulikaa kujadili lakini hatukufikia mwafaka ndiyo maana leo (juzi) asubuhi nimeamka kuingia kwenye kikao kati ya mkuu wa wilaya, wasanii na mwakilishi wa GGM,” alisema.
Katika mazungumzo hayo, naibu waziri alisema GGM walitishia kwenda mahakamani. Hata hivyo, hakufafanua zaidi huku akisema amegundua kwamba kuna tatizo kubwa kati ya ofisa utamaduni na bodi ya filamu; ofisa utamaduni na mkuu wa mkoa; na pia ofisa utamaduni na wasanii.
“Kutokana na hali hiyo, ndiyo maana niliacha kuizindua ili tumalize kwanza haya mambo na wananchi wasiwe na wasiwasi tutakuja tena kwa ajili ya kuizindua,” alisema naibu waziri.
Lakini Kanyasu alipinga hatua hiyo ya kuzuiwa kwa uzinduzi huo akisema waliolalamika hawakufanya hivyo kwa maandishi na hakuna eneo wanaloonyesha kuwa linawahusu. Alisema inasikitisha Serikali ya mkoa kusikiliza maneno ya mdomo na kuzuia uzinduzi wa filamu hiyo.
Mbali ya mbunge huyo, wasanii waliocheza filamu hiyo, Rose Michael na Michael Kapaya nao walieleza kushangazwa kwao na uamuzi wa Serikali ya mkoa kumzuia naibu waziri kuizindua kwa kuwa waliipeleka kwa ofisa utamaduni miezi miwili iliyopita na hawakuelezwa kama ina kasoro yoyote.
“Filamu hii imesajiliwa na Bodi ya Filamu na imepewa daraja 16. Tumeileta kwenye ofisi ya mkoa miezi miwili iliyopita wanayo na hata kualika mgeni rasmi tuliwashirikisha. Tunashangaa tumeshajipanga na mgeni amefika Geita ndiyo wanazuia bila kujali gharama kubwa iliyotumika kuiandaa,” alisema Kapaya.
Rose alisema filamu hiyo ingekuwa na makosa ingezuiwa na bodi, hivyo wameshangaa kusikia malalamiko kutoka GGM ilhali filamu imezungumzia uhalisia wa maisha ya wachimbaji wadogo ambao ndiyo wananchi wengi wa Mkoa wa Geita.
Meneja Uhusiano wa GGM anayehusika na masuala ya jamii, Manase Ndoroma alisema si lengo la kampuni kuzuia filamu hiyo lakini kuna maeneo ambayo yanaeleza mgodi kuua na kunyanyasa watu jambo ambalo si la kweli.
Alisema mgodi unafanya kazi kwa mujibu wa sheria chini ya Serikali ya mkoa na endapo wangekuwa wanafanya shughuli zao kinyume cha sheria wangechukuliwa hatua kwa mujibu wa sheria.
Agizo la Rais Magufuli
Julai mwaka jana, Rais John Magufuli akihutubia wakazi wa Geita mjini akitokea Kahama aliagiza masalia ya mawe hayo wapewe wananchi maskini.
Aliagiza viongozi wa mkoa na Baraza la Taifa la Usimamizi wa Mazingira (Nemc) waandae utaratibu wa kuwagawia wananchi magwangala hayo ili yawasaidie kuendesha maisha yao.
Pia, alipiga marufuku kuwanyima wananchi udongo huo wenye masalia ya dhahabu ambao humwagwa na mgodi wa GGM kwa kuwa wamiliki wa mgodi walikuja kutafuta dhahabu na si magwangala.
“Natoa wiki tatu, mchakato wa kuyagawa magwangala uanze mara moja, naagiza NEMC (Baraza la Taifa la Usimamizi wa Mazingira) kwa kushirikiana na taasisi nyingine, waanze utaratibu wa kuyagawa magwangala mara moja na asije akajitokeza mtu kuzuia agizo langu,” alisema.
Baada ya agizo hilo, Waziri wa Nishati na Madini wakati huo, Profesa Sospeter Muhongo aliingia katika mzozo na wanasiasa wa Mkoa wa Geita alipowashutumu kuwa wanamchongea yeye na viongozi wa mkoa kwa Rais Magufuli ili waonekane hawatekelezi agizo hilo la kuwagawia wananchi magwangala.
Akitangaza utaratibu wa kuanza kugawa magwangala hayo, Profesa Muhongo alisema wanasiasa wa Mkoa wa Geita wamekosa subira na badala yake kwenda kwa Rais kuwachongea ili viongozi wa mkoa na wizara waonekane hawafanyi kazi.
Profesa Muhongo ambaye Mei 24 aliondolewa katika wadhifa huo na Rais Magufuli mara baada ya kupokea ripoti ya kamati ya kwanza aliyoiunda kuchunguza shehena ya makontena yenye mchanga wa dhahabu (makinikia) yaliyozuiliwa katika bandari tangu Machi alisema:
“Wanasiasa tuliwaeleza wazi kwamba kwa kushirikiana na Nemc tunatafuta maeneo ambayo ni rafiki na hayana madhara ya kimazingira, lakini nyinyi wanasiasa mkapeleka kilio kwa Rais mara ya tatu mkidai mpewe magwangala,” alisema Profesa Muhongo“Mmekosa uvumilivu.
Tulisema mvumilie tukague na tuone hakuna madhara, lakini hamkukubali. Tunakubaliana hapa baadaye nyie mnaenda kudai kwa Rais wakati huku kuna zebaki yenye madhara makubwa. Lakini kutokana na nyie kutokuwa wavumilivu, ndio imesababisha haya yote.”
Maeneo ambayo yalitengwa kwa ajili ya kumwaga magwangala hayo ni Nyamikoma, Lwenge, Kasota na Samina B.
Hata hivyo, Kanyasu alijibu shutuma hizo za Profesa Muhongo akisema wabunge walilazimika kumweleza Rais suala hilo kutokana na muda mrefu kupita bila ya ahadi hiyo kutekelezwa.
Msimamo wa mkoa
Kuhusu uamuzi huo, Kapufi alisema mkuu wa mkoa alifikia hatua hiyo baada ya kupokea malalamiko kutoka GGM kwamba, “Kuna kipande (cha filamu) kinamwonyesha mtu anayeigiza kama ofisa uhusiano wa GGM akiwahonga waandishi wa habari ili taarifa mbaya za kampuni hiyo zisiripotiwe; ingawa ni maigizo, maudhui hayo yakienda kwa jamii yanaweza kuibua hisia kuwa ndiyo hali halisi.”
Hoja nyingine aliyosema inalalamikiwa na GGM ni suala la malipo ya fidia na baadhi ya maeneo yanayotajwa kwenye filamu kuwa fidia haijalipwa, malipo hayo yalishafanyika.
“Baada ya kikao cha pamoja kilichoongozwa na naibu waziri na kuhudhuriwa na pande zote pamoja na wadau wakiwamo wabunge, tumekubaliana kukutana saa tisa alasiri ya Jumatatu Julai 31, kufikia muafaka wa jambo hili,” alisema.
Mkuu huyo wa wilaya alisema kikao hicho kitakachofanyika ofisini kwake pia kitajadili suala la mabadiliko ya jina la filamu kutoka ‘Tuijenge Geita Yetu’ iliyosajiliwa katika ofisi ya utamaduni, kwenda ‘Magwangala’ ambayo ndiyo iliyokuwa imetarajiwa kuzinduliwa.
Kapufi alisema kwa maelekezo ya mkuu wa mkoa, uzinduzi huo utafanyika siku itakayopangwa baada ya majadiliano na maridhiano kati ya wadau na marekebisho ya kasoro hizo zilizobainika.
Alisema GGM ambao ndiyo wanaolalamikia kasoro hizo, watalazimika kubeba dhamana ya kulipia gharama za marekebisho na hafla ya uzinduzi wa filamu hiyo ambayo pia inalenga kutangaza fursa za kiuchumi zinazopatikana mkoani Geita kupitia sekta za uchimbaji madini, uvuvi na kilimo pamoja na vita dhidi uvuvi haramu.
Nyongeza na Peter Saramba

Majaliwa: Meli zisitumike kuvushia wahamiaji haramu



Waziri Mkuu Kassim Majaliwa amezindua meli za MV Njombe na MV Ruvuma zitakazosafirisha mizigo Ziwa Nyasa huku akionya zisitumike kuvushia wahamiaji haramu na dawa za kulevya.
Alisema kukamilika kwa ujenzi wa meli hizo zilizogharimu Sh11.253 bilioni ni utekelezaji wa ahadi ya Rais John Magufuli alizozitoa katika Ilani ya Uchaguzi ya CCM ya mwaka 2015-2020 kwa lengo la kutatua changamoto ya usafiri wa abiria na mizigo katika Ziwa Nyasa.
Alisema ni jambo la faraja na la kujivunia kwa Serikali na wananchi kwa pamoja kushuhudia meli zilizotengenezwa na Mtanzania, zikiwa zimekamilika tayari kwa kuanza kazi ya kuwahudumia wananchi.
Waziri Mkuu alizindua meli hizo zilizojengwa na Kampuni ya Kitanzania ya M/S Songoro Marine Transport zilizopo Bandari ya Kiwira wilayani Kyela akiwa katika ziara yake ya kikazi mkoani Mbeya.
Alisema meli hizo zitumike kukuza uchumi wa wananchi kwa kusafirisha mizigo na biashara halali kati ya Tanzania na Malawi na zisitumike kama eneo la kuingiza wahamiaji haramu pamoja na dawa za kulevya nchini.
Waziri Mkuu aliwataka wananchi wa maeneo hayo kuwa walinzi na kuhakikisha meli hizo zinafanya shughuli halali za kiuchumi zitakazoleta tija kwao na Taifa na wasikubali zikatumika kama kichaka cha uhalifu.
Awali, Naibu Mkurugenzi wa Mamlaka ya Bandari Tanzania (TPA) anayeshughulikia Miundombinu, Mhandisi Karim Mataka alisema ujenzi wa meli hizo ulianza Juni 2015 na zina uwezo wa kubeba tani 1,000 za mizigo kwa kila moja.
Mhandisi huyo alisema mbali na kukamilika kwa mradi huo, pia TPA imeingia mkataba na Kampuni ya M/S Songoro kwa ujenzi wa meli yenye uwezo wa kubeba abiria 200 na tani 300 za mizigo.
Mradi huo ambao upo katika hatua za mwisho kukamilika utagharimu Sh9.12 bilioni.

Mchimbaji madini adaiwa kufariki dunia kwa bomu



Mchimbaji wa tanzanite katika mji mdogo wa Mirerani wilayani Simanjiro Mkoa wa Manyara, amefariki dunia na wengine 13 kujeruhiwa kwa madai ya kulipuliwa na bomu la kienyeji mgodini.
Aliyefariki dunia ni Lembris Mbatia (22) mkazi wa Sekei jijini Arusha, ambaye mwili wake umehifadhiwa katika Hospitali ya Mount Meru.
Pia, Polisi wa Kituo cha Mirerani wamejeruhiwa kwa kukwaruzwa na miamba usoni, kichwani na mikononi wakati wakiingia kwenye mgodi huo kukagua chanzo cha tatizo.
Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Manyara, Kamishna Msaidizi Francis Massawe alisema tukio hilo lilitokea usiku wa kuamkia jana.
Alisema wafanyakazi wengine wa mgodi huo waliishiwa hewa na kupelekwa hospitali kupatiwa huduma ya kwanza.
“Bado tunafanya uchunguzi wa tukio hili, ila chanzo ni mtobozano wa mgodi huo (Gem & Rock Ventures) na mgodi wa CT unaomilikiwa na kampuni ya TanzaniteOne,” alisema Kamanda Massawe.
Alipoulizwa, meneja ulinzi wa TanzaniteOne, Abubakary Yombe alisema hawezi kuzungumza chochote kwa kuwa anashughulikia suala la usalama wa wafanyakazi wake waliokuwa eneo la tukio.
“Tufanye mawasiliano baadaye, nazama kwenye mgodi wa CT kuangalia mambo yanavyokwenda nitaongea na waandishi wa habari nikipanda juu,” alisema Yombe.
Meneja wa Gem & Rock, Joel Saitoti alisema mgogoro na kampuni hiyo ndiyo umesababisha hali hiyo kwa kuwa walifanya mtobozano.
Mkuu wa Wilaya ya, Simanjiro, Zephania Chaula aliwataka wachimbaji hao kuwa watulivu kipindi hiki cha kuondokewa na mwenzao na wengine kujeruhiwa baada ya kutokea tatizo hilo.
“Ninyi ni wangu, mimi ndiyo baba yenu, hivyo nimesikiliza malalamiko yenu ila fanyeni subira tunafanya kikao na kamati ya ulinzi na usalama ya wilaya na kamishna msaidizi wa madini na RPC yupo, tutatoa uamuzi,” alisema Chaula.
Kamishna Msaidizi wa Madini Kanda ya Kaskazini, Adam Juma alisema hawezi kuzungumza chochote hadi watu wote waliopo kwenye migodi hiyo miwili watakapopandishwa juu.
“Bado nafanya mawasiliano na Kamishna wa Madini, Benjamin Mchwampaka juu ya tukio hilo hivyo vuta subira nitatoa tamko kinachofuata,” alisema Juma.