Sunday, July 30

Majaliwa: Meli zisitumike kuvushia wahamiaji haramu



Waziri Mkuu Kassim Majaliwa amezindua meli za MV Njombe na MV Ruvuma zitakazosafirisha mizigo Ziwa Nyasa huku akionya zisitumike kuvushia wahamiaji haramu na dawa za kulevya.
Alisema kukamilika kwa ujenzi wa meli hizo zilizogharimu Sh11.253 bilioni ni utekelezaji wa ahadi ya Rais John Magufuli alizozitoa katika Ilani ya Uchaguzi ya CCM ya mwaka 2015-2020 kwa lengo la kutatua changamoto ya usafiri wa abiria na mizigo katika Ziwa Nyasa.
Alisema ni jambo la faraja na la kujivunia kwa Serikali na wananchi kwa pamoja kushuhudia meli zilizotengenezwa na Mtanzania, zikiwa zimekamilika tayari kwa kuanza kazi ya kuwahudumia wananchi.
Waziri Mkuu alizindua meli hizo zilizojengwa na Kampuni ya Kitanzania ya M/S Songoro Marine Transport zilizopo Bandari ya Kiwira wilayani Kyela akiwa katika ziara yake ya kikazi mkoani Mbeya.
Alisema meli hizo zitumike kukuza uchumi wa wananchi kwa kusafirisha mizigo na biashara halali kati ya Tanzania na Malawi na zisitumike kama eneo la kuingiza wahamiaji haramu pamoja na dawa za kulevya nchini.
Waziri Mkuu aliwataka wananchi wa maeneo hayo kuwa walinzi na kuhakikisha meli hizo zinafanya shughuli halali za kiuchumi zitakazoleta tija kwao na Taifa na wasikubali zikatumika kama kichaka cha uhalifu.
Awali, Naibu Mkurugenzi wa Mamlaka ya Bandari Tanzania (TPA) anayeshughulikia Miundombinu, Mhandisi Karim Mataka alisema ujenzi wa meli hizo ulianza Juni 2015 na zina uwezo wa kubeba tani 1,000 za mizigo kwa kila moja.
Mhandisi huyo alisema mbali na kukamilika kwa mradi huo, pia TPA imeingia mkataba na Kampuni ya M/S Songoro kwa ujenzi wa meli yenye uwezo wa kubeba abiria 200 na tani 300 za mizigo.
Mradi huo ambao upo katika hatua za mwisho kukamilika utagharimu Sh9.12 bilioni.

No comments:

Post a Comment