Sunday, July 30

Mchimbaji madini adaiwa kufariki dunia kwa bomu



Mchimbaji wa tanzanite katika mji mdogo wa Mirerani wilayani Simanjiro Mkoa wa Manyara, amefariki dunia na wengine 13 kujeruhiwa kwa madai ya kulipuliwa na bomu la kienyeji mgodini.
Aliyefariki dunia ni Lembris Mbatia (22) mkazi wa Sekei jijini Arusha, ambaye mwili wake umehifadhiwa katika Hospitali ya Mount Meru.
Pia, Polisi wa Kituo cha Mirerani wamejeruhiwa kwa kukwaruzwa na miamba usoni, kichwani na mikononi wakati wakiingia kwenye mgodi huo kukagua chanzo cha tatizo.
Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Manyara, Kamishna Msaidizi Francis Massawe alisema tukio hilo lilitokea usiku wa kuamkia jana.
Alisema wafanyakazi wengine wa mgodi huo waliishiwa hewa na kupelekwa hospitali kupatiwa huduma ya kwanza.
“Bado tunafanya uchunguzi wa tukio hili, ila chanzo ni mtobozano wa mgodi huo (Gem & Rock Ventures) na mgodi wa CT unaomilikiwa na kampuni ya TanzaniteOne,” alisema Kamanda Massawe.
Alipoulizwa, meneja ulinzi wa TanzaniteOne, Abubakary Yombe alisema hawezi kuzungumza chochote kwa kuwa anashughulikia suala la usalama wa wafanyakazi wake waliokuwa eneo la tukio.
“Tufanye mawasiliano baadaye, nazama kwenye mgodi wa CT kuangalia mambo yanavyokwenda nitaongea na waandishi wa habari nikipanda juu,” alisema Yombe.
Meneja wa Gem & Rock, Joel Saitoti alisema mgogoro na kampuni hiyo ndiyo umesababisha hali hiyo kwa kuwa walifanya mtobozano.
Mkuu wa Wilaya ya, Simanjiro, Zephania Chaula aliwataka wachimbaji hao kuwa watulivu kipindi hiki cha kuondokewa na mwenzao na wengine kujeruhiwa baada ya kutokea tatizo hilo.
“Ninyi ni wangu, mimi ndiyo baba yenu, hivyo nimesikiliza malalamiko yenu ila fanyeni subira tunafanya kikao na kamati ya ulinzi na usalama ya wilaya na kamishna msaidizi wa madini na RPC yupo, tutatoa uamuzi,” alisema Chaula.
Kamishna Msaidizi wa Madini Kanda ya Kaskazini, Adam Juma alisema hawezi kuzungumza chochote hadi watu wote waliopo kwenye migodi hiyo miwili watakapopandishwa juu.
“Bado nafanya mawasiliano na Kamishna wa Madini, Benjamin Mchwampaka juu ya tukio hilo hivyo vuta subira nitatoa tamko kinachofuata,” alisema Juma.

No comments:

Post a Comment