Monday, May 4

Waziri Mkuu Aunda Kamati Kushughulikia Usafiri



Waziri Mkuu, Mizengo Peter Pinda ameunda kamati maalumu ya kudumu ya kusimamia Usafiri wa barabarani nchini ili kutatua changamoto zinazoikabali sekta ya Usafiri.

Katika kamati hiyo mwenyekiti wake atakuwa katibu mkuu wa wizara ya chukuzi, Katibu akiwa kamishna wa polisi barabarani na Mkurugenzi wa SUMATRA huku wajumbe wakiwa ni pamoja na katibu mkuu wizara ya kazi ya na ajira, katibu mkuu ujenzi, mwanasheria mkuu wa serikali na naibu katibu mkuu ofisi ya waziri mkuu.

Mkuu wa ratibu wa idara ya maafa toka ofisi ya waziri mkuu, mwenyekiti wa TABOA na TATOA, CHAKUA nao wanatakiwa kuanza kufanya vikao leo na kila mwezi watakutana kujadili na kutatua changamoto zote kasoro zile za kisheria ambazo zitapelekwa serikalini kwa mchakato zaidi wa kuzirekebisha.

Wakati huo huo umoja wa vyama vya madereva nchini Tanzania umesema hauna taarifa juu ya wao kutakiwa kukutana na waziri mkuu Mh. Mizengo Pinda kwa ajili ya mazungumzo kama inavyozungumzwa na kusisitiza kuwa wao wataendelea na mgomo wao ulioanza leo mpaka masuala yao yatapofanyiwa kazi.

Akizungumza na East Africa Radio leo Makamu Mwenyekiti wa Muungano wa vyama vya Madereva Abdallah Lubala amesema kauli ya kuwa wamekubaliana kukutana na Mh. Pinda ni za kisiasa na hazina ukweli wowote hivyo wataendelea na mgomo wao.

Wakati huo huo mgomo huo ambao umetangazwa kwa nchi nzima athari zake zimejitokeza katika mikoa mingine tofauti ambapo madereva wa mabasi ya abiria wamegoma huku wasafiri wakitumia usafiri mbadala wa bajaji pamoja bodaboda.

Wakizungumza kwa nyakati tofauti baadhi ya wakazi wa jiji la Mbeya, Arusha na Mwanza wamesema kuwa wanalazimika kutembea umbali mrefu kwenda makazini na wangine wakitumia gharama kubwa kutokana na vyombo hivyo wanavyotumia kupandisha bei za nauli kuliko kawaida.

Taarifa Ya Wizara Ya Mambo Ya Ndani Kuhusu Raia Wa Burundi Walioingia Nchini Kuomba Hifadhi

Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi inapenda kutoa taarifa kuwa hadi jana tarehe 03 Mei, 2015 raia wa Burundi waliongia nchini kuomba hifadhi walikuwa 1,852. 
 
Raia hawa wa Burundi waliingia nchini kupitia vijiji mbalimbali vya mkoa wa Kigoma. Vijiji hivyo ni pamoja na kijiji cha Kigaye, Sekeoya na Kakonko.  Vingine ni Kosovo, Kagunga na Kibuye, huku wengine wakiwa wamepitia katika Kituo cha Uhamiaji cha Manyovu kilichopo mkoani Kigoma.
  
Baada ya kufanyiwa mahojiano ya kina katika kituo maalumu kilichopo mjini Kigoma, 1,252 kati yao wamehamishiwa katika Kambi ya Wakimbizi ya Nyarugusu iliyoko wilayani Kasulu Mkoani Kigoma na mahojiano yanaendelea kwa waliobaki na wanaoendelea kuwasili.
 
Shughuli ya kuwahoji na kuwahamishia katika Kambi ya Wakimbizi ya Nyarugusu inafanywa na Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi kwa kushirikiana na Shirika la Umoja wa Mataifa linalohudumia Wakimbizi (UNHCR), pamoja na wadau wengine.
 
Aidha Serikali za vijiji zinasaidia kuwapokea na baada ya kufanyiwa ukaguzi, hatimaye wanasafirishwa hadi mjini Kigoma. 
 
Pamoja na ujio wa raia hawa wa Burundi, hali ya ulinzi na usalama katika maeneo wanapoingilia ni shwari na hadi sasa hakuna matukio yoyote ya uhalifu yalitolewa taarifa. Vyombo vya ulinzi na usalama vya Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi vilivyopo katika maeneo hayo vinaendelea na kazi zake kama kawaida.
 
Hata hivyo raia wanaoishi katika maeneo ya mpakani mwa Tanzania na Burundi mkoani Kigoma wametakiwa kutoa taarifa kwa Serikali za Vijiji vyao kuhusu wageni wanaofika katika maeneo yao, badala ya kuwahifadhi kiholela majumbani mwao, na kuwa watakaobainika kukiuka maagizo hayo watachukuliwa hatua za kisheria.
 
Raia hawa wa Burundi ambao wamekuwa wakiingia nchini wakiwa katika vikundi vidogovidogo wataendelea kupokelewa kufuatana na taratibu na sheria zinazotawala upokeaji wa waomba hifadhi.

Imetolewa na:
Isaac J. Nantanga
MSEMAJI WA WIZARA YA MAMBO YA NDANI YA NCHI