Monday, May 4

Waziri Mkuu Aunda Kamati Kushughulikia Usafiri



Waziri Mkuu, Mizengo Peter Pinda ameunda kamati maalumu ya kudumu ya kusimamia Usafiri wa barabarani nchini ili kutatua changamoto zinazoikabali sekta ya Usafiri.

Katika kamati hiyo mwenyekiti wake atakuwa katibu mkuu wa wizara ya chukuzi, Katibu akiwa kamishna wa polisi barabarani na Mkurugenzi wa SUMATRA huku wajumbe wakiwa ni pamoja na katibu mkuu wizara ya kazi ya na ajira, katibu mkuu ujenzi, mwanasheria mkuu wa serikali na naibu katibu mkuu ofisi ya waziri mkuu.

Mkuu wa ratibu wa idara ya maafa toka ofisi ya waziri mkuu, mwenyekiti wa TABOA na TATOA, CHAKUA nao wanatakiwa kuanza kufanya vikao leo na kila mwezi watakutana kujadili na kutatua changamoto zote kasoro zile za kisheria ambazo zitapelekwa serikalini kwa mchakato zaidi wa kuzirekebisha.

Wakati huo huo umoja wa vyama vya madereva nchini Tanzania umesema hauna taarifa juu ya wao kutakiwa kukutana na waziri mkuu Mh. Mizengo Pinda kwa ajili ya mazungumzo kama inavyozungumzwa na kusisitiza kuwa wao wataendelea na mgomo wao ulioanza leo mpaka masuala yao yatapofanyiwa kazi.

Akizungumza na East Africa Radio leo Makamu Mwenyekiti wa Muungano wa vyama vya Madereva Abdallah Lubala amesema kauli ya kuwa wamekubaliana kukutana na Mh. Pinda ni za kisiasa na hazina ukweli wowote hivyo wataendelea na mgomo wao.

Wakati huo huo mgomo huo ambao umetangazwa kwa nchi nzima athari zake zimejitokeza katika mikoa mingine tofauti ambapo madereva wa mabasi ya abiria wamegoma huku wasafiri wakitumia usafiri mbadala wa bajaji pamoja bodaboda.

Wakizungumza kwa nyakati tofauti baadhi ya wakazi wa jiji la Mbeya, Arusha na Mwanza wamesema kuwa wanalazimika kutembea umbali mrefu kwenda makazini na wangine wakitumia gharama kubwa kutokana na vyombo hivyo wanavyotumia kupandisha bei za nauli kuliko kawaida.

No comments:

Post a Comment