MADAKTARI kutoka Taasisi ya Moyo ya Jakaya kikwete kwa ushirikiana na wenzao wa Hospitali ya B.L.K ya nchini India wamewafanyia wagonjwa 64 upasuaji wa moyo ambao ni wa kufungua na bila kufungua kifua.
Kati ya hao wagonjwa nane walifanyiwa upasuaji wa kufungua kifua na 52 walifanyiwa upasuaji wa bila kufungua kifua (catheterization) kwa kutumia mtambo wa Cathlab.
Pia madaktari hao wamepata mafunzo ya kufanya upasuaji wa milango miwili ya moyo ambapo awali huduma hiyo ilikuwa haitolewi kwenye taasisi hiyo .Mafunzo hayo ya siku tano yaliyo ongozwa na wataalamu kutoka Hosipitali ya BLK ya Nchini India itasaidia serikali kuokoa zaidi ya milioni 30 ambazo zingetumika kwaajili ya matibabu ya mgonjwa wa moyo wenye uhitaji wa upasuaji wa milango miwili ambapo asilimia 25 ya wagonjwa wana uhitaji huo.
Akizungumza na Waandishi wa habari jana Dar es Salaam Daktari bingwa wa magonjwa ya moyo Peter kisenge alisema kupitia kambi ya siku tano ya madaktari nane wanaotibu maradhi ya moyo ,Wataalamu wa usingizi ,Wataalamu wa kutoa damu kwenye mapafu ,kutoka Hosipitali ya BLK ya nchini India imesaidia kutoa mafunzo ya uwekaji na upasuaji wa milango miwili kwenye moyo kwa wagonjwa wenye matatizo hayo ambapo huduma hiyo itakuwa ya kwanza kutolewa hapa nchini.
Mbali na huduma hiyo Dk Kisenge alisema tayari madaktari watatu wa taasisi hiyo wanaweza kutoa huduma ya uwekaji wa milango miwili ya damu kwenye moyo huku Daktari mmoja akipata mafunzo ya miaka miwili nchini india.Kuanza kwa huduma hiyo alisema watasaidia watoto wadogo ambao milango yao imeziba ambapo awali walikuwa hawafanyiwi upasuaji kutokana kutokuwepo kwa ujuzi wa upasuaji wa milango hiyo.
Alisema kwa wagonjwa 64 waliofanyiwa upasuaji katika taasisi hiyo wangesafirishwa nchini india serikali ingepoteza zaidi ya bilioni 6 .
Kwa upande wake Daktari Bingwa Upasuaji wa moyo na mishipa ya damu kutoka Hosipitali ya BLK ya Nchini India Dk Ajal Kajul alisema wataendelea kutoa ushirikiano kwa madaktari hapa nchini ambapo baadhi ya madaktari walioambatana nao watabaki katika taasisi hiyo kwaajili ya kuendelea kutoa mafunzo zaidi.
Dk. Kaul alisema wataendelea kuonyesha ushirikiano wa kutoa ujuzi kwa madaktari wa hapa nchini ambapo octoba mwaka huu watatoa mafunzo ya upandikizaji wa figo,na wagonjwa wenye matatizo ya mgongo katika Hosipitali ya Taifa ya Muhimbili.
Daktari Bingwa wa upasuaji wa Moyo na Mishipa ya damu kutoka Hospitali ya B.L.K ya nchini India Ajal Kajul akizungumza na waandishi wa habari kuhusu uhusiano wao na Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) ambapo kwa pamoja wameweza kuwafanyia upasuaji wa kufungua na bila kufungua kifua wagonjwa 64. Kushoto ni Daktari Bingwa wa Magonjwa ya Moyo Peter Kisenge.
Daktari Bingwa wa Magonjwa ya Moyo kutoka Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Peter Kisenge akizungumza na waandishi wa habari kuhusu uhusiano wao na Hospitali ya B.L.K ya nchini India ambapo kwa pamoja wameweza kuwafanyia upasuaji wa kufungua na bila kufungua kifua wagonjwa 64. Kulia ni Daktari Bingwa wa upasuaji wa Moyo na Mishipa ya damu kutoka Hospitali ya B.L.K ya nchini India Ajal Kajul.
Wafanyakazi wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) wakimsikilliza Daktari Bingwa wa upasuaji wa Moyo na Mishipa ya damu kutoka Hospitali ya B.L.K ya nchini India (hayupo pichani) wakati akizungumza na waandishi wa habari kuhusu uhusiano wao na Taasisi hiyo ambapo kwa pamoja wameweza kuwafanyia upasuaji wa kufungua na kufungua kifua wagonjwa 64. (Picha na JKCI)