Kaimu Balozi wa Marekani nchini Tanzania Dk. Inmi Patterson aliwaapisha wafanyakazi wa kujitolea wa Peace Corps wapatao 57 kuhudumu nchini Tanzania katika kipindi cha miaka miwili katika hafla iliyofanyika katika ofisi za Peace Corps jijini Dar es Salaam.
Wafanyakazi hawa wa kujitolea wa Kimarekani watakaofanya kazi katika sekta ya elimu watapangiwa kuhudumu katika wilaya za Iringa, Mufindi, Same, Kyela, Masasi, Maswa, Singida Vijijini, Lushoto, Chamwino, Hai, Rombo, Wete, Rungwe, Njombe, Iringa Vijijini, Sumbawanga, Kusini Unguja, Kaskazini Unguja, Hanang, Mbeya, Nachingwea, Hanang, Iramba, Kiomboi, Mbeya Rural, Shinyanga na Singida Mjini.
Mgeni rasmi katika hafla hii alikuwa ni Katibu Mkuu wa Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi Dk. Leonard D. Akwilapo. Hafla hii ilihudhuriwa pia na wafanyakazi wa kujitolea wa Peace Corps wanaoendelea kuhudumu na wale waliohudumu hapo zamani pamoja na maafisa kutoka mashirika mengine yanayojihusisha na wafanyakazi wa kujitolea.
Akizungumza na wafanyakazi hao wa kujitolea Kaimu Balozi Patterson alisema: "Wakati ambapo kuna uwezekano kwamba mnaweza kuwa Wamarekani wa kwanza kuishi na wafanyakazi wenzenu au majirani wa Kitanzania, ni wazi kwamba kwa Watanzania hao nyinyi mtaendelea kuwa wawakilishi wa Watu wa Marekani."
Peace Corps ni taasisi ya Serikali ya Marekani iliyoanzishwa na Rais John F. Kennedy mwaka 1961 ambayo hivi sasa inahudumia zaidi ya wafanyakazi wa kujitolea zaidi ya 7,000 katika zaidi ya nchi 70 duniani. Kwa zaidi ya miaka 50, Peace Corps imekuwa taasisi inayoendesha shughuli za mabadilishano ya kiufundi na kitamaduni zisizoegemea mrengo wowote wa kisiasa na kidini. Peace Corps ina dhamira ya kukuza amani na urafiki duniani kwa kutekeleza malengo matatu yafuatayo:
• Kutoa wafanyakazi wa kujitolea wa Kimarekani watakaochangia kuleta maendeleo ya kijamii na kiuchumi katika nchi itakayohitaji wafanyakazi hao;
• Kukuza uelewa kuhusu Wamarekani miongoni mwa watu katika jamii zinazohudumiwa na Wafanyakazi wa kujitolea;
• Kuimarisha uelewa wa Wamarekani kuhusu dunia na watu wake.
Zaidi ya wafanyakazi wa kujitolewa wa Peace Corps 2,500 wamehudumu nchini Tanzania toka mwaka 1961. Peace Corps hutoa wafanyakazi wa kujitolea wa Kimarekani wenye utaalamu katika nyanja mbalimbali ambao hupangiwa kufanyakazi katika jamii wakifundisha katika shule za sekondari (hisabati, sayansi na Kiingereza), wakitoa elimu ya afya na utunzaji wa mazingira.
No comments:
Post a Comment