Friday, November 3

HOSPITALI YA AGA KHAN YAANZA KUTOA BURE HUDUMA YA UPANDIKIZAJI WA MATITI KWA AKINA MAMA

Hospitali ya Aga Khan imeanza kutoa bure huduma ya kupandikiza matiti kwa akina mama waliopatwa na magonjwa mbalimbali yaliyowapelekea kukatwa kwa kiungo hicho muhimu, ikiwemo wale waliokatwa kutokana na magonjwa ya Kansa, ukatili na kuungua moto.

Akizungumza na waandishi wa habari leo hii Jijini Dar es Salaam, Daktari bingwa wa kitengo cha upasuaji katika hospitali ya Aga Khan, Dr. Aidan Njau amesema huduma iliyoanza leo ni kuhudumia mgonjwa mmoja mmoja ili kusaidia wanawake wengi wenye matatizo hayo ambao wamekuwa wakiishi na maumivu makali hata kujisikia vibaya katika jamii .

“Kwa kuanzia tunaanza na wale wanawake waliokatwa matiti yao, tutatoa nyama kwenye sehemu yake ya mwili na kuipandikiza kwenye sehemu iliyokatwa na kuufanya muonekano wake urudi kama ulivyokuwa" amesema Dk. Njau.

Amesema huduma hiyo, itawafanya watanzania kushuhudia wanawake wakipandikizwa matiti jambo ambalo halijawahi kutokea hapa nchini na kuwaasa wanawake wenye matatizo hayo wajitokeze hospitalini hapo kwa wingi kwa ajili ya kupatiwa huduma hii ya bure.

Amesema, upasuaji huo utafanywa na madaktari wawili ambao ni Daktari bingwa wa kitengo cha upasuaji katika hospitali ya Aga Khan, Dr. Aidan Njau na Daktari bingwa Edwin Mrema kutoka Hospitali ya Taifa Muhimbili wote wakiwa na lengo la kurudisha furaha kwa wanawake wenye matatizo haya waliyokwisha ipoteza.
 Daktari bingwa wa upasuaji wa Hospitali ya Agakhan, Dkt Aidan Njau (kushoto) akizungumza na waandishi wa habari juu ya huduma ya Upandikizaji wa Matiti kwa wanawake waliokatwa matiti kutokana na majanga mbalimbali ikiwemo karatani ya matiti kulia ni daktari bingwa wa upasuaji kutoka hospitali ya Taifa Muhimbili, Dkt Edwin Mrema. 
Dkt Edwin akiwa na baadhi ya wataalam wa magonjwa mbalimbali ya upasuaji

MITAMBO YA KUZALISHA UMEME (SYSTEM TURBINE, NO 2) YAWASILI KINYEREZI II

Mitambo ya kuzalisha umeme (System Turbine, no 2) kwa ajili ya mradi wa kutumia gesi asilia wa Kinyerezi II iliingia nchini kupitia Bandarini Oktoba 16, 2017 na leo hii Novemba 03, 2017 imetolewa Bandarini na hivi sasa inaelekea kituo cha kuzalisha umeme kwa gesi Kinyerezi II (MW 240) Jijini Dare es Salaam.

Mradi huu wa Kinyerezi II uliwekwa jiwe la msingi na Mhe. Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli achi 16, 2016. Mradi unatarajiwa kukamilika ifikapo Septemba 2018. 
Moja ya Gari iliyobeba Mitambo ya kuzalisha umeme (System Turbine, no 2) kwa ajili ya mradi wa kutumia gesi asilia wa Kinyerezi II ikielekea eneo Kutakapojengwa Mradi huo.

TOT PLUS WAJIFUA KUIPUA NYIMBO TATU MPYA UKIWEMO WA KUMUUNGA MKONO JPM KATIKA VITA YA KUTETEA RASILIMALI ZA NCHI


Kundi la Tanzania One Theatre (TOT Plus), limo kambini Wanamuziki wake wakijifua vikali katika mazoezi ya nyimbo tatu ambazo kundi hilo litaziipua hivi karibuni.


Akizungumza wakati wa mazoezi ya nyimbo hizo, Mkurugezi wa TOT Plus inayomilikiwa na Chama Cha Mapinduzi (CCM), Gasper Tumaini amezitaja nyimbo hizo kuwa ni 'Tumuunge mkono JPM',  'Amani ya Tanzania' na Hongera awamu ya tano'.



Tumaini amsema, wimbo wa 'Tumuunge mkono JPM' ni wa kuwahamasisha Watanzania popote walipo kumuunga mkono Rais Dk John Magufuli katika vita ya uchumi anayoongoza kwa kuhakikisha inaziba mianya inayotishia upotevu au matumizi mabaya ya rasilimali za nchi.



"Kama unavyoona Rais tayari ameshaamua kwa dhati kupigana katika vita ya kubana mianya inayotishia upotevu au matumizi mabaya yanayofanya na baadhi ya watu kutumia rasilimali za nchi vibaya kwa kujinufaisha wao huku taifa likiendelea kuwa masikini



Hii siyo vita ndogo, ni kubwa sana inayohitaji ujasiri na ari kubwa ya kujituma, hivyo ni lazima Watanzania wote tumuunge mkono ili asiyumbishwe na waliokuwa wanajinufaisha na rasilimali hizi", alisema Tumaini wakati wa mazoezi ya nyimbo hizo kwenye ukumbi wa Ofisi ya CCM Mwinjuma, Mwananyamala, Dar es Salaam.



Amesema, wimbo wa 'Amani ya Tanzania' kunahimiza Watanzania ndani na nje ya Nchi kuhakikisha pia wanaienzi amani ya nchi kwa kuunga mkono juhudi za kuiimanrisha zinazofanywa na viongozi wakiongozwa na misingi imara iliyowekwa na Baba wa Taifa Mwalimu Julius Nyerere na pia Rais wa Kwanza wa Zanzibar  Hayati Sheikh Abeid Amani Karume.



Akizungumzia wimbo wa tatu wa 'Hongera awamu ya Tano', Tumaini amesema, wimbo huo ni wa pongezi kwa Mwenyekiti wa CCM, Rais Dk. John Magufuli kwa kutimiza kwa vitendo ahadi zilizotolewa na CCM wakati wa kampeni za kuomba ridhaa ya wananchi katika uchaguzi mkuu uliopita.



"Tumeona ni vizuri kutunga wimbo huu wa kumpongeza kwa sababu utekelezaji wa ilani na ahadi alizokuwa akizitoa kwenye kampeni unaonekana wazi japokuwa sasa ni miaka miwili tu tangu tumchague, kwa kweli Rais Dk. Magufuli amechapa kazi hivyo inastahili kumpongeza", alisema tumaini.



Amesema, nyimbo hizo ambazo ni kwaya tayari zimeshakamilika na sasa wanamuziki wanazifanyia mazoezi ya mwisho mwisho  kabla ya kuzirekodi ili zianze kusikika katika maeneo mbalimbali na hasa pale kundi hilo litakapokuwa likitumbuiza.



Mmiliki wa theNkoromoBlog aliyefika kwenye mazoezi ya kundi hilo, alishuhudia wanamuziki wote wakiwajibika kila mmoja katika eneo lake, huku baadhi yao wakitokwa jasho kuliko hata wanapokuwa wakitumbuiza jukwaani katika maonyesho maalum.

 Mwanamuziki nguli Juma Abdallah 'Jerry' akikipapasa kinanda kwa mkoni mmoja kuonyesha umahiri wake, Kundi la TOT Plus lilipokuwa katika mazoezi ya nyimbo tatu, leo katika ukumbi wa CCM Mwinjuma, Mwananyamala Dar es Salaam
 Waimbaji Neca Twalib aliyechukua nafasi iliyoachwa na aliyekuwa mwimbaji nguli na Mkurugenzi wa TOT Plus Marehemu Kampteni John Komba, akiimba na mwenzake Corobian Mkinga wakati wa mazoezi hayo
 Patrick Thomas akizicharaza tumba wakati wa mazoezi hayo
 Mkurugenzi wa TOT Plus Gasper Tumaini (mwenye suti) akizungumza na baadhi ya wadau waliofika kushuhudia mazoezi hayo
 Jerry akikicharaza kinanda kwa madaha wakati wa mazoezi hayo
 Waimbaji Rosemary William, Sharifa Mohammed na Mwasiti Suleimani wakiimba wakati wa mazoezi hayo
 Mwimbaji nguli Hadija Kopa na wenzake wakiimba wakati wa mazoezi hayo
 Tumaini akiwa na wadau wakati wakifuatilia mazoezi hayo. Kulia ni Jerry
 Waimbaji wa TOT Plus wakiwa kwenye mazoezi hayo
 Waimbaji wa TOT Plus wakiwa kwenye mazoezi ya wimbo wa 'Amani ya Tanzania'
 Jerry na Tumaini wakifuatilia kwa makini mazoezi hayo. Kushoto ni mdau wa TOT Plus
 Alen Elias aka Mchungaji akikicharaza kinanda kwa makini
 Evans Peter na said Mpiluka wakiyacharaza magita wakati wa mazoezi hayo
 Godfrey Kanuti akilicharaza gita wakati wa mazoezi hayo
 Neka twalib na Mkinga wakishauriana jambo wakati wa mazoezi hayo
 Fundi mitambo akiwajibika wakati wa mazoezi hayo
 Tumaini akijadiliana jambo na viongozi wa bendi ya Vijana Jazz ambao walihudhuria mazoezi hayo
Wanamuziki wa TOT Plus wakiwa katika picha ya pamoja na baadhi ya wadau wakati wa mazoezi hayo.

PROFESA MWAKALILA AWAASA WANAFUNZI MWALIMU NYERERE KUACHANA NA SIASA WAKIWA SHULENI


MKUU wa chuo cha Kumbukumbu ya Mwalimu Nyerere kilichopo kigamboni,Profesa , Shadrack Mwakalila  ameagiza wanafunzi wa chuo hicho, waliojiunga katika mwaka wa Masomo wa 2017 kutojiusisha na masuala ya siasa pindi wanapokuwa chuo na badala yake wazingatie katika suala zima la taaluma ili waweze kupata kile kilicho wapeleka chuoni hapo.
Profesa Mwakalila amesema hayo alipokuwa akizungumza na wanafunzi wa Mwaka wa kwanza juu ya nini wanatakiwa kufanya wakiwa chuoni hapo na kutambua nini cha msingi kilichowaleta.
"Hapa sio mahali pakufanya Siasa ni sehemu mliyokuja kuchukua taaluma, kamwe msikubali wanasiasa kuwatumia kwa ajili ya maslahi yao kwani mkifanya hivyo mtakuwa mmepoteza lengo ambalo limewaleta hapa katika kufanikisha malengo yenu ya kitaaluma"amesema Profesa Mwakalila.
Profesa Mwakalila ameongeza kuwa kama wanavyojua chuo hicho kimetokana na Muasisi wa Taifa hili Mwalimu Julius .K. Nyerere hivyo wanapaswa kufuata maadili na kuwa waadilifu ili  kumuenzi muasisi Baba wa Taifa ambaye alikuwa na ndoto ya kuwa sehemu hiyo iweze kupika viongozi wenye maadili mema kwa Taifa hili.
alimaliza kwa kutoa wito kwa wote waweze kukazana katika masomo yao hili waweze kuwa alama ya chuo hicho pindi wanapomaliza masomo yao na kufika hapo kwao isiwe majuto.
 Mkuu wa Chuo cha Kumbukumbu ya Mwalimu Nyerere Kigamboni Dar es Salaam,Profesa. Shadrack Mwakalila akizungumza na Wanafunzi wa Chuo hicho wa Mwaka wa kwanza ambao wamechaguliwa katika muhula wa Masomo 2017 kwa ngazi ya Cheti, Astashahada na Shahada juu ya umuhimu wa kufuata Maadili.
 Mshauri  wa Wanafunzi wa Chuo cha Kumbukumbu ya Mwalimu Nyerere akikazia jambo juu ya kuwa na maadili shuleni
 Sehemu ya Wanafunzi wa wapya wa Chuo cha Kumbukumbu ya Mwalimu Nyerere kilichopo Kigamboni wakifuatilia hotuba ya Mkuu wa chuo hicho Profesa Shadrack Mwakalila
  Sehemu ya Wanafunzi wa wapya wa Chuo cha Kumbukumbu ya Mwalimu Nyerere kilichopo Kigamboni wakifuatilia hotuba ya Mkuu wa chuo hicho Profesa Shadrack Mwakalila
 Sehemu ya Wanafunzi wa wapya wa Chuo cha Kumbukumbu ya Mwalimu Nyerere kilichopo Kigamboni wakifuatilia hotuba ya Mkuu wa chuo hicho Profesa Shadrack Mwakalila

MOHAMMED DEWJI APONGEZA JITIHADA ZA RAIS MAGUFULI KUFUFUA VIWANDA

Afisa Mtendaji Mkuu wa kampuni ya Mohammed Enterprises Tanzania Limited (MeTL Group), Mohammed Dewji akizungumza katika mkutano wa Global Business Forum 2017 kuhusu Viwanda kwa Nchi za Afrika, mkutano huo wa siku mbili umefanyika Dubai, UAE na kuhudhuriwa na watu 5860 wakiwepo viongozi wa serikali za nchi za Afrika na wafanyabiashara. (Picha na Clouds Media)

Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya Mohammed Enterprises (MeTL Group), Mohammed Dewji amepongeza uamuzi wa Rais wa Tanzania, Dkt. John Pombe Magufuli kuifanya Tanzania kuwa nchi ya viwanda kwa kufufua viwanda ambavyo vilikuwa havifanyi kazi.

Dewji ametoa pongezi hizo wakati akizungumza katika mkutano wa siku mbili wa Global Business Forum 2017 (GBF) kuhusu Viwanda kwa Nchi za Afrika uliofanyika Dubai, Falme za Kiarabu (UAE).

Mfanyabiashara huyo ambaye anamiliki viwanda 41 alisema uamuzi aliochukua Rais Magufuli ni mzuri hasa katika kipindi hiki ambacho Tanzania inaelekea katika uchumi wa kati.

Dewji alisema kampuni yake ya MeTL Group itaendelea kushirikiana na serikali na katika kipindi cha miaka kadhaa ijayo amejipanga kuhakikisha anatoa ajira kwa Watanzania 100,000 jambo ambalo litasaidia kukuza uchumi wa nchi na kwa wananchi..

 “Nianze kwa kumpongeza Mhe. Rais John Pombe Magufuli kwa shabaha yake ya viwanda, ni nzuri sababu kuna ongezeko la thamani lakini pia watu wanaweza kupata ajira na pia hizi biashara zitalipa kodi ambazo zitaisaidia serikali kuwekeza kwenye mambo ya afya na maji na huduma za jamii. Mimi shabaha yangu kwenye miaka saba au nane ijayo MeTL Group tunataka tuajiri watu 100,000,” alisema Dewji.

Dewji ambaye kwa mujibu wa jarida la Forbes ni tajiri namba moja nchini aliongeza kuwa utendaji wa Rais Magufuli ni wa kasi hivyo anategemea kuwa katika kipindi cha miaka michache ijayo uchumi wa Tanzania utakuwa umekuwa  sana.

“Mimi naona kwa kasi ya Mhe. Rais kwenye miaka miwili au mitatu ijayo tutakuwa tumefika mbali sana, uchumi wetu kwasasa ni asilimia sita au saba lakini kama tukitaka kuondoa umaskini lazima nchi yetu ukuaji wa uchumi uanze kukua kwa zaidi ya asimilia 10, mimi nina muamini sana Mhe. Rais na shabaha yake kwahiyo Mungu atutangulie na sisi tupo nyuma yake tutafika hivi karibuni,” alisema Dewji.

Pia Dewji alizungumzia umuhimu wa mkutano wa GBF ambao umekutanisha watu kutoka mataifa mbalimbali ya Afrika wakiwepo viongozi wa serikali za nchi za Afrika na wawekezaji alisema ni nafasi ya kipekee kwani pamoja na kujadili viwanda pia amepata nafasi ya kuwaelezea washiriki wa mkutano fursa za uwekezaji zilizopo hapa nchini.

“Umuhimu ni mkubwa sana nakuja hapa kama MO lakini pia nawakilisha nchi yangu Tanzania, nimeitangaza nchi yangu ili watu waje na wawekeze, nimewaeleza mazingira yetu ya uwekezaji ni mazuri, tuna malighafi na tunahitaji viwanda angalau watu wetu wa Tanzania wapate ajira na serikali ipate kodi,” aliongeza Dewji.

Kuchoma vifaranga ni kukomoa au adhabu?


Mjadala mzito umeibuka tangu vifaranga 6,400 vilivyodaiwa kuingizwa nchini kinyume cha sheria, vilivyopochomwa moto Namanga mkoani Arusha.
Vifaranga hivyo, mali ya Mary Matia na vyenye thamani ya Sh12.5 milioni, vilikamatwa kwenye mpaka mjini Namanga, ambako ni mpaka wa Tanzania na Kenya.
Hatutetei uvunjwaji wa sheria wala kitendo chochote kinachokwenda kinyume na taratibu tulizojiwekea kama nchi, lakini, tunaamini busara ingeweza kutumika katika kushughulikia kadhia hiyo.
Tangu habari hii ianze kusambaa, baadhi ya wadau na watetezi wa haki za wanyama wamekuwa wakitoa maoni yao kuhusu hatua stahiki ambayo ilipaswa kuchukuliwa na mamlaka husika.
Kwa walio wengi, busara kuu ingekuwa kumuamuru mmiliki kuvirudisha vifaranga hivyo alikovitoa.
Kuwarudisha vifaranga hao walikotoka, si jambo geni. Mathalani, mara kadhaa tumeshuhudia mifugo hususan ng’ombe inayokamatwa kwa kuingizwa kiholela nchini, ama ikitaifishwa na vyombo vya dola au ikirudishwa ilikotoka.
Inasikitisha kuwa wahusika katika uchomaji wa vifaranga hivi hawakulitazama suala hili kwa upande mwingine, hasa wa ukatili dhidi ya viumbe hai.
Tukikopa maneno ya mkurugenzi mtendaji wa Shirika la Ustawi wa Wanyama Tanzania (Taweso), busara nyingine ingekuwa kuwapima vifaranga hao na kama ingebainika kutokuwa na maambukizi, mamlaka husika zingevitaifisha na hata kuvigawa kwa wajasiriamali, magereza au vituo vya watoto yatima.
Inawezekana wahusika wana hoja nzito tena za kisheria zilizowasukuma kuteketeza vifaranga hivyo, lakini hawakuona haja ya kutafuta njia mbadala zaidi ya kuvichoma, njia ambayo unadhani ni ya kikatili.
Katika sakata hili, utu ungeweza kuchukua nafasi zaidi, huku wahusika wakitekeleza sheria na taratibu zilizopo. Tujifunze kutoka kwa mahakimu na majaji ambao wakati fulani hutoa uamuzi kwa kutumia busara hasa baada ya kusoma mazingira ya tukio.
Walioshiriki kuteketeza vifaranga hivi, wangeweza kutumia njia nyingine kama ya kumtia adabu mmiliki wa mzigo huo. Kinachogusa hisia za wengi ni kuwa mmiliki huyo alishakuwa tayari kuwarudisha alikowatoa.
Kwa maneno mengine, alishakubali kupata hasara, jambo ambalo lingeweza kuwa funzo kwake kuwa anapaswa kutii sheria na taratibu za nchi.
Hatudhani kama sheria, taratibu na hata adhabu tunazojiwekea nchini zinalenga kukomoa, bali kutoa fundisho ili kosa kama hilo lisitokee tena.
Wakati ni wajibu kwa kila raia kufuata taratibu na sheria, mamlaka nazo zinawajibika kuwa mstari wa mbele kutoa elimu kwa umma ili kupunguza vitendo vya ukiukwaji wa sheria.
Hivi ndivyo inavyopaswa kufanywa sio tu na vyombo vinavyosimamia masuala ya ufugaji, lakini pia vyombo vya usalama barabarani, usimamizi wa kodi na vinginevyo nchini.
Tujitahidi kuepuka kuwa Taifa linaloamini katika adhabu hasa zenye mrengo wa kukomoa badala ya kufundisha. Ndio maana kiunatakiwa kuwepo uchunguzi wa mazingira ya kosa kama ni makusudi au kwa kutojua.
Baadhi ya makosa hufanywa si kwa nia mbaya bali kwa kutojua au kukosea. Haya yanaweza kushughulikiwa kwa kuangalia njia mbadala ambayo ni ya kielimu zaidi kwa manufaa ya baadaye.

Acheni tabia ya kuwasimanga wanaohama vyama vyenu vya siasa



Kulwa Magwa
Kulwa Magwa 
Kuna mambo unapoyafikiria yanakera na yanahitaji majibu ya papo kwa hapo na ndicho ambacho nakijadili hapa. Wiki hii mmoja wa wanasiasa waliojipatia umaarufu miaka michache iliyopita, Lazaro Nyalandu aliondoka CCM na kuhamia Chadema. Binafsi nampongeza.
Kwanza, nampongeza Nyalandu kwa sababu alichofanya hakukifanya kinyume na matakwa ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inayompa haki ya kuamua kuhusu uhuru wake wa kushirikiana na wengine kupitia chama anachokiamini.
Kwa mujibu wa Ibara ya 20(1) ya Katiba, kila mtu anastahili kuwa huru bila ya kuathiri sheria za nchi, kukutana na watu wengine kwa hiari yake na kwa amani, kuchanganyika na kushirikiana na watu wengine, kutoa mawazo hadharani na hasa zaidi, kuanzisha au kujiunga na vyama au mashirika yaliyoanzishwa kwa madhumuni ya kuhifadhi au kuendeleza imani au masilahi yake au masilahi mengineyo.
Nyalandu amefanya kile anachoamini kwamba kuendelea kukaa ndani ya CCM hakumpi nafasi ya ‘kupumua’ atakavyo na hivyo kuitumia haki yake kuondoka mahala anapopaona hapafai kuendelea kupatukuza.
Jambo la pili, Nyalandu si wa kwanza kufanya hivyo. Kuhama vyama kulianza miaka mingi iliyopita pengine kizazi cha wengi wetu hakikuwapo, lakini kupitia historia tunajifunza hata waasisi wa nchi hii waliwahi kufanya hivyo huko nyuma.
Zipo nyakati walizoamua kuvunja vyama vyao na kuanzisha chama kimoja na kuna nyakati walihama kabisa na kuhamia vyama vingine enzi za ukoloni ili kuendeleza mapambano ya ukombozi wa Taifa hili. Hivyo, uhamaji wa vyama haujaanzishwa na Nyalandu.
Hata hivyo, katika miaka ya karibuni tumeshuhudia wanasiasa wakitoka chama kimoja kwenda kingine. Wapo waliotoka CCM wakahamia upinzani, wapo walioondoka upinzani wakarudi au kujiunga na CCM.
Vilevile wapo waliobadilikia huko huko upinzani kwa kutoka chama kimoja cha upinzani kuhamia kingine wakiamini kama alivyoamini Nyalandu kwamba walikokuwa hakuna demokrasia wanayoitaka.
Hizo ndizo siasa na hata Katiba ya nchi ambayo ni sheria mama inaruhusu kufanya hivyo.
Bahati mbaya sana, hii tabia ambayo nadariki kusema ni ya kishamba na iliyopitwa na wakati tusiyotaka kuachana nayo ya kuwaponda watu wanaohama vyama inatufanya kuonekana watu tusiofikiria na kutokuwa na uelewa mpana juu ya siasa.
Kwa muda sasa zimekuwapo kejeli juu ya watu wanaohama vyama, hususana wanaotoka CCM zinazotolewa na ama viongozi au wanachama wao. Kejeli hizo zinakera, zinauma na kuudhi.
Hivi kwa nini mtu anapohama tu ndipo arushiwe ‘makombora’ kuwa anaondoka kwa sababu amekosa uwaziri, ukuu wa mkoa au wa wilaya? Mbona mnapokuwa naye huwa hamumtupii ‘madongo’ ya wizi na kadhalika na mnasubiri hadi ahame? Huu ndio ushamba wa kisiasa ninaosema.
Jirani zetu Wakenya kuhama chama ni suala la kawaida. Ni kawaida kumuona mtu anakuwa Kanu asubuhi, lakini anapokwenda kula mlo wa mchana anakuwa mwanachama mpya wa Narc na hakuna kiongozi au mwanachama wa Kanu anayesimama kumshutumu au kumkejeli. Hizo ndizo siasa za kisasa.
Kabla ya Uchaguzi Mkuu uliofanyika Agosti 8, Wakenya wengi walihama vyama vyao, wapo pia walioamua kujiunga na miungano ambayo waliona itakuwa na manufaa kwao lakini vilevile kuna makundi ya watu walioamua kujiweka kando na siasa.
Hapa kwetu tunaamini mtu akiwa CCM basi awe mwanachama wa maisha hata kama haridhishi na hali ya chama hicho. Tunashindwa kujifunza kutoka katika nchi za wenzetu kuwa siasa sio uadui, bali ni utaratibu wa maisha ambao mtu anaamua kuufuata.
Ndio maana mtu anaweza kuwa katika chama hiki na baada ya muda akahamia chama kingine.
Februari 16, 2015 Rais wa mstaafu wa Nigeria, Olusegun Obasanjo alichana kabisa kadi ya chama chake kilichokuwa kikitawala nchi hiyo cha Peoples Democratic (PDP) na kutangaza kuachana na siasa akiorodhesha udhaifu mwingi ambao aliamini ulikuwa ‘umekimeza’ chama hicho.
Obasanjo alisema chama hicho kilikuwa kimeshindwa kukabiliana na ukosefu wa usalama, ajira, mfumuko wa bei na ufisadi na hivyo asingependa kuwa mmoja wa watu wanaonyoshewa kidole kwa wananchi. Hata hivyo chama chake kilitoa tamko la kumtakia maisha mema nje ya PDP.
Ni vyema tuache siasa za kishamba na ulimbukeni wa kuamini kwamba kila mtu uliye naye ama unayeishi naye anapaswa kuridhika na mtazamo wako, wengine hawaupendi na ndiyo hao wanaotafuta mahala wanapoamini kwamba patawafaa ‘kupumulia’.

Wanafunzi wote wenye sifa kupewa mikopo chuo kikuu



Meneja Mawasiliano wa bodi hiyo, Omega Ngole.
Meneja Mawasiliano wa bodi hiyo, Omega Ngole. 
Bodi ya Mikopo ya Elimu ya juu nchini (HESLB) imewatoa hofu wanafunzi waliokosa mikopo kwakuwa ipo katika hatua za mwisho kutoa majina ya awamu ya tatu.
Kauli hiyo imekuja ikiwa leo   ni siku ya mwisho iliyotolewa na Naibu Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia William Ole Nasha ya kuitaka bodi hiyo kuhakikisha kila mwanafunzi mwenye sifa anapewa mkopo.
Akizungumza na gazeti hili leo Novemba 3,Meneja Mawasiliano wa bodi hiyo, Omega Ngole amesema agizo hilo linaendelea kutekelezwa na kwamba hadi kufikia kesho  kila mwanafunzi mwenye sifa atapata mkopo.
Amesema kwa wale watakaokosa mkopo wanaweza kukata rufaa kupitia bodi hiyo ili kupitia upya taarifa zao.
“Maelekezo hayo yote yanatekelezwa na tutakamilisha leo na tutatoa taarifa ya kuhusu utekelezaji wake wiki ijayo,” amesema
Katika mwaka wa masomo wa 2017/18 Serikali imetenga bajeti ya Sh427 bilioni kwaajili ya mikopo ambapo wanafunzi 30,000 wa mwaka wa kwanza watanufaika na fungu hilo.
Hadi sasa Jumla ya wanafunzi 21,677 maombi yao yamekubaliwa ikiwa ni awamu mbili zilizotolewa na bodi hiyo ambapo awamu ya kwanza ilitoa majina 10,196 na ya pili 11,481.
Meneja huyo amesema kwa wale waliodahiliwa kwenye vyuo walivyothibitisha kupitia Tume ya Vyuo Vikuu (TCU) tayari fedha zimeanza kutumwa kwenye vyuo husika.
“Mwanafunzi akipangiwa mkopo halafu asipoliridhika, akaona uhitaji wake ni mkubwa kuliko kiwango alichokipata kuna nafasi ya kukata rufaa ambayo itaanza wiki ijayo,”amesema.
Baadhi ya wanafunzi waliozungumza na gazeti hili walieleza kuwa hatua ya kuchelewa kwa majina imeibua wasiwasi huku wakikosa kufanya udahili kwa muda uliopangwa.
Mwanafunzi Athuman Mohamed, aliyechaguliwa kujiunga na Chuo Kikuu cha Dar es Saalam ,alisema ameanza kukata tamaa baada ya jina lake kutooneka kwenye awamu zote mbili huku mzazi akieleza hana uwezo wa kugharamia.
“Mimi mpaka muda huu nimekata  tama mchana huu nimewasiliana na mzazi kaniambia uwezo huo yeye hana,”
 “Kwa sasa nasubiri awamu ya tatu nione kama ntapata kama nikikosa ntaangalia kama naweza kuandika barua ya kuahirisha mwaka au niache moja kwa moja,”amesema
Naye, Ebrania Sanga alisema ameshindwa kufanya udahili kutokana na kutegemea mkopo wa bodi.
“Sina uwezo kabisa hatma yangu ipo kwenye mkopo hapa nilikuja na nauli tu na ndiyo kwanza inamalizika kesho nikishindwa kusoma basi nitafanya shughili nyingine,”amesema
Wakati wanafunzi hao wakilalama kukosa mikopo, Justine Joshua (Udsm) alisema bado ana matumaini kwani hata akikosa mkopo wa bodi ataomba kwenye taasisi ya Msaada wa Kijamii (TSSF).
Taasisi hiyo imewataka wanafunzi waliokosa mkopo kwa mwaka wa masomo 2017/18 kutuma maombi kwaajili ya kupata ufadhili.
Hatahivyo bodi hiyo imesema licha ya kuendelea na mchakato huo kuna baadhi ya wanafunzi wamekosa sifa kutokana na uzembe ikiwamo kutojaza taarifa sahihi.
“Mwanafunzi asibaki pembeni akisema nina asifa wakati maombi ya mkopo yenyewe hayajielezi wala hayajaambatanisha,”amesema Meneja huyo.

Mjane aliyedai kudhulumiwa ardhi apewa ulinzi


Mwanza. Jeshi la Polisi Mkoa wa Mwanza limetekeleza agizo la Rais John Magufuli kwa kumpatia ulinzi Ana-Joyce Francis, mjane mwenye watoto sita, aliyeangua kilio mbele ya Rais John Magufuli akilalamikia kuporwa ardhi.
Mjane huyo alimtajana mwanasheria Alex Bantulaki kwamba ndiye aliyemdhulumu ardhi yake huku akiachwa anataabika na familia yake asijue lakufanya.
Kaimu Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza, Faustine Shilogile ameiambia Mwananchi ofisini kwake leo Novemba 3, kwamba agizo hilo limetekelezwa, ingawa hakua tayari kufafanua aina ya ulinzi aliopewa mjane huyo, mkazi wa eneo la Isamilo, jijini Mwanza.
“Kwa sababu za kiusalama, siwezi kuweka wazi ni aina gani ya ulinzi tumempatia; isitoshe tu kusema kuwa agizo la Rais limetekelezwa,” amesema Shilogile
Oktoba 30, mjane huyo, akiwa na lundo la nyaraka alizozifungia kwenye kanga yake, alijipenyeza na kufanikiwa kufikia macho ya Rais Magufuli wakati wa mkutano wa hadhara uliofanyika eneo la Nyakato jijini Mwanza.
Baada ya kuitwa mbele na Rais Magufuli, mjane huyo, huku akimwaga machozi, amesema  kuna njama za kumpora kiwanja chake alichokinunua tangu mwaka 2005.
Baada ya kusikiliza malalamiko hayo, Rais akauagiza uongozi wa Serikali Mkoa, jiji la Mwanza na Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi kushughulikia suala hilo kwa kuitisha na kupitia nyaraka za pande zote mbili na kumpatia taarifa.
Licha ya kumkabidhi mjane huyo fedha taslimu ambayo kiasi chake hakikujulikana, Rais Magufuli pia aliagiza apewe ulinzi ili asibughudhiwe na yeyote wakati suala lake likishughulikiwa.

Wanafunzi watakiwa wasijiingize kwenye siasa



Profesa Shadrack Mwakalila
Profesa Shadrack Mwakalila 
Dar es Salaam. Mkuu wa Chuo Kikuu cha Kumbukumbu ya Mwalimu Nyerere, Profesa Shadrack Mwakalila amewataka wanafunzi wa chuo hicho wasitumiwe na wanasiasa bali wajikite kwenye masuala yao ya kitaaluma.
Profesa Mwakalila amesema hayo leo Novemba 3 wakati alipozungumza na wanafunzi waliojiunga na chuo hicho mwaka huu ikiwa ni kuwakaribisha na kuwapatia maelekezo na taratibu za chuo.
Amesema kipindi hiki siyo cha kujihusisha wala kukubali kutumika na wanasiasa kwani ndoto zao zinaweza kuishia njiani na kupoteza dira.
“Sisi hatuwaruhusu wanafunzi wetu kujihusisha na masuala ya kisiasa au kutumika kwani tunaona vyuo vingine vinavyokumbwa na mambo kama hayo kwetu ikibainika sheria kali zitachukuliwa dhidi ya mwanafunzi atakaye husika,”amesema Profesa Mwakalila.
Amesema ikiwa baadhi ya vyuo wanafunzi wake kujihusisha na masuala ya siasa inasababisha migomo na maandamano yasiyo na tija wakati wa kudai haki zao.
Profesa Mwakalila amebainisha kwamba katika chuo hicho kuna utaratibu maalumu kwa wanafunzi kuwasililisha hoja zao kupitia serikali ya wanafunzi ambayo inaingia moja kwa moja katika maamuzi ya bodi na taasisi kwa ujumla.
“Kama kuna malalamiko yeyote taasisi yetu imejikita katika kutafutia ufumbuzi na kushirikiana moja kwa moja na Serikali  ya wanafunzi katika kutolea ufafanuzi,”amesema Profesa Mwakalila.
Mbali na hilo mkuu huyo alibainisha changamoto iliyopo ya ni  nyumba za kulala  wanafunzi ambao wengi wao wanaishi nje na wanapendelea kuishi  ndani ya chuo hicho lakini  kuna utaratibu ambao wameweka kama chuo.

“Mabweni tuliyonayo ni machache kuna ambayo yanamilikiwa na watu binafsi kwa makubaliano ya kuweka bei elekezi kwa wanafunzi na miundombinu ambayo inaridhisha,”amesema Profesa Mwakalila.
Profesa Mwakalila amewatoa  hofu wanafunzi wa ngazi mbalimbali kuanzia Astashahada, stashahada na shahada kuwa na amani na utulivu na watapatiwa elimu ambayo itakuwa na tija katika soko la ajira na kujenga uchumi wa taifa.
Mmoja wa wanafunzi waliojiunga na chuo hicho mwaka huu Stela Martin amesema anafurahi kupata nafasi ndani ya chuo hicho na kwamba maelekezo waliyoyapata yatawasaidia kuwajenga na kuwaandaa kuwa viongozi hodari.

Lungu awaonya majaji Zambia wasiige majaji wa Kenya

Edgar LunguHaki miliki ya pichaAFP
Image captionRais Edgar Lungu
Rais wa Zambia Edgar Lungu amewatahadharisha majaji nchini humo kwamba kutazuka vurugu nchini humo iwapo watathubutu kumzuia kuwania katika uchaguzi wa urais wa mwaka 2021.
Amesema hawafai "kuwaiga" majaji wa Kenya ambao walitumbukiza nchi hiyo kwenye mzozo baada ya kufuta matokeo ya uchaguzi wa urais uliofanyika Agosti ambapo Rais Kenyatta alikuwa ametangazwa kuwa mshindi.
Bw Kenyatta Jumatatu alitangazwa mshindi wa uchaguzi wa marudio uliofanyika Alhamisi wiki iliyopita baada ya kiongozi wa upinzani Raila Odinga kususia.
Kumezuka mjadala kuhusu iwapo Lungu anafaa kuwania au la, huku wakosoaji wake wakisema kwamba anahudumu muhula wa pili na hivyo hawezi kuwania tena.
Wanasema kipindi ambacho alihudumu baada ya kifo cha Rais Michael Sata mwaka 2014 kinafaa kuhesabiwa kama muhula wa kwanza.
Wafuasi wa Lungu wanasisitiza kwamba alimaliza tu muhula wa mtangulizi wake na kwamba muhula wake wa wkanza ulianza aliposhinda uchaguzi wa 2016, ambao ulikumbwa na utata.
Rais anaruhusiwa kuhudumu kwa mihula miwili pekee kwa mujibu wa katiba nchini humo.
Akiwahutubia wafuasi wake kaskazini magharibi mwa nchi hiyo, Bw Lungu amesema:
"Kwa wenzangu katika idara ya mahakama, ujumbe wangu kweni ni kwamba mfanye kazi yenu, mfasiri sheria bila woga au kupendelea upande wowote na mzingatie maslahi ya nchi. Msiwe watu wa kuiga na mfikirie kwamba mtakuwa mashujaa iwapo mtatumbukiza nchi hii kwenye vurugu.
Ningependa kumalizika kwa kusema kwamba wale watu ambao hawapendi amani na uhuru watasema kwamba Rais Lungu anatoa vitisho kwa mahakama za kisheria. Mimi sitoi vitisho kwa mahakama. Ninawatahadharisha tu kwa sababu nina habari kwamba baadhi yenu huenda mkapenda kujaribu mambo. Majaribio hayo yenu yasituingize kwenye fujo, tafadhali.
Watu wanasema kwamba mahakama za Zambia zinafaa kufuata mfano wa mahakama za Kenya...Watu wanasema mahakama za Zambia zinafaa kwua na ujasiri na kufanya maamuzi ambayo yanazingatia maslahi ya raia, lakini hebu tazameni yanayotokea Kenya sasa.
Mimi ninasema mahakama za Zambia zinafaa kutazama yanayotokea. Hazifai kuchukua hatua kana kwamba majaji hao si sehemu ya bara letu la Afrika. Jambo muhimu zaidi ninaweza kusema sasa ni kwamba, 2021, nipo na nitawania iwapo chama changu kitanichagua."
Mahakama ya Juu nchini Kenya ilisifiwa sana kwa kufanya uamuzi wa 'kijasiri' kufuta matokeo ya uchaguzi huo.
Jaji wa makama ya juu David Maraga na wenzake watatu wameweka historia kwa kubatilisha uchaguzi wa urais wa mwezi AgostiHaki miliki ya pichaEPA
Image captionJaji wa Makama ya Juu Kenya David Maraga na wenzake watatu waliweka historia kwa kubatilisha uchaguzi wa urais wa mwezi Agosti
Majaji wanne wa mahakama hiyo waliunga mkono uamuzi huo ingawa wawili waliupinga.
Siku moja kabla ya uchaguzi wa marudio hata hivyo, mahakama hiyo ya juu ilishindwa kusikiliza kesi ambayo ilihusu kuahirishwa kwa uchaguzi huo baada ya kukosekana kwa majaji wa kutosha mahakamani.
Ni Jaji Mkuu David Maraga na Jaji Isaac Lenaola pekee waliofika kortini.
Kikao cha mahakama hiyo huhitajika kuwa na angalau majaji watano kwa mujibu wa Katiba.