Kauli hiyo imekuja ikiwa leo ni siku ya mwisho iliyotolewa na Naibu Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia William Ole Nasha ya kuitaka bodi hiyo kuhakikisha kila mwanafunzi mwenye sifa anapewa mkopo.
Akizungumza na gazeti hili leo Novemba 3,Meneja Mawasiliano wa bodi hiyo, Omega Ngole amesema agizo hilo linaendelea kutekelezwa na kwamba hadi kufikia kesho kila mwanafunzi mwenye sifa atapata mkopo.
Amesema kwa wale watakaokosa mkopo wanaweza kukata rufaa kupitia bodi hiyo ili kupitia upya taarifa zao.
“Maelekezo hayo yote yanatekelezwa na tutakamilisha leo na tutatoa taarifa ya kuhusu utekelezaji wake wiki ijayo,” amesema
Katika mwaka wa masomo wa 2017/18 Serikali imetenga bajeti ya Sh427 bilioni kwaajili ya mikopo ambapo wanafunzi 30,000 wa mwaka wa kwanza watanufaika na fungu hilo.
Hadi sasa Jumla ya wanafunzi 21,677 maombi yao yamekubaliwa ikiwa ni awamu mbili zilizotolewa na bodi hiyo ambapo awamu ya kwanza ilitoa majina 10,196 na ya pili 11,481.
Meneja huyo amesema kwa wale waliodahiliwa kwenye vyuo walivyothibitisha kupitia Tume ya Vyuo Vikuu (TCU) tayari fedha zimeanza kutumwa kwenye vyuo husika.
“Mwanafunzi akipangiwa mkopo halafu asipoliridhika, akaona uhitaji wake ni mkubwa kuliko kiwango alichokipata kuna nafasi ya kukata rufaa ambayo itaanza wiki ijayo,”amesema.
Baadhi ya wanafunzi waliozungumza na gazeti hili walieleza kuwa hatua ya kuchelewa kwa majina imeibua wasiwasi huku wakikosa kufanya udahili kwa muda uliopangwa.
Mwanafunzi Athuman Mohamed, aliyechaguliwa kujiunga na Chuo Kikuu cha Dar es Saalam ,alisema ameanza kukata tamaa baada ya jina lake kutooneka kwenye awamu zote mbili huku mzazi akieleza hana uwezo wa kugharamia.
“Mimi mpaka muda huu nimekata tama mchana huu nimewasiliana na mzazi kaniambia uwezo huo yeye hana,”
“Kwa sasa nasubiri awamu ya tatu nione kama ntapata kama nikikosa ntaangalia kama naweza kuandika barua ya kuahirisha mwaka au niache moja kwa moja,”amesema
Naye, Ebrania Sanga alisema ameshindwa kufanya udahili kutokana na kutegemea mkopo wa bodi.
“Sina uwezo kabisa hatma yangu ipo kwenye mkopo hapa nilikuja na nauli tu na ndiyo kwanza inamalizika kesho nikishindwa kusoma basi nitafanya shughili nyingine,”amesema
Wakati wanafunzi hao wakilalama kukosa mikopo, Justine Joshua (Udsm) alisema bado ana matumaini kwani hata akikosa mkopo wa bodi ataomba kwenye taasisi ya Msaada wa Kijamii (TSSF).
Taasisi hiyo imewataka wanafunzi waliokosa mkopo kwa mwaka wa masomo 2017/18 kutuma maombi kwaajili ya kupata ufadhili.
Hatahivyo bodi hiyo imesema licha ya kuendelea na mchakato huo kuna baadhi ya wanafunzi wamekosa sifa kutokana na uzembe ikiwamo kutojaza taarifa sahihi.
“Mwanafunzi asibaki pembeni akisema nina asifa wakati maombi ya mkopo yenyewe hayajielezi wala hayajaambatanisha,”amesema Meneja huyo.
No comments:
Post a Comment