Friday, November 3

Acheni tabia ya kuwasimanga wanaohama vyama vyenu vya siasa



Kulwa Magwa
Kulwa Magwa 
Kuna mambo unapoyafikiria yanakera na yanahitaji majibu ya papo kwa hapo na ndicho ambacho nakijadili hapa. Wiki hii mmoja wa wanasiasa waliojipatia umaarufu miaka michache iliyopita, Lazaro Nyalandu aliondoka CCM na kuhamia Chadema. Binafsi nampongeza.
Kwanza, nampongeza Nyalandu kwa sababu alichofanya hakukifanya kinyume na matakwa ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inayompa haki ya kuamua kuhusu uhuru wake wa kushirikiana na wengine kupitia chama anachokiamini.
Kwa mujibu wa Ibara ya 20(1) ya Katiba, kila mtu anastahili kuwa huru bila ya kuathiri sheria za nchi, kukutana na watu wengine kwa hiari yake na kwa amani, kuchanganyika na kushirikiana na watu wengine, kutoa mawazo hadharani na hasa zaidi, kuanzisha au kujiunga na vyama au mashirika yaliyoanzishwa kwa madhumuni ya kuhifadhi au kuendeleza imani au masilahi yake au masilahi mengineyo.
Nyalandu amefanya kile anachoamini kwamba kuendelea kukaa ndani ya CCM hakumpi nafasi ya ‘kupumua’ atakavyo na hivyo kuitumia haki yake kuondoka mahala anapopaona hapafai kuendelea kupatukuza.
Jambo la pili, Nyalandu si wa kwanza kufanya hivyo. Kuhama vyama kulianza miaka mingi iliyopita pengine kizazi cha wengi wetu hakikuwapo, lakini kupitia historia tunajifunza hata waasisi wa nchi hii waliwahi kufanya hivyo huko nyuma.
Zipo nyakati walizoamua kuvunja vyama vyao na kuanzisha chama kimoja na kuna nyakati walihama kabisa na kuhamia vyama vingine enzi za ukoloni ili kuendeleza mapambano ya ukombozi wa Taifa hili. Hivyo, uhamaji wa vyama haujaanzishwa na Nyalandu.
Hata hivyo, katika miaka ya karibuni tumeshuhudia wanasiasa wakitoka chama kimoja kwenda kingine. Wapo waliotoka CCM wakahamia upinzani, wapo walioondoka upinzani wakarudi au kujiunga na CCM.
Vilevile wapo waliobadilikia huko huko upinzani kwa kutoka chama kimoja cha upinzani kuhamia kingine wakiamini kama alivyoamini Nyalandu kwamba walikokuwa hakuna demokrasia wanayoitaka.
Hizo ndizo siasa na hata Katiba ya nchi ambayo ni sheria mama inaruhusu kufanya hivyo.
Bahati mbaya sana, hii tabia ambayo nadariki kusema ni ya kishamba na iliyopitwa na wakati tusiyotaka kuachana nayo ya kuwaponda watu wanaohama vyama inatufanya kuonekana watu tusiofikiria na kutokuwa na uelewa mpana juu ya siasa.
Kwa muda sasa zimekuwapo kejeli juu ya watu wanaohama vyama, hususana wanaotoka CCM zinazotolewa na ama viongozi au wanachama wao. Kejeli hizo zinakera, zinauma na kuudhi.
Hivi kwa nini mtu anapohama tu ndipo arushiwe ‘makombora’ kuwa anaondoka kwa sababu amekosa uwaziri, ukuu wa mkoa au wa wilaya? Mbona mnapokuwa naye huwa hamumtupii ‘madongo’ ya wizi na kadhalika na mnasubiri hadi ahame? Huu ndio ushamba wa kisiasa ninaosema.
Jirani zetu Wakenya kuhama chama ni suala la kawaida. Ni kawaida kumuona mtu anakuwa Kanu asubuhi, lakini anapokwenda kula mlo wa mchana anakuwa mwanachama mpya wa Narc na hakuna kiongozi au mwanachama wa Kanu anayesimama kumshutumu au kumkejeli. Hizo ndizo siasa za kisasa.
Kabla ya Uchaguzi Mkuu uliofanyika Agosti 8, Wakenya wengi walihama vyama vyao, wapo pia walioamua kujiunga na miungano ambayo waliona itakuwa na manufaa kwao lakini vilevile kuna makundi ya watu walioamua kujiweka kando na siasa.
Hapa kwetu tunaamini mtu akiwa CCM basi awe mwanachama wa maisha hata kama haridhishi na hali ya chama hicho. Tunashindwa kujifunza kutoka katika nchi za wenzetu kuwa siasa sio uadui, bali ni utaratibu wa maisha ambao mtu anaamua kuufuata.
Ndio maana mtu anaweza kuwa katika chama hiki na baada ya muda akahamia chama kingine.
Februari 16, 2015 Rais wa mstaafu wa Nigeria, Olusegun Obasanjo alichana kabisa kadi ya chama chake kilichokuwa kikitawala nchi hiyo cha Peoples Democratic (PDP) na kutangaza kuachana na siasa akiorodhesha udhaifu mwingi ambao aliamini ulikuwa ‘umekimeza’ chama hicho.
Obasanjo alisema chama hicho kilikuwa kimeshindwa kukabiliana na ukosefu wa usalama, ajira, mfumuko wa bei na ufisadi na hivyo asingependa kuwa mmoja wa watu wanaonyoshewa kidole kwa wananchi. Hata hivyo chama chake kilitoa tamko la kumtakia maisha mema nje ya PDP.
Ni vyema tuache siasa za kishamba na ulimbukeni wa kuamini kwamba kila mtu uliye naye ama unayeishi naye anapaswa kuridhika na mtazamo wako, wengine hawaupendi na ndiyo hao wanaotafuta mahala wanapoamini kwamba patawafaa ‘kupumulia’.

No comments:

Post a Comment