Friday, November 3

Kuchoma vifaranga ni kukomoa au adhabu?


Mjadala mzito umeibuka tangu vifaranga 6,400 vilivyodaiwa kuingizwa nchini kinyume cha sheria, vilivyopochomwa moto Namanga mkoani Arusha.
Vifaranga hivyo, mali ya Mary Matia na vyenye thamani ya Sh12.5 milioni, vilikamatwa kwenye mpaka mjini Namanga, ambako ni mpaka wa Tanzania na Kenya.
Hatutetei uvunjwaji wa sheria wala kitendo chochote kinachokwenda kinyume na taratibu tulizojiwekea kama nchi, lakini, tunaamini busara ingeweza kutumika katika kushughulikia kadhia hiyo.
Tangu habari hii ianze kusambaa, baadhi ya wadau na watetezi wa haki za wanyama wamekuwa wakitoa maoni yao kuhusu hatua stahiki ambayo ilipaswa kuchukuliwa na mamlaka husika.
Kwa walio wengi, busara kuu ingekuwa kumuamuru mmiliki kuvirudisha vifaranga hivyo alikovitoa.
Kuwarudisha vifaranga hao walikotoka, si jambo geni. Mathalani, mara kadhaa tumeshuhudia mifugo hususan ng’ombe inayokamatwa kwa kuingizwa kiholela nchini, ama ikitaifishwa na vyombo vya dola au ikirudishwa ilikotoka.
Inasikitisha kuwa wahusika katika uchomaji wa vifaranga hivi hawakulitazama suala hili kwa upande mwingine, hasa wa ukatili dhidi ya viumbe hai.
Tukikopa maneno ya mkurugenzi mtendaji wa Shirika la Ustawi wa Wanyama Tanzania (Taweso), busara nyingine ingekuwa kuwapima vifaranga hao na kama ingebainika kutokuwa na maambukizi, mamlaka husika zingevitaifisha na hata kuvigawa kwa wajasiriamali, magereza au vituo vya watoto yatima.
Inawezekana wahusika wana hoja nzito tena za kisheria zilizowasukuma kuteketeza vifaranga hivyo, lakini hawakuona haja ya kutafuta njia mbadala zaidi ya kuvichoma, njia ambayo unadhani ni ya kikatili.
Katika sakata hili, utu ungeweza kuchukua nafasi zaidi, huku wahusika wakitekeleza sheria na taratibu zilizopo. Tujifunze kutoka kwa mahakimu na majaji ambao wakati fulani hutoa uamuzi kwa kutumia busara hasa baada ya kusoma mazingira ya tukio.
Walioshiriki kuteketeza vifaranga hivi, wangeweza kutumia njia nyingine kama ya kumtia adabu mmiliki wa mzigo huo. Kinachogusa hisia za wengi ni kuwa mmiliki huyo alishakuwa tayari kuwarudisha alikowatoa.
Kwa maneno mengine, alishakubali kupata hasara, jambo ambalo lingeweza kuwa funzo kwake kuwa anapaswa kutii sheria na taratibu za nchi.
Hatudhani kama sheria, taratibu na hata adhabu tunazojiwekea nchini zinalenga kukomoa, bali kutoa fundisho ili kosa kama hilo lisitokee tena.
Wakati ni wajibu kwa kila raia kufuata taratibu na sheria, mamlaka nazo zinawajibika kuwa mstari wa mbele kutoa elimu kwa umma ili kupunguza vitendo vya ukiukwaji wa sheria.
Hivi ndivyo inavyopaswa kufanywa sio tu na vyombo vinavyosimamia masuala ya ufugaji, lakini pia vyombo vya usalama barabarani, usimamizi wa kodi na vinginevyo nchini.
Tujitahidi kuepuka kuwa Taifa linaloamini katika adhabu hasa zenye mrengo wa kukomoa badala ya kufundisha. Ndio maana kiunatakiwa kuwepo uchunguzi wa mazingira ya kosa kama ni makusudi au kwa kutojua.
Baadhi ya makosa hufanywa si kwa nia mbaya bali kwa kutojua au kukosea. Haya yanaweza kushughulikiwa kwa kuangalia njia mbadala ambayo ni ya kielimu zaidi kwa manufaa ya baadaye.

No comments:

Post a Comment