Saturday, March 19

Wakuu 21 wa wilaya kwenye chekeche

Baada ya kufanya uteuzi wa wakuu wa mikoa uliowaondoa makada 12, homa ya chekeche la Rais John Magufuli sasa linahamia kwa wakuu wa wilaya, ambao baadhi wameshaanza kuaga wakisema hawana uhakika wa kuendelea kushika nafasi zao.
Hali hiyo inatokana na Rais kuweka bayana vigezo atakavyotumia kufanya uteuzi wa wakuu hao wa wilaya ambavyo ni pamoja na suala la migogoro ya ardhi, tatizo la elimu hasa upungufu wa madawati, njaa na mlipuko wa ugonjwa wa kipindupindu.
“Nikisikia wilaya inaomba chakula wakati mvua zinanyesha wakati huu, nitakuwa na shaka na viongozi waliopo. Wanashindwaje kuhamasisha kilimo?” alihoji Rais.
Vigezo hivyo alivitangaza wakati akizungumza na wazee wa Jiji la Dar es Salaam, lakini katika uteuzi wa wakuu wa mikoa alizungumzia pia suala la wafanyakazi hewa ambao wamekuwa wakilipwa mishahara bila ya wahusika kuchukua hatua kudhibiti.
Kwa maana hiyo, vigezo vya Dk Magufuli vinaweza kuwa vingi zaidi kulingana na matatizo ya eneo la wilaya, hasa baada ya mkuu huyo wa nchi kuamua kutumia vijana wake kwenda kuchunguza matatizo kwenye maeneo ambayo anataka kusimika uongozi.
Suala la udhibiti wa fedha za umma, hasa mishahara ya wafanyakazi hewa, linaweza kuwa kigezo kikubwa cha Dk Magufuli hasa kutokana na tatizo hilo kuzungumzwa kwa muda mrefu bila ya kutafutiwa ufumbuzi na udhibiti wa mapato kuwa moja ya ajenda kubwa za Serikali ya Awamu ya Tano.
Kwa mujibu wa uchunguzi ambao Mwananchi imeufanya kwenye baadhi ya mikoa, chekeche hilo la Rais linawaweka kwenye hali ngumu wakuu wa wilaya 21 iwapo watabainika hawajachukua hatua madhubuti za kukabiliana na matatizo hayo manne.
Suala la njaa litakuwa limewagusa viongozi wa Wilaya ya Isimani mkoani Iringa, Chamwino (Dodoma) na Rorya (Mara) pamoja na Kilindi mkoani wa Tanga ambako kuliripotiwa baa la njaa.
Akizungumza katika mkutano ulioandaliwa na wazee mkoani Dar es Salaam Februari 15, Rais Magufuli aliitoa mfano wa Wilaya ya Bariadi iliyopo Mkoa wa Simiyu, akisema imejenga kilomita 4.5 za barabara ya lami kwa Sh9.2 bilioni, fedha ambazo zingetosha kujenga kilomita 22 mpaka 23 za lami.
“Viongozi wao wapo, mkuu wa mkoa yupo, mkuu wa wilaya yupo, mkurugenzi wa manispaa yupo, injinia yupo! Kwa hiyo, ninapozungumza kutumbua majipu, mniunge mkono nitumbue kwelikweli,” alisema.
Mkuu wa wilaya hiyo, Ponsiano Nyami, ambaye aliwahi kumuomba Rais wa Serikali ya Awamu ya Nne, Jakaya Kikwete atengue uteuzi wake kwa kushindwa kushughulikia kikamilifu ujenzi wa maabara, atakuwa akiangalia mlango wa kutokea.
Siku chache zilizopita alitoa kauli iliyoonekana kama anaaga baada ya kusema kwenye mkutano kuwa hakuna mwenye uhakika wa kubaki kwenye nafasi hizo.
Migogoro ya ardhi isiyokwisha mkoani Morogoro, hasa Wilaya ya Mvomero ambayo ilisababisha Dk Rajab Rutengwe avuliwe ukuu wa mkoa, itamuweka kwenye hali mbaya mkuu wa wilaya hiyo, Betty Mkwasa baada ya mapigano kutokea mara mbili tangu Serikali ya Awamu ya Tano iingie madarakani Novemba mwaka jana.
Hivi karibuni, zaidi ya mbuzi na kondoo 38 waliuawa kutokana na migogoro ya wakulima na wafugaji. Hii ilitokea wiki chache baada ya mtu mmoja kuuawa sawia na ng’ombe zaidi ya 71.
Wakati mapigano yalipotokea Desemba, Mkwasa alisema mapigano hayo yamekuja wakati Serikali ya wilaya ikijipanga kufanya operesheni ya kuwaondoa wafugaji wavamizi kwa kuwa asilimia kubwa kijiji hicho ni wakulima.
Mkwasa alisema mifugo inayoingia ni ile inayoondolewa katika Hifadhi ya Wami Mbiki na mingine inayotokea wilaya za Handeni na Kilindi za mkoani Tanga na Manyara, hivyo imekuwa ikiingia katika vijiji vya wakulima na kusababisha migogoro.
Migogoro ya ardhi pia iko wilayani Nyamagana ambako Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi, William Lukuvi aliunda kamati ya ushauri kuhusu kuhusika kwa maofisa ardhi kwenye migogoro hiyo.
Kutokana na wafanyakazi wa halmashauri kuwa chanzo cha migogoro ya ardhi Nyamagana, tayari Waziri Lukuvi amesimamisha kazi wafanyakazi mara mbili baada ya kupelekewa malalamiko na wananchi.
Mkuu wa wilaya aaga watumishi
Suala la elimu ambalo lilimfanya Paul Makonda kupanda cheo kutoka mkuu wa wilaya hadi mkoa, litakuwa mwiba mchungu kwa mkuu wa Wilaya ya Nyamagana ambayo ina upungufu wa madawati 16,558 katika shule zake 153 za msingi na sekondari.
Mkuu wa wilaya hiyo, Baraka Konisaga jana alitumia mkutano wa kujitambulisha kwa mkuu mpya wa Mkoa wa Mwanza, kuaga watumishi wa Serikali akisema anaweza asiwemo kwenye uteuzi mpya.
“Naweza kuongea nanyi hapa muda huu nikiwa mkuu wa wilaya, lakini jioni mkasikia uteuzi wa wakuu wapya wa wilaya. Naweza kuwamo na nikabakishwa hapahapa Nyamagana, nikahamishiwa wilaya nyingine au nisiwemo kabisa kutokana na vigezo kadhaa ikiwamo utendaji na umri.”
Hata hivyo, alijimwagia sifa kuwa kwa kipindi chote alichokuwa mkuu wa wilaya hiyo kwa vipindi vitatu tofauti vya uteuzi, alifanya kazi kubwa kusimamia maendeleo, ulinzi na usalama wa wananchi, huku akikaimu nafasi ya mkuu wa mkoa.
Alipoulizwa mara baada ya kikao hicho kumalizika kwa nini aliamua kuaga, Konisaga alisema: “Ni jambo la kawaidia kuwaandaa kisaikolojia watumishi wenzako iwapo kutatokea mabadiliko yoyote. Hakuna ajabu na wala hii haimaanishi kwamba sijiamini katika utendaji wangu. Najiamini sana na nimetekeleza wajibu wangu kikamilifu.”
Mkoani Tanga, aliyekuwa mkuu wa mkoa huo, Mwantumu Mahiza alisema wakati akimkabidhi rasmi ofisi mbadala wake, Martin Shigela kuwa kwa migogoro ya ardhi kwenye maeneo sugu kama Jiji la Tanga na wilaya za Kilindi na Handeni, kamati iliyoundwa kushughulikia tatizo hilo imeshamaliza kazi na dawa imeshapatikana.
Pamoja na maelezo hayo ya Mwantumu, migogoro ya ardhi ni tatizo kubwa mkoani Tanga na kumekuwa na malalamiko mara kwa mara ya kutokuwa na imani hata na kamati ilivyofanya kazi hiyo ya kutafuta dawa ya migogoro isiyokwisha baina ya wafugaji na wakulima, pia ugomvi wa mipaka ya vijiji mkoa wa Tanga na Manyara.
Ikiwa kitafuatwa kigezo cha  migogoro ya ardhi basi wakuu wa Wilaya za mkoa huo, Abdullah Lutavi (Tanga) Selemani Liwowa (Kilindi ) na Husna Rajab (Handeni) wanaweza kuwa katika hatihati ingawa maeneo yao kwa kipindi hiki yametulia ikilinganishwa na miaka ya nyuma.
Kipindupindu jipu Kyela
Mkoa wa Mbeya, Mkuu wa Wilaya ya Kyela, Thea Ntara yuko kwenye hali ngumu kutokana na tatizo la ugonjwa wa kipindupindu.
Mkurugenzi wa halmashauri hiyo, Clemence Kasongo alisema ugonjwa huo unamnyima usingizi kutokana na kuibuka kwenye mwambao wa Ziwa  Nyasa ambako kuna wagonjwa wengi ambao alisema hutokea Wilaya ya Ludewa.
Kutokana na tatizo hilo kuwa kubwa wilayani Kyela, mwezi uliopita wazee wawili wa kitongoji cha Bulinda waliuawa na wananchi kwa madai kuwa ndiyo wanaosababisha watu waugue kipindupindu kwa njia za kishirikina.
Ugonjwa huo pia uko kwenye wilaya za Musoma Vijijini, Ilala na Mpanda.
Wakuu wa wilaya mbili za mkoani Kilimanjaro wamekalia kuti kavu katika vigezo hivyo.
Wilaya ya Same inakabiliwa na migogoro ya ardhi baina ya wananchi wa jamii ya wafugaji wa Kimasai katika Kijiji cha Ruvu Mferejini na mwekezaji wa kampuni ya IBIS International Ltd.
Tangu mwaka 1988, mmiliki wa IBIS International Ltd ambaye ni raia wa Sweden aliingia mkataba na wananchi wa Kijiji cha Ruvu kabla ya kijiji hicho kugawanyika na kuunda kijiji kingine cha Ruvu Mferejini kwenye shamba lenye ukubwa wa ekari 642.
Pia, Wilaya ya Mwanga inakabiliwa  na mgogoro wa ardhi baina ya wanakijiji cha Jipe na mwekezaji wa kampuni ya kitalii ya Asante Tours kuhusu eneo la ekari 3,000. Migogoro yote hiyo bado haijatatuliwa.
Mkoani Dodoma ukiacha Wilaya ya Chamwino ambayo imekuwa ikabiliwa na njaa, Kongwa kumekuwa na mgogoro wa ardhi wa muda mrefu kati ya wakulima na wafugaji ambao pia umekuwa ukihusisha Wilaya ya Wilaya ya Kiteto na kusababisha mgongano kwa wanasiasa.
Mgogoro wa wakulima na wafugaji katika wilaya hizo mbili umekuwa wa muda mrefu na uliingia kwenye Bunge la Kumi.
Mauaji mengi yamekuwa yakitokea upande wa Kiteto lakini yakihusisha wakazi wa Kongwa, kiasi cha kusababisha mbunge wao, Job Ndugai, ambaye sasa ni Spika wa Bunge, kulalamika bungeni dhidi ya ungozi wa Wilaya ya Kiteto.
Arusha na migogoro ya ardhi
Wilaya tatu za Mkoa wa Arusha; Ngorongoro, Monduli na Arumeru, bado zinakabiliwa na tatizo la migogoro ya ardhi lakini kuna jitihada zinaendelea kuitatua.
Wilaya ya Ngorongoro ambayo mkuu wake ni Hashim Mgandilwa bado ina migogoro ya mipaka ambayo imekuwa ikisababisha mapigano ya jamii ya Wasonjo na Wamasai. Monduli, ambayo mkuu wake ni Francis Miti kulikuwa na migogoro ya ardhi ya mashamba kutokana na maofisa ardhi kugawa ovyo viwanja kwa masilahi yao.
Wilayani Arumeru, hasa eneo la Meru, ambako Mkuu wa Wilaya ni Wilson Nkumbaku kuna migogoro ya ardhi baina ya wamiliki wakubwa na vijiji. Wakuu wa wilaya hizo wameeleza changamoto zote zinaendelea kupatiwa ufumbuzi. Mkuu wa Wilaya ya Ngorongoro, Mngandilwa alisema wilaya yake ni salama baada ya migogoro kupungua, wakati Mkuu wa Wilaya ya Arusha, Fadhili Nkurlu alisema Arusha sasa ni shwari na wananchi wanashiriki mambo ya maendeleo.
Imeandaliwa na Burhani Yakub, Lauden Mwambona, Happiness Tesha, Sharon Sauwa, Ngollo John na Mussa Juma.     

‘Namuunga mkono Mpungwe kuhusu Z’bar’


Dar es Salaam. Ikiwa imebaki siku moja kabla ya Uchaguzi wa Marudio kufanyika Zanzibar, mfanyabiashara maarufu nchini, Hashim Ismail amesema Taifa haliwezi kujidanganya kwamba kila kitu ni shwari visiwani humo.
Alisema hayo jana akiunga mkono kauli ya Balozi Ami Mpungwe aliyoitoa katika mahojiano na gazeti hili wiki hii akisema, Taifa halipaswi kujidanganya kwamba Zanzibar hakuna tatizo. Alisema: “Mtanzania yeyote aliyesoma yale aliyozungumza Ami (Mpungwe) hana budi kumuunga mkono. Pia, mimi nakubaliana naye; kuna shida, hatari kubwa na ufisadi mkubwa wa kisiasa. Na kama alivyosema hatuwezi “ku-pretend everything in the garden is rosy (hatuwezi kujidanganya kwamba kila kitu kilichopo katika bustani ni waridi).
“Lakini kama ilivyo kawaida yetu ya uchwara, woga na kujikomba, yale aliyozungumzia Ami yalienda na gazeti la jana (juzi) na kubaki karatasi tu ya kufungia vitumbua.
“Jambo hili si la ZEC (Tume ya Uchaguzi Zanzibar), CCM na CUF tu, ni suala la haki za binadamu. Linatuhusu sote.”
Mzee Ismail alisema Balozi Mpungwe alipendekeza kurudi kwenye meza ya mazungumzo akisisitiza kwamba ni jambo sahihi kabisa lakini akahoji:
“Uchaguzi unaorudiwa Machi 20 (kesho) chini ya ulinzi mkali wa vyombo vya dola... Unaosusiwa na vyama vingine vya siasa, utakuwa umeshamalizika. Sasa itakuwaje?
Hoja ni kuufuta kwanza kisha turudi katika meza.” Katika mahojiano maalumu na Mwananchi, Mpungwe ambaye ni balozi wa zamani wa Afrika Kusini alihadharisha kuhusu hali ya kisiasa Zanzibar akisema “tusijidanganye kuwa hakuna matatizo” kwenye visiwa hivyo na kutaka ufumbuzi utafutwe kabla haujasababisha madhara.    

Mji Mkongwe; hazina hatarini kupoteza hadhi


Zanzibar ina visiwa viwili vya Unguja na Pemba, ikitambulika duniani kutokana na historia na utamaduni wake wa asili ulioambatana na vivutio mbalimbali. Miongoni mwa mambo hayo ni Mji Mkongwe. Ni mji wa kale ambao mwaka 2000, Shirika la Kimataifa la Elimu, Sayansi na Utamaduni (Unesco) liliamua kuupa hadhi kuwa Eneo la Urithi wa Dunia.
Kama ilivyo kwa miji mengine mikongwe duniani, Mji Mkongwe una utajiri wa historia na vivutio tofauti ukijengeka kwa ramani kwa umbo la sambusa. Ni eneo dogo lenye wastani wa majengo 1,700 ya kila aina. Kuna chochoro (Narrow Street)23, makanisa mawili, misikiti 52, maghorofa 50, varandaa na baraza zenye milango zaidi ya 200 iliyonakishiwa kwa ufundi wa hali ya juu.
Katika Mji Mkongwe kuna jumla ya majengo 1,100 yaliyotambuliwa kuwa yenye thamani kubwa katika utaalamu wa ujenzi, hivyo ni kivutio kikubwa kwa watalii. Kwa mujibu wa takwimu za Kamisheni ya Utalii Zanzibar, zaidi ya asilimia 80 ya wageni wanaotembelea Zanzibar hutembelea maeneo ya Mji Mkongwe. Majengo hayo ni Jumba la Ajabu maarufu Baitil Ajaib (House ofWonder), Old Dispensary, Bandari Kuu,
Mahakama, Hospitali ya Rufani, Ikulu, Hamamu ya Hamamni, Ngome Kongwe Jengo la Tiptip, Kanisa Kuu Katoliki la Minara Miwili na Mkunazini (Soko la Watumwa), Mahekalu ya Wahindu, Jumba la Maparisi na Jamati sita za Mashia.
Mwaka 1830, nyumba za Mji Mkongwe zilijengwa chini ya utawala wa Sultani Sayyid Said, alipohamishia makao makuu yake Zanzibar kutoka Oman.
Licha ya vivutio hivyo vya asili, kuna utamaduni unaombatana na matamasha mbalimbali ambayo hufanyika kila mwaka likiwamo la Nchi za Majahazi na Sauti za Busara, yote ni vivutio kwa watalii na hufanyika Mji Mkongwe.
Hata hivyo, mji huo umeingizwa katika maeneo ya urithi wa dunia ulio hatarini kutoweka kutokana na Serikali kushindwa kufuata vigezo na masharti yaliyowekwa na Unesco lililoupa hadhi hiyo miaka 15 iliyopita.
Mkutano wa Kamati ya Urithi wa Kimataifa uliofanyika Juni 2015 mjini Bonn nchini Ujerumani, umetoa mwaka mmoja kwa State Party kutekeleza baadhi ya mambo yaliyoonekana kuwa na athari kwa Mji Mkongwe wa Zanzibar, iwapo hayatatekelezwa yatauweka Mji Mkongwe katika orodha ya urithi uliopo hatarini (World Heritage in Danger List).
Katibu Mtendaji wa Kamisheni ya Utalii, Saleh Ramadhan Feruz anaona tishio hilo la Unesco siyo tu litaathiri sekta ya utalii Zanzibar, bali Taifa nzima.
“Mji Mkongwe ukitolewa kwenye urithi wa dunia utatuathiri kiuchumi, kwani uchumi wetu unategemea utalii kwa sababu kati ya watalii wote wanaokuja kutembelea Zanzibar, asilimia 85 wanatembelea mji huo,” anasema Feruzi.
Inaelezwa kwamba tangu miaka ya 1970, baadhi ya majengo yamekuwa yakiporomoka ndiyo sababu ya Zanzibar kuiomba dunia iyahifadhi majengo hayo, ikiwamo jengo maarufu la Bait El-ajaib au Jumba la Maajabu.
Kuna changamoto kadhaa zinazoweza kuuweka Mji Mkongwe kwenye orodha ya urithi wa dunia unaotoweka, tayari hatua mbalimbali zimeanza kuchukuliwa ili kuuhifadhi usiondolewe kwenye orodha hiyo.
Tatizo linalouweka Mji Mkongwe hatarini ni kutofuata taratibu zilizowekwa na Unesco na kuacha magari makubwa yenye uzito usiostahiki kupita eneo hilo, kwa mujibu wa utafiti uliofanywa na Mamlaka ya Mji Mkongwe, huingia magari 17,000 kwa siku yenye uzito tofauti wakati inatakiwa magari yasiyozidi uzito wa tani mbili.
Dosari nyingine ni ujenzi holela wa hoteli za kitalii ulioongezeka bila ya kuzingatia masharti ya Mji Mkongwe, jambo ambalo hutia doa urithi huo wa dunia.
Sheha wa Mji Mkongwe, Mohammed Juma Mugheiry anasema suala la kujengwa hoteli kubwa ndani ya mji huo ni jambo lisilokubalika.
“Ujenzi wa hoteli kubwa za kitalii ni hatari kwa mji wetu, ndiyo sababu ya Zanzibar kupewa onyo la kuwekwa kwenye miji hatari, kwani huwezi kuwa na hoteli kubwa kama hizi na usihitaji huduma ambazo zitachangia kuongeza magari yenye uzito wa tani kubwa kuingia Mji Mkongwe,” anasema Mugheiry.
Tatizo jingine ni watendaji wa Serikali kushindwa kuchukuwa hatua kwa makosa mbalimbali ya utendaji yanayofanywa.
“Sijui tunaogopa nini kuwachukulia hatua wale watendaji wenye kukaidi masharti hayo?” anahoji.Katika mkutano wake wa Julai mwaka jana nchini Ujerumani, Unesco ilitoa mwaka mmoja kwa Zanzibar kurekebisha kasoro zinazoonekana, ikiwamo ujenzi holela na uingizwaji magari mazito ili kuhifadhi mji huo.
Mwanahistoria na mkazi wa Mji Mkongwe, Profesa Abdul Shareef anasema hofu yake ni kutolewa kwa mji huo katika orodha ya urithi wa dunia hali itakayoiathiri Zanzibar.
“Ni hatari kubwa Zanzibar tukija kutolewa kwenye urithi wa dunia kwa sababu tutashindwa tena kuwapata watalii wengi, kwani wengi wanapokuja hufika Mji Mkongwe,” anasema Profesa Shareef.
Zanzibar imekuwa ikionywa juu ya usalama na utunzaji Mji Mkongwe katika mikutano ya wadau wanaokutana duniani, ambayo huandaliwa na Unesco.
Kuoneana tatizo la rushwa, kuogopana na ukosefu wa fedha ni miongoni mwa changamoto zinazotajwa kukwamisha maendeleo ya Mji Mkongwe hata kusababisha Zanzibar kutishiwa kuondolewa miongoni mwa vivutio hivyo.
Hata hivyo, Mkurugenzi wa Mamlaka ya Mji Mkongwe Zanzibar, Issa Sariboko Makarani amesema kuna hatua ambazo lazima zichukuliwe ili kuuhami na kuuweka salama mji huo.
Makarani anasema Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, kupitia Mamlaka ya Mji Mkongwe iliamua kutekeleza mpango mkuu wa matumizi ya vyombo vya moto na watembea kwa miguu mwaka 2006.
Amesema mpango huo ulitayarishwa kwa kushirikishwa taasisi mbalimbali kama wadau wa mpango huo, hivyo kutakiwa kutangazwa mara moja kwa utekelezaji.
Licha ya hilo, Unesco kupitia Kamati ya Urithi wa Dunia iliitaka Serikali ya Jamhuri wa Muungano wa Tanzania SMZ, kutayarisha mpango mkuu wa matumizi ya vyombo vya moto na watembea kwa miguu na kuuwasilishwa mara moja kwa ajili ya utekelezaji.
“Matumizi ya vyombo vya moto ndani ya Mji Mkongwe umezidi kupitia kiwango, kutokana na uongezekaji huo utasababisha athari kubwa kwa mji ambao ni urithi wa dunia,” anasema Makarani.
Anasema Mji Mkongwe unapokea wageni wengi wa kitalii na kusababisha kuleta usumbufu mkubwa wakati wa matembezi yao, wakati wakifanya shughuli zao za kitalii maeneo mbalimbali huku magari makubwa na mazito yakihatarisha majengo hayo ya kale.
Tayari, Serikali imezishirikisha taasisi zote na wadau kwa kuupitia vizuri mpango huo kwa ajili ya utekelezaji wake mara moja, kufuatia vikao mbalimbali kutoka ngazi za juu hadi utekelezaji.
Hatua zilizochukuliwa hadi sasa zimeanza Februari 2016, ni kufunga baadhi ya njia ili kupunguza msongamano wa magari yanayoingia maeneo ya Mji Mkongwe.
Haiba ya Mji Mkongwe hupungua kila kukicha kutokana na kutoweka kidogokidogo vitu vya asili, hivyo kuingia vitu vipya ambavyo havina asili ya Zanzibar.
Kwa mfano; malalamiko makubwa ya wakazi wa Mji Mkongwe ni kukithiri kwa vinyago kama tingatinga na kuongezeka watumiaji wa dawa za kulevya.
“Wazanzibari hatuna asili ya tingatinga na vinyago, hivyo ni vitu vyenye asili ya Tanzania Bara, lakini leo Mji Mkongwe kila kona unayopita kumezagaa vinyago vya kuchongwa na vile vya Kimasai, kwa hiyo ile hadhi ya mji sasa imepotea” anasema mkazi wa Shangani, Maryam Hamid.
Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Habari, Utamaduni, Utalii na Michezo, Issa Mringoti anasema tatizo kubwa katika Mji Mkongwe ni watembeza watalii wanaoleta usumbufu kwa wageni hao wanaotembelea maeneo ya kihistoria.
Mringoti anasema Serikali imeanzisha kikosi cha ulinzi kwa watalii na vitega uchumi vya utalii eneo lote la Mji Mkongwe, lengo likiwa ni kuondoa tatizo la watu ambao wanapotembelea.
“Mji Mkongwe wenyewe umeshaona kama una tatizo na hilo ni kubwa la kuwasumbua watalii na wakazi wake wamebaini kwamba, kuna tatizo ndiyo sababu wakabuni mambo yatakayosaidia kupata ufumbuzi,” anasema Mlingoti.
Serikali inatakiwa kuchukua hatua za makusudi kuhakikisha mji huo unabaki kwenye orodha ya Urithi wa Dunia, kwa sababu unasaidia kuingiza fedha za kigeni, lakini kuendelea kuwapo kwa manthari yanayoakisi utamaduni, silka na mila za Wazanzibari.
Kama wataalamu wanavyobainisha ukiondolewa kwenye orodha, itakuwa vigumu kuurudisha na nchi itakosa mapato hasa fedha za kigeni.