Saturday, March 19

Mji Mkongwe; hazina hatarini kupoteza hadhi


Zanzibar ina visiwa viwili vya Unguja na Pemba, ikitambulika duniani kutokana na historia na utamaduni wake wa asili ulioambatana na vivutio mbalimbali. Miongoni mwa mambo hayo ni Mji Mkongwe. Ni mji wa kale ambao mwaka 2000, Shirika la Kimataifa la Elimu, Sayansi na Utamaduni (Unesco) liliamua kuupa hadhi kuwa Eneo la Urithi wa Dunia.
Kama ilivyo kwa miji mengine mikongwe duniani, Mji Mkongwe una utajiri wa historia na vivutio tofauti ukijengeka kwa ramani kwa umbo la sambusa. Ni eneo dogo lenye wastani wa majengo 1,700 ya kila aina. Kuna chochoro (Narrow Street)23, makanisa mawili, misikiti 52, maghorofa 50, varandaa na baraza zenye milango zaidi ya 200 iliyonakishiwa kwa ufundi wa hali ya juu.
Katika Mji Mkongwe kuna jumla ya majengo 1,100 yaliyotambuliwa kuwa yenye thamani kubwa katika utaalamu wa ujenzi, hivyo ni kivutio kikubwa kwa watalii. Kwa mujibu wa takwimu za Kamisheni ya Utalii Zanzibar, zaidi ya asilimia 80 ya wageni wanaotembelea Zanzibar hutembelea maeneo ya Mji Mkongwe. Majengo hayo ni Jumba la Ajabu maarufu Baitil Ajaib (House ofWonder), Old Dispensary, Bandari Kuu,
Mahakama, Hospitali ya Rufani, Ikulu, Hamamu ya Hamamni, Ngome Kongwe Jengo la Tiptip, Kanisa Kuu Katoliki la Minara Miwili na Mkunazini (Soko la Watumwa), Mahekalu ya Wahindu, Jumba la Maparisi na Jamati sita za Mashia.
Mwaka 1830, nyumba za Mji Mkongwe zilijengwa chini ya utawala wa Sultani Sayyid Said, alipohamishia makao makuu yake Zanzibar kutoka Oman.
Licha ya vivutio hivyo vya asili, kuna utamaduni unaombatana na matamasha mbalimbali ambayo hufanyika kila mwaka likiwamo la Nchi za Majahazi na Sauti za Busara, yote ni vivutio kwa watalii na hufanyika Mji Mkongwe.
Hata hivyo, mji huo umeingizwa katika maeneo ya urithi wa dunia ulio hatarini kutoweka kutokana na Serikali kushindwa kufuata vigezo na masharti yaliyowekwa na Unesco lililoupa hadhi hiyo miaka 15 iliyopita.
Mkutano wa Kamati ya Urithi wa Kimataifa uliofanyika Juni 2015 mjini Bonn nchini Ujerumani, umetoa mwaka mmoja kwa State Party kutekeleza baadhi ya mambo yaliyoonekana kuwa na athari kwa Mji Mkongwe wa Zanzibar, iwapo hayatatekelezwa yatauweka Mji Mkongwe katika orodha ya urithi uliopo hatarini (World Heritage in Danger List).
Katibu Mtendaji wa Kamisheni ya Utalii, Saleh Ramadhan Feruz anaona tishio hilo la Unesco siyo tu litaathiri sekta ya utalii Zanzibar, bali Taifa nzima.
“Mji Mkongwe ukitolewa kwenye urithi wa dunia utatuathiri kiuchumi, kwani uchumi wetu unategemea utalii kwa sababu kati ya watalii wote wanaokuja kutembelea Zanzibar, asilimia 85 wanatembelea mji huo,” anasema Feruzi.
Inaelezwa kwamba tangu miaka ya 1970, baadhi ya majengo yamekuwa yakiporomoka ndiyo sababu ya Zanzibar kuiomba dunia iyahifadhi majengo hayo, ikiwamo jengo maarufu la Bait El-ajaib au Jumba la Maajabu.
Kuna changamoto kadhaa zinazoweza kuuweka Mji Mkongwe kwenye orodha ya urithi wa dunia unaotoweka, tayari hatua mbalimbali zimeanza kuchukuliwa ili kuuhifadhi usiondolewe kwenye orodha hiyo.
Tatizo linalouweka Mji Mkongwe hatarini ni kutofuata taratibu zilizowekwa na Unesco na kuacha magari makubwa yenye uzito usiostahiki kupita eneo hilo, kwa mujibu wa utafiti uliofanywa na Mamlaka ya Mji Mkongwe, huingia magari 17,000 kwa siku yenye uzito tofauti wakati inatakiwa magari yasiyozidi uzito wa tani mbili.
Dosari nyingine ni ujenzi holela wa hoteli za kitalii ulioongezeka bila ya kuzingatia masharti ya Mji Mkongwe, jambo ambalo hutia doa urithi huo wa dunia.
Sheha wa Mji Mkongwe, Mohammed Juma Mugheiry anasema suala la kujengwa hoteli kubwa ndani ya mji huo ni jambo lisilokubalika.
“Ujenzi wa hoteli kubwa za kitalii ni hatari kwa mji wetu, ndiyo sababu ya Zanzibar kupewa onyo la kuwekwa kwenye miji hatari, kwani huwezi kuwa na hoteli kubwa kama hizi na usihitaji huduma ambazo zitachangia kuongeza magari yenye uzito wa tani kubwa kuingia Mji Mkongwe,” anasema Mugheiry.
Tatizo jingine ni watendaji wa Serikali kushindwa kuchukuwa hatua kwa makosa mbalimbali ya utendaji yanayofanywa.
“Sijui tunaogopa nini kuwachukulia hatua wale watendaji wenye kukaidi masharti hayo?” anahoji.Katika mkutano wake wa Julai mwaka jana nchini Ujerumani, Unesco ilitoa mwaka mmoja kwa Zanzibar kurekebisha kasoro zinazoonekana, ikiwamo ujenzi holela na uingizwaji magari mazito ili kuhifadhi mji huo.
Mwanahistoria na mkazi wa Mji Mkongwe, Profesa Abdul Shareef anasema hofu yake ni kutolewa kwa mji huo katika orodha ya urithi wa dunia hali itakayoiathiri Zanzibar.
“Ni hatari kubwa Zanzibar tukija kutolewa kwenye urithi wa dunia kwa sababu tutashindwa tena kuwapata watalii wengi, kwani wengi wanapokuja hufika Mji Mkongwe,” anasema Profesa Shareef.
Zanzibar imekuwa ikionywa juu ya usalama na utunzaji Mji Mkongwe katika mikutano ya wadau wanaokutana duniani, ambayo huandaliwa na Unesco.
Kuoneana tatizo la rushwa, kuogopana na ukosefu wa fedha ni miongoni mwa changamoto zinazotajwa kukwamisha maendeleo ya Mji Mkongwe hata kusababisha Zanzibar kutishiwa kuondolewa miongoni mwa vivutio hivyo.
Hata hivyo, Mkurugenzi wa Mamlaka ya Mji Mkongwe Zanzibar, Issa Sariboko Makarani amesema kuna hatua ambazo lazima zichukuliwe ili kuuhami na kuuweka salama mji huo.
Makarani anasema Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, kupitia Mamlaka ya Mji Mkongwe iliamua kutekeleza mpango mkuu wa matumizi ya vyombo vya moto na watembea kwa miguu mwaka 2006.
Amesema mpango huo ulitayarishwa kwa kushirikishwa taasisi mbalimbali kama wadau wa mpango huo, hivyo kutakiwa kutangazwa mara moja kwa utekelezaji.
Licha ya hilo, Unesco kupitia Kamati ya Urithi wa Dunia iliitaka Serikali ya Jamhuri wa Muungano wa Tanzania SMZ, kutayarisha mpango mkuu wa matumizi ya vyombo vya moto na watembea kwa miguu na kuuwasilishwa mara moja kwa ajili ya utekelezaji.
“Matumizi ya vyombo vya moto ndani ya Mji Mkongwe umezidi kupitia kiwango, kutokana na uongezekaji huo utasababisha athari kubwa kwa mji ambao ni urithi wa dunia,” anasema Makarani.
Anasema Mji Mkongwe unapokea wageni wengi wa kitalii na kusababisha kuleta usumbufu mkubwa wakati wa matembezi yao, wakati wakifanya shughuli zao za kitalii maeneo mbalimbali huku magari makubwa na mazito yakihatarisha majengo hayo ya kale.
Tayari, Serikali imezishirikisha taasisi zote na wadau kwa kuupitia vizuri mpango huo kwa ajili ya utekelezaji wake mara moja, kufuatia vikao mbalimbali kutoka ngazi za juu hadi utekelezaji.
Hatua zilizochukuliwa hadi sasa zimeanza Februari 2016, ni kufunga baadhi ya njia ili kupunguza msongamano wa magari yanayoingia maeneo ya Mji Mkongwe.
Haiba ya Mji Mkongwe hupungua kila kukicha kutokana na kutoweka kidogokidogo vitu vya asili, hivyo kuingia vitu vipya ambavyo havina asili ya Zanzibar.
Kwa mfano; malalamiko makubwa ya wakazi wa Mji Mkongwe ni kukithiri kwa vinyago kama tingatinga na kuongezeka watumiaji wa dawa za kulevya.
“Wazanzibari hatuna asili ya tingatinga na vinyago, hivyo ni vitu vyenye asili ya Tanzania Bara, lakini leo Mji Mkongwe kila kona unayopita kumezagaa vinyago vya kuchongwa na vile vya Kimasai, kwa hiyo ile hadhi ya mji sasa imepotea” anasema mkazi wa Shangani, Maryam Hamid.
Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Habari, Utamaduni, Utalii na Michezo, Issa Mringoti anasema tatizo kubwa katika Mji Mkongwe ni watembeza watalii wanaoleta usumbufu kwa wageni hao wanaotembelea maeneo ya kihistoria.
Mringoti anasema Serikali imeanzisha kikosi cha ulinzi kwa watalii na vitega uchumi vya utalii eneo lote la Mji Mkongwe, lengo likiwa ni kuondoa tatizo la watu ambao wanapotembelea.
“Mji Mkongwe wenyewe umeshaona kama una tatizo na hilo ni kubwa la kuwasumbua watalii na wakazi wake wamebaini kwamba, kuna tatizo ndiyo sababu wakabuni mambo yatakayosaidia kupata ufumbuzi,” anasema Mlingoti.
Serikali inatakiwa kuchukua hatua za makusudi kuhakikisha mji huo unabaki kwenye orodha ya Urithi wa Dunia, kwa sababu unasaidia kuingiza fedha za kigeni, lakini kuendelea kuwapo kwa manthari yanayoakisi utamaduni, silka na mila za Wazanzibari.
Kama wataalamu wanavyobainisha ukiondolewa kwenye orodha, itakuwa vigumu kuurudisha na nchi itakosa mapato hasa fedha za kigeni.     

No comments:

Post a Comment