Friday, May 18
'Amali Za Kutenda Na Ya Kujiepusha Nayo Katika Mwezi Mtukufu Wa Rajab
Nasiha Za Minasaba Mbalimbali
AlhamduliLLaah. Inapasa tumshukuru Allaah (Subhaanahu wa Ta’ala) Kutupa umri hadi kutufikisha mwezi mtukufu wa Rajab ambao ni fursa kwetu kutenda mema yatakayotuchumia thawabu nyingi kuliko miezi mingine. Mema ambayo hatuna budi kuyatenda kwa ajili ya kujenga Aakhirah yetu kabla ya siku hii kufika. Siku ambayo hakuna mmoja wetu yeyote atakayeweza kuikwepa. Basi hebu kila mmoja wetu ajiulize: "Nimetanguliza nini kwa ajili ya siku hiyo?" Siku ambayo safari yake ni ndefu mno. Vyovyote tutakavyobeba kama ni zawadi huko Aakhirah, hazitoshi wala hatuna hakika nazo kama zitapendekezeka au zitakuwa na thamani huko tuendako ambako kuna makazi ya milele tusiyokuwa na hakika nayo; ima moto au Pepo.
Anasema Allaah (Subhaanahu wa Ta'ala):
(( يَا أَيُّهَا الَّذِينَ آمَنُوا اتَّقُوا اللَّهَ وَلْتَنظُرْ نَفْسٌ مَّا قَدَّمَتْ لِغَدٍ وَاتَّقُوا اللَّهَ إِنَّ اللَّهَ خَبِيرٌ بِمَا تَعْمَلُونَ))
((Enyi mlioamini! Mcheni Allaah, na kila nafsi iangalie inayoyatanguliza kwa ajili ya Kesho. Na mcheni Allaah, Hakika Allaah, Anazo khabari ya mnayoyatenda)) [Al-Hashr: 18].
Vile vile ni miezi miwili tu imebakia kutufikia mgeni wetu tunayemsubiri kwa hamu kila mwaka, mwezi mtukufu wa Ramadhaan. Kwa hiyo ni fursa nyingine pia kujitayarisha kuupokea mwezi huo kwa kujizoesha ibada mbali mbali kama Swawm, tahajjud, na pia kutenda mema mengi ili tutakapofikia mwezi wa Ramadhaan tuwe na nguvu za kufanya zaidi ya tuliyoyazoea kutenda katika miezi hii iliyobakia miwili ijayo.
Anasema Allaah (Subhaanahu wa Ta'ala):
(( إِنَّ عِدَّةَ الشُّهُورِ عِندَ اللّهِ اثْنَا عَشَرَ شَهْرًا فِي كِتَابِ اللّهِ يَوْمَ خَلَقَ السَّمَاوَات وَالأَرْضَ مِنْهَا أَرْبَعَةٌ حُرُمٌ ذَلِكَ الدِّينُ الْقَيِّمُ فَلاَ تَظْلِمُواْ فِيهِنَّ أَنفُسَكُم ))
((Hakika idadi ya miezi kwa Allaah ni miezi kumi na mbili katika hukumu ya Allaah, tangu Alipoumba mbingu na ardhi. Katika hiyo iko mine mitakatifu. Hiyo ndiyo Dini iliyo sawa. Basi msidhulumu nafsi zenu humo)) [At-Tawbah: 36]
Miezi minne hiyo imetajwa katika Hadiyth ifuatayo:
عَنْ أَبَى بَكْرَة أَنَّ رَسُول اللَّه - صَلَّى اللَّه عَلَيْهِ وَسَلَّمَ - قَالَ فِي حَجَّة الْوَدَاع : (( إِنَّ الزَّمَان قَدْ اِسْتَدَارَ كَهَيْئَتِهِ يَوْم خَلَقَ اللَّه السَّمَوَات وَالْأَرْض السَّنَة اِثْنَا عَشَر شَهْرًا مِنْهَا أَرْبَعَة حُرُم : ثَلَاث مُتَوَالِيَات ذُو الْقَعْدَة وَذُو الْحِجَّة وَالْمُحَرَّم وَرَجَب مُضَر الَّذِي بَيْن جُمَادَى وَشَعْبَان)) صَحِيح الْبُخَارِيّ
Kutoka kwa Abu Bakrah ambaye amesema: "Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa wa sallam) amesema alipokuwa katika Hijjah ya kuaga (Hijjah wa mwisho): ((Mgawanyo wa nyakati umerudi kama ulivyo (wakati) Allaah Alipoumba mbingu na ardhi. Mwaka una miezi kumi na mbili, minne ambayo ni mitukufu; mitatu inafuatana pamoja (nayo ni) Dhul-Qa'adah, Dhul-Hijjah na Muharram, na (wa nne ni) Rajab wa (kabila la) Mudhwar ambao upo baina ya Jumaada na Sha'abaan)) [Al-Bukhaariy]
Katika miezi yote kumi na mbili Allaah (Subhaanahu wa Ta'ala) Ameichagua hii minne na Ameifanya kuwa ni mitukufu na kusisitiza kuitakasa, na kwamba dhambi zitakazofanyika humo ni zaidi na hali kadhalika thawabu za vitendo vyema zinakuwa maradufu na zaidi. [Atw-Twabariy 14: 238]
Ni sawa kama Anavyoonya Allaah (Subhaanahu wa Ta'ala) kufanya maasi katika sehemu tukufu Alipotaja Masjidul-Haraam (Msikiti Mtukufu Makkah):
((إِنَّ الَّذِينَ كَفَرُوا وَيَصُدُّونَ عَن سَبِيلِ اللَّهِ وَالْمَسْجِدِ الْحَرَامِ الَّذِي جَعَلْنَاهُ لِلنَّاسِ سَوَاء الْعَاكِفُ فِيهِ وَالْبَادِ وَمَن يُرِدْ فِيهِ بِإِلْحَادٍ بِظُلْمٍ نُذِقْهُ مِنْ عَذَابٍ أَلِيمٍ))
((Hakika wale waliokufuru na wakazuilia Njia ya Allaah na Msikiti Mtakatifu, ambao tumeufanya kwa ajili ya watu wote sawasawa, kwa wakaao humo na wageni. Na kila atakayetaka kufanya upotofu humo kwa dhulma, basi Tutamwonjesha adhabu iumizayo)) [Al-Hajj: 25]
Qataadah amesema kuhusu kauli ya Allaah:
(( فَلاَ تَظْلِمُواْ فِيهِنَّ أَنفُسَكُم))
((Basi msidhulumu nafsi zenu humo))
"Dhulma itakayotendeka katika miezi mitukufu ni mbaya na kubwa (au hatari) kuliko dhulma itakayotendeka katika miezi mingine. Hakika dhulma daima ni makosa, lakini Allaah Hufanya baadhi ya vitu kuwa ni vizito kuliko vingine kama Anavyopenda". Akaendelea kusema: "Allaah Amechagua baadhi ya viumbe Vyake na baadhi ya vitu kuwa bora zaidi kuliko vingine. Amechagua Wajumbe kutoka Malaika na kutoka binaadamu. Vile vile Amechagua baadhi ya kauli Zake kuwa ni bora kuliko nyingine, Misikiti kuwa bora kuliko sehemu nyingine za ardhi, Ramadhaan na miezi mitukufu kuwa bora kuliko miezi mingine, siku ya Ijumaa kuwa ni bora kuliko siku nyingine, na usiku wa Laylatul-Qadr kuwa ni bora kuliko masiku mengine. Kwa hiyo takasa vile Alivyovitakasa Allaah, kwani kufanya hivyo ni vitendo vya watu wenye akili na wenye kufahamu" [Tafsiyr ya Ibn Kathiyr]
Miongoni mwa yaliyokatazwa katika miezi hii mitukufu ni kama Anavyosema Allaah (Subhaanahu wa Ta'ala):
(( يَسْأَلُونَكَ عَنِ الشَّهْرِ الْحَرَامِ قِتَالٍ فِيهِ قُلْ قِتَالٌ فِيهِ كَبِيرٌ وَصَدٌّ عَن سَبِيلِ اللّهِ وَكُفْرٌ بِهِ وَالْمَسْجِدِ الْحَرَامِ وَإِخْرَاجُ أَهْلِهِ مِنْهُ أَكْبَرُ عِندَ اللّهِ وَالْفِتْنَةُ أَكْبَرُ مِنَ الْقَتْلِ ))
((Wanakuuliza juu ya kupigana vita katika mwezi mtakatifu. Sema: Kupigana vita wakati huo ni dhambi kubwa Lakini kuzuilia watu wasiende katika Njia ya Allaah na kumkanusha Yeye, na kuzuilia watu wasiende kwenye Msikiti Mtakatifu na kuwatoa watu wake humo, ni makubwa zaidi mbele ya Allaah. Na fitina ni mbaya zaidi kuliko kuua..))[Al-Baqarah: 217]
Hivyo basi katika mwezi mtukufu wa Rajab, maasi na mema yafuatayo yanatupasa kuzingatia:
Maasi Mengine Ambayo Tunatakiwa Tujikumbushe Kuyaacha:
- Kuiba;
- Kumshirikisha Allaah (Subhaanahu wa Ta'ala) kama kwenda kwa wachawi na waganga na kuwaamini wanayoyatabiri kwa watu;
- Kuzini;
- Kulewa;
- Kumdhulumu mtu haki yake;
- Kugombana, kutukanana, kuvunjiana heshima, kudharauliana n.k.;
- Kusengenya (Ghiybah);
- Kusema uongo, na kila aina ya uovu mwengine.
Mambo Mema Ya Kukumbushana Kufanya Katika Mwezi Huu Mtukufu
- Kuongeza Sunnah za Swalah; *(tazama maelezo chini)
- Kufunga Swawm za Sunnah kama Jumatatu na Alkhamiys, Masiku meupe (Ayyaamul-biydhw) (tarehe 13, 14 na 15) na Swawm ya Nabii Daawuud (kufunga kila baada ya siku moja);
- Kujielimisha mambo ya Dini kwa kusoma vitabu na kusikiliza mawaidha;
- Kuomba Maghfirah na Tawbah;
- Kufanya kila aina ya dhikr (kumkumbuka na kumtaja Allaah), kwa kusoma Qur-aan kwa wingi, kumshukuru, kumtukuza, kuomba du'aa n.k.;
- Kuwasiliana au kutembeleana na ndugu na jamaa;
- Kutenda wema kwa jirani, marafiki na watu wote kwa ujumla;
- Kutoa sadaka;
- Kulisha masikini;
- Kupatanisha waliogombana;
- Kuamrishana mema na kukatazana maovu, na mengi mengineyo katika vitendo vyema.
* Swalah za Sunnah
Ratiba Ya Swalah Za Sunnah Zilizosisitizwa Na Zisizosisitizwa
ALFAJIRI
Kabliya Rakaa 2
ADHUHURI
Kabliya Rakaa 4
Baadiya Rakaa2
ALASIRI
Kabliya Rakaa 4
MAGHARIBI
Kabliya Rakaa 2
Baadiya Rakaa 2
'ISHAA
Kabliya Rakaa 2
Baadiya Rakaa 2
Fadhila Zake:
(( مَا مِنْ عبْدٍ مُسْلِم يُصَلِّي للَّهِ تَعَالى كُلَّ يَوْمٍ ثِنْتَيْ عشْرةَ رَكْعَةً تَطوعاً غَيْرَ الفرِيضَةِ ، إِلاَّ بَنَى اللَّه لهُ بَيْتاً في الجَنَّةِ ، أَوْ : إِلاَّ بُنِي لَهُ بيتٌ في الجنَّةِ )) رواه مسلم
* ((Hatoswali mja Rakaa 12 zisizo za fardhi kwa siku, ila atajengewa [na Allaah] nyumba peponi)) [Muslim]
Nazo ni hizo Muakkadah (Zilosisitizwa) jumla yake ni 12
(( ركْعتا الفجْرِ خيْرٌ مِنَ الدُّنيا ومَا فِيها )) رواه مسلم
** ((Rakaa mbili (za Sunnah) kabla ya Alfajiri ni kheri kuliko duniya na yaliyomo ndani yake) [Muslim]
((ما من عبد يسجد لله سجدة إلا كتب الله له بها حسنة ومحا عنه بها سيئة ورفع له بها درجة فاستكثروا من السجود)) رواه ابن ماجه
((Mja yeyote atakayesujudu sijda moja ataandikiwa wema mmoja, na atafutiwa baya moja, na atapandishwa daraja yake, kwa hiyo zidisheni kusujudu)) [Ibn Maajah]
Swalah ya Tahajjud
(( أفضل الصلاة بعد الفريضة صلاة الليل)) رواه مسلم
((Swalah iliyo bora kabisa baada ya Fardh ni Swalah ya usiku)) [Muslim]
Swalah Ya Dhuhaa na Swalah Ya Witr
عـَن أبي هـُريْرَة رضيَ الله عنه قال : أوصـَانـِي خـَليلي صـَلـَّى الله عليه وسلم بـِصـِيامِ ثـَلاثـَة ِ أيـَّام ٍ مـِنْ كـُل شـَهر ٍ، وَ ركـْعـَتي الضـُّحى ، وأنْ أوتـِرَ قبلَ أنْ أرقـُـد " ـ متفق عليه ـ
Kutoka kwa Abu Hurayrah (Radhiya Allaahu ‘anhu) kwamba “Ameniusia rafiki yangu Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam [mambo matatu]; kufunga siku tatu katika kila mwezi, Rakaa mbili Dhuhaa na niswali Witr kabla ya kulala” [Al-Bukhaariy na Muslim]
Tunamuomba Allaah (Subhaanahu wa Ta'ala) Atuwezeshe kujitenga na maasi na kuzidisha mema katika mwezi huu mtukufu na Atufikishe Ramaadhaan. Aamiyn
Subscribe to:
Posts (Atom)