ALIYESHINDA mnada wa nyumba tatu za kifahari zinazomilikiwa na mfanyabiashara maarufu, Said Lugumi, zenye thamani ya Sh bilioni 2.3, Dk. Louis Shika, anaishi kwenye chumba kimoja katika nyumba ya kupanga, MTANZANIA Jumapili linaripoti kwa uhakika.
Dk. Shika, ambaye anashikiliwa na Jeshi la Polisi kwa siku ya tatu sasa kwa tuhuma za kuvuruga mnada, alijitokeza kununua nyumba mbili zilizopo Mbweni JKT na moja iliyopo Upanga, katika mnada uliokuwa ukifanywa na Kampuni ya Udalali ya Yono kwa amri ya Mamlaka ya Mapato nchini (TRA).
Jeshi la Polisi linamshikilia Dk. Shika kutokana na kushindwa kulipa asilimia 25 ya manunuzi ya nyumba hizo kama masharti ya mnada yanavyoelekeza.
Gazeti hili jana lilifika nyumbani kwa Dk. Shika, eneo la Tabata Mawenzi, Mtaa wa Chonde, kwa msaada wa Ofisa wa Ofisi ya Serikali ya Mtaa ya Darajani, baada ya kupatafuta kwa zaidi saa tatu.
Baada ya kufika katika nyumba hiyo yenye geti la rangi nyeusi na maua meupe, mwandishi aligonga na kisha alitoka kijana wa kiume ambaye hakutaka kutaja jina lake anayekadiriwa kuwa na umri kati ya miaka 15-17, ambaye alishindwa kujibu kama daktari huyo yupo au la, kwakuwa alishindwa kutambua jina.
Mwandishi wa habari hizi alilazimika kumwonyesha kijana huyo picha ya Dk. Shika kupitia simu yake ya mkononi na baada ya kumtambua, alikiri kuwa ni mmoja wa wapangaji wa nyumba, lakini alisema kwa wakati huo hakuwapo na kwamba ana zaidi ya siku mbili haonekani.
“Humu ndani wote ni wapangaji na hawapo, kila mtu anakwenda kwenye shughuli zake anarudi jioni, nipo mimi hapa na si mwenyeji, huwa nakuja mara moja moja, lakini huyu mzee namfahamu huwa namkuta hapa nikija kwa ndugu yangu anakaa chumba hiki hapa (anaonyesha kijana huyo chumba ambacho kilikuwa kinaning’inia kufuli ndogo)”.
Kwa mujibu wa kijana huyo, nyumba hiyo yenye uzio na geti jeusi ina wapangaji watano na kila mmoja anakaa kwenye chumba chenye choo ndani, isipokuwa cha Dk. Shika kipo tofauti, kwakuwa anatumia choo cha nje.
Baada ya maelezo hayo, mwandishi alijaribu kuangalia chumba hicho kwa upande wa dirishani na kukuta hakina pazia, tofauti na vyumba vingine.
MPANGAJI MWENZAKE
Gazeti hili lilielezwa kuwa, mmoja wa wapangaji wa nyumba hiyo aitwaye Amina, ambaye anaweza kueleza kwa uhakika Dk. Shika ni nani, ofisi yake ipo hatua chache kutoka mahali ilipo nyumba hiyo.
Kutokana na hali hiyo, gazeti hili lililazimika kumfuata Amina, ambaye anauza duka la nguo maarufu kama ‘madela’, ambaye alisema Dk. Shika akiwa peke yake alifika kuishi katika nyumba hiyo baada ya kupelekwa na mwenye nyumba aitwaye Leonard Ntakamulenga, ambaye anaishi eneo tofauti na hapo.
“Dada mimi siwezi kuongea sana kwa sababu huwa simfuatilii, sema ninachojua aliletwa na mwenye nyumba wetu na alituambia kuwa ni mpangaji kama tulivyo sisi, sasa sijawahi kumfuatilia anafanya nini, maana muda mwingine mimi huwa nawahi kutoka na ninarudi usiku,” alisema Amina.
Amina alisema aliwahi kusikia kuwa Dk. Shika huwa anatumiwa fedha za kujikimu na mmiliki wa nyumba hiyo, ingawa alikiri kutofahamu uhusiano wao.
MWENYE NYUMBA
Gazeti hili liliwasiliana kwa njia ya simu na mmiliki wa nyumba hiyo, Ntakamulenga, ambaye kwa sasa yupo Dodoma kikazi na kukiri kumfahamu Dk. Shika.
Akieleza alivyomfahamu, Ntakamulenga alisema aliletewa na madalali kama mpangaji na alijitambulisha kwake kama daktari wa binadamu katika hospitali ya Songea.
“Alikuja miezi sita iliyopita na alilipa kodi ya mwezi mmoja shilingi 50, na tangu wakati huo hajawahi kulipa tena, aliniambia nisubiri ana fedha nyingi nje ya nchi, lakini aliniambia anakaa hapo ili aweka mambo yake vizuri katika kituo chake cha kazi Songea,” alisema Ntakamulenga.
Ntakamulenga alisema kadiri siku zilipokuwa zinayoyoma alipokuwa akimkumbusha habari za kodi yake, Dk. Shika alikuwa akisisitiza kuwa hana fedha.
“Nilipomchunguza niligundua kuwa si tu kodi, bali alikuwa anakosa hata fedha ya kula, sasa kwa sababu mimi ni Mkristo nikaamua kumuacha iwe kama sehemu ya sadaka,” alisema baba huyo mwenye nyumba ambaye alikiri kusikia kwamba Dk. Shika amekamatwa.
Alipoulizwa kwamba aliwahi kumchunguza kufahamu kama kweli Dk. Shika ni daktari wa binadamu, Ntakamulenga alisema kuwa, hakuwahi kufanya hivyo, kwa kuwa si jambo rahisi kwa sababu yeye anaishi mbali na nyumba hiyo.
MAJIRANI
Gazeti hili lilifika lilipo duka ambalo linatumiwa na wenyeji wa mtaa huo, ikiwamo nyumba anayoishi Dk. Shika.
Mmiliki wa duka hilo, ambalo lipo nyumba ya tatu kutoka anapoishi Dk. Shika, Hashim Said, alisema taarifa za daktari huyo kununua nyumba zilimshtua, kwakuwa kwa jinsi alivyokuwa anamfahamu si mtu wa kuwa na kiasi kile cha fedha kilichotajwa.
“Huyu mzee mimi namfahamu anakuja hapa dukani kwangu, nilivyoona kwenye mitandao anataka kununua nyumba za Lugumi nilishangaa, maana mtu mwenyewe tangu nilipomuona siku ya kwanza sijawahi kumuelewa,” alisema Hashim.
Alisema alianza kupata wasiwasi na Dk. Shika baada ya siku moja kumuagiza bidhaa ambazo dukani kwake hazikuwapo zenye thamani ya Sh 30,000, lakini alipozileta alimwambia amhifadhie, huku akimuagiza nyingine.
“Siku ile ile niliyoleta vile vitu, akaniagiza vingine ambavyo dukani havikuwapo, tena vyenye thamani hiyo hiyo ya Sh 30,000 na nilikwenda kumchukulia kwa kuwa aliniahidi kuvichukua, cha kushangaza akaniambia hawezi kuvichukua hivyo niviache watanunua wengine,” alisema Hashim.
Alisema hata siku ya mnada alipata wasiwasi na kwamba alidhani kuwa anaahidi kulipa Sh milioni 300, aliposikiliza kwa makini akasikia ni Sh bilioni tatu, jambo ambalo lilimshtua.
Akiuelezea mwonekano wa Dk. Shika, mmiliki huyo wa duka alisema siku zote amekuwa akionekana msafi na kwamba kutokana na umaridadi wake aliwahi kufikiri hata nyumba anayoishi huenda kuwa ni yake na anaishi na familia yake.
Alisema mbali na hulka yake ya utanashati, Dk. Shika pia anao utaratibu wa kila siku kwenda kusoma magazeti katika kituo cha mabasi cha Kimanga.
“Yaani huyu mzee huu mnada itakuwa aliusoma kwenye magazeti, maana ana ratiba yake huwa anapita asubuhi hapa anakwenda barabarani kusoma magazeti na muda mwingine huwa ananunua,” alisema Hashim.
Alisema mara nyingi anapokaa mahali huongelea habari za fedha, japokuwa hajawahi kusikika akisema atazipata wapi.
“Kwa mazungumzo yake anaonekana kipindi cha nyuma alikuwa akishika fedha nyingi, lakini kwa sasa anaonekana hana ndiyo maana akikaa kama anawaweweseka mambo ya fedha,” alisema Hashim.
Hashimu alisema mara ya mwisho walimuona Dk. Shika juzi akishuka katika gari la polisi huku akiongozana na polisi watatu ambao walikwenda naye moja kwa moja hadi katika chumba chake.
Alisema baadaye walimuona Dk. Shika na polisi hao wakitoka nje na kumwingiza tena kwenye gari na kuondoka naye.
Naye mmoja wa jirani ambaye ni mama wa makamo ambaye alihofia kutaja jina, alisema alianza kumuona Dk. Shika katika kipindi cha miezi kadhaa na kwa mujibu wa taarifa alizokuwa akizipata kutoka kwa wapangaji wenzake ni kwamba, ni rafiki wa mwenye nyumba.
“Huyu mtu inasemekana ni rafiki wa mwenye nyumba amemuweka hapa akae kwa muda sasa, lakini huwa hafanyi kazi yoyote, mara nyingi anatoka amevaa vizuri anakwenda mpaka Mawenzi pale kituoni baada ya muda anarudi, sijawahi kumuona katoka akarudi jioni,” alisema mama huyo.
Alisema alishawahi kulalamikiwa na baadhi ya wapangaji wenzake kuwa Dk. Shika anaweza akalala na njaa hata siku mbili na wakati mwingine wamekuwa wakimsaidia chakula.
Alisema kwa maisha anayoishi Dk. Shika, hawezi kununua nyumba za gharama kama zinazoonyeshwa mitandaoni.
Naye Mwenyekiti wa Serikali ya Mtaa wa Kimanga Darajani, Chacha Mwenge, alisema alianza kusikia taarifa za Dk. Shika kupitia mitandaoni, lakini baada ya kuandikwa magazetini akajua ni mmoja wa wananchi wake.
“Mimi huyu mtu nilikuwa simjui, nilivyosikia anaishi mtaani kwangu nilijaribu kuulizia kwa watu wanaomjua kupitia simu, wengine walisema hawamfahamu, wapo waliokuwa wanasema huwa wanamuona tu anapita barabarani, nadhani ni mgeni huku,” alisema Mwenge.
Alisema baada ya gazeti hili kufika ofisini kwake alilazimika kufanya juhudi, ndipo alipogundua kuwa Dk. Shika anakaa Mtaa wa Chonde.
Dk. Shika, ambaye kwa sasa yupo katika kituo cha polisi kwa uchunguzi, siku ya mnada alijitambulisha kwa waandishi wa habari kama Rais wa kampuni ya kimataifa inayojishughulisha na kemikali za viwandani iitwayo Ralcefort, iliyopo nchini Urusi na aliahidi kutoa fedha hizo kutoka nchini huko ndani ya saa 48.