Sunday, November 12

Watoto 270 hufariki dunia kila siku nchini


Watoto 270 walio chini ya miaka mitano hufariki dunia nchini kila siku kutokana na sababu mbalimbali, imeelezwa.
Idadi hiyo imepungua ikilinganishwa na takwimu za mwaka 2015 zinazoonyesha kuwa watoto waliokuwa wakipoteza maisha kila siku ni 2,015.
Akizungumza katika mafunzo ya kuandika habari za watoto yanayoendeshwa na Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF), mtaalamu wa masuala ya kuzuia maambukizo ya Virusi vya Ukimwi (VVU) kutoka kwa mama kwenda kwa Mtoto, Hafsa Khalfani alisema malaria na magonjwa yatokanayo na lishe duni yanachangia vifo hivyo.
Khalfani ambaye ni mtaalamu kutoka Shirika la Afya Duniani (Unicef), alisema asilimia 34 ya watoto nchini wana utapiamlo, 20 hawapati mlo kamili, 40 hawapati haki zao za msingi wakati asilimia 75 wameshafanyiwa ukatili.
Alisema changamoto zinazowahusu watoto zinaweza kutatuliwa ikiwa kila mmoja atashiriki kuzitatua.
Mwenyekiti wa TEF, Theophil Makunga alisema mafunzo hayo yanafanyika ili kuwanoa waandishi kuhusu habari za watoto kutokana na umuhimu wa kuandika kiweledi.
Ofisa Habari wa Unicef, Usia Nkoma alisema wazazi wana jukumu la kuhakikisha watoto wanakwenda shule na kurejea nyumbani wakiwa salama.
Alisema wazazi na walezi wamekumbushwa wajibu wao wa kuwalinda watoto baada ya baadhi ya tafiti kuonyesha moja ya maeneo wanayofanyiwa ukatili wa ngono ni kwenye mabasi ya shule.
Nkoma alisema mtoto wa kwanza kuingia kwenye gari la shule na wa mwisho kushuka wapo hatarini kufanyiwa ukatili huo, ikiwa usafiri huo utabaki kwa watumishi bila usimamizi wa walimu au walezi.
“Hata kama mzazi umebanwa na kazi bado una jukumu la kuhakikisha mtoto kama yupo salama, mfano tu kwenye masuala ya usafiri, ikiwa basi hilo halina muhudumu mwingine au mwalimu ni hatari kwa hiyo, wanafanyiwa ukatili wa kingono,” alisema Nkoma.
Akifundisha masuala ya sheria za watoto, Jesse Kwayu alisema chanzo kikubwa cha uhalifu ni malezi hafifu.
“Hivi mmewahi kujiuliza mtoto wa mtaani anapokuwa mtu mzima anakwenda wapi? Jambo hili kila mmoja anapaswa kutafakari kwa sababu vinginevyo kila mmoja ataathirika,” alisema.

No comments:

Post a Comment