Saturday, March 17

Makonda awaagiza wananchi kutupa taka kwa wenyeviti Serikali za Mitaa


Dar es Salaam. Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda, amewataka wananchi wa mkoa huo ambao maeneo yao yamekaa na takataka muda mrefu bila kuzolewa kwenda kuzitupa nyumbani kwa wenyeviti wa Serikali za Mitaa.
Ameyasema hayo leo Machi 17, kwenye hafla ya uzinduzi wa mpango wa Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam wa kuendeleza utalii wa jiji hilo.
Makonda amesema haiwezekani tunakuja na mpango wa utalii lakini jiji bado linaonekana chafu na kutaka kila kiongozi kuwajibika katika kulisimamia hilo.
“Nawaambieni wananchi kuanzia leo kama mna uhakika mmelipa tozo ya kuzolea taka na taka hizo hazijazolewa kwa muda mrefu, zipelekeni nyumbani kwa Mwenyekiti wa Serikali ya Mitaa yenu halafu yeye atajua wapi pa kuzipeleka,” amesema Makonda.
Amesema katika mpango huo anategemea kuona mambo manne yakifanyika ikiwamo suala zima la usafi, utalii, stendi za mabasi za kisasa na masoko ya kisasa ambayo yatawawezesha wafanyabiashara kufanya shughuli zao mahali pazuri.
Kwa upande wake Waziri wa Tamisemi, Suleiman Jaffo, ambaye alikuwa mgeni rasmi katika hafla hiyo, ameupongeza uongozi wa mkoa wa Dar es Salaam kwa kuja na mpango huo na kuahidi kwamba ofisi yake itatoa ushirikano kuona jambo hilo linafanikiwa.

Facebook yasimamisha akaunti ya kampuni iliyompigia debe Uhuru


Nairobi, Kenya. Mtandao maarufu wa Facebook umetangaza kusimamishwa kwa akaunti ya Strategic Communication Laboratories kampuni mama ya Cambridge Analytica, kampuni ya uchambuzi wa data inayotuhumiwa kuratibu kampeni za mgawanyiko kuelekea uchaguzi mkuu wa rais mwaka 2017 nchini
Kusimamishwa kwa akaunti hiyo kumetokana na kampuni ya Cambridge Analytica kukiuka sera zake, mtandao huo mkubwa wa mawasiliano ya kijamii ulisema katika taarifa yake Ijumaa.
Facebook imedai kwamba mnamo mwaka 2015 Cambridge Analytica ilipewa maelezo jinsi ya kutumia Facebook bila idhini kutoka mtandao huo kupitia kazi iliyofanywa kwa ushirikiano na Profesa wa Saikolojia ya Chuo Kikuu cha Cambridge aitwaye Dr Aleksandr Kogan.
"Profesa huyo alisema uongo na kukiuka sera zetu za jukwaa kwa kupitisha data kutoka kwenye programu ambayo ilikuwa ikitumia kuingia FB kwenda SCL / Cambridge Analytica, ambayo inafanya kazi za kisiasa, serikali na za kijeshi kote ulimwenguni. Pia alimpatia data Christopher Wyloe wa kampuni ya Teknolojia ya Eunoia," ilisema Facebook.
Ripoti iliyotolewa mwaka jana na kampuni ya kimataifa ya masuala ya faragha yenye makao yake London, Uingereza, inayopigana haki ya faragha duniani, ilisema kabla ya Uchaguzi Mkuu wa 2017, kampuni ya Cambridge Analytica iliongoza kampeni za mtandao ambazo zililenga ama kumshambulia kiongozi wa Nasa Raila Odinga au kumpigia debe Rais Kenyatta.
Facebook ilisema kuwa kampuni hiyo kipekee ilimfanyia kazi Rais Kenyatta wakati wa kampeni yake ya uchaguzi.
Cambridge Analytica ilikanusha madai na ikasema kuwa haikuhusika katika maudhui yoyote hasi ya kisiasa.

Makunga ajiuzulu uenyekiti TEF


Dar es Salaam. Mwenyekiti wa Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF), Theophil Makunga ametangaza kujiuzulu wadhifa wake kwa sababu binafsi.
Taarifa ya TEF iliyotolewa leo Machi 17, 2018 imesema: “Makunga amechukua hatua hiyo kwa kutumia uhuru wake binafsi kama mwanachama wa TEF.”
Imesema kutokana na uamuzi huo, mkutano mkuu wa dharura wa TEF uliokutana leo umeridhia kujizulu kwake huku ikieleza TEF itakosa uongozi na busara za Makunga ambazo zilikuwa bado zinahitajika kwa ajili ya ujenzi wa tasnia hii ya kitaaluma.
Kutokana na kujizulu, Makamu wake, Deodatus Balile atakaimu nafasi ya Makunga hadi taratibu za kujaza nafasi hiyo itakapokamilika.

JPM amrudishia hadhi ya ubalozi Profesa Mahalu


Dar es Salaam. Rais John Magufuli amemrudishia Profesa Costa Mahalu hadhi ya ubalozi kuanzia leo Machi 17, 2018.
Profesa Mahalu alisimamishwa kazi na kuvuliwa hadhi ya ubalozi mwaka 2007 baada ya kufunguliwa mashtaka ya Jinai na Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Hata hivyo, mwaka 2012, Mahakama ilitoa hukumu kwamba, Profesa Mahalu hakuwa na hatia.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika MasharikiProfesa Adolf Mkenda  inabainisha kuwa kutokana na taratibu za utumishi, mtu yeyote ambaye amewahi kutumikia katika cheo cha balozi, huendelea kupewa heshima ya balozi katika maisha yake yote hata baada ya kustaafu katika nafasi ya utumishi wa umma.  
“Kutokana na uamuzi wa rais, Profesa Mahalu sasa ataendelea kuwa na heshima ya kuitwa balozi,” ilinukuu sehemu ya taarifa hiyo.

UN yazitaka nchi kuwekeza katika rasilimali watu



Dar es Salaam. Mkurugenzi mkazi wa Umoja wa Mataifa (UN) nchini Alvaro Rodriguez amesema ili nchi zote duniani zitatue changamoto zake ni muhimu wananchi na viongozi wao kuwa na utashi wa kuwekeza katika rasilimali watu.
Rodriguez amesema hayo leo Machi 17 wakati alipotembelea maonyesho ya picha zinazohamasisha utekelezaji wa malengo endelevu ya dunia (SDGs), yaliyoandaliwa na kampuni ya Sahara Ventures na kufanyika katika makumbusho ya taifa jijini hapa.
"Kumaliza umasikini sasa si suala linalohitaji utaalamu bali utashi wa watu na utashi wa kisiasa  ili kila mmoja ajue namna ya kukabiliana na changamoto zinazomkabili," amesema Rodriguez.
Amesema jambo hili si la nchi zinazoendelea tu bali hata zile zilizoendelea kwa kuwa kila siku kuna changamoto mpya huibuka hususani za mabadiliko ya tabia ya nchi ambazo haziwezi kuzuilika bali kuzikabili.
"Kama tunaweza kuwekeza watu wakaeda mwezini tunashindwa nini kuwekeza kutoa elimu bora kwa vijana wetu. Tayari tunajua kuzalisha chakula cha kutosha, kupata maji hata kama yapo umbali gani ardhini na kuyatibu yale yasiyofaa," amesema.
Amesema hali ya sasa ni tofauti na miongo kadhaa iliyopita ambapo dunia ilikuwa inahofia ongezeko la watu na changamoto za baadaye lakini sasa nyingi zinaweza kutatuliwa kikubwa uwekezaji wa kutosha kwa watu.
Kuhusu maonyesho hayo Rodriguez amesema UN miaka yote imekuwa ikihamasisha kueleweka kwa malengo hayo kupitia nyaraka mbalimbali lakini huenda hata nyaraka hizo zimekuwa hazieleweki kwa watu kama ambavyo picha zinaweza kueleweka.

Mwanaharakati ailaumu Serikali kuipuuzia hoja yake kuhusu mitandao ya kijamii


Dar es Salaam. Mwanaharakati wa masuala ya ustawi wa jamii, Lawrence Mabawa ameiomba Serikali kumuunga mkono katika kampeni yake ya kuelimisha jamii kuhusu matumizi chanya ya mitandao ya kijamii.
Mabawa amesema amefikia uamuzi wa kuanzisha kampeni hiyo itakayoitwa 'Washa data tetea Ttaifa' baada ya kubaini ongezeko la watu wanaoitumia vibaya mitandao.
Akizungumza leo Machi 17, Mabawa amesema kwa sasa kuna watu wanahamasisha maandamano wakiamini kuwa hawawezi kukamatwa kwa kuwa wamejificha kwenye kivuli cha mitandao.
"Kuna watu hawana nia njema wanataka kuleta maandamano yasiyo na tija, wanawahamisha Watanzania waende barabarani  haya yote ni matokeo ya kutokuwa na elimu sahihi ya mitandao," amesema na kuongeza:
“Hili suala nililiona mapema na nikawafuata baadhi ya viongozi ili nifanye kampeni hii lakini wakanipuuza matokeo yake ndiyo haya.”
Akizungumzia maandamano hayo amesema hayana tija na hayawezi kufanikiwa.
"Huwezi kuitisha maandamano kwenye nchi ambayo  wanyonge na maskini wanasikilizwa na watawala, wananchi wanatatuliwa shida zao na serikali ni sikivu, nina uhakika hayatafanikiwa.
"Hata hivyo, hatutakiwi kupuuzia kwa kuwa nchi zilizoingia kwenye machafuko ilianza kama hivi taratibu lazima tutafute ufumbuzi na sio mwingine zaidi ya kuwapa elimu wananchi watumie mitandao vizuri,"amesema Mabawa.
Pia, alimuomba Rais John Magufuli kuitumia kauli mbiu ya ‘Washa data, tetea Taifa’ Siku ya Muungano inayotarajiwa kuadhimishwa Aprili 26.

Polisi wamkamata, wamhoji Mchungaji KKKT



Mchungaji Fred Njama
Mchungaji Fred Njama 
Dar es Salaam. Jeshi la Polisi Mkoa wa Kilimanjaro limekiri kumhoji Mkuu wa pili wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT) Dayosisi Kilimanjaro Kati, Mchungaji Fred Njama.
Hatua ya polisi kumkamata na kumhoji Mchungaji Njama inakuja ikiwa zimepita siku chache tangu kiongozi huyo wa kiroho kutaja mambo sita aliyodai yanaitafuna nchi.
Akizungumza na Mwananchi leo Machi 17, 2018, Kamanda wa Polisi Mkoa huo, Hamis Issah amesema; “suala hilo limeshughulikiwa na kamati ya ulinzi ya wilaya na mimi bado halijanifikia ili niwe na nafasi nzuri ya kulizungumzia.”
Mwenyekiti wa Kamati ya Ulinzi na Usalama ambaye pia ni Mkuu wa Wilaya ya Moshi, Kippi Warioba amesema; “suala hilo siwezi kulizungumza katika simu.” Huku akimtaka mwandishi kufika ofisini kwake na atalizungumzia.
 Akiwasilisha taarifa yake ya hali ya usharika katika mkutano mkuu wa  21 wa usharika huo wa Kiranga,  alitaja mambo hayo kuwa ni kuminywa kwa uhuru wa vyombo vya habari, hali ya uchumi kuwa ngumu, miili ya watu kuokotwa, kuminywa kwa vyama vya siasa na ukosefu wa ajira.

Ma-RC, DC wanatambua kwamba ‘maendeleo hayana vyama’?


Jambo lolote linaporudiwa mara nyingi, hasa na kiongozi mkubwa wa kitaifa, huaminika katika jamii kuwa jambo hilo ndio ukweli wenyewe.
Rais John Magufuli amewazoeza Watanzania jambo moja miongoni mwa mengi. Amekuwa akisisitiza mara kwa mara kwamba “maendeleo hayana chama”. Hivyo ndivyo ilivyo na ndivyo kila mmoja anapaswa kuamini ukweli huo.
Kauli hiyo Rais Magufuli aliirejea hivi karibuni alipokuwa akizindua barabara ya Uyovu- Bwanga, akisema Serikali imefanya maendeleo kwa ujenzi wa barabara, kitu ambacho anachokihitaji kwenye Serikali yake.
Huku akieleza kuna watu hawafurahii maendeleo na ndiyo maana wamekuwa wakijitahidi kufanya chokochoko, Rais alihoji: “Nani afurahi nchi hii inavyokaa kwa amani, nyinyi pale mmekaa yupo wa ACT-Wazalendo na wa Chadema yupo pale amekaa sawasawa, kila mtu na kila mahali wote tunajiona ndugu kwa sababu maendeleo hayana chama.”
Anaongeza: “Tunajenga hospitali ile, huyu wa ACT atashindwa kwenda pale? Barabara hii, wa Chadema si ndiyo wanawahi kwenda kuandamana mle. Hayo ndio maendeleo ninayotaka ya nchi yangu, hayo ndiyo maendeleo ya Watanzania,” alisema Rais Magufuli.
Pamoja na wananchi, viongozi wa ngazi mbalimbali, wakiwamo wateule wake, wanatazamiwa kuwa ndio waumini wakuu wa msemo huu maarufu.
Hata hivyo, baadhi ya wateule wa Rais, hasa wakuu wa mikoa na wilaya, wanaonekana ama hawajaielewa kauli hii au wameamua kutenda kinyume nayo; yaani kwao inaonekana maendeleo yana vyama.
Si jambo la ajabu kuona au kusikia baadhi ya wakuu wa mikoa na wilaya wakitoa kauli au kufanya matendo ambayo ni tofauti na maana ya kauli hii ya “maendeleo hayana vyama”. Wanaona maendeleo hayawezi kupatikana endapo watu wa vyama tofauti vya siasa watawekwa katika kapu moja.
Hawa, ama wametangaza wazi kutoshirikiana na wapinzani au wanafanya vitendo vinavyoonyesha kuwatenga viongozi wa vyama vya upinzani.
Kwa mfano, hivi karibuni Mkuu wa Mkoa wa Manyara, Alexander Mnyeti aliwataka madiwani wa Chadema mkoani humo kuhamia CCM ili aweze ashirikiane nao.
Akizungumza katika mkutano wa hadhara kata ya Haydom wilayani Mbulu Februari 11, 2018, Mnyeti alisema yupo tayari kupokea simu ya diwani wa CCM hata akipigiwa usiku wa manane ili kumpa msaada lakini si diwani kutoka vyama vya upinzani.
kwamba diwani wa Chadema ni ngumu kufanikisha maendeleo ya wananchi kwa kuwa hakuna atakayemsikiliza akiwasilisha hoja zake katika vikao vya halmashauri husika.
“Hata hapa Haydom najua ni ngome ya Chadema..., sasa ondokeni huko mje huku tutekeleze ilani ya uchaguzi ya CCM ya mwaka 2015 - 2020 kwa kuleta maendeleo,” alinukuliwa akisema Mnyeti.
Kauli hiyo ilitokana na swali na mkazi wa kata ya Hayderer, John Tluway kuhusu kutofika kwa mkuu wa Wilaya ya Mbulu, Chelestino Mofuga katika kata yao inayoongozwa na diwani wa Chadema.
Akijibu swali hilo, Mnyeti anasema: “Mkuu wa wilaya ninakupongeza kwa kutofika kwenye kata hiyo kwani ningepata taarifa umefika mara ya kwanza, mara ya pili na mara ya tatu ningekuwa na shaka na wewe, lakini hongera sana kwa kutokwenda,” alinukuliwa akisema Mnyeti.
Katika kusisitiza uamuzi wake huo, Mnyeti akahoji, “Kwanza niwatambue Chadema kama nani? Mimi si NEC (Tume ya Taifa ya Uchaguzi) wala Msajili wa Vyama vya Siasa. Pili nishirikiane nao katika kutekeleza ilani ipi? Nimesoma ilani yote ya uchaguzi ya CCM ya mwaka 2015 sijaona mahali pametajwa Chadema, sasa nalazimika vipi kushirikiana nao?”
Awali alipokaribishwa katika mkoa huo mwishoni mwa mwaka jana, Mnyeti aliweka wazi adhma yake ya kutofanya kazi na wapinzani.
“Chama kinachotawala ni CCM, kama kuna mtu ana itikadi yake aifiche isionekane milele amina mpaka watakapotawala wao. Kwa hiyo tunategemea wote wanatekeleza ilani ya chama, tukikubaini unatekeleza ilani ya chama chako lazima tutakushughulikia.”
Jimbo la Babati Mjini lina mbunge wa upinzani (Chadema) na kwa upande wa madiwani katika kata nane CCM ilipata tatu.
Mbali na Mnyeti, mfano mwingine ni wa Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni, Ally Hapi ambaye amekaririwa akikiri kuwafukuza kwenye ofisi za umma wabunge wa Chadema, Halima Mdee (Kawe) na Saed Kubenea (Ubungo) akisema hakuna sheria inayomlazimisha kuwapa ofisi kwenye jengo la ofisi yake.
Hapi ameongeza kuwa wabunge hao wanapaswa kuwa na ofisi kwenye majimbo yao na siyo kwenye ofisi yake iliyopo katika jimbo la Kinondoni.
“Nimewaondoa ili waende wakakae na wananchi wao huko majimboni. Wanafanya nini kwenye ofisi yangu? Tunataka wabunge wawe karibu na wananchi wao ili wawatumikie,” alisema Hapi akisisitiza hiyo ilikuwa hisani tu.
“Isitoshe, hakuna sheria inayotulazimisha kuwapa ofisi, ‘it is just a privilege’” aliongeza Hapi.
Mwishoni mwaka jana, Mkuu wa Mkoa wa Mbeya, Amos Makala aliomba radhi uongozi wa CCM Taifa baada ya mgombea wa chama hicho kushindwa ubunge katika kata ya Ibighi iliyokuwa miongoni mwa kata 43 zilizofanya uchaguzi wa marudio na chama hicho kushinda katika maeneo mengine yote.
Makalla alisema CCM kushindwa kupata ushindi katika kata hiyo kumeutia doa mkoa wa Mbeya na wapaswa kujitafakari upya.
Wakuu hao wa wilaya ya mikoa ambao ni wenyeviti wa kamati za ulinzi na usalama kwenye maeneo yao, ni miongoni mwa wengine wengi wanaojitokeza kwenye kampeni za vyama vya siasa na ama kuwanadi wagombea wa chama kimojawapo au kuvikandamiza vyama vingine kinyume na majukumu hayo.
Wakizungumzia majukumu ya wakuu wa mikoa na wilaya, wachambuzi wa masuala ya kisiasa wanasema pamoja na wakuu hao kuwa makada wa chama kinachotawala, hawatakiwi kufanya kazi kwa kubagua vyama bali kujikita katika majukumu yao yaliyoainishwa kikatiba.
Maoni ya wasomi
Mhadhiri wa Sayansi ya Siasa wa Chuo Kikuu cha Dar es Dar es Salaam, Dk Richard Mbunda anasema katika sheria ya tawala za mikoa ya mwaka 1997, hakuna kifungu kinachowataka wakuu wa mikoa au wilaya kufanya au kubagua wananchi kwa itikadi za siasa.
“Sheria haijaelekeza popote wakuu wa mikoa na wilaya kufanya shughuli za chama. Wanaofanya hivyo wanafanya kwa utashi wao wenyewe,” anasema Dk Mbunda.
“Ni kweli maendeleo hayana vyama, lakini tunaona viongozi wanaowasumbua wapinzani wanapandishwa vyeo, hii ni tofauti,” anaongeza.
Akijadili kuhusu sheria hiyo, Mhadhiri wa Sheria wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Dk Jesse James anasema licha ya Sheria ya tawala za mikoa ya mwaka 1997 kutokuwa na kifungu cha kuwaruhusu wakuu wa mikoa na wilaya kufanya shughuli za vyama vya siasa, tatizo lake ni kuwa haitoi adhabu kwa anayekiuka.
“Ni makosa kabisa kwa mkuu wa mkoa au wilaya kufanya shughuli za vyama vya siasa, sheria haiwapi mamlaka hayo. Ndiyo maana tumeona wakati wa kampeni kuna wakuu wa wilaya walioshiriki kwenye kampeni walitakiwa kuripotiwa kwenye kamati ya Maadili ya Tume ya Taifa ya uchaguzi (NEC),” anasema Dk James.
Anasema licha ya kuwa wakuu hao ni makada wa CCM, hawapaswi kuonyesha mapenzi yao kwa vyama fulani vya siasa wala kuonyesha ubaguzi kwa vyama vingine.
Hata hivyo, Dk James anasema, “Sheria haisemi hatua watakazochukuliwa hata wakikiuka, labda ukitaka kuwashtaki utumie sheria ndogo na ukusanye ushahidi wa kutosha na mwisho wake mahakama itaishia tu kueleza kosa lake.”
“Kuna watu wanauliza mbona hamshtaki? Ni lazima ujue mfumo wa mahakama zetu, kesi kama hiyo inaweza kuchukua miaka mitatu minne, sasa ina faida gani? Mfumo wa mahakama wenyewe haushawishi watu kushtaki,” anaongeza.
Katiba na majukumu yao
Katiba ya Jamhuri ya Muungano ibara ya 61 (1-5) inawatambua wakuu wa mikoa na kueleza kwa ujumla majukumu yao ambao kwa maoni ya wachambuzi ndiyo yangekuwa mpaka wa utendaji wa kazi kwa kuwa maendeleo hayana vyama.
Inasema, (1) Kutakuwa na Mkuu wa mkoa kwa kila mkoa katika Jamhuri ya Muungano ambaye, bila ya kuathiri ibara ndogo ya (3), atakuwa kiongozi katika Serikali ya Jamhuri ya Muungano.
(2) Wakuu wa Mikoa katika Tanzania Bara watateuliwa na Rais baada ya kushauriana na Waziri Mkuu.
(3) Wakuu wa Mikoa katika Tanzania Zanzibar watateuliwa na Rais wa Zanzibar baada ya kushauriana na Rais.
(4) Bila ya kuathiri masharti ya ibara ndogo ya (5), kila Mkuu wa Mkoa, atakuwa na wajibu wa kusimamia utekelezaji wa kazi na shughuli zote za Serikali ya Jamhuri ya Muungano katika mkoa aliokabidhiwa; na kwa ajili hiyo, atatekeleza kazi na shughuli zote zilizotajwa na sheria, au kwa mujibu wa sheria kama hizi au shughuli za Mkuu wa Mkoa na atakuwa na madaraka yote yatakayotajwa na sheria yoyote iliyotungwa na Bunge.
(5) Pamoja na wajibu na madaraka yake yaliyotajwa kwenye masharti yaliyotangulia ya ibara hii, Mkuu wa Mkoa kwa mkoa wowote katika Tanzania Zanzibar atatekeleza kazi za shughuli za Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar atakazokabidhiwa na Rais wa Zanzibar, na kwa mujibu wa Katiba ya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar 1984 au sheria yoyote iliyotungwa na Baraza la Wawakilishi.
Sheria inayowaongoza
Mbali na Katiba, pia Sheria ya Tawala za Mikoa ya mwaka 1997, inaeleza mamlaka na majukumu ya wakuu wa mikoa.
Miongoni mwa majukumu hayo ni kuhakikisha ulinzi wa sheria na utulivu katika mkoa, kuongoza na kusimamia operesheni za maafa na kufariji, kama mwenyekiti wa Kamati ya Ushauri ya Mkoa (RCC), Mkuu wa mkoa atawajibika kufanya jitihada za kuhakikisha kutimizwa kwa sera za Serikali juu ya mkoa husika.
Kwa kushirikiana na Katibu tawala, RC atahakikisha na kufanya yale yote yatakayosaidia kuimarisha ulinzi na usalama wa mkoa na kuhakikisha serikali za mitaa zinatimiza wajibu wake na kupata hati safi.

NDANI YA BOKSI: Siyo sanaa tu... mpaka mapenzi kama Big G


Mtu mwenye upeo mkubwa, si tu atawapenda adui zake wakifanya vizuri, bali pia atawachukia marafiki zake wakikosea.
Hata serikali yetu pia inafurahishwa na mafanikio ya wanamuziki, na inachukizwa wanapokosea na kwenda kinyume na maadili yanayostahili.
Tuachane na hayo bana. Maana tukiamua kuzama sana hatutamaliza. Na hizi ‘stress’ katikati ya mwezi tukisubiri mabosi wateme mzigo. Tutaishia kurushiana maneno kisha ngumi.
Sasa sikia. Unajua hizi totoz hapo kabla hazikuwa lolote wala chochote. Ni vile tu wamekutana na hawa mabishoo wa sasa watoto wa mama.
Enzi hizo kuna maneno yaliwaponza watoto wazuri na walishituka wakiwa wamechelewa sana. Silaha kuu ilikuwa maneno siyo “siksi paki’ na pesa kama sasa.
Ukitazama kwa jicho la haki kwa maana ya haki. Zamani kulikuwa na masela vichwa sana kuliko mabishoo wa sasa. Madogo wa sasa wamerahisishiwa sana.
Mizuka ya zamani ili ukamatie mtoto mzuri wakati huo ufundi ulihitajika. Ufundi wa kucheza na maneno.
Watoto wa mjini walikuwa mafundi wa maneno bana. Siyo kulamba lips kama hawa wa kizazi hiki. Wakati huo mtoto anabanwa kwenye kona dakika sifuri anaelekea kibra.
Siongelei ‘bushi’ na mitama yao. Kule maneno machache vitendo vingi. Yaani dem anasubiri akatwe mtama badala ya kusubri udambwi udambwi wa maneno.
‘Bushi’ ilikuwa mizinguo sana. Kifupi usijivunie historia ya mapenzi kwa tabia za watu wa Sitimbi huko. Walikuwa wanazingua. Naongelea watoto wa mjini.
Siwezi kujivunia kitu cha kale kama kumtokea demu kupitia rafiki yake ndo akulainishie njia. Ule ulikuwa ubwege kama ubwege mwingine.
Eti baada ya kuonana mara mbili mnapanga siku. Yaani aje kichakani. Au kama vipi chini ya Mwembe fulani hivi amazing hapo kijijini.
Akifika tu swali bila salamu: “Ester alikupa ujumbe wangu?” Naye anajibu “Ndiyo” badala ya kuuliza angekuwa hajaniambia ningekuja hapa?
Anaona aibu. Akijisugua mguu juu ya mguu mwingine. Anang’ata vidole na macho yake yakijenga undugu wa ghafla na ardhi.
Wakati huo naye mwanaume kama bwege utasikia. “Basi ndo hivyo si upo tayari mpenzi wangu... mwenzio nipo hoi juu yako.”
Msichana naye alijikuta “Mi sijui ila nyie wanaume nyie mnajifanya mnatupenda kumbe mnatuchezea tu. Mi naogopa bwana.”
Mpaka hapo kwa sisi wanaume kutoka Tarime. Hatukuchelewesha. Hapo ndo kakubali tayari. Ni kata funua miguu juu. Mtama wa hatari.
Usianze kurudia maneno.
Watoto wa town ndo kuna maneno yalikuwa yanawaponza sana. Utasikia: “Unajua Salome nilipokuona tu moyo ulilia paaaah! nikajiukiza huyu malaika kashuka lini duniani?”
Toka siku hiyo silali kwa ajili yako. Naweweseka juu ya penzi lako Salome. Nalala nikikuota nikishituka usingizini napapasa pembeni sikuoni mpenzi.
Nagundua niko peke yangu kitandani. Sononeko la moyo linaingia na kukaa eneo la usingizi. Matokeo yake mpaka kunakucha nakuwaza wewe tu Salome.
Basi ni vile sina pesa. Lakini wewe Salome ulistahili kununuliwa bahari yote. Coco Beach (Ndege beach ilikuwa maarufu sana wakati huo) iwe yako. Nakupenda Salome.
Yaani hata nikinywa maji nakuona kwenye glasi. Tabasamu lako tamu kama noti mpya ya Nyerere. Niko radhi kufa kwa ajili yako Salome. Naomba unipe nafasi kwenye uvungu wa moyo wako.
Hata kama uvungu umejaa. Niweke kwenye kibaraza. Kama napo hakuna nafasi nitafutie hata banda la uwani nipange kwa muda nikisubiri uniweke ndani ya moyo rasmi. Salome nafsi yangu inateketea kikatili kama siyo kindava juu ya penzi lako. Kuna miale ya moto inachoma kifuani kwangu kila upitapo.
Napenda unavyotabasamu. Unavyocheka. Ukitembea mimi hoi. Hata ukinuna navutiwa na uso wako. Wewe ni malaika unayeishi kimakosa duniani. Tena Tanzania badala ya Ulaya.
Nakupenda sana Salome. Haki ya nani tena. Eh eh eh eh (Kidume unalamba ulimi unapangusa mchanga kisha unalamba tena ulimi), kama mimi muongo nife hapa hapa. (Eti ndo umekula kiapo).
Mpaka hapo mtoto Salome utamuona anazungusha shingo. Miguu ikichora maroroso chini. Tayari hamna kitu tena. Yaani umechukua jimbo bila kusubiri sauti ile ya Jaji Lubuva.
Kama umemwandikia barua unakakikisha ndani umenyunyizia na poda. Umemchorea ua na mkuki umepenya kwenye alama ya kopa (moyo).
Wakati madem wa sasa watakuuliza “Kwani shingapi?”
Zamani ungeambiwa ngoja afikirie kwanza. Hapo masela wa kitambo tulijua tayari. Mtoto kaelewa. Kishatafunwa.
Miluzi mingi hata kama siyo ya mdomoni basi ya kwenye bandama, figo, mapafu na kongosho. Lazima zipige makofi. Humuachii aondoke unakaza zaidi ili zigo upewe siku za karibuni.
Siku hizi bana siyo poa hata kidogo. Siku ya kwanza mnakutana baa mitungi mingi michemsho na stori kadhaa. Jiwe mbili mezani anajikataa. Ndo tayari hivyo.
Totoz za kitambo kile maneno matamu yaliwavua nguo. Siku hizi pesa mezani ndo inawavua nguo. Kifupi wanaingiza pesa kila mwisho wa wiki kama kina Ronaldo.
Mtoto hotelini haangalii runinga wala sura yako. Yeye macho kayaelekeza kwenye pesa mezani akikadiria ziko ngapi na yeye utampa ngapi.
Unadhani hapo atafika Kibo au Mawenzi? Hawezi. Wanaishia kusema wanaume wa Dar hamna kitu. Kumbe wao ndiyo matango pori kutoka Ikwiriri.
Unampa pesa. Unamlisha na kumnywesha na bado anataka akupe adhabu ya kumfikisha Kibo au Mawenzi. Zamani dem ukimpa hela anakataa kwa kuogopa kwao ataulizwa kaitoa wapi. Siku hizi sijui pesa zenyewe wanafanyia nini maana hawaendelei na zaidi wanachoka nyuso zao kama kuta za selo za polisi.
Mkikutana iwe njiani, kwenye starehe au katika magroup ya whatsApp. Mnapeana namba. Mnachati, mnaalikana. Tayari wapenzi na wivu juu.
Kuna siku nilileta za kizamani. Nikaanza maneno yangu dem ananikodolea macho tu. Mwisho nikaambiwa nimekusikia andaa changu kesho nakuja kwako.
Duh...
Magufuli kaweka watu sawa kabisa. Warembo waliokuwa wanategemea kuwekwa mjini na wanaume siku hizi wamefulia. Wengine ‘bize’ na matangazo ya Waganga mitandaoni wapate pesa za saluni.
Demu ambaye umetumia nguvu nyingi na muda mrefu kumpiga ‘saundi’ anavutia sana, kuliko wa kumnyakua kaa bando la chuo.
Siyo muziki tu pia mapenzi ya sasa yanakinai upesi. Yaani watu hawadumu kwenye uhusiano kama zamani. Nyakati za sasa na mazingira yake yanahatarisha neno upendo.
Kinachotokea ni kwamba wanaume wanatongoza kirahisi wasichana. Na wasichana wanakubali kirahisi sana. Sasa kwa nini mwisho wa mapenzi uwe mgumu? Lazima uwe rahisi tu.
Ndani ya mwaka jana tu. Aslay alitoa nyimbo nyingi sana. Wasafi na bosi wao Diamond walitoa nyimbo nyingi sana ndani ya mwaka mmoja. Kama “Bigi Jii’ vile. Nyimbo zilibamba ghafla na kutoweka ghafla.
Muziki wa sasa unaisha utamu haraka kama ambavyo uhusiano wa sasa unavyoisha haraka kwa wapendanao. Utandawazi umekuja na faida kubwa sambamba na ukubwa wa matatizo.
Zari ‘The Boss lady’. Alikutana kwenye ndege na mzazi mwenzake na kuanza penzi ghafla. Mimba ghafla. Mimba ya pili ghafla. Kisha wameachana ghafla kupitia Instagram.
Siyo sanaa tu. Ukifuatilia sana kila kitu hakidumu dunia ya sasa. Kanumba kaondoka 2012 bila kuijua whatsApp. Kaacha BBM na Facebook. Leo hii ndani ya miaka sita tu kuna mpaka Snapchat.

Mama Kanumba azungumzia kumtembelea Lulu na tofauti zake na familia ya mwigizaji huyo


Mama wa marehemu Steven Kanumba, Flora Mtegoa, amesema anatamani kwenda kumuona mwigizaji Lulu anayetumikia kifungo cha miaka miwili jela lakini kwa bahati mbaya hawana maelewano na familia yake .
Akizungumza na gazeti hili amesema kama mzazi anaumizwa na hali anayopitia Lulu na angetamani kwenda kumuona ili kumpa moyo lakini ndio hivyo ndugu zake wanamuona kama yeye ndiyo kasababisha afungwe.
Amesema wanaomlaumu wanapaswa waelewe kwamba yeye alishasamehe kwani hata angefungwa miaka 100, haiwezi kumfanya Kanumba arudi.
“Tangu Lulu kahukumiwa nimekuwa nikipokea lawama na watu kunitusi kuwa mimi ndio sababu huku wakisahau kwamba mimi nilishasamehe kama binadamu na pia sio niliyekuwa mlalamikaji katika kesi hiyo isipokuwa alishatakiwa na Serikali, lakini yote namuachia Mungu kwani naamini kufungwa kwa msichana huyo hakuwezi kunirudishia mtoto wangu,” amesema.
Novemba 13, mwaka jana Lulu alihukumiwa kifungo cha miaka miwili baada ya kupatikana na hatia ya kumuua bila kukusudia mwigizaji mwenzake, kanumba.
Kauli hiyo ya mama Kanumba imepokelewa tofauti mtandaoni wengi wakinukuu kauli yake ya kusema anashukuru mahakama imetenda haki kwa kumpa adhabu ya kifungo binti huyo.

Sababu ya Dk Masanja kuanzisha chuo cha kilimo


Wakati mtazamo wa wawekezaji wengi katika sekta ya elimu ukiwa ni kufungua shule au taasisi zinazotoa kozi ambazo kwa wengi ni kozi zinazolipa, wapo wenye mtazamo tofauti.
Uzoefu unaonyesha ili ujihakikishie wanafunzi wa kutosha unapofungua chuo nchini, huna budi kutoa kozi kama kompyuta, uhasibu, afya, uandishi wa habari, utawala na nyinginezo. Huko ndipo walipowekeza wawekezaji wengi binafsi.
Hata hivyo, kuna wawekezaji wachache wanaoona fursa kwenye sekta ya kilimo. Miongoni mwao ni Dk Aloyce Masanja aliyeamua kuanzisha chuo cha masuala ya kilimo na ufugaji.
Kwa muda mrefu Serikali ndiyo imekuwa mwekezaji pekee kwenye sekta hiyo, lakini sasa nguvu imeongezeka kwa kuwapo taasisi binafsi kikiwamo chuo hiki.
Dk Masanja ambaye pia ni Mkurugenzi wa Chuo kijulikanacho kwa jina la Canre, anasema haikuwa kazi rahisi kuwavutia wanafunzi kusoma kozi za kilimo lakini sasa mwitikio umekuwa mkubwa.
Chuo hicho kilichopo Bonyokwa, Segerea jijini Dar es Salaam, kilianzishwa mwaka 2006 huku kikiwa na wanafunzi wawili, lakini sasa kina zaidi ya wanafunzi 600.
“Mwitikio ulikuwa mdogo sana kwa wanafunzi kusomea masomo ya kilimo; kuna wakati nilikuwa najiuliza hivi mimi nitaweza kweli mana niliona kama masomo haya ya kilimo hayapendwi hata hivyo sikukaata tama,”anasema.
Anasema baada ya chuo hicho kusajiliwa mwaka 2010 wanafunzi waliongezeka huku mwitikio kwa wasichana kusomea kilimo ukiwa mdogo.
“Lakini sasa hivi naona vijana wanaongezaka na kwa mtazamo huu natarajia kuona wataalamu wengi wa kilimo wanatoka hapa na kwenda kukomboa wananchi katika masuala ya kilimo na ufugaji,”anaongeza.
Kilichomsukuma kuanzisha chuo cha kilimo
Anasema wazo la kuanzisha chuo cha kilimo lilikuja baada ya kuona sekta ya kilimo haina maendeleo ya kuridhisha kwa maana kwamba watu wengi wanaikimbia na hata waliokuwa wakilima na kufuga, hawakufanya kitaalamu.
Anasema kilimo ni uti mgongo lakini hakiwezi kuwa na tija kama hakutakuwa na wataalamu wa kutosha watakoashauri wakulima hasa katika maeneo ya vijijini.
Kabla ya hapo alikuwa na utaratibu wa kwenda kutembelea nchi mbalimbali kuona maeneo gani yanakwamisha Watanzania wenye nia ya kufanya kilimo na ufugaji.
“Mfano nilipokwenda Japani nilikuta watu wanalima tena kwa kutumia enao dogo tu lakini wanavuna mazao mengi, nikasema kwani sisi Tanzania tunashindwaje?
Nikaweka nia kwamba lazima niikomboe nchi yangu katika masuala ya kilimo,”anasema.
Anasema pia kilichomvuta kuanza chuo hicho ni kwamba alizaliwa kwenye familia ya wakulima hivyo kuanzia elimu ya msingi, sekondari hadi chuo alijikita zaidi katika masomo ya kilimo.
“Nimefikiria sana nikaona hapa nchini vyuo vingi vya binafsi ni vya fani nyigine nikaona kwa nini nisianzishe chuo cha kilimo ili kuongeza nguvu kile cha Serikali tuweze kuzalisha wataalamu wa kutosha,” anasema.
Anasema alichokiona ni kwamba jamii inashindwa kutambua kuwa kilimo ni sehemu ya ajira. Wapo wanaolima zao la aina moja tu wakidhani kwamba mazao mangine hayana faida.
“Sasa hivi kilimo ni biashara, nchi za wenzetu wanafanya kilimo hadi cha maua lakini kinalipa lakini kwa Tanzania mtu anaona maua ni kwa ajili ya kupendezesha nyumba yake tu lakini kumbe maua ni mtaji,”anasema.
Alivyoanzisha chuo hicho
Kwa kuwa alikuwa mwajiriwa katika Wizara ya Kilimo kwa miaka 20, hakutaka kupoteza ujuzi wake hivyo wazo la kuanzisha chuo hicho likaanzia hapo.
“Katika eneo hili kulikuwa pori kubwa kwa bahati nzuri nilikuwa nalima mahindi, migomba, nilikuwa pia nafuga kuku na samaki nikaona ni vyema nianzishe chuo cha kilimo na ufugaji,”anasema Dk Masanja.
Hata alipokuwa masomoni nje ya nchi akichukua Shahada ya Uzamivu, aalijikita kwenye masuala ya kilimo na ufugaji, lengo likiwa kuja kuisaidia jamii nchini baada ya kuona haijahamasika katika sekta hiyo.
“Basi baada ya hapo nilianza na wanafunzi wawili na walimu wawili nilienda nao hivyo hivyo japo mwanzo ulikuwa mgumu lakini sikukata tamaa na safari yangu ya kuwakomboa wakulima,”anasema.
Kwa nini watu wanakimbia kilimo?
Dk Massanja anasema: “Nilichokiona hapa ni mtazamo wa wengi kufikiria kwamba kiilimo ni cha wazee na hata ukiangalia asilimia kubwa watu wanaishi kijijini kwa hiyo huku mjini mtu anaona kilimo hakina tija.’’
Kutokana na zana zinazotumika kutokuwa za kisasa ndiyo maana wengi wanasema kilimo hakilipi.
“Mkulima anatakiwa kujua kilimo kina maana gani kwake, wengi wanalima kimazoea na wengi wanashindwa kwa sababu hawajapata elimu ya kutosha kilimo kina maana kubwa sana ndani ya jamii,”anasema.
Anasema uwepo wa vyuo vya kilimo nchini utakiongezea tija kilimo kwani ni wachache wenye mwamko na kutambua umuhimu wa kilimo, hivyo ni vyema Serikali ikaongeza juhudi ikiwemo kuongeza sehemu za mafunzo.
“Lakini pia hata sera ya Serikali ya kilimo ya mwaka 2013 mimi nilivyoiona imetoa mwelekeo mzuri na imegusa karibu maeneo yote muhimu, kwa hiyo sasa hivi watu wameanza kupata ufahamu kuwa kilimo sio kwa ajili ya chakula tu bali kilimo ni biashara,”anaongeza.
Changamoto
Dk Masanja anasema tangu ameanzisha chuo hicho amepitia changamoto mbalimbali ambazo kama sio ujasiri wake zingeweza kumkatisha tamaa na kurudisha nyuma malengo yake ya kukomboa wakulima.
Moja ya changamoto hizo ni kutoaminiwa na taasisi za kifedha wakati wa kuomba mkopo, kwani anasema kutokana na chuo hicho kuwa na wanafunzi wachache walihisi asingeweza kulipa.
Changamoto nyingine ni kutoungwa mkono na Serikali.
Anasema mbali na chuo hicho ni kuiinua sekta ya kilimo kwa kuzalisha wataalamu wa kilimo, lakini bado Serikali haiungi mkono juhudi zao.
“Mimi sikufichi nimetoa zaidi ya wanafunzi 2000 tangu naanzisha hiki chuo, lakini hakuna hata kiongozi mmoja aliyekuja kuona wala kuangalia ninachokifanya. Ningefarijika pengine hata masuala ya kodi wangenipunguzia,” anaeleza
Anasema suala la kodi lina mtesa kwani wakati mwingine hadi vifaa anavyopatiwa kama msaada analazimika kuvilipia kodi.
Mbali na changamoto hizo anasema kwa kuwa amedhamiria kuwa mkombozi wa kilimo na ufugaji. Anasema mbali na kutoa elimu kwa ngazi ya astashahada na stashahada, ana lengo la kuanzisha chuo kikuu.
“Mimi sitoishia hapa, nitaenda mbali zaidi kwa kuanzisha shahada ya kilimo na mifugo na tayari eneo nimeshalitenga kwa ajili hiyo,”anasema.
Mafanikio yake
Masanja anajivunia kuona wanafunzi waliotoka chuoni kwake wakiajiriwa katika halmasahauri mbalimbali wakitoa huduma ya masuala ya kilimo kwa Watanzania.
“Hayo ndiyo mafanikio yangu mimi, siwezi kujivunia nyumba wala mali nilizonazo kwa kuwa lengo langu ni kutoa elimu ya kilimo kwa vijana kwa hiyo najivunia kupiga hatua kubwa,” anasema.

Varshita Staa wa maigizo Afrika Mashariki


Anatamba katika mchezo mpya wa kuigiza Varshita unaorushwa katika chaneli ya Maisha Magic East. Varshita ni zao la tamthilia pendwa ya Auntie Boss uliomtambulisha mwanamke huyu.
Kabla ya kuwa staa wa mchezo huo, alishiriki kutayarisha na kucheza kama mwigizaji mkuu wa Tamthilia ya Aunt Boss inayorushwa pia katika kituo cha telecisheni cha NTV cha nchini Kenya.
Ni mmoja kati ya mastaa wa maigizo Afrika Mashariki anayependwa kwa wakati huu. Eve D’souza, ndiyo jina lake halisi lakini Varshita ndio linalotambulika zaidi.
Varshita amezungumza na mwandishi wa Gazeti la Daily Nation, Hilary Kimuyu na kueleza mengi kuhusu sanaa ya maigizo, maisha yake binafsi na matatarajio yake.
Unajisikiaje kuwa Mkenya wa kwanza kuwa na tamthilia iliyotokana na tamthilia?
Nadhani hatujapata muda wa kutafakari kuhusu mafanikio hayo mimi na mwenzangu (Lucy Mwangi). Ilipoanza tamthilia ya Auntie Boss watu walikuwa wakitupongeza lakini kwa sababu tulikuwa bize tukiendelea kurekodi hata hatukupata wasaa wakujua kinachoendelea mtaani. Hata sasa nipo bize narekodi vipande vya Varshita kusema ukweli sipati muda wa kukaa kutafakari kwa sababu kila kunapokucha nipo kazini na ninafanya kazi mpaka usiku mkubwa.
Ni ipi tofauti kati ya tamthilia hizi mbili: Auntie Boss na Varshita
Waigizaji wakuu katika tamthilia ya Auntie Boss ni wafanyakazi wa ndani (House girl). Wazo la kutengeneza tamthilia ya Auntie Boss lilikuja baada ya mimi na rafiki yangu Lucy kuzungumza kwa saa mbili kuhusu visa vya wafanyakazi wa ndani tulivyokutanan navyo. Hapo ndipo tukaulizana kwanini tusitengeneze tamthilia ambayo wafanyakazi wa ndani watakuwa mastaa. Kuhusu kuanzisha tamthilia ya Varshita kulitokana na kinachoendelea katika Auntie Boss.
Unaweza kuona Varshita alivyoingia katika tamthilia. Ni mwanamke mkorofi, aliyejaa vituko na mwenye hila. Hata kwenye kurekodi Auntie Boss ilibidi watayarishaji wapunguze nafasi ya Varshita na Don kwa kuwa walikuwa waking’ara kuliko wahusika wakuu.
Lucy akasema hapana, inabidi tutenganishe stori ya hao watu wawili na kwa bahati nzuri tulipopeleka wazo letu Mnet walilifurahia sana.
Walifurahi kwa sababu hakukuwahi kutokea shoo yenye maudhui kama hii ya wapenzi wenye asili ya India na Kenya na kwamba kumekuwa na ubaguzi wa hali ya juu.
Varshita imepokelewaje?
Imepokelewa vizuri sana lakini kuna kitu kinanisumbua kichwa kwamba mashabiki wetu wengi ni watoto. Unakutana na mzazi anakwambia mtoto wangu anakupenda sana anasema akiwa mkubwa anataka kukuoa. Yaani watoto wanatuona kama katuni.
Una mpango wa kuzipeleka tamthilia katika filamu?
Varshita ilipoanza nilijisemea sipendi kutoa tatmhilia ndani ya tamthilia kama tulivyofanya kwa sababu nyingi ninazozifahamu hazikufanikiwa. Tulipokubaliana kutengeneza Varshita nilikuwa na wasiwasi sana huenda isifanikiwe. Ndivyo ninavyofikiri kwenye filamu. Sipendi filamu na kama itabidi kufanya hivyo tutatumia staili ya Bollywood.
Kuna uwiano wowote kati ya Varshita na maisha yako halisi?
Ninachopenda kucheza nafasi ya Varshita ni kwa sababu ni watu wa aina tofauti na mimi. Mimi ni mkimya nisiyependa migogoro na watu wala mabishano.
Varshita ni mkorofi, mimi ni mpole. Varshita hana huruma wakati mimi siwezi hata kusikiliza simulizi ya kusikitisha bila kutoa machozi.
Unautumiaji muda wa ziada?
Napenda kupika lakini kwa bahati mbaya napata siku oja tu ya kuwa jikoni. Ninafanya kazi kuanzia Jumatatu mpaka Jumamosi.

Raia wakimbia kutoka Ghouta mashariki

Mashambulizi ya anga yamewauwa dazeni kadhaa za raia Ghouta mashariki Ijumaa (16.03.2018)na maelfu wengine kulazimika kukimbia, wakati majeshi ya Syria yakiendelea na mashambulizi makali katika ngome ya mwisho ya waasi.

Syrien Massenflucht aus Ghuta (Getty Images/AFP/L. Beshara)
Vifo  hivyo vya  hivi  karibuni  kabisa  vimefikisha  idadi  jumla ya mashambulizi yaliyodumu karibu  mwezi  mmoja  kufikia  watu 1,350,  huku  mataifa  makubwa  duniani  bado yakishindwa  kuzuwia  moja kati  ya  mizozo  mibaya  kabisa iliyosababisha  uharibifu.
Vita  nchini  Syria  vinaingia mwaka  wa  nane  kwa mashambulizi mengine  yanayosababisha  mauaji yakijitokeza  pia  upande  wa kaskazini, ambako majeshi  yanayoongozwa  na  Uturuki yameendelea  na  mashambulizi kulikamata jimbo  linaloishi  Wakurdi wengi  la  Afrin.
Syrien Massenflucht aus Ghuta (Getty Images/AFP/L. Beshara)
Misururu ya watu wakikimbia kutoka Ghouta mashariki
Operesheni  hiyo imesababisha  maelfu  ya  watu  kukimbia, huku mashambulizi  ya  mabomu  dhidi  ya  mji  wa  Afrin jana  Ijumaa yakiuwa  watu 43, theluthi  yao  wakiuwawa  katika  mashambulizi ya anga katika  hospitali.
Ukingoni mwa  mji  wa  Ghouta, eneo  kubwa linaloishi  watu  wa vijijini likiwa umbali mfupi  kutoka Damascus na rahisi  kufika makombora, zaidi ya  raia  2,400 walikimbia  kutoka  katika  miji iliyoharibiwa, wakibeba vitu  vichache katika  mifuko  na vilivyofungwa  katika  nguo.
Makundi ya  watu  yalijikusanya  katika  vituo  vya  serikali nje kidogo  ya  Ghouta  mashariki jana  Ijumaa, wakiwa  hawana uhakika watafanya  nini baada  ya  hapo  baada  ya  kuingia  moja kwa  moja  katika  udhibiti  wa  majeshi  ya  serikali  ambayo yamekuwa  yakishambulia  bila  kukoma nyumba  zao kwa  wiki kadhaa.
"Tulikuwa  tuna hofu ya  kuondoka, walituambia  jeshi  litatukamata," alisema  Abu Khaled  mwenye  umri  wa  miaka  35, ambaye  alikuwa akifanya  biashara  ya  kuuza  nguo mjini  Ghouta.
Syrien Flüchtlinge aus Ost-Ghuta (Imago/Xinhua)
Watu darzeni kadhaa wakiwa katika maeneo ya serikali kutoka Ghouta mashariki
"Tulikutana  na  jeshi  na  hatukuona  hivyo, lakini sasa  kimsingi tunaishi kambini," aliliambia  shirika  la  habari  la  Ufaransa  AFP.
Watu wengi zaidi wamekimbia
Balozi wa  Syria  katika  Umoja  wa  Mataifa  Bashar al-Jaafari amesema watu 40,000  wamekimbia  kutoka  Ghouta siku  ya Alhamis, na hatua  hiyo  ya  kukimbia watu  kwa  wingi inaonekana kutokea  bila  ya  serikali  kujitayarisha.
Misururu  mirefu ya  watu  ilionekana  nje  ya  vyoo  vya  umma, na familia  zilizokimbia  makaazi  yao  zililalamikia kukosekana  kwa  maji ama  magodoro.
Katika  ujumbe uliotangazwa kupitia  televisheni  ya  taifa  jeshi  la Syria  liliwataka  raia  wote kutumia eneo  maalum  lililotengwa na jeshi  hilo  kuondoka  kutoka  katika  eneo  hilo, likisema  limekamata asilimia  70  ya ardhi  iliyokuwa  ikidhibitiwa  na  waasi.
Mashambulizi  ya  ardhini  yaliyokuwa  yakifanywa  na  jeshi  la Syria  pamoja  na  wanamgambo  washirika wao yameligawa  eneo la  Ghouta  mashariki  katika  sehemu  mbali  mbali, kila  moja  likiwa linashikiliwa  na  kundi  tofauti.
Genf Syrischer UN-Botschafter Bashar al-Jaafari (Getty Images/AFP/F. Coffrini)
Balozi wa Syria katika Umoja wa Mataifa Bashar al-Jaafari
Yale makundi matatu  ya  wapiganaji  wa  Kiislamu  yamesema  jana Ijumaa yatakuwa  tayari  kufanya  majadiliano  ya  moja  kwa  moja na  Urusi  kuhusiana  na  usitishaji  mapigano  katika  Ghouta, lakini hayakutaja  mazungumzo na  serikali  ya  Syria.
Taarifa  yao imekuja  masaa  machache  baada  ya  mjumbe  maalum wa  Umoja  wa  Mataifa  nchini  Syria Staffan de Mistura  kusema mazungumzo  yanaendelea  kati  ya  Urusi  na  moja  kati  ya makundi, Jaish al-Islam.
Mazungumzo  hayo  tayari  yamesababisha  kuwapo  na  siku  sita za  utulivu katika  mji  mkubwa wa eneo  la  Ghouta wa  Douma. Mji wa Douma  pia ulishuhudia  upelekaji  wa  chakula, na  mamia  ya raia  walipata usafiri  wa  mabasi  kuondoka  kutoka  katika  mji  huo kama  sehemu ya kuwaondoa  watu  kwa  ajili  ya  kupatiwa matibabu.