Ujumbe wa mwenyekiti huyo ambaye pia ni mbunge wa Hai ulitolewa jana na mbunge wa Viti Maalumu wa chama hicho, Anatropia Theonist aliyekwenda Gereza la Segerea kumjulia hali na kubainisha kuwa viongozi zaidi watakwenda ‘kula’ Pasaka na Mbowe na wenzake mahabusu leo.
Mbowe na viongozi wengine watano wa chama hicho wapo Gereza la Segerea tangu Alhamisi iliyopita na watatakiwa kufika katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu Jumanne ijayo kila mmoja akiwa na wadhamini wawili ambao watasaini hati ya dhamana ya Sh20 milioni na kuwa na barua kutoka kwa viongozi wao ama wa vijiji au mtaa.
Uamuzi wa mahakama kuwapa dhamana viongozi hao wa Chadema ulitolewa Alhamisi huku washtakiwa wakiwa hawapo mahakamani ikielezwa kuwa gari lililopaswa kuwapeleka mahakamani limeharibika jambo ambalo limewafanya waendelee kukaa mahabusu mpaka Sikukuu za Pasaka zitakapomalizika.
Kuendelea kwao kuwa mahabusu, kumewaibua viongozi wa Chadema na kubainisha kuwa watawatembelea viongozi hao ili kuwatia moyo.
Waliokumbukwa si viongozi wa Chadema walio mahabusu ya Segerea, pia watafanya hivyo kwa mbunge wa Mbeya Mjini, Joseph Mbilinyi ‘Sugu’ anayetumikia kifungo cha miezi mitano jela na katibu wa chama hicho Kanda ya Nyasa, Emmanuel Masonga.
Mbowe na wenzake wanakabiliwa na jumla ya makosa manane, likiwamo la kuhamasisha uasi, chuki na maandamano yaliyosababisha kifo cha mwanafunzi wa Chuo cha Taifa cha Usafirishaji (NIT), Akwilina Akwilini.
Akizungumza na Mwananchi kuhusu ujumbe wa Mbowe, Anatropia alisema, “Mimi na baadhi ya viongozi tumekwenda kumtembelea leo (jana). Kiukweli viongozi wapo imara sana.”
“Kesho (leo) watakwenda viongozi wengine kuwajulia hali viongozi wetu sita pale Segerea. Mbowe amesema yuko imara, ameniambia niwaeleze wananchi kuwa yuko imara, amewataka wasimlilie yeye, bali waililie Tanzania. Nashukuru tumewakuta wakiwa salama kabisa.”
Mbali na Mbowe, viongozi wengine wanaokabiliwa na mashtaka hayo ni katibu mkuu wa Chadema, Dk Vicent Mashinji, mbunge wa Iringa Mjini, Mchungaji Peter Msigwa, manaibu katibu wakuu John Mnyika (Bara) na Salum Mwalimu (Zanzibar) na mweka hazina wa Baraza la Wanawake la chama hicho (Bawacha), Esther Matiko.
Mjumbe wa kamati kuu ya Chadema na meya wa Ubungo, Boniface Jacob ambaye ni miongoni mwa viongozi watakaokwenda kumuona Mbowe na wenzake leo, alisema maandalizi yamekamilika kwa ajili ya safari hiyo ya gerezani.
Alisema viongozi wa Chadema wa wilaya na kata za Dar es Salaam, wabunge, wanachama na wajumbe wa kamati kuu ya chama hicho wamekubaliana kwenda mahabusu ili kuwapa moyo sambamba na kula nao Sikukuu ya Pasaka.
“Tutawabebea zawadi za Pasaka ikiwamo vyakula viongozi wetu hawa. Sikukuu tutaanzia Gereza la Segerea baada ya kuwaona kila mtu atakwenda nyumbani kwake kwa ajili ya kumalizia Pasaka akiwa na familia yake,” alisema.
Jacob alisema, “lengo la kwenda kuwaona ni kuwapa moyo na mshikamano viongozi wetu. Pia hii itakuwa historia kwa wafungwa na mahabusu wa Segerea.”
Alisema viongozi hao watajigawa, kwani wapo watakaokwenda kuwatembelea Sugu na Masonga waliofungwa katika Gereza la Ruanda, mkoani Mbeya.
Diwani huyo wa Ubungo alisema watafuata taratibu zote zilizowekwa na Jeshi la Magereza kwa ajili ya kupata ruhusa ya kuwaona viongozi wao.
Bavicha nao wamo
Naye mwenyekiti wa Baraza la Vijana la Chadema (Bavicha), Patrick Ole Sosopi alisema ataongoza msafara wa viongozi wa baraza hilo watakaokwenda kuwatembelea viongozi waliopo Segerea.
“Tunataka viongozi wetu wafahamu kuwa kuwekwa magereza ni kusudi jingine la kukipeleka chama chetu mbele, kule kuna watu watapata fursa ya kuzijua siasa za chama chetu, naweza kusema wameendelea kutusaidia kueneza chama chetu katika mazingira yoyote yawe magumu au rahisi,” alisema.
Ole Sosopi pia aliwataka vijana wa baraza hilo kuwa tayari kupambana kwa ajili ya chama.
“Vijana kazi yetu ni kulinda chama na kazi hiyo tutaifanya kwa nguvu zote bila woga, hatutaogopa kufa, tumekaa kimya kwa muda mrefu ila sasa tutapambana kulinda haki ya chama chetu na viongozi wetu ndipo amani ya nchi iweze kuwepo,” alisema.
Magereza watoa kauli
Alipoulizwa kuhusu ujio wa viongozi wa Chadema, Mkuu wa Gereza la Segerea, Kamishna Msaidizi wa Magereza (ACP), Mwanangwa Mandarasi aliliambia Mwananchi kuwa milango ipo wazi.
Alisema utaratibu wa kutembelea wafungwa na mahabusu haujabadilika kikubwa wahusika wafuate utaratibu uliowekwa ili wasivunje sheria. “Kama kuna watu wengi huwa wanaingia kwa awamu ili wote wapate fursa ya kuwaona wanaowahitaji. Sitarajii kama hao viongozi wa Chadema watakuwa wengi kesho (leo) kwa sababu baadhi yao walishaanza kwenda tangu Ijumaa (juzi) na Jumamosi (jana)” alisema Mandarasi.
Mjumbe wa kamati kuu Chadema, Profesa Mwesiga Baregu alisema hatua ya baadhi ya viongozi, wanachama na wabunge kwenda kumuona Mbowe na wenzake ni njema na inawapa faraja kubwa viongozi hao waliopo gerezani.