Sunday, April 1

Daktari: Figo ikipandikizwa, si lazima kuondoa ya zamani


Dar es Salaam. Kama ulidhani upandikizaji wa figo humlazimu daktari kuondoa figo ya zamani ili kuweka mpya, basi umekosea.
Daktari Mkuu wa Kitengo cha Figo, Hospitali ya Taifa Muhimbili, Dk Jackline Shoo alisema hayo na kuongeza kuwa upandikizaji wa figo hauiondoi iliyoathirika au iliyoshindwa kufanya kazi, bali huachwa.
Hata hivyo, daktari huyo alisema figo hiyo huweza kuondolewa pale tu, itakapobainika inaweza kumletea madhara makubwa mhusika lakini kwa kufuata vigezo maalumu.
“Si kila mgonjwa anaweza kuondolewa figo iliyoshindwa kufanya kazi kwa sababu siyo kila mgonjwa anayepandikizwa figo hulazimika kuondolewa ile iliyoshidwa kufanya kazi,” alisema Dk Shoo.
Alifafanua kuwa siyo jambo rahisi kuondoa figo ya zamani kama wengi wanavyodhani.
“Hivyo, wataalamu wanaona hakuna haja ya kuisumbua kwa sababu hata ikibaki haina madhara kwa mgonjwa anayepandikiziwa nyingine,” alisema Dk Shoo.
Alisema kuendelea kuiacha figo ambayo imekuwa kubwa wakati mwingine huleta madhara kwa mgonjwa kama kujaza nafasi ndani na wakati mwingine hata kuisumbua figo mpya.
Dk Shoo alisema kama figo za mgonjwa haziondolewi, kuna namna ambayo wataalamu hufanya katika upandikizaji wa figo mpya.
“Kuiondoa figo ni utaratibu mwingine na sisi hatutaki kuisumbua hii ambayo ilikuwapo, kwa hiyo tunachokifanya ni kuichukua hii mpya na kuipandikiza eneo tofauti na mara nyingi huwa tunaipandikiza kwenye eneo la kibofu.
“Tunavyosema kwenye kibofu, haipandikizwi hapo moja kwa moja, bali kwenye maeneo ambayo figo za zamani zipo.
“Eneo hilo ni juu zaidi, lakini ule mrija ambao hupeleka mkojo kwenye kibofu ndiyo unauchukua kutoka kwenye figo ya zamani na kwenda kuupandikiza kwenye kibofu na mirija ya damu ambayo inatakiwa kuilisha figo inapandikizwa kwenye mirija ya damu ambayo inapita kwenye maeneo ilipowekwa figo mpya.”
Hata hivyo anasema kuendelea kuiacha figo ambayo imekuwa kubwa wakati mwingine huleta madhara kwa mgonjwa kama kujaza nafasi ndani na wakati mwingine hata kuisumbua figo mpya.
Figo mpya hupandikizwa kwenye eneo gani?
Iwapo figo ya au za mgonjwa haziondolewi, Dk Shoo anasema kuna namna ambayo wataalamu hufanya katika upandikizaji wa figo mpya. “Kuiondoa figo ni utaratibu mwingine na sisi hatutaki kuisumbua hii ambayo ilikuwapo, kwa hiyo tunachokifanya ni kuichukua hii mpya na kuipandikiza eneo tofauti na mara nyingi huwa tunaipandikiza kwenye eneo la kibofu,” anasema na kuongeza:
“Tunavyosema kwenye kibofu, haipandikizwi hapo moja kwa moja, bali kwenye maeneo ambayo figo za zamani zipo, eneo hilo ni juu zaidi lakini ule mrija ambao hupeleka mkojo kwenye kibofu ndiyo unauchukua kutoka kwenye figo ya zamani na kwenda kuupandikiza kwenye kibofu na mirija ya damu ambayo inatakiwa kuilisha figo unapandikizwa kwenye mirija ya damu ambayo inapita maeneo ilipowekwa figo mpya.”
Dk Shoo anasema figo hiyo mpya hupandikizwa katika maeneo ya ubavuni lakini mrija unaopeleka mkojo kwenye kibofu unakwenda kupandikizwa kwenye kibofu na mrija wa damu uliokuwa unalisha figo mpya unapandikizwa kwenye mirija ya damu ambayo inaingiliana ili kuifanya figo mpya kufanya kazi.
Mbali ya Muhimbili, kuna hospitali zingine zinazotibu na kupandikiza figo nchini?
Dk Shoo ambaye pia ni bingwa wa maradhi ya figo anasema, kwa sasa huduma za upandikizaji wa figo na kutibu wanazifanya kwa kushirikiana na Hospitali za Benjamin Mkapa (Dodoma), Bugando (Mwanza), Hospitalia ya Rufaa Mbeya na KCMC, ambao baadhi yao wanatoa huduma za usafishaji damu huku Benjamin Mkapa wakiwa tayari wameanza upandikizaji.
Figo wanazopandikizwa wagonjwa zinatoka wapi?
Akizungumzia kuhusu figo anayopandikizwa mgonjwa hutoka wapi, Dk Shoo anasema kabla ya kuanza matibabu kuna vigezo wanavyoviangalia.
Anasema kinachoangaliwa ni iwapo mgonjwa ana vigezo vya kupandikizwa figo mpya na mara zote, figi anayopandikizwa mara nyingi hutolewa na ndugu wa damu.
“Zipo kliniki ambazo wagonjwa huandaliwa kwa kupatiwa maelekezo na anayemtolea figo lazima awe ndugu, ambaye amekidhi vigezo kitaalamu na kisheria na baada ya hapo, uchunguzi wa kiafya hufanyika kwa mchangiaji na anayetakiwa kuchangiwa na vikikamilika, utaratibu wa upandikizaji ndipo huanza.
“Upandikizaji wa figo ni matibabu ya daraja la juu ambayo yanapendekezwa kwa wagonjwa sugu wa ugonjwa huo. Kwasababu humsaidia mgonjwa kupata nafuu na kujisikia vizuri. Lakini kabla ya kupandikizwa, inampasa ahudhurie matibabu ya uchujaji wa damu ambao hufanyika mara tatu hadi nne kwa wiki,” anasema Dk Shoo.
Figo zinavyofanya kazi
Akizungumzia kazi za figo, Dk Shoo anasema figo zina jukumu kubwa katika mwili, sio tu kuchuja uchafu kwenye damu ili kuepukana nao, bali kuratibu madini yaliyomo ndani ya damu, shinikizo la damu na kuchochea uzalishaji wa chembechembe nyekundu za damu.
Anasema figo zina uwezo wa kufuatilia kiwango cha umajimaji wa damu na uongezekaji wa madini kama vile sodiamu na potasiamu na pia tindikali katika mwili mzima, lakini pia huchuja uchafu wa vyakula vilivyosharabiwa mwilini.
Anasema uchafu mkubwa unaochujwa mwilini ni pamoja na urea ya nitrojeni (blood urea nitrogen-BUN) na creatinine (Cr).
“Damu inaposhuka kwenye figo, vichocheo vyake huamua kiasi gani cha maji kiende kuwa mkojo kulingana na wingi wa madini yaliyomo ndani ya damu.”
Gharama za matibabu ya figo
Kuanzishwa kwa kitengo cha figo nchini kitasaidia kuokoa zaidi ya Sh12.4 bilioni ambazo Serikali ilikuwa ikizitumia kwa kipindi cha miaka mitatu kusafirisha wagonjwa wa figo 160 nje ya nchi kwa matibabu.
Utaratibu wa kusafirisha wagonjwa nje ya nchi umekuwa ukifanyika kwa kuratibiwa na Wizara ya Afya, huku ukiigharimu Serikali zaidi ya Sh80 milioni kwa mgonjwa mmoja.
Mkurugenzi wa MNH, Profesa Lawrence Museru anasema huduma ya upandikizaji wa figo ni mwendelezo wa jitihada za hospitali hiyo kuhakikisha huduma hizo sasa zinaanza kupatikana nchini baada ya Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete (JKCI) na Taasisi ya Upasuaji wa Mifupa (MOI) kufanikiwa kwa asilimia 100.
Hata hivyo, takwimu kutoka Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto zinaonyesha maradhi ya figo yameonekana kuwakumba zaidi watu wazima kwa miaka mitatu mfululizo na hakuna mtoto aliyekwenda nje ya nchi kwa matibabu ya figo.
Takwimu hizo zinaonyesha kuanzia Julai 2013 hadi June 2016, Watanzania 160 walikwenda nchini India kwa ajili ya kupandikizwa figo, wakiambatana na ndugu 160 waliokwenda kuwatolea figo hizo.
Dk Shoo anasema baada ya nchi kuanza upandikizaji, gharama ya kumpandikiza mgonjwa imeshuka na kufikia Sh12 milioni ambayo hugharamia mtoaji wa figo na mtolewaji pia, japokuwa anasema bado huduma hiyo haijaanza kutolewa kwa bima ya afya.
“Bima ya afya wanatoa dawa na kuwachangia wagonjwa wanaosafishwa damu, lakini kuhusu gharama za upandikizaji mazungumzo bado yanaendelea baina ya Serikali na Mfuko wa Bima ya Afya (NHIF) ambao wanashauriwa waziingize kwenye gharama zao,” anasema Profesa Museru.
Anasema matibabu ya figo ni gharama na Watanzania wengi wanahudumiwa kwa kadi za bima za afya.
“Mwingine analipa kutokana na uwezo, hatuwezi kumuacha mgonjwa kwa sabbau hana fedha lazima achangie kidogo, wagonjwa wa NHIF ni Sh300,000 kwa dialysis na wanaolipia matibabu ni Sh300,000 na mgonjwa anatakiwa kwa wiki kufanyiwa mara tatu hadi nne, hivyo gharama yake huwa ni Sh900,000 au Sh1.2 milioni,” anasema Dk Shoo.
Hata hivyo bado kuna ukakasi kuhusu gharama za dawa kwa wagonjwa waliopandikizwa figo kwani wamekuwa wakilalamikia gharama za dawa kuwa kubwa. Wagonjwa ambao wamepandikizwa figo, hulazimika kutumia dawa za maisha ambazo kwa mujibu wao, dozi ya mwezi mmoja inagharimu Sh1.7 milioni hadi Sh2.5 milioni.
Imelda Chuwa mgonjwa aliyepandikizwa figo kwa gharama za Serikali Januari 2017, baada ya kugundulika na tatizo hilo Juni 2016, anasema gharama zipo juu na kwa walio wengi wanashindwa kuzimudu. “Changamoto baada ya kupandikizwa figo kwa Watanzania wengi ni dawa za figo zipo juu sana, tunaiomba Serikali ishushe bei ya dawa hizo itusaidie. Utakuta mtu anapata mchangiaji wa figo, lakini analazimika kununua dawa kwa bei ghali, hata kama utapewa figo huwezi kuishi maisha marefu kwasababu bila dawa huwezi kuishi na figo haiwezi ikadumu,” anasema Imelda.
Daktari wa maradhi ya figo Hospitali ya Muhimbili, Priyank Punatar anasema dawa za figo ni kwa wagonjwa ambao wamepandikizwa na wanahitaji kuzitumia kwa maisha yao yote ili Figo walizopandikizwa ziendelee kufanyakazi vizuri.
Anakiri kuwapo kwa changamoto kuhusu dawa hizo kwa wananchi wa kawaida hasa wale wasiokuwa na bima ambao ni vigumu kwao kuzipata kutokana na gharama. “Tanzania tunaziagiza kutoka India au nchi zingine ambazo zinatengeneza ndiyo maana zikifika nchini gharama zinakuwa juu,” anasema Dk Punatar.
Alipoulizwa namna gani wanawasaidia wagonjwa; Dk Punatar anasema “Hospitali na Serikali tunaweza kujitahidi kuwasaidia wananchi ambao hawana bima kupata dawa hizi kwa bei nafuu kidogo, bima wanafanya kazi nzuri wanacover hizi dawa kwa walio na bima ya NHIF wanazipata, lakini wasio nazo tunawatu wa usatawi wa jamii wanasaidia kupunguza gharama kidogo.”

No comments:

Post a Comment