Tuesday, May 28

Waunda timu ya urais Uchaguzi Mkuu wa 2015


Mwanza. Waziri wa Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Samuel Sitta amesema wakati ukifika, yeye na rafiki zake Waziri Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Bernard Membe, Waziri wa Ujenzi, Dk John Magufuli na Waziri wa Uchukuzi, Dk Harrison Mwakyembe, watachagua mmoja wao watakayeona anafaa kuwania urais katika Uchaguzi Mkuu wa 2015.

Waziri Sitta aliyasema hayo jana katika Kongamamo la Mawasiliano katika Nyanja za Digitali la wanafunzi wa Idara ya Uhusiano na Masoko, Chuo Kikuu cha St. Augustine (SAUT), Mwanza.

Mara ya kwanza, Sitta aliwataja rafiki zake hao juzi wakati wa harambee ya kuchangia Kanisa Katoliki, Josephine Bakita, Parokia ya Igoma, Mwanza.

Pia alisema hatagombea tena Ubunge Urambo ya Mashariki baada ya kuwa katika ulingo wa siasa kwa miaka 35 na badala yake ataangalia namna nyingine ya kuwatumikia wananchi huku akigusia mchakato wa kuwania urais ambao, alisema anamwachia Mungu.

“Kwa ubunge nimekwisha waeleza inatosha sitagombea tena kwani miaka 35 inatosha, … lakini hatima yangu ni nini siwezi kujua lakini nina afya nzuri na mmoja wa wanasiasa wakongwe, wenye afya nzuri, mnaona ninavyopendeza... kwa urais namwachia Mungu tutaona,” alisema Sitta.

Alisema yeye rafiki zake hao wana mawazo yanayolingana katika mustakabali wa nchi hii na kwamba wataendelea kutembea sehemu mbalimbali za nchi kuwajengea wananchi uelewa ili wajue kuwa uongozi ni lazima ukae katika mikono salama.

“Tutaendelea kupita katika nchi hii kuwaeleza wananchi kujua uongozi wa nchi hii lazima ukae katika mikono safi na ikitokea mmoja wetu akatamani urais, basi tutaona inavyofaa, lakini tutasubiri watu wanavyosema pia kuhusiana na nasi,” alisema.

Akijibu swali la mwanafunzi wa SAUT kuhusiana na kumuunga mkono Rais Jakaya Kikwete wakati wa Uchaguzi Mkuu uliopita ilhali akijua kwamba hawezi kuwaletea maisha bora wananchi, alisema kwake ilikuwa ni sawa na kuchumbia na kwamba wakati wa uchumba, mchumba huonekana kuwa bora lakini anaweza kubadilika wakati wa ndoa.

“Sikufanya kosa kuwa katika mtandao wa Rais Kikwete, hii ni sawa na kuoa. Unachumbia. Mchumba hawezi kuwa sawa wakati wa ndoa au wa kuwa mke, inawezekana katika kugombea mtu akawa sawa lakini baadaye akajifunua zaidi mambo yake, huwezi kumjua zaidi mtu labda uwe na Umungu,” alisema Sitta na kusema: “Hata wapiga kura huwakuta hilo kwa kuchagua mtu ambaye huenda kinyume na matarajio yao.”

Hata hivyo, alisema kauli hiyo haina maana kwamba Rais Kikwete hakufanya kitu, bali amefanya mambo mengi na kusema uzuri wa uongozi unapimika wakati anapotoka madarakani hasa pale historia inapoandikwa na kulinganishwa na marais wengine wajao na waliopita.

Katika kongamano hilo la SAUT, Waziri Sitta alifuatana na kada wa CCM, Paul Makonda.