Thursday, July 27

Nilichosema Kupitia Sauti Ya America Kuhusu Sakata La Acacia Na Serikali Ya Tanzania

Image may contain: mountain, sky, outdoor and nature

Mbali ya mambo mengine..
- Acacia kwa namna yeyote hawawezi kulipa deni hilo. Itachukua karne nyingi.
- Acacia watapenda kulimaliza jambo hili haraka kwa mazungumzo kwa kutambua kuna makosa wameyafanya.
- Kiasi hicho kimekokotolewa na TRA kwa kufuata ripoti zile mbili na kinaipa nafasi Serikali kuingia kwenye meza ya majadiliano na nguvu ya kushinikiza kupata ( Si kiasi kilichokokotolewa) bali kipande kikubwa zaidi cha keki kwa maslahi ya Watanzania.
- Tutakachokiona hivi karibuni ni kuongezeka kwa spidi ya mazungumzo kati ya Acacia na Serikali.

Serikali: Bei ya karafuu haishuki

anzibar. Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar (SMZ) imesisitiza kuwa bei ya karafuu inayotolewa kwa wakulima haitashuka hata kama bei ya soko la nje itashuka.
Waziri wa Biashara, Viwanda na Masoko Zanzibar, Balozi  Amina Salum Ali amesema  lengo la Serikali katika ni kuwanufaisha wakulima zaidi ili kuwajengea ari ya kulihudumia vyema zao hilo kwa manufaa yao na Taifa kwa jumla.
“Hakuna nchi yoyote duniani inayolipa wakulima bei ya asilimia 80 ya soko la nje kwa mazao ya biashara na wala hakuna zao lolote hapa Zanzibar linalofikia bei ya Sh14,000 kwa kilo zaidi ya karafuu, hivyo nawaahidi wakulima wetu kuwa Serikali haitothubutu kushusha bei ya zao hilo,” amesema Balozi Amina.
Amesema huu ni wakati kwa wakulima na wananchi kwa jumla kushirikiana na Serikali ili kuona zao hilo linaendelea kuimarishwa zaidi ili vizazi vijavyo navyo viweze kunufaika na urithi wa zao hilo ambalo ni mkombozi kwa wanyonge walio wengi.
 “Nawaombeni sana tuliendeleze na tulitunze hili zao letu la karafuu ili vizazi vijavyo visije tulaaumu kwa kutowaachia urithi huu ambao ndio mkombozi wetu katika maisha’’ amesema Balozi Amina.
Akizungumzia magendo ya karafuu, Balozi Amina amewataka wananchi kila mmoja kuwa askari dhidi ya watu wanaofanya magendo ya karafuu na wawe tayari kuwafichua kwa kuwa ni adui wa zao hilo.
Amesema suala la magendo ya karafuu halikubaliki na tayari Serikali imejizatiti kwa kutunga kanuni kwenye Sheria ya Maendeleo ya Karafuu na kuimarisha ulinzi.
Mkuu wa Mkoa wa Kusini Pemba, Mwanajuma Majid Abdalla amewataka wazazi kuacha tabia ya kuwatumikisha watoto katika uchumaji  karafuu.
Amesema uchumaji wa karafuu ni miongoni mwa kazi ngumu hivyo si busara kuwaajiri watoto kufanya kazi hiyo badala yake wawahimize kwenda shule.
 Amesema kuwatumia watoto katika kazi za uchumaji karafuu ni kwenda kinyume cha haki za watoto na wanapopata ajali hukosa haki ya kulipwa fidia kwa vile kwa mujibu wa masharti ya bima hawatambuliki.
Pia, amewaonya wafanyabiashara wanaopita vijijini kununua karafuu mbichi kinyume na uratibu kuwa watashughulikiwa kwa mujibu wa sheria kwa vile kufanya hivyo ni kosa.

Lowassa afunguka miaka miwili nje ya CCM

Waziri Mkuu wa zamani, Edward Lowassa

Waziri Mkuu wa zamani, Edward Lowassa akizungumza wakati wa mahojiano na waandishi wa gazeti la Mwananchi, ofisini kwake jijini Dar es Salaam jana. Picha na Said Khamis. 
Dar es Salaam. Waziri Mkuu wa zamani, Edward Lowassa leo ametimiza miaka miwili tangu aweke historia ya kuwa kiongozi wa kwanza wa ngazi ya juu serikalini kuihama CCM na anasema hajutii uamuzi wake, yuko imara na licha ya kuzuiwa kufanya mikutano, kura zake zinazidi kuongezeka.
Lowassa alichomoka CCM Julai 27, 2015 ikiwa ni siku chache baada ya Kamati Kuu ya CCM kuondoa jina lake na mengine katika kinyang’anyiro cha urais, uamuzi ambao ulizua mtafaruku mkubwa uliosababisha wajumbe wa Halmashauri Kuu kuimba wimbo wa kuonyesha kuwa na imani naye wakati mwenyekiti wa wakati huo, Jakaya Kikwete akiingia mkutanoni.
Siku moja baada ya kujiengua CCM, Lowassa alitangaza kujiunga na Chadema, chama ambacho kilimpa fursa ya kuendeleza “Safari ya Matumaini” aliyoianzisha CCM, kwa kushirikiana na vyama vingine vitatu vilivyoundwa Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa).
Akihojiwa na Mwananchi jana kuhusu miaka yake miwili nje ya CCM, Lowassa alisema pamoja na kupata kura zaidi ya milioni sita za urais, yeye na wapinzani wenzake wanasononeshwa na kunyimwa haki ya kufanya mikutano na kukutana wanachama wao.
Hata hivyo, alipoulizwa ni kwa kiwango gani kunyimwa fursa ya mikutano kumemuathiri, alisema: “Kura zangu zimeongezeka sana, tena sana. Ile tu kutoniona kunaniongezea (kura).
“Nataka kwenda kuwaona (wananchi) lakini siruhusiwi. Nataka kufanya mikutano ya hadhara, siruhusiwi. Sio mimi tu, ni pamoja na wenzangu wote kwenye vyama vya upinzani, hii ndiyo kauli yao.
“Waeleze wananchi na wanachama wa Chadema, nawapenda sana. Natamani kwenda kwao, kuzungumza nao, lakini sipati nafasi.”
Alikuwa akizungumzia amri ya kuzuia mikutano ya hadhara ya wanasiasa hadi mwaka 2020 iliyowekwa na Serikali. Zuio hilo halihusu mikutano ya wabunge na wananchi wao, lakini hawaruhusiwi kualika wanasiasa kutoka maeneo mengine.
Hana lolote la kujutia
Lowassa, ambaye sasa ni Mjumbe wa Kamati Kuu ya Chadema, alisema pamoja na hali hiyo wanayokumbana nayo, hana cha kujutia kutokana na uamuzi wake wa kujiunga na upinzani.
“Sina cha kujutia hata kidogo,” alisema katika mahojiano hayo yaliyofanyika ofisini kwake jijini Dar es Salaam.
“Nadhani ulikuwa uamuzi sahihi. Baada ya kuutafakari wakati ule na sasa, bado naamini ulikuwa uamuzi sahihi.”
Pamoja na hayo, Lowassa aliyewania urais na kupata kura milioni 6.07 sawa na asilimia 39.97 dhidi ya Rais Magufuli aliyepata kura milioni 8.8 (asilimia 58.46), alisema kuna tofauti kubwa kufanya siasa ukiwa CCM na ukiwa upinzani.
Alisema hali ni tofauti kwa sababu kuna changamoto nyingi zaidi kwenye chama cha upinzani ukilinganisha na CCM.
Alisema kuna maswali mengi ambayo yanajitokeza na CCM ilikuwa na muundo na miundombinu ya kukabili mambo hayo, tofauti na ilivyo kwenye vyama vya upinzani kutokana na uchanga wake.
“Hivi vyama bado ni vichanga, havina capacity (uwezo) kama ilivyo CCM. Kweli kuna changamoto nyingi, leo kuna changamoto hii, kesho kuna hii, lakini kubwa ni kuwahusisha wananchi, tupate nafasi ya kuzungumza na wanachama, kujadiliana nao na kufanya nao kazi kutatua changamoto zilizopo,” alisema Lowassa ambaye alikuwa Waziri Mkuu kuanzia mwaka 2005 hadi 2008 alipoachia ngazi.
Kuhusu Chadema, alisema chama hicho kikuu cha upinzani kinakua haraka, kinaongeza idadi ya wanachama na viongozi wengi, hivyo akasema kinachotakiwa ni kujenga uwezo wao.
Alisema uzoefu huo hauwezi kuja kwa siku moja, bali kwa muda mrefu kama ilivyo kwa CCM.
“CCM ni moja ya vyama vikongwe Afrika na ina uzoefu mkubwa. Ukitulinganisha sisi (utaona) tuko nyuma yao, lakini tunayo majukumu makubwa na makali zaidi mbele yetu kuliko wao,” alisema.
Kuzuiwa mikutano
Akizungumzia changamoto zinazoukabili upinzani katika uendeshaji siasa kwa sasa, Lowassa alisema Watanzania wanajua, wanaona na wanasikia kwamba vyama vya upinzani vinanyimwa haki hiyo.
“Pamoja na kura milioni sita tulizozipata za urais, hatuna haki. Haturuhusiwi kufanya mikutano ya hadhara. Hili ni jambo gumu sana kulielewa. Ni jambo baya sana katika demokrasia,” alisema Lowassa ambaye mikutano yake ya kampeni ilikuwa ikifurika watu kila alipoenda.
“Ni jambo lisilokubalika katika jamii ya kimataifa, lakini imewekwa kwamba ukifanya mkutano wa hadhara unakamatwa unapelekwa mahakamani.
“Sasa hiyo inatunyima nafasi ya kuwasiliana na wanachama wetu. Lakini Katiba ya nchi hii imeruhusu vyama vya siasa vishindane bila kupigana. Tupingane bila kupigana. Vyama vimeruhusiwa kufanya hivyo. Serikali kuzuia mikutano ya hadhara ni blow (pigo) kubwa kuliko zote tulizopata katika uongozi wa vyama vya upinzani.”
Alisema kuzuia mikutano ni kukwaza wananchi.
“Kama hatupati nafasi ya kushindanisha sera zenu, mtakuwa mnawakwaza wananchi na mtakuwa mnakwaza demokrasia katika nchi,” alisema.
Atajwa uchaguzi Kenya
Wakati Lowassa na wenzake wakiwa wamezuiwa kufanya mikutano ya hadhara, jina lake limeibuka kuwa gumzo nchini Kenya ambako kampeni za Uchaguzi Mkuu utakaofanyika Agosti 8, zinaendelea.
Baada ya kuhudhuria mazishi ya aliyekuwa Waziri wa Mambo ya Ndani wa Kenya, Joseph Nkaissery, Lowassa alifanya mahojiano na vyombo tofauti vya habari, na tangu hapo amekuwa akitajwa kila mara kwenye majukwaa ya kisiasa.
“Sijisikii lolote jina langu kutajwa Kenya, ila hiyo ndiyo siasa. Mimi ni mwenyekiti wa Malaigwanani (viongozi wa kabila la Wamasai) wa Afrika Mashariki. Kwa nafasi hiyo nina nafasi ya kwenda Kenya kuzungumza na Malaigwanani wenzangu umasaini juu ya nafasi za kisiasa,” alisema Lowassa ambaye anatuhumiwa na wapinzani wa Nasa kumfanyia kampeni Rais Uhuru Kenyatta wa Jubilee.
“Na kule sikuzungumza siasa. Chama changu kilikaa, tukasema kati ya wagombea wote, anayefaa kuliko wenzake ni Uhuru Kenyatta. Ni bora kuliko wengine wote. Baraza Kuu lilitoa kauli ya kumuunga mkono. Kwa hivyo chama kilitoa uamuzi huo na mimi nautekeleza kumuunga mkono Uhuru Kenyatta.”
Upinzani wa Simba, Yanga
Akizungumzia sababu za kufikia uamuzi huo, Lowassa alisema: “Na nieleze, hatukufikia uamuzi huo hivihivi, sisi tuna vigezo vyetu. Tunamwona Kenyatta kama mtu anayependa ushirikiano wa Afrika Mashariki. Pale mpakani Wamasai wanapita kwenda na kurudi kila siku ya maisha yao. Usipompata mtu anayependa ushirikiano huo, mtakuwa mmenoa sana.
“La pili, tunaona katika utawala wake, Kenyatta anapenda, anaheshimu sana wapinzani. Anauona upinzani kama ushindani. Na hiyo ni vizuri, ushindani unatakiwa uwe kama wa Simba na Yanga, sio chuki za kisiasa au chuki za kuuana na kupigana.
“Kwa hiyo nilipokwenda kumzika marehemu Nkaissery, walinialika niseme kidogo, na mimi nikasema ‘msirudi mlikotoka maana ni aibu, nikasema mchague mtu atakayesimamia masilahi ya Afrika Mashariki, mtu ambaye ataheshimu upinzani, mtu ambaye mtakubaliana kufanya kazi naye pamoja na nchi zetu zikawa na amani na utulivu.
“Hayo ndiyo niliyasema, nafurahi yamesikika, najua wamenijibujibu lakini ukweli utabaki palepale. Nawatakia wote kila la heri na uchaguzi uende kwa amani. Amani ya nchi ile ni muhimu sana, amani ikiwapo Kenya, pia itakuwapo Tanzania.”
Lowassa alirudia kauli yake kuwa katika Uchaguzi Mkuu 2020 atashinda kwa kishindo na atakuwa tayari kwa uchaguzi huo, lakini kwa sasa wamwachie Rais Magufuli afanye kazi yake.
“Yapo mambo mazuri anayofanya Rais Magufuli, aungwe mkono. Na kwa kiasi kikubwa anafanya mazuri, lakini haya hayajatoka mbinguni, bali ni wajibu wake,” alisema Lowassa.
“Isionekane kama ni salamu kutoka mbinguni, ni wajibu wake kama Rais. Kazi ya Serikali ni kutoa huduma, ni kujenga shule, ni kujenga hospitali. Ndiyo kazi ya Serikali, kwa hiyo watu wasihesabu kuwa ni hisani.
“Wamefanya kazi yao, kwa kweli nawapongeza, lakini wasionekane wamefanya hisani. Kazi za Serikali zote duniani ni kuleta maendeleo kwa watu au kuandaa mazingira ya kuleta maendeleo.”
Mbunge huyo wa zamani wa Monduli alitoa angalizo dhidi ya siasa za chuki alizosema zimeanza kujitokeza nchini, akisema zisipokomeshwa zitaiingiza nchi pabaya.
Alisema vitendo vya wakuu wa wilaya kushindana kukamata viongozi, wanachama na wafuasi wa upinzani kama njia ya kuwakomoa ni vibaya na havikubali.
Alisema sheria hiyo ya kuweka watu ndani kwa saa 48 iliwekwa kwa ajili ya watu wanaofanya fujo kama kwenye mkutano, lakini si kuwakomoa.
Aliwapongeza viongozi walioamua kuwashtaki wakuu wilaya binafsi waliochukua uamuzi huo, akisema mahakama zina uhuru, zitarekebisha hali hiyo.
Kuhusu wimbi la madiwani wa Chadema kujiuzulu mkoani Arusha na sasa Kilimanjaro, Lowassa alisema ingawa kuhama ni haki yao, inasikitisha kusikia kuna watu wanashawishiwa kwa fedha.
“Wale wanaosema wanapenda sera za Rais Mafuguli, nawatakia heri, lakini si wangesubiri hadi 2020, kuhama ni haki yao lakini waeleze sababu halisi,” alisema

Ukawa ilivyoendeleza Safari ya Matumaini


Dar es Salaam. Lilikuwa ni jambo lisilotarajiwa kwamba mmoja wa wagombea urais ndani ya CCM aliyeonekana kuwa na ushawishi mkubwa, angekihama chama tawala.
Mbali na hilo, hakuna aliyeweza kufikiria kuwa mtu aliyewahi kushika nafasi ya juu kama ya uwaziri mkuu, angeweza kuchukua uamuzi mzito kama huo katika nchi ambayo chama tawala ni ‘chama dola’.
Lakini Edward Lowassa alithubutu kufanya hivyo mwaka 2015 alipotangaza kuihama CCM siku kama ya leo na kujiunga na upinzani, ambao hapo awali ulimrushia kila aina ya kombora ukimhusisha na kashfa ya Richmond.
Huo ulikuwa ni mwanzo mpya wa kisiasa kwa Lowassa, mbunge wa zamani wa Monduli, aliyekulia ndani ya CCM na kufanya shughuli zake zote ndani ya chama hicho tawala. Alikuwa na kazi nzito ya kuanza kazi ya kuendeleza “Safari ya Matumaini” nje ya CCM.
Wengi waliamini kuwa uamuzi wake wa kujiondoa CCM na kwenda upinzani ulikuwa ni wa hasira na kama ilivyo kwa wanasiasa wengi, angerejea chama tawala baada ya hasira kutulia licha ya kupewa nafasi ya kugombea urais kwa tiketi ya Chadema na kuungwa mkono na vyama vingine vitatu.
Lakini leo, anapotimiza miaka miwili tangu ajiondoe CCM, Lowassa bado hafikirii wala kuwaza kurejea chama hicho na zaidi ya yote hajilaumu kujiunga upinzani.
“Sijutii kujiunga upinzani,” alisema Lowassa jana katika mahojiano na Mwananchi kuhusu mtazamo wake wa kisiasa katika kipindi cha miaka miwili alichokuwa nje ya chama tawala hadi sasa.
Aliingia kwenye mtihani mkubwa wa kuwania urais akipambana na chama ambacho alikitumikia kwa muda mrefu na kuanzisha “Safari ya Matumaini” ya kuwa Rais, lakini iliyokatishwa na Kamati Kuu ya CCM.
Lakini matokeo ya Uchaguzi Mkuu yalimpa mwanga. Alishika nafasi ya pili katika mbio za urais, akipata kura 6.072,848, ambazo ni zaidi ya mara mbili ya kura ambazo wapinzani walikuwa wakipata tangu mwaka 1995 wakati Uchaguzi Mkuu wa vyama vingi ulipofanyika kwa mara ya kwanza tangu kurejeshwa kwa siasa za ushindani mwaka 1992.
Kura hizo ni sawa na asilimia 39.97 dhidi ya Rais Magufuli aliyepata kura 8,882,935 (asilimia 58.46), kiwango ambacho ni kidogo kwa mgombea urais wa CCM tangu mwaka 1995.
Haikuwa rahisi Lowassa kukubaliwa na kupewa dhamana hiyo ya kugombea urais akiungwa mkono na vyama vinne, baada ya CUF, NLD na NCCR-Mageuzi kuamua kutosimamisha mgombea kwa makubaliano ya Ukawa.
Julai 26, 2015 ikiwa ni siku moja kabla ya kuondoka CCM, mwandishi wetu alimshuhudia Lowassa akihudhuria kikao cha dharura cha Kamati Kuu ya Chadema. Aliwasili lango la Hoteli ya Ledger Bahari Beach, Dar es Salaam saa 3:02 usiku na kupokewa na viongozi mbalimbali wa Chadema wakiongozwa na mwenyekiti wake, Freeman Mbowe. Baada ya hapo aliongozwa kuelekea chumba cha Watu Mashuhuri (VIP) na kukutana na viongozi wachache wa chama hicho akiwamo makamu mwenyekiti (Zanzibar), Said Issa Mohammed. Mazungumzo hayo yalidumu kwa takribani dakika 18 na ilipofika saa 3:20 usiku, walitoka na kuingia ukumbini kwenye kwa ajili ya kikao cha Kamati Kuu.
Lowassa alishiriki kikao hicho kwa takriban dakika 98 na ilipofika saa 4:58 usiku, alitoka akisindikizwa na Mbowe, Willibrod Slaa (katibu mkuu wakati huo), Profesa Abdallah Safari (makamu mwenyekiti) na Salum Mwalimu (naibu katibu mkuu, Zanzibar).
Saa 18 baada ya Lowassa kutambulishwa Kamati Kuu ya Chadema, Julai 28 viongozi wengine wa Ukawa waliitisha mkutano wa wanahabari mchana na kumkaribisha.
Waliokuwapo katika mkutano huo ni wenyeviti wa Ukawa; James Mbatia (mwenyekiti NCCR – Mageuzi), Emmanuel Makaidi (mwenyekiti wa NLD - sasa ni marehemu), Mbowe na Profesa Ibrahim Lipumba (mwenyekiti CUF).
Walitumia mkutano huo kuzungumzia tuhuma dhidi ya Lowassa walizoshiriki kuzitoa, hasa sakata la mkataba wa kuzalisha umeme wa dharura baina ya Tanesco na kampuni ya Richmond Development ya Marekani.
“Sisi tunaponda ufisadi na mfumo wa kifisadi. Chanzo kikubwa cha ufisadi ni mfumo ndani ya CCM. Kwanza tuing’oe CCM, hapo ndipo tutakapoweza kuondoa ufisadi na kujenga msingi wa kupambana na ufisadi na rushwa iliyopo,” alisema Profesa Lipumba.
“Lowassa alikumbwa na tuhuma za ufisadi mwaka 2008, leo ni 2015. Ufisadi umeongezeka au umepungua? Lowassa hayupo serikalini, akaunti ya Tegeta Escrow imetokea wakati gani? Lowassa alikuwapo? Tatizo ni mfumo na jambo la kwanza ni kuing’oa CCM.”
Kuhusu kushirikiana naye wakati walikuwa wanamtuhumu kwa ufisadi, makamu mwenyekiti wa CUF wa wakati huo, Juma Duni Haji alihoji: “Mbona CUF iliwahi kupigana na kuuana na CCM mwaka 2000 lakini leo wameunda Serikali ya Umoja wa Kitaifa?”
Dk Makaidi alisema kama Lowassa angekuwa mbaya kiasi hicho, angekuwa ameshashtakiwa kama ilivyo kwa viongozi wengine ambao tayari wameshahukumiwa vifungo kwa matumizi mabaya ya madaraka au rushwa.
Mbatia alisema Ukawa inamwalika kila Mtanzania aliye tayari kuuondoa mfumo kandamizi na dhalimu wa CCM na watashirikiana naye kujenga Taifa imara na kwamba Lowassa ni miongoni mwa wanaokaribishwa.
Siku moja baadaye, Lowassa alitangaza rasmi kujiunga na Chadema akisema, “Sasa basi, imetosha”.
Alisema amejiunga na chama hicho ili kutekeleza azma yake ya kuwakomboa Watanzania na kuendeleza Safari ya Matumaini kupitia Ukawa.
“CCM imepotoka, imepoteza mwelekeo na sifa za kuendelea kuiongoza Tanzania,” alisema Lowassa katika mkutano wa kumkaribisha Chadema uliofanyika ukumbi wa Hoteli ya Ledger Bahari Beach na kurushwa moja kwa moja na vituo kadhaa vya televisheni na redio.
Lowassa alitumia dakika 13 kueleza sababu za kujiunga na Chadema, mbele ya wenyeviti wenza wa Ukawa katika mkutano huo, ambao haukuhudhuriwa na Dk Slaa, naibu wake (Bara), John Mnyika na Mwanasheria Mkuu wa Chadema, Tundu Lissu.
Wakati Lowassa akizungumza, wanachama wa Chadema walikuwa wakiitikia ‘peoples power’, na alipomaliza hotuba yake waliimba wimbo maalumu wa “Tuna Imani na Lowaasaa”, ambao ni wa kuonyesha mshikamano na ambao uliimbwa na wajumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM kupinga jina la Lowassa kutopitishwa kuwania urais.
Huo ndio ulikuwa mwanzo wa misukosuko ya kisiasa inayohusisha kupambana na vyombo vya dola ambayo hakuwahi kukutana nayo wakati akiwa CCM.
Agosti 29, 2016, akiwa pamoja na wajumbe wa Kamati Kuu ya Chadema na wabunge, walikamatwa na polisi wakiwa katika kikao cha ndani jijini Dar es Salaam na kupelekwa Kituo Kikuu cha Polisi ambako walihojiwa na kuachiwa huru.
Mmoja wa mashuhuda wa tukio hilo alisema: “Tulikuwa kwenye msafara wa kumpokea, lakini tulipofika hapa stendi wananchi walitaka kuongea na Lowassa. Kabla hata hajashuka kwenye gari, askari walituvamia wakasema tuondoke moja kwa moja twende kituoni.”
Ilikuwa ni wakati Lowassa alipofanya ziara kwenye maeneo ya wananchi kuzungumza nao kama sokoni, vituo vya mabasi na hospitali.
Agosti 12, 2015 msafara wake na viongozi wengine wa upinzani waliounda Ukawa ulizuiwa wilayani Mwanga, Kilimanjaro wakati wakielekea kuhudhuria mazishi ya kada wa CCM, Peter Kisumo.
Polisi walitaka Lowassa pekee ndiye aende na viongozi wengine warudi, pendekezo ambalo alilikataa.
Si hilo tu, Januari 16, 2017 polisi mkoani Geita walimkamata Lowassa akiwa anakwenda kwenye kampeni za uchaguzi mdogo wa Kata ya Nkome na baadaye aliachiwa, huku taarifa za polisi zikidai kuwa walimzuia kwa sababu za kiusalama.
Tukio jingine lilimkuta Agosti 23, mwaka jana wakati msafara wake ulipouiwa kwenda mikoa ya Rukwa na Katavi baada ya polisi kuhofu kuwa ungeweza kuingilia ziara ya Waziri Mkuu Kassim Majaliwa.
Na Juni 27, 2017 Lowassa aliitwa polisi kuhojiwa kuhusu kauli zake za kutaka kesi masheikh wa Uamsho wanaoshikiliwa na polisi ziharakishwe na wapewe dhamana. Hadi sasa anaripoti Makao Makuu ya Polisi upelelezi ukiendelea.
Pamoja na misukosuko hiyo, jina la mwanasiasa huyo limeibuka kwenye siasa za nchi jirani ya Kenya, hasa baada ya chama chake kutangaza hadharani kumuunga mkono Rais Uhuru Kenyatta anayepambana na mwanasiasa mkongwe, Raila Odinga.

Profesa Mwaghembe akiri kuendelea kwa ujangili nchini


Tanga. Waziri wa Maliasili na Utalii, Profesa Jumanne Maghembe amesema licha ya vita kubwa ya kupambana na ujangili nchini, bado unaendelea.
Akizungumza leo Alhamisi, Julai 27 katika mkutano na wahariri wa vyombo vya habari nchini Profesa Maghembe amesema wiki tatu zilizopita aliona mizoga mitatu ya tembo katika Rifadhi ya Taifa ya Ruaha.
“Lakini majangili wengi waliokamatwa, kesi zao zimeisha na wamehukumiwa vifungo jela. Tunavishukuru vyombo vya habari kwa kushiriki vita hii, kwani imefanikisha kulipunguza kwa kiwango kikubwa,” amesema.
Akizungumzia suala la kuingiza mifugo ndani ya hifadhi, Maghembe amesema sheria iko wazi inakataza, lakini watu wanaikaidi kwa makusudi.
“Hatari ya kuingiza mifugo ndani ya hifadhi ni kubwa kwa sababu wanyamapori huambukizwa magonjwa mengi. Kama kukiwa na mlipuko wa magonjwa kama ya bonde la ufa, ni hatari kwa mifugo kama ng'ombe kuambukizwa kirahisi na hii inaweza kuwaathiri hata binadamu licha ya watu kuliona kuwa ni jambo dogo,” amesema.
Amesema waandishi wa habari wanapaswa kuielimisha jamii juu ya hilo, ingawa wafugaji huvutiwa na mzingira ya hifadhi wakidhani kuwa wamepata malisho, lakini akasema ni hatari kwa jamii na mifugo yao.
Amesema yapo magonjwa mengi kama ya homa za vipindi ambazo husababisha wanyama kuharibu mimba.

Manji afungua maombi Mahakama Kuu akiiomba mahakama hiyo imuondolee zuio la dhamana

SeeBait
Mahakama Kuu ya Tanzania imesema inatarajia kuanza kusikiliza maombi ya dhamana yaliyotolewa na Mfanyabiashara maarufu Tanzania Yusuf Manji, August 4, 2017.

Jaji Isaya Arufani amesema hayo jana baada ya Mawakili wa Serikali Paul Kadushi na Simon Wankyo kuyapokea maombi hayo na kusema wana nia ya kuyapinga huku Jaji akisema anakubaliana na hoja zao na August 4, 2017 maombi hayo ya dhamana yataanza kusikilizwa.

Katika maombi hayo Yusuf Manji anaiomba Mahakama Kuu itengue hati ya kunyimwa dhamana iliyowasilishwa na Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP) kwa kuwa ana matatizo ya kiafya akisumbuliwa na matatizo ya moyo.

Waziri Mkuu Majaliwa avionya vyuo vilivyozuiwa kudahili wanafunzi

SeeBait
WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa ameiagiza Tume ya Vyuo Vikuu Tanzania (TCU) na Baraza la Taifa la Elimu ya Ufundi (NACTE) kuhakikisha kwamba programu zote zinazotolewa na taasisi za elimu ya juu zinawawezesha wahitimu kujiajiri na kuwa na sifa za ushindani katika soko la ajira kimataifa.

Amesema wakati umefika sasa kwa wasomi katika vyuo vyetu vikuu tujiridhisha kuwa mitaala inayotolewa kama inawaandaa wahitimu kupata taaluma na stadi za kuweza kujiajiri na kupambana na changamoto za kimaisha.

Amesema taasisi za elimu ya juu nchini ziangalie mitaala yake na kuimarisha mfumo wa ithibati na udhibiti wa ubora wa elimu na mafunzo ili kwenda sambamba na dunia ya kazi inayoendana na agenda ya maendeleo ya Taifa.

Waziri Mkuu ametoa agizo hilo jana (Jumatano, Julai 26, 2017) wakati wa ufunguzi wa maonesho ya 12 ya Elimu ya Juu, jijini Dar es Salaam ambapo amevutaka vyuo hivyo badala ya kuendelea kulumbana kwenye makongamano na vyombo vya habari, vifanye maboresho yanayotakiwa ili viweze kuendelea na ufundishaji.

 Aidha alisema kuwa, lengo la serikali ni kuhakikisha elimu inayotolewa inakuwa bora na kwamba maboresho yanayotakiwa kufanyika yanawezekana.

Waziri Mkuu alisema maonesho hayo ni jukwaa la kipekee ambalo litaibua mjadala sahihi kuhusu uhalali wa kozi zinazotolewa na vyuo husika vya elimu ya juu. “Hivyo mnayo nafasi ya kuonesha kwa vitendo uwezo wenu katika utafiti, ubunifu na matumizi ya sayansi na teknolojia zinazotumika katika maendeleo ya viwanda.”

Alisema ni vema mfumo wa ithibati na udhibiti wa ubora wa elimu na mafunzo ukaimarishwa ili kuhakikisha asilimia 60 ya wanafunzi wanahitimu shahada kwenye sekta ambazo zinachangia kwa kiasi kikubwa kukua kwa uchumi.

Alisema taasisi za elimu ya juu ziweke mikakati ya kuinua na kuboresha taaluma wanayoitoa ili ilete tija kwa maendeleo ya Taifa na Dunia. Pia kuanzisha program za mafunzo zenye kukidhi mahitaji na kuleta maendeleo ya kijamii na kiuchumi kwa kuzingatia mahitaji ya kitaifa, kikanda na kimataifa.

Hata hivyo, Waziri Mkuu amezitaka taasisi hizo kuendelea kuimarisha mfumo wa udahili na kujipanga kutumia fursa za elimu na mafunzo ndani na nje ya nchi kwa makundi yote ya jamii kwa usawa katika ngazi zote hususan ufundi, hisabati, sayansi na teknolojia.

Pia Waziri Mkuu alisema ni wakati muafaka kwa taasisi za elimu ya juu nchini kuandaa mikakati ya kuongeza udahili kwa kuzingatia mahitaji ya rasilimali watu na ujuzi unaohitajika katika sketa zinazokua haraka mfano mafuta, gesi na madini.

IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU,
ALHAMISI, JULAI 26, 2017

RC Gambo Ampa Onyo Godbless Lema

SeeBait
Wakati Mbunge wa Arusha Mjini (Chadema), Godbless Lema akisema haogopi kusema ukweli, Mkuu wa mkoa huo, Mrisho Gambo amemtahadharisha kuwa hataacha kumchukulia hatua iwapo atamtukana Rais John Magufuli na Serikali yake.

Lema ambaye ameanza kufanya mikutano ya hadhara katika jimbo lake jana kwenye Soko Kuu la Arusha mjini alisema haogopi kusema ukweli hata kama akipingwa na baba yake mzazi.

“Taifa lipo kwenye mgawanyiko mkubwa, wakuu wa wilaya na mikoa wanafanya maamuzi kwa maelekezo kutoka ngazi za juu,” alisema.

Aliongeza kuwa hali ya demokrasia nchini ni mbaya kwa kuwa hakuna usawa na kuwataka viongozi kuomba hekima wanapopata mamlaka ya uongozi.

Kadhalika amezungumzia hatua ya kujiuzulu kwa Diwani wa Muriet, Credo Kifukwe akisema kuwa Chadema haihitaji jeshi la watu wengi bali la wachache wenye umoja. 

“Nimeteswa sana katika mji wa Arusha, lakini nawataka wafuasi wa Chadema msilipize kisasi kwa wanaohama chama. Leo wapinzani hawaruhusiwi kufanya siasa, lakini Rais anazunguka nchi nzima,”alisema.

Mbunge huyo alisema Tanzania inahitaji demokrasia ya kweli na amani ya nchi haiwezi kutunzwa na polisi isipokuwa kwa upendo wa Watanzania.

Pia, alimtaka Gambo kujipanga wakati wa uchaguzi mdogo wa madiwani kwa kuwa Chadema imejipanga kikamilifu. 

Katika mkutano huo, Lema aliwapandisha jukwaani madiwani wawili wa Chadema jijini Arusha, Obeid Meng’roriki wa Kata ya Terat na Ruben Ngowi wa Kimandolu huku akisema amesikia wanataka kujiuzulu nyadhifa zao.

Hata hivyo, madiwani hao waliposimama walisema wao hawana bei ya kuweza kununuliwa na mtu yeyote.

Wakati Lema akiyasema hayo, Gambo alisema Serikali ya Awamu ya Tano imejipambanua katika utendaji wake, hivyo mwanasiasa yeyote hataruhusiwa kutoa matamshi yenye kumdhihaki Rais na Serikali.

Akizungumza katika mkutano na viongozi wa madhehebu ya dini uliofanyika jana kwenye ukumbi wa mikutano wa AICC alisema:“Tumempa mbunge wa jimbo hili (Arusha Mjini) kibali cha kufanya mikutano na wananchi wake kwa sababu ni kiongozi aliyechaguliwa na wananchi, hatuna sababu ya kumzuia, ila hatutakubali kusikia kwenye mikutano yake akimtukana Rais wetu na Serikali yake. Akifanya hivyo tutamshughulikia.”

“Mtu yeyote anayetaka kuichezea Serikali na kutaka kukwamisha ajenda zake tutawang’oa iwe kwa greda au kwa namna nyingine yoyote, Rais Magufuli alipita nchi nzima akitoa ahadi zake na wamemchagua sasa wamwache atekeleze alichowaahidi wananchi.”

Gambo alitumia mkutano huo kuzungumzia kadhia ya rambirambi zilizotolewa kufuatia ajali ya wanafunzi wa Lucky Vincent iliyopoteza maisha ya watoto na wafanyakazi wapatao 35 na baadaye Meya wa Jiji la Arusha, Kalist Lazaro na Lema kutilia shaka matumizi yake.

TAKUKURU MWANZA YATHIBITISHA KUWAHOJI WANAFAMILIA WA SOKA NA KUWAACHILIA KWA DHAMANA




Mkuu wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa Mkoani Mwanza Mhandisi Ernest Makale.


Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa Mkoani Mwanza (TAKUKURU) imethibitisha kuwahoji wanafamilia wa soka wakiwemo Mjumbe Chama cha Soka Wilaya ya Ubungo (UFA) Shaffi Dauda na Mwenyekiti wa Chama cha Mpira wa Miguu Mkoa wa Dar es salaam (DRFA) Almas Kasongo.


Mbali na hao TAKUKURU wamethibitisha pia kuwahoji Elias Mwanjali, Katibu Mkuu wa Chama cha Soka mkoa wa Mwanza, Leonard Malongo, Mwenyekiti wa chama cha mpira wa miguu Mkoa wa Mbeya Bw. Elias Mwanjaa , Mwenyekiti wa Chama cha Mpira wa Mguu mkoa wa Shinyanga Benasta Lugola na wajumbe wa mikoa ya jirani kwasababu ya kuwepo kwa viashiria vya rushwa na kampeni.

Mkuu wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa Mkoani Mwanza Mhandisi Ernest Makale amethibitisha kuwahoji kwa wanafamilia hao wa mpira ambapo waliwashikilia tokea jana saa 3 usiku na wameachiwa kwa dhamana huku uchunguzi ukiendelea na watakapojiridhisha wanaweza kuwakamata tena.

Taarifa inasema kuwa wanafamilia hao walitumia mgongo wa Ndondo Cup kufanya jambo lao usiku wa saa 3 jana na ndipo walipotiliwa shaka na kufuatiliwa na kutiwa mikononi mwa Takukuru ambao wamethibitisha kuwashikilia tokea jana usiku na kuwaachia kwa dhamana

WABUNGE NENE (8) WA CUF WALIOFUKUZWA KWENYE CHAMA WATOSWA UBUNGE





CHUO CHA MUSLIM MOROGORO WATOA FURSA YA WATANZANIA KUSOMA LUGHA YA KICHINA

MAONESHO ya Elimu ya Juu yanayoendelea katika Viwanja vya Mnazi Mmoja yamefunguliwa rasmi leo na Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano Tanzania Kassim Majaliwa Kassim huku yameonesha mwitikio mzuri kwa vyuo mbalimbali vilivyojitokeza kudahili wanafunzi wanaotaka kujiunga na kozi  tofauti kwenye vyuo vyao.

Ili kutoa fursa ya elimu kwa wanafunzi wanaojiunga na vyuo hivyo, Chuo cha Muslim Morogoro kimewataka wanafunzi wachangamkie fursa ya elimu ya lugha ya Kichina inayopatikana katika chuo chao kwani kimeweza kuwasaidia wanafunzi wengine kufahamu lugha hiyo pamoja na kupata nafasi za kusoma nchini China bure.

Akizungumza na Globu ya Jamii, Afisa Habari wa Chuo cha Muslim Morogoro Ngaja Mussa amesema kuwa wanatoa kozi ya elimu hiyo ya lugha ya kichina kwa wanafunzi wote wanaotaka kuifahamu na pia utakaposoma kwa mwaka mmoja na kuifahamu vizuri lugha hiyo unapata nafasi ya kusoma nchini China.

Ngaja amesema kwa sasa kuna walimu takribani saba wanatoa mafunzo ya elimu hiyo katika chuo chao, mbali na kozi hiyo ya lugha ya Kichina wanatoa pia kozi mbalimbali katika ngazi ya astashahada, stashahada na shahada.

Kwa ngazi ya shahada kwa mwaka 2017/18  wana kozi za Bachelor of Arts with Education pamoja na Bachelor of law with Shariah huku ngazi ya Astashahada na Stashahada wana kozi za  Procurement and Logistics Management, Journalism, Medical Labaratory Technology, Science and Laboratory Technology, Laws with Shariah pamoja na Islamic Bankinga and Finance.
 Afisa Habari wa Chuo cha Muslim Morogoro Ngaja Mssa akitoa maelezo wa wageni waliotembelea banda la Chuo hicho na kuwaelezea namna wanavyofanya udahili wa wanafunzi kwa mwaka 2017/18 pamoja na elimu ya lugha ya Kichina inayopatikana katika chuo chao kwenye Maonesho ya Elimu ya Juu yanayoendelea katika Viwanja vya Mnazi Mmoja Jijini Dar es salaam.
Mkufunzi wa Chuo cha Muslim Morogoro Faraji akitoa maelezo wa wageni waliotembelea banda la Chuo hicho na kuwaelezea namna wanavyofanya udahili wa wanafunzi kwa mwaka 2017/18 pamoja na elimu ya lugha ya Kichina inayopatikana katika chuo chao kwenye Maonesho ya Elimu ya Juu yanayoendelea katika Viwanja vya Mnazi Mmoja Jijini Dar es salaam.
 Wanafunzi akitoa maelezo wakati walipotembelea banda la Chuo hicho na kuwaelezea namna wanavyofanya udahili wa wanafunzi kwa mwaka 2017/18 pamoja na elimu ya lugha ya Kichina inayopatikana katika chuo chao kwenye Maonesho ya Elimu ya Juu yanayoendelea katika Viwanja vya Mnazi Mmoja Jijini Dar es salaam.
Mkufunzi wa Lugha ya Kichina Sun Fei akielezea jambo kwa mwanafunzi aliyefika katika banda la Chuo cha Muslim Morogoro namba ya kujiunga na Chuo chao na kusoma elimu ya lugha ya Kichina. 

Mzazi akielezwa maana mbalimbali ya Lugha ya Kichina inayopatikana katika Chuo cha Muslim Morogoro.Picha na Zainab Nyamka, Globu ya Jamii.

Lissu aachiwa kwa dhamana



Lissu akipelekwa mahakamani.

MAHAKAMA ya Hakimu Mkazi Kisutu imemwachia kwa dhamana Mbunge wa Singida Mashariki (Chadema) na Rais wa Chama cha Wanasheria nchini, Tundu Lissu mapema leo asubuhi.

Lissu ametakiwa kudhaminiwa na wadhamini wawili ambao kila mmoja ataweka bondi ya dhamana ya shilingi milioni 10 huku akiwekewa zuio la kutoka nje ya Mkoa wa Dar es Salaam bila kibali maalum cha mahakama.
Aidha kesi yake imepangwa kusikilizwa Agosti 24 mwaka huu baada ya wadhamini wake kukamilisha taratibu zote za kumdhamini.

Tundu  Lissu ambaye alikamatwa Alhamisi, Julai 20 mwaka huu, katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNIA) wakati akijiandaa kuelekea Kigali, Rwanda kwenye kikao cha Chama cha Wanasheria cha Afrika Mashariki (EALS), alifikishwa Mahakamani hapo Jumatatu Julai 24 na kusomewa mashtaka  ya kutoa lugha ya uchochezi dhidi ya Serikali, kosa ambalo anadaiwa kulitenda Julai 17.

Inadaiwa kuwa maneno hayo yalikuwa na lengo ya kuleta chuki dhidi ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Alipotakiwa kukubali ama kukataa  makosa hayo na Hakimu Mashauri, Lissu alisema kusema kweli haijawahi kuwa kosa la jinai. Mahakama ya Kisutu ilimnyima dhamana Tundu Lissu, kesi iliahirishwa hadi leo Julai 27, 2017 ambapo amepewa dhamana.

AUDIO RELEASE: MRISHO MPOTO KUACHIA 'KITENDAWILI' BAADA YA 'SIZONJE' KUBAKI NJIA PANDA


Msanii mkongwe wa muziki wa asili nchini Tanzania, Mrisho Mpoto baada ya kufanya vizuri na wimbo ‘Sizonje’ ambao ulipendwa na watu wa rika zote ndani ya nchi na kimataifa, hatimaye Jumatatu hii (tarehe 1 August 2017) anatarajia kuachia wimbo wake mpya ‘Kitendawili’ akiwa amemshirikisha mkali wa nyimbo za mahaba, Kassim Mganga.

Wimbo uliopita ‘Sizonje’ wa muimbaji huyo uliacha maswali mengi kwa wapenzi wa muziki wake kutokana namna maishiri ya wimbo huo yalivyokuwa magumu huku wengi wakidai huwenda wimbo huo alimuimbia Rais John Pombe Magufuli kitu ambacho hakuwahi kukiweka wazi licha ya Rais huyo kutamka mara kadhaa katika mikutano yake kwamba wimbo huo alikuwa kwaajili yake.

Sasa mshairi huyo ametangaza ujio wake mpya na wimbo ‘Kitendawili’ akiwa Kassim Mganga ikiwa ni wimbo wa kwanza ambao unawakutanisha wawili hao ambao kila mmoja ni mkali kwa upande wake.
Mpoto amesema amerekodi wimbo wake huo mpya katika studio za Combination Sound chini ya producer mahiri, Man Walter ili kupata ladha tofauti ya muziki wake.

“Mimi naamini muziki ni ladha, nyimbo zangu nyingi nimefanya ndani ya studio yangu chini ya producer Alan Mapigo na zilifanya vizuri. Lakini katika project hii mpya nikaona sio mbaya kama nikibadili dhala ya beat na kupata kitu tofauti na kweli Man Walter amefanya kitu kizuri sana, menejimenti pamoja na watu wangu wa karibu wamefurahishwa na kile ambacho amefanya ,” alisema Mpoto.

Aliongeza, “Pia katika wimbo huu utamsikia Kassim Mganga, huyo ni mtu mpya kabisa katika nyimbo zangu, amefanya kitu kikubwa sana ambacho bila shaka kitawashangaza mashabiki wengi wa muziki. Kwahiyo napenda kuwaambia mashabiki wakae mkao wa kula, Mpoto nimerudi upya na kazi ni nzuri.”
Mjomba amewataka mashabiki wake wa muziki kuusubiria kwa hamu wimbo huo ambao utaachiwa siku ya Jumatatu (tarehe 1 mwezi August) kupitia mitandao ya kijamii (blogs) pamoja na redio.
Pia mshairi huyo amesema siku hiyo ataachia kwanza audio na baada ya siku kadhaa atatoka video ambayo amedai ndani yake kuna mambo mengi mapya ambayo hayajazoeleka kwenye muziki wake.
Kwa upande wa muimbaji Kassim Mganga ambaye ameshiriki ndani project ya namna hiyo kwa mara ya kwanza na Mrisho Mpoto, amesema amefurahishwa na namna wimbo huo ulivyoandaliwa huku akiwataka mashabiki kusubiria muziki mzuri.
“Kusema kweli hii ni mara yangu ya kwanza kufanya kazi ya namna hii na Mrisho Mpoto ambaye hata mimi ni shabiki wa muziki wake. Nimefurahishwa sana na kile tulichokifanya, binafsi nafarijika kuona ushirikiano wetu jinsi ulivyozalisha kitu kikubwa katika muziki, natamani ngoma itoke hata kesho ili mashabiki waone kitu ambacho nakizungumzia. Kwahiyo mashabiki wa muziki kwa umoja wetu tusubirie muziki mzuri ambao utateka fikra na kutoa burudani kwa mashakibiki,” alisema Kassim Mganga.