Thursday, July 27

Ukawa ilivyoendeleza Safari ya Matumaini


Dar es Salaam. Lilikuwa ni jambo lisilotarajiwa kwamba mmoja wa wagombea urais ndani ya CCM aliyeonekana kuwa na ushawishi mkubwa, angekihama chama tawala.
Mbali na hilo, hakuna aliyeweza kufikiria kuwa mtu aliyewahi kushika nafasi ya juu kama ya uwaziri mkuu, angeweza kuchukua uamuzi mzito kama huo katika nchi ambayo chama tawala ni ‘chama dola’.
Lakini Edward Lowassa alithubutu kufanya hivyo mwaka 2015 alipotangaza kuihama CCM siku kama ya leo na kujiunga na upinzani, ambao hapo awali ulimrushia kila aina ya kombora ukimhusisha na kashfa ya Richmond.
Huo ulikuwa ni mwanzo mpya wa kisiasa kwa Lowassa, mbunge wa zamani wa Monduli, aliyekulia ndani ya CCM na kufanya shughuli zake zote ndani ya chama hicho tawala. Alikuwa na kazi nzito ya kuanza kazi ya kuendeleza “Safari ya Matumaini” nje ya CCM.
Wengi waliamini kuwa uamuzi wake wa kujiondoa CCM na kwenda upinzani ulikuwa ni wa hasira na kama ilivyo kwa wanasiasa wengi, angerejea chama tawala baada ya hasira kutulia licha ya kupewa nafasi ya kugombea urais kwa tiketi ya Chadema na kuungwa mkono na vyama vingine vitatu.
Lakini leo, anapotimiza miaka miwili tangu ajiondoe CCM, Lowassa bado hafikirii wala kuwaza kurejea chama hicho na zaidi ya yote hajilaumu kujiunga upinzani.
“Sijutii kujiunga upinzani,” alisema Lowassa jana katika mahojiano na Mwananchi kuhusu mtazamo wake wa kisiasa katika kipindi cha miaka miwili alichokuwa nje ya chama tawala hadi sasa.
Aliingia kwenye mtihani mkubwa wa kuwania urais akipambana na chama ambacho alikitumikia kwa muda mrefu na kuanzisha “Safari ya Matumaini” ya kuwa Rais, lakini iliyokatishwa na Kamati Kuu ya CCM.
Lakini matokeo ya Uchaguzi Mkuu yalimpa mwanga. Alishika nafasi ya pili katika mbio za urais, akipata kura 6.072,848, ambazo ni zaidi ya mara mbili ya kura ambazo wapinzani walikuwa wakipata tangu mwaka 1995 wakati Uchaguzi Mkuu wa vyama vingi ulipofanyika kwa mara ya kwanza tangu kurejeshwa kwa siasa za ushindani mwaka 1992.
Kura hizo ni sawa na asilimia 39.97 dhidi ya Rais Magufuli aliyepata kura 8,882,935 (asilimia 58.46), kiwango ambacho ni kidogo kwa mgombea urais wa CCM tangu mwaka 1995.
Haikuwa rahisi Lowassa kukubaliwa na kupewa dhamana hiyo ya kugombea urais akiungwa mkono na vyama vinne, baada ya CUF, NLD na NCCR-Mageuzi kuamua kutosimamisha mgombea kwa makubaliano ya Ukawa.
Julai 26, 2015 ikiwa ni siku moja kabla ya kuondoka CCM, mwandishi wetu alimshuhudia Lowassa akihudhuria kikao cha dharura cha Kamati Kuu ya Chadema. Aliwasili lango la Hoteli ya Ledger Bahari Beach, Dar es Salaam saa 3:02 usiku na kupokewa na viongozi mbalimbali wa Chadema wakiongozwa na mwenyekiti wake, Freeman Mbowe. Baada ya hapo aliongozwa kuelekea chumba cha Watu Mashuhuri (VIP) na kukutana na viongozi wachache wa chama hicho akiwamo makamu mwenyekiti (Zanzibar), Said Issa Mohammed. Mazungumzo hayo yalidumu kwa takribani dakika 18 na ilipofika saa 3:20 usiku, walitoka na kuingia ukumbini kwenye kwa ajili ya kikao cha Kamati Kuu.
Lowassa alishiriki kikao hicho kwa takriban dakika 98 na ilipofika saa 4:58 usiku, alitoka akisindikizwa na Mbowe, Willibrod Slaa (katibu mkuu wakati huo), Profesa Abdallah Safari (makamu mwenyekiti) na Salum Mwalimu (naibu katibu mkuu, Zanzibar).
Saa 18 baada ya Lowassa kutambulishwa Kamati Kuu ya Chadema, Julai 28 viongozi wengine wa Ukawa waliitisha mkutano wa wanahabari mchana na kumkaribisha.
Waliokuwapo katika mkutano huo ni wenyeviti wa Ukawa; James Mbatia (mwenyekiti NCCR – Mageuzi), Emmanuel Makaidi (mwenyekiti wa NLD - sasa ni marehemu), Mbowe na Profesa Ibrahim Lipumba (mwenyekiti CUF).
Walitumia mkutano huo kuzungumzia tuhuma dhidi ya Lowassa walizoshiriki kuzitoa, hasa sakata la mkataba wa kuzalisha umeme wa dharura baina ya Tanesco na kampuni ya Richmond Development ya Marekani.
“Sisi tunaponda ufisadi na mfumo wa kifisadi. Chanzo kikubwa cha ufisadi ni mfumo ndani ya CCM. Kwanza tuing’oe CCM, hapo ndipo tutakapoweza kuondoa ufisadi na kujenga msingi wa kupambana na ufisadi na rushwa iliyopo,” alisema Profesa Lipumba.
“Lowassa alikumbwa na tuhuma za ufisadi mwaka 2008, leo ni 2015. Ufisadi umeongezeka au umepungua? Lowassa hayupo serikalini, akaunti ya Tegeta Escrow imetokea wakati gani? Lowassa alikuwapo? Tatizo ni mfumo na jambo la kwanza ni kuing’oa CCM.”
Kuhusu kushirikiana naye wakati walikuwa wanamtuhumu kwa ufisadi, makamu mwenyekiti wa CUF wa wakati huo, Juma Duni Haji alihoji: “Mbona CUF iliwahi kupigana na kuuana na CCM mwaka 2000 lakini leo wameunda Serikali ya Umoja wa Kitaifa?”
Dk Makaidi alisema kama Lowassa angekuwa mbaya kiasi hicho, angekuwa ameshashtakiwa kama ilivyo kwa viongozi wengine ambao tayari wameshahukumiwa vifungo kwa matumizi mabaya ya madaraka au rushwa.
Mbatia alisema Ukawa inamwalika kila Mtanzania aliye tayari kuuondoa mfumo kandamizi na dhalimu wa CCM na watashirikiana naye kujenga Taifa imara na kwamba Lowassa ni miongoni mwa wanaokaribishwa.
Siku moja baadaye, Lowassa alitangaza rasmi kujiunga na Chadema akisema, “Sasa basi, imetosha”.
Alisema amejiunga na chama hicho ili kutekeleza azma yake ya kuwakomboa Watanzania na kuendeleza Safari ya Matumaini kupitia Ukawa.
“CCM imepotoka, imepoteza mwelekeo na sifa za kuendelea kuiongoza Tanzania,” alisema Lowassa katika mkutano wa kumkaribisha Chadema uliofanyika ukumbi wa Hoteli ya Ledger Bahari Beach na kurushwa moja kwa moja na vituo kadhaa vya televisheni na redio.
Lowassa alitumia dakika 13 kueleza sababu za kujiunga na Chadema, mbele ya wenyeviti wenza wa Ukawa katika mkutano huo, ambao haukuhudhuriwa na Dk Slaa, naibu wake (Bara), John Mnyika na Mwanasheria Mkuu wa Chadema, Tundu Lissu.
Wakati Lowassa akizungumza, wanachama wa Chadema walikuwa wakiitikia ‘peoples power’, na alipomaliza hotuba yake waliimba wimbo maalumu wa “Tuna Imani na Lowaasaa”, ambao ni wa kuonyesha mshikamano na ambao uliimbwa na wajumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM kupinga jina la Lowassa kutopitishwa kuwania urais.
Huo ndio ulikuwa mwanzo wa misukosuko ya kisiasa inayohusisha kupambana na vyombo vya dola ambayo hakuwahi kukutana nayo wakati akiwa CCM.
Agosti 29, 2016, akiwa pamoja na wajumbe wa Kamati Kuu ya Chadema na wabunge, walikamatwa na polisi wakiwa katika kikao cha ndani jijini Dar es Salaam na kupelekwa Kituo Kikuu cha Polisi ambako walihojiwa na kuachiwa huru.
Mmoja wa mashuhuda wa tukio hilo alisema: “Tulikuwa kwenye msafara wa kumpokea, lakini tulipofika hapa stendi wananchi walitaka kuongea na Lowassa. Kabla hata hajashuka kwenye gari, askari walituvamia wakasema tuondoke moja kwa moja twende kituoni.”
Ilikuwa ni wakati Lowassa alipofanya ziara kwenye maeneo ya wananchi kuzungumza nao kama sokoni, vituo vya mabasi na hospitali.
Agosti 12, 2015 msafara wake na viongozi wengine wa upinzani waliounda Ukawa ulizuiwa wilayani Mwanga, Kilimanjaro wakati wakielekea kuhudhuria mazishi ya kada wa CCM, Peter Kisumo.
Polisi walitaka Lowassa pekee ndiye aende na viongozi wengine warudi, pendekezo ambalo alilikataa.
Si hilo tu, Januari 16, 2017 polisi mkoani Geita walimkamata Lowassa akiwa anakwenda kwenye kampeni za uchaguzi mdogo wa Kata ya Nkome na baadaye aliachiwa, huku taarifa za polisi zikidai kuwa walimzuia kwa sababu za kiusalama.
Tukio jingine lilimkuta Agosti 23, mwaka jana wakati msafara wake ulipouiwa kwenda mikoa ya Rukwa na Katavi baada ya polisi kuhofu kuwa ungeweza kuingilia ziara ya Waziri Mkuu Kassim Majaliwa.
Na Juni 27, 2017 Lowassa aliitwa polisi kuhojiwa kuhusu kauli zake za kutaka kesi masheikh wa Uamsho wanaoshikiliwa na polisi ziharakishwe na wapewe dhamana. Hadi sasa anaripoti Makao Makuu ya Polisi upelelezi ukiendelea.
Pamoja na misukosuko hiyo, jina la mwanasiasa huyo limeibuka kwenye siasa za nchi jirani ya Kenya, hasa baada ya chama chake kutangaza hadharani kumuunga mkono Rais Uhuru Kenyatta anayepambana na mwanasiasa mkongwe, Raila Odinga.

No comments:

Post a Comment