Thursday, July 27

Lowassa afunguka miaka miwili nje ya CCM

Waziri Mkuu wa zamani, Edward Lowassa

Waziri Mkuu wa zamani, Edward Lowassa akizungumza wakati wa mahojiano na waandishi wa gazeti la Mwananchi, ofisini kwake jijini Dar es Salaam jana. Picha na Said Khamis. 
Dar es Salaam. Waziri Mkuu wa zamani, Edward Lowassa leo ametimiza miaka miwili tangu aweke historia ya kuwa kiongozi wa kwanza wa ngazi ya juu serikalini kuihama CCM na anasema hajutii uamuzi wake, yuko imara na licha ya kuzuiwa kufanya mikutano, kura zake zinazidi kuongezeka.
Lowassa alichomoka CCM Julai 27, 2015 ikiwa ni siku chache baada ya Kamati Kuu ya CCM kuondoa jina lake na mengine katika kinyang’anyiro cha urais, uamuzi ambao ulizua mtafaruku mkubwa uliosababisha wajumbe wa Halmashauri Kuu kuimba wimbo wa kuonyesha kuwa na imani naye wakati mwenyekiti wa wakati huo, Jakaya Kikwete akiingia mkutanoni.
Siku moja baada ya kujiengua CCM, Lowassa alitangaza kujiunga na Chadema, chama ambacho kilimpa fursa ya kuendeleza “Safari ya Matumaini” aliyoianzisha CCM, kwa kushirikiana na vyama vingine vitatu vilivyoundwa Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa).
Akihojiwa na Mwananchi jana kuhusu miaka yake miwili nje ya CCM, Lowassa alisema pamoja na kupata kura zaidi ya milioni sita za urais, yeye na wapinzani wenzake wanasononeshwa na kunyimwa haki ya kufanya mikutano na kukutana wanachama wao.
Hata hivyo, alipoulizwa ni kwa kiwango gani kunyimwa fursa ya mikutano kumemuathiri, alisema: “Kura zangu zimeongezeka sana, tena sana. Ile tu kutoniona kunaniongezea (kura).
“Nataka kwenda kuwaona (wananchi) lakini siruhusiwi. Nataka kufanya mikutano ya hadhara, siruhusiwi. Sio mimi tu, ni pamoja na wenzangu wote kwenye vyama vya upinzani, hii ndiyo kauli yao.
“Waeleze wananchi na wanachama wa Chadema, nawapenda sana. Natamani kwenda kwao, kuzungumza nao, lakini sipati nafasi.”
Alikuwa akizungumzia amri ya kuzuia mikutano ya hadhara ya wanasiasa hadi mwaka 2020 iliyowekwa na Serikali. Zuio hilo halihusu mikutano ya wabunge na wananchi wao, lakini hawaruhusiwi kualika wanasiasa kutoka maeneo mengine.
Hana lolote la kujutia
Lowassa, ambaye sasa ni Mjumbe wa Kamati Kuu ya Chadema, alisema pamoja na hali hiyo wanayokumbana nayo, hana cha kujutia kutokana na uamuzi wake wa kujiunga na upinzani.
“Sina cha kujutia hata kidogo,” alisema katika mahojiano hayo yaliyofanyika ofisini kwake jijini Dar es Salaam.
“Nadhani ulikuwa uamuzi sahihi. Baada ya kuutafakari wakati ule na sasa, bado naamini ulikuwa uamuzi sahihi.”
Pamoja na hayo, Lowassa aliyewania urais na kupata kura milioni 6.07 sawa na asilimia 39.97 dhidi ya Rais Magufuli aliyepata kura milioni 8.8 (asilimia 58.46), alisema kuna tofauti kubwa kufanya siasa ukiwa CCM na ukiwa upinzani.
Alisema hali ni tofauti kwa sababu kuna changamoto nyingi zaidi kwenye chama cha upinzani ukilinganisha na CCM.
Alisema kuna maswali mengi ambayo yanajitokeza na CCM ilikuwa na muundo na miundombinu ya kukabili mambo hayo, tofauti na ilivyo kwenye vyama vya upinzani kutokana na uchanga wake.
“Hivi vyama bado ni vichanga, havina capacity (uwezo) kama ilivyo CCM. Kweli kuna changamoto nyingi, leo kuna changamoto hii, kesho kuna hii, lakini kubwa ni kuwahusisha wananchi, tupate nafasi ya kuzungumza na wanachama, kujadiliana nao na kufanya nao kazi kutatua changamoto zilizopo,” alisema Lowassa ambaye alikuwa Waziri Mkuu kuanzia mwaka 2005 hadi 2008 alipoachia ngazi.
Kuhusu Chadema, alisema chama hicho kikuu cha upinzani kinakua haraka, kinaongeza idadi ya wanachama na viongozi wengi, hivyo akasema kinachotakiwa ni kujenga uwezo wao.
Alisema uzoefu huo hauwezi kuja kwa siku moja, bali kwa muda mrefu kama ilivyo kwa CCM.
“CCM ni moja ya vyama vikongwe Afrika na ina uzoefu mkubwa. Ukitulinganisha sisi (utaona) tuko nyuma yao, lakini tunayo majukumu makubwa na makali zaidi mbele yetu kuliko wao,” alisema.
Kuzuiwa mikutano
Akizungumzia changamoto zinazoukabili upinzani katika uendeshaji siasa kwa sasa, Lowassa alisema Watanzania wanajua, wanaona na wanasikia kwamba vyama vya upinzani vinanyimwa haki hiyo.
“Pamoja na kura milioni sita tulizozipata za urais, hatuna haki. Haturuhusiwi kufanya mikutano ya hadhara. Hili ni jambo gumu sana kulielewa. Ni jambo baya sana katika demokrasia,” alisema Lowassa ambaye mikutano yake ya kampeni ilikuwa ikifurika watu kila alipoenda.
“Ni jambo lisilokubalika katika jamii ya kimataifa, lakini imewekwa kwamba ukifanya mkutano wa hadhara unakamatwa unapelekwa mahakamani.
“Sasa hiyo inatunyima nafasi ya kuwasiliana na wanachama wetu. Lakini Katiba ya nchi hii imeruhusu vyama vya siasa vishindane bila kupigana. Tupingane bila kupigana. Vyama vimeruhusiwa kufanya hivyo. Serikali kuzuia mikutano ya hadhara ni blow (pigo) kubwa kuliko zote tulizopata katika uongozi wa vyama vya upinzani.”
Alisema kuzuia mikutano ni kukwaza wananchi.
“Kama hatupati nafasi ya kushindanisha sera zenu, mtakuwa mnawakwaza wananchi na mtakuwa mnakwaza demokrasia katika nchi,” alisema.
Atajwa uchaguzi Kenya
Wakati Lowassa na wenzake wakiwa wamezuiwa kufanya mikutano ya hadhara, jina lake limeibuka kuwa gumzo nchini Kenya ambako kampeni za Uchaguzi Mkuu utakaofanyika Agosti 8, zinaendelea.
Baada ya kuhudhuria mazishi ya aliyekuwa Waziri wa Mambo ya Ndani wa Kenya, Joseph Nkaissery, Lowassa alifanya mahojiano na vyombo tofauti vya habari, na tangu hapo amekuwa akitajwa kila mara kwenye majukwaa ya kisiasa.
“Sijisikii lolote jina langu kutajwa Kenya, ila hiyo ndiyo siasa. Mimi ni mwenyekiti wa Malaigwanani (viongozi wa kabila la Wamasai) wa Afrika Mashariki. Kwa nafasi hiyo nina nafasi ya kwenda Kenya kuzungumza na Malaigwanani wenzangu umasaini juu ya nafasi za kisiasa,” alisema Lowassa ambaye anatuhumiwa na wapinzani wa Nasa kumfanyia kampeni Rais Uhuru Kenyatta wa Jubilee.
“Na kule sikuzungumza siasa. Chama changu kilikaa, tukasema kati ya wagombea wote, anayefaa kuliko wenzake ni Uhuru Kenyatta. Ni bora kuliko wengine wote. Baraza Kuu lilitoa kauli ya kumuunga mkono. Kwa hivyo chama kilitoa uamuzi huo na mimi nautekeleza kumuunga mkono Uhuru Kenyatta.”
Upinzani wa Simba, Yanga
Akizungumzia sababu za kufikia uamuzi huo, Lowassa alisema: “Na nieleze, hatukufikia uamuzi huo hivihivi, sisi tuna vigezo vyetu. Tunamwona Kenyatta kama mtu anayependa ushirikiano wa Afrika Mashariki. Pale mpakani Wamasai wanapita kwenda na kurudi kila siku ya maisha yao. Usipompata mtu anayependa ushirikiano huo, mtakuwa mmenoa sana.
“La pili, tunaona katika utawala wake, Kenyatta anapenda, anaheshimu sana wapinzani. Anauona upinzani kama ushindani. Na hiyo ni vizuri, ushindani unatakiwa uwe kama wa Simba na Yanga, sio chuki za kisiasa au chuki za kuuana na kupigana.
“Kwa hiyo nilipokwenda kumzika marehemu Nkaissery, walinialika niseme kidogo, na mimi nikasema ‘msirudi mlikotoka maana ni aibu, nikasema mchague mtu atakayesimamia masilahi ya Afrika Mashariki, mtu ambaye ataheshimu upinzani, mtu ambaye mtakubaliana kufanya kazi naye pamoja na nchi zetu zikawa na amani na utulivu.
“Hayo ndiyo niliyasema, nafurahi yamesikika, najua wamenijibujibu lakini ukweli utabaki palepale. Nawatakia wote kila la heri na uchaguzi uende kwa amani. Amani ya nchi ile ni muhimu sana, amani ikiwapo Kenya, pia itakuwapo Tanzania.”
Lowassa alirudia kauli yake kuwa katika Uchaguzi Mkuu 2020 atashinda kwa kishindo na atakuwa tayari kwa uchaguzi huo, lakini kwa sasa wamwachie Rais Magufuli afanye kazi yake.
“Yapo mambo mazuri anayofanya Rais Magufuli, aungwe mkono. Na kwa kiasi kikubwa anafanya mazuri, lakini haya hayajatoka mbinguni, bali ni wajibu wake,” alisema Lowassa.
“Isionekane kama ni salamu kutoka mbinguni, ni wajibu wake kama Rais. Kazi ya Serikali ni kutoa huduma, ni kujenga shule, ni kujenga hospitali. Ndiyo kazi ya Serikali, kwa hiyo watu wasihesabu kuwa ni hisani.
“Wamefanya kazi yao, kwa kweli nawapongeza, lakini wasionekane wamefanya hisani. Kazi za Serikali zote duniani ni kuleta maendeleo kwa watu au kuandaa mazingira ya kuleta maendeleo.”
Mbunge huyo wa zamani wa Monduli alitoa angalizo dhidi ya siasa za chuki alizosema zimeanza kujitokeza nchini, akisema zisipokomeshwa zitaiingiza nchi pabaya.
Alisema vitendo vya wakuu wa wilaya kushindana kukamata viongozi, wanachama na wafuasi wa upinzani kama njia ya kuwakomoa ni vibaya na havikubali.
Alisema sheria hiyo ya kuweka watu ndani kwa saa 48 iliwekwa kwa ajili ya watu wanaofanya fujo kama kwenye mkutano, lakini si kuwakomoa.
Aliwapongeza viongozi walioamua kuwashtaki wakuu wilaya binafsi waliochukua uamuzi huo, akisema mahakama zina uhuru, zitarekebisha hali hiyo.
Kuhusu wimbi la madiwani wa Chadema kujiuzulu mkoani Arusha na sasa Kilimanjaro, Lowassa alisema ingawa kuhama ni haki yao, inasikitisha kusikia kuna watu wanashawishiwa kwa fedha.
“Wale wanaosema wanapenda sera za Rais Mafuguli, nawatakia heri, lakini si wangesubiri hadi 2020, kuhama ni haki yao lakini waeleze sababu halisi,” alisema

No comments:

Post a Comment