anzibar. Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar (SMZ) imesisitiza kuwa bei ya karafuu inayotolewa kwa wakulima haitashuka hata kama bei ya soko la nje itashuka.
Waziri wa Biashara, Viwanda na Masoko Zanzibar, Balozi Amina Salum Ali amesema lengo la Serikali katika ni kuwanufaisha wakulima zaidi ili kuwajengea ari ya kulihudumia vyema zao hilo kwa manufaa yao na Taifa kwa jumla.
“Hakuna nchi yoyote duniani inayolipa wakulima bei ya asilimia 80 ya soko la nje kwa mazao ya biashara na wala hakuna zao lolote hapa Zanzibar linalofikia bei ya Sh14,000 kwa kilo zaidi ya karafuu, hivyo nawaahidi wakulima wetu kuwa Serikali haitothubutu kushusha bei ya zao hilo,” amesema Balozi Amina.
Amesema huu ni wakati kwa wakulima na wananchi kwa jumla kushirikiana na Serikali ili kuona zao hilo linaendelea kuimarishwa zaidi ili vizazi vijavyo navyo viweze kunufaika na urithi wa zao hilo ambalo ni mkombozi kwa wanyonge walio wengi.
“Nawaombeni sana tuliendeleze na tulitunze hili zao letu la karafuu ili vizazi vijavyo visije tulaaumu kwa kutowaachia urithi huu ambao ndio mkombozi wetu katika maisha’’ amesema Balozi Amina.
Akizungumzia magendo ya karafuu, Balozi Amina amewataka wananchi kila mmoja kuwa askari dhidi ya watu wanaofanya magendo ya karafuu na wawe tayari kuwafichua kwa kuwa ni adui wa zao hilo.
Amesema suala la magendo ya karafuu halikubaliki na tayari Serikali imejizatiti kwa kutunga kanuni kwenye Sheria ya Maendeleo ya Karafuu na kuimarisha ulinzi.
Mkuu wa Mkoa wa Kusini Pemba, Mwanajuma Majid Abdalla amewataka wazazi kuacha tabia ya kuwatumikisha watoto katika uchumaji karafuu.
Amesema uchumaji wa karafuu ni miongoni mwa kazi ngumu hivyo si busara kuwaajiri watoto kufanya kazi hiyo badala yake wawahimize kwenda shule.
Amesema kuwatumia watoto katika kazi za uchumaji karafuu ni kwenda kinyume cha haki za watoto na wanapopata ajali hukosa haki ya kulipwa fidia kwa vile kwa mujibu wa masharti ya bima hawatambuliki.
Pia, amewaonya wafanyabiashara wanaopita vijijini kununua karafuu mbichi kinyume na uratibu kuwa watashughulikiwa kwa mujibu wa sheria kwa vile kufanya hivyo ni kosa.
No comments:
Post a Comment