Tuesday, May 19

LICHA YA JANGA LA CORONA, HUDUMA ZA CHANJO NA UFUATILIAJI WA MAGONJWA YANAYOZUILIKA KWA CHANJO ZAENDELEA KWA UANGALIFU MKUBWA TANGA

Ofisa Mradi wa Ofisi ya Mpango wa Taifa wa Chanjo, Richard Magodi akipitia data za chanjo kwenye mfumo maalumu wa kieletroniki wakati wa ziara maalum ya muongozo wa kujikinga na COVID19 kwa watoa huduma za chanjo katika kituo cha Chanjo Zabanati ya Bushiri, Pangani Mkoani Tanga.


Ofisa Mradi wa Ofisi ya Mpango wa Taifa wa Chanjo, Richard Magodi akipitia data za chanjo kwenye mfumo maalumu wa kieletroniki wakati wa ziara maalum ya muongozo wa kujikinga na COVID19 kwa watoa huduma za chanjo katika kituo cha Chanjo Zabanati ya Bushiri, Pangani Mkoani Tanga.



***********************************

Na Mwandishi Maalum –Pangani,Tanga.

LICHA ya janga la Virusi vya Corona vinavyosababisha ugonjwa wa homa kali ya Mapafu (COVID19), Watoa huduma za chanjo na ufuatiliaji wa magonjwa yanayozuilika kwa Chanjo hizo Wilayani Pangani Mkoani Tanga zinaendelea kama kawaida huku wahudumu wakichukua tahadhari kubwa kwa kuzingatia muongozo wa kujikinga na janga hilo.

Hayo yameelezwa na Mratibu wa Huduma za Chanjo Mkoa wa Tanga, Seif Shaib wakati wa ziara maalum ya usimamizi elekezi na uhamasishaji wa muongozo wa kujikinga na COVID 19 kwa watoa huduma hizo iliyofanywa na Ofisa Mradi wa Ofisi ya Mpango wa Taifa wa Chanjo, Richard Magodi.

Mratibu huyo wa Chanjo mkoa, Seif Shaib alisema chanjo zipo na huduma vituoni zinaendelea kwa kuzingatia muongozo.

Kwa upande wake, Ofisa Mradi wa Ofisi ya Mpango wa Taifa wa Chanjo, Richard Magodi ameweza kushuhudia uwepo wa chanjo hizo kwenye vituo sambamba na watoa huduma wakifuata miongozo ikiwemo kukaa umbali wa mita moja kati ya mtu na mtu kwa kuacha nafasi, uwapo wa maji safi na tiririka ya kunawa mikono na uvaaji barakoa.

“Watoa huduma za chanjo na wafuatiliaji wa magonjwa yanayozuilika kwa chanjo kwa watoto wanatakiwa waendelee kulingana na ratiba za chanjo zao lakini kwa kuzingitia muongozo wa kujikinga dhidi ya COVID 19.” Alisema Richard Magodi

Akielezea upande wa chanjo ya kukinga ugonjwa wa Saratani ya mlango wa kizazi (HPV) inayotolewa kwa wasichana wa umri wa miaka 14 ipo na inatolewa kwa walengwa hao.

“Chanjo hii ya HPV bado ipo lakini tunacho sisitiza kwa watoto ambao ratiba zao zinafikia hivi sasa wanaweza kufika kwenye vituo vya kutolea huduma za afya.

Kamati za afya za kituo na Uongozi wa vijiji ama mtaa wahusishwe kuhamasisha wananchi kuwapeleka watoto wa kike wenye miaka 14 kupatiwa chanjo hiyo.” Alisema Magodi.

Sambamba na hilo, watoa huduma hao wametakiwa kufuatiliaji pia magonjwa yanayozuilika kwa chanjo hususani ugonjwa wa Surua, Polio na Pepopunda kwa watoto kwa kipindi hiki cha COVID19.

“Tuongeze jitihada za chanjo. Kwani tusipofanya hivyo watu wengi wanaweza kufariki na magonjwa yanayozuilika kwa chanjo.

“Mfano tukiangalia takwimu za mwaka jana nchini Congo (DRC), ugonjwa wa Ebola uliua watu wachache kuliko Surua hii ni kutokana na kuipa kipaumbele Ebola na kuacha magonjwa yanayozuilika kwa chanjo nchini humo..Hivyo sisi Tanzania tunaendelea na huduma kwa kufuata muongo na tahadhari kubwa ikiwemo kuhimiza suala hilo la chanjo.” Alisema Magodi.

Aidha aliwataka watoa huduma hao kuzingatia matumizi sahihi ya mfumo wa kieletroniki ngazi ya kituo (Tanzania Immunizations Registry -TImR) ili kuwa na takwimu sahihi na zitakazosaidia kufanya maamuzi bora kwa wakati kwenye ngazi ya kituo hadi ngazi ya Taifa.

“Katika vituo ambavyo tumetembelea Watumishi wameendelea kutumia mfumo huu kwa kuchanja na kuomba dawa, vifaa vya chanjo na kupata taarifa mbalimbali wanazozihitaji kwa wakati kupitia Vishishwambi (tablets) na wamefundishwa namna ya kutumia mfumo huo ambao umekuwa ukisaidia sana” alisema.

Awali Magodi aliweza kutembelea vituo vya chanjo hizo katika Hospitali ya Wilaya ya Pangani, kituo cha chanjo Zahanati ya Bushiri, kituo chanjo Zahanati ya Madanga na kituo cha Chanjo Zahanati ya Kimang’a.

Nae Muuguzi mkunga wa Kituo cha Chanjo Zahanati ya Madanga alisema tokea uwepo wa COVID 19, wamechukua hatua mbalimbali na kutoa elimu kwa wananchi wa Kijiji hicho cha Madanga.

Kwa upande wake Mganga Mfawidhi wa Zahanati ya Kimang’a, Dkt. Mohammed Kombo alisema wameweza kuchukua hatua dhidi ya COVID19 ikiwemo kutoa elimu kwa wanakijiji.

“Tumechukua tahadhari ya COVID19 ikiwemo pia kutoa elimu kwa wanakijiji. Lakini wanakijiji nao wameweka utaratibu mgeni akija kijijini hapa lazima ajitenge kwa maangalizio na kuchukuliwa taarifa zake mpaka tunapojiridhisha” alisema Dkt kombo.

Ziara ya usimamizi elekezi inaendelea tena katika Wilaya mbalimbali za mkoa huo wa Tanga kwa uratibu wa Mpango wa Taifa wa Chanjo kwa kushirikiana na wadau wake.

UZALISHAJI WA VAZI KINGA (PPE) MUHIMBILI WAONGEZEKA KWA 400% HUKU MAMLAKA YA DAWA NA VIFAA TIBA (TMDA) IKIRIDHIA NA KULITAMBUA


Mafundi wa kitengo cha Ushonaji MNH wakiendelea na ushonaji wa vazi la PPE 
Vazi la PPE likiwa tayari kupelekwa kwa wateja .
Mafundi wa Kitengo cha Ushonaji MNH wakiwa katika maandalizi ya awali ya ushonaji wa vazi la PPE
Muonekano wa vazi la PPE linaloshonwa na Hospitali ya Taifa Muhimbili.
*******************************
  Dar es Salaam, Jumanne Mei 19, 2020.
  Uzalishaji wa vazi kinga linalovaliwa na watoa huduma ili kuhudumia wagonjwa walioambukizwa Covid 19 umeongezeka kutoka mavazi 120 hadi kufikia 600 kwa siku sawa na ongezeko la 400% katika kipindi cha mwezi mmoja tangu lilipozinduliwa na Hospitali ya Taifa Muhimbili Aprili 17, 2020.
 
 Mpaka sasa Hospitali imezalisha PPE 10,553 kati ya hizo 5,000 zimesambazwa MSD na nyingine katika baadhi ya Hospitali za Rufaa za Kanda, Hospitali za Rufaa za Mikoa, Vituo vya Afya, Taasisi zisizo za kiserikali, Hospitali binafsi, makampuni, Halmashauri za Wilaya na Manispaa nchini. Tunaendelea kupokea mahitaji mbalimbali kwani sasa uwezo wa kuzalisha tunao. Bei ya PPE moja ni TZS. 50,000.
 
 Katika hatua nyingine, Mamlaka ya Dawa na Vifaa Tiba (TMDA) ilitambua vazi hili kupitia barua yenye Kumb. Na. BC.248/383/01/13 ya tarehe 23 Aprili, 2020 hivyo kuiruhusu Hospitali kuendelea kushona na kufanya usambazaji kote nchini.
 
 “Tunapenda kukufahamisha kuwa Mamlaka imepitia na kuridhia ombi lako la utambuzi wa nguo za kujikinga na maambukizi (coverall, shoe cover na apron) zinazotengenezwa na Muhimbili Tailoring Unit kwa kutumia malighafi ya nylon” inaeleza sehemu ya barua hiyo.
 
 Kwa hiyo utengenezaji na usambazaji wa vifaa hivi unazingatia matumizi na uhifadhi unaofuata kanuni za udhibiti wa vifaa tiba nchini, The Tanzania Food, Drugs and Cosmetics (Control of Medical Devices) Regulation, 2015 kama ambavyo tulivyoelekezwa na TMDA.  Pia vazi hili linafanyiwa utasishaji kabla ya kwenda kwa mtumiaji.

KORTI YAMUHUKUMU RAIA WA SOMALIA KWENDA JELA MIAKA MITATU


MAHAKAMA ya Hakimu Mkazi Kisutu imemuhukumu raia wa Somalia, Jama Jes (50), kulipa faini ya Sh. Milioni moja ama kwenda jela miaka mitatu baada ya kupatikana na hatia ya kuishi nchini bila kuwa na kibali.

Hukumu hiyo imetolewa jana Hakimu Mkazi Mkuu, Thomas Simba baada ya mshtakiwa huyo kukiri shtaka lake na hivyo kutiwa hatiani.

Akisoma hukumu hiyo Hakimu Simba amesema amezingatia maombi ya mshtakiwa kuwa anategemewa na familia na hivyo, mahakama imemuhukumu kulipa faini ya Sh. Milioni moja au kwenda jela miaka mitatu.

Hata hivyo, kabla ya kutolewa kwa hukumu hiyo , Wakili wa Serikali, Ngwijo Godfrey akisaidiana na  Sitta Shija, aliiomba mahakama itoe adhabu kali dhidi mshtakiwa huyo ili fundisho kwa wengine.

Katika kesi ya msingi, mshtakiwa anadaiwa kuingia nchini bila kuwa na kibali katika kesi ya jinai namba 76/2020.

Anadaiwa kutenda kosa hilo, Mei 12, 2020 mtaa wa Ohio wilaya ya Ilala, ambapo alikutwa hati ya kusafiria ilisha muda wake na hivyo kuishi nchini bila kuwa na kibali  huku akijua kufanya hivyo ni kinyume cha sheria.

WARAKA WA WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI KUHUSU UENDESHAJI WA TAASISI ZA KIDINI NCHINI




SPIKA JOB NDUGAI AONGOZA KIKAO CHA KAMATI YA UONGOZI, AZUNGUMZA NA WAANDISHI WA HABARI JIJINI DODOMA



Spika wa Bunge, Mhe. Job Ndugai akizungumza na waandishi wa habari katika kikao kilichofanyika leo nyumbani kwake uzunguni Jijini Dodoma. Mmoja ya agenda ya kikao hicho ilikuwa ni kupokea Mapendekezo ya Mabadiliko ya Ratiba ya Mkutano wa 19 wa Bunge.

Wajumbe kamati ya uongozi wakimsikiliza Spika wa Bunge, Mhe. Job Ndugai wakati wa kikao cha kamati hiyo kilichokaa ili kupokea Mapendekezo ya Mabadiliko ya Ratiba ya Mkutano wa 19 wa Bunge leo nyumbani kwake uzunguni Jijini Dodoma.