Tuesday, May 19

KORTI YAMUHUKUMU RAIA WA SOMALIA KWENDA JELA MIAKA MITATU


MAHAKAMA ya Hakimu Mkazi Kisutu imemuhukumu raia wa Somalia, Jama Jes (50), kulipa faini ya Sh. Milioni moja ama kwenda jela miaka mitatu baada ya kupatikana na hatia ya kuishi nchini bila kuwa na kibali.

Hukumu hiyo imetolewa jana Hakimu Mkazi Mkuu, Thomas Simba baada ya mshtakiwa huyo kukiri shtaka lake na hivyo kutiwa hatiani.

Akisoma hukumu hiyo Hakimu Simba amesema amezingatia maombi ya mshtakiwa kuwa anategemewa na familia na hivyo, mahakama imemuhukumu kulipa faini ya Sh. Milioni moja au kwenda jela miaka mitatu.

Hata hivyo, kabla ya kutolewa kwa hukumu hiyo , Wakili wa Serikali, Ngwijo Godfrey akisaidiana na  Sitta Shija, aliiomba mahakama itoe adhabu kali dhidi mshtakiwa huyo ili fundisho kwa wengine.

Katika kesi ya msingi, mshtakiwa anadaiwa kuingia nchini bila kuwa na kibali katika kesi ya jinai namba 76/2020.

Anadaiwa kutenda kosa hilo, Mei 12, 2020 mtaa wa Ohio wilaya ya Ilala, ambapo alikutwa hati ya kusafiria ilisha muda wake na hivyo kuishi nchini bila kuwa na kibali  huku akijua kufanya hivyo ni kinyume cha sheria.

No comments:

Post a Comment