Wednesday, August 16

MRADI WENYE FURSA KEDEKEDE WATANZANIA WANAPASWA KUZICHANGAMKIA



Hivi Karibuni, Rais wa Tanzania, Dkt. John Pombe Magufuli na Rais Yoweri Kaguta Museveni wa Uganda kwa pamoja waliweka jiwe la msingi la Ujenzi wa Bomba la Mafuta Ghafi kutoka Hoima nchini Uganda hadi Tanga Tanzania. Katika Makala hii pamoja na mambo mengine Mwandishi Said Ameir wa Idara ya Habari- MAELEZO anaeleza kwani nini mradi huu ni kipimo cha utayari na ujasiri wa watanzania katika kuchangamkia fursa.

Mradi huu unaojulikana kama Mradi wa Bomba la Kusafirisha Mafuta Ghafi la Afrika Mashariki (EACOP) unatekelezwa kwa ubia kati ya washirika wa sekta binafsi na sekta za umma za nchi za Tanzania na Uganda.

Washirika hao ni Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC), Kampuni ya Taifa ya Petroli ya Uganda (UNOC), Kampuni ya Mafuta ya Total ya Ufaransa, Kampuni ya TULLOW yenye makao makuu yake London nchini Uingereza na Kampuni ya China National Offshore Oil Company (CNOOC).

Bomba ambalo litagharimu dola za kimarekani 3.5 bilioni, sehemu yake kubwa yaani kilomita 1,115 kati ya kilomita 1,445 litajengwa katika ardhi ya Tanzania na kupita mikoa 8, wilaya 24 na vijiji 184.

Kutokana na hali hiyo, inaelezwa kuwa, mradi huu wakati wa ujenzi na utakapokamilika, utatoa na fursa nyingi za kiuchumi ambazo zitasaidia sana kuchangamsha shughuli za kiuchumi hivyo kuchangia ukuaji uchumi na kuinua kiwango cha maisha ya watanzania kwa namna mbalimbali.

Mradi huu ni mfano wa ushirikiano kati ya nchi za Tanzania na Uganda na kwa upande mwingine ni mfano mzuri wa ushirikiano kati ya sekta binafsi na sekta za umma katika nchi hizi. 
Katika hatua mbalimbali za utekelezaji wake, mradi huu utahitaji ushiriki wa sekta binafsi katika nchi zote mbili na wakati mwingine hata taasisi nyingine za umma ambazo zinatoa huduma zitakazohitajika na mradi.

Kwa hiyo, wakati tukisifia kuwa ni mfano wa mradi wa ubia wa sekta ya umma na sekta binafsi katika nchi zetu, watanzania hawana budi kuelewa kuwa wana wajibu mkubwa wa kuzitumia vyema fursa za mradi huu.

Kwa Tanzania, mradi huu unaweza kuonesha picha halisi ya ushirikiano wa sekta hizo kwa kuzingatia namna makampuni na taasisi za humu nchini zitakavyoweza kushiriki na kufanikisha mradi huu.

Kwa maana nyingie ni mradi ambao unaweza kutumika kupima utayari, umakini, uwezo na ujasiri wa watanzania katika kuchangamkia fursa za kiuchumi.

Kama alivyoeleza Rais Magufuli wakati wa sherehe za uwekaji wa jiwe la msingi kuwa katika mradi huu, Serikali imesamehe mambo mengi ili uweze kutekelezwa kwa kuishirikisha Tanzania. Wataalamu wa nchi walichambua na kupembua hadi kubaini kuwa kusamehe huko kutafidiwa na fursa nyingi zitakazoletwa na mradi huu.

Kwa maana hiyo bila ya watanzania kuchukua hatua madhubuti za kuhakikisha wanazitumia kadri itakavyowezekana fursa hizo uamuzi huo wa Serikali kusamehe hivyo ilivyovisamehe hautakuwa na maana yeyote.

Kuja kwa mradi huu Tanzania, watanzania hawana budi kuipongeza Serikali chini ya Rais John Pombe Magufuli kwa jitihada kubwa kwa kutumia ushawishi wa kisiasa, kidiplomasia, uchumi na ukaribu wa viongozi wa nchi hizo mbili pamoja na hoja nyingine hadi kufanikisha mradi huu kuja Tanzania.

Jitihada hizi ni kielelezo cha dhamira ya kweli iliyonayo Serikali ya Awamu ya Tano ya kutafuta kila aina ya fursa za kiuchumi ambazo zitasaidia kutimiza ahadi zake kwa watanzania ya kujenga Tanzania yenye uchumi imara.

Serikali imejitwika mzigo mkubwa wa kushiriki katika kutekeleza mradi huu mkubwa wa aina yake lakini imefanya hivyo kwa kuamini kuwa watanzania wako tayari na wako imara kuupokea kwa hali na mali.

Imeelezwa mara kwa mara kuwa mradi huu utaliingizia taifa mapato makubwa, utaleta tekinolojia na utalaamu na fursa za kiuchumi ambazo watekelezaji wake kwa kiwango kikubwa ni kutoka sekta binafsi. Kwa mnasaba huo, Serikali hapa imefanya zaidi ya wajibu wake ambao ni wa kujenga mazingira mazuri ya kuvutia uwekezaji.

Wale wahenga wa Cambrigde walisema“give us the tools and lets finish the job” na hivi ndivyo ilivyofanya Serikali kwa mradi huu. Imeleta mradi na kufungua fursa tele ambazo watanzania wanapaswa kuzitumia kujenga kiuchumi wao binafsi na uchumi wa taifa.

Haitakuwa na maana hata kidogo katika ngazi ya serikali na katika ngazi ya Mtanzania mmoja mmoja kufika wakati fursa za mradi huu kuchukuliwa na wageni kwa sababu zozote na katika mazingira yeyote yale. Ikifikia hatua hiyo watanzania watakuwa wamewaangusha viongozi wao.

Hii kutokana na mazingira ambayo Serikali imeyaweka kuwawezesha watanzania kushiriki katika sekta ya mafuta na gesi asilia. Mbali ya kupitisha Sheria ya Local Content Act ya 2015 ambayo inasisitiza ushiriki wa watanzania lakini zaidi dhamira ya kweli ya kisiasa iliyonayo uongozi wa Serikali ya kuhakikisha kuwa watanzania wanafaidika ipasavyo na mradi huu.

Ni jambo la kutia moyo kuona kuwa baadhi ya Taasisi za Serikali na za sekta binafsi zimeshaanza maandalizi au zimejitokeza kuwaandaa watanzania kuchangamkia fursa hizo na kuhakikisha wanazitumia vyema.

Miongoni mwa taasisi hizo ni Jumuiya ya Watoa Huduma katika Sekta ya Mafuta na Gesi (ATOGS) ambayo inawakusanya pamoja watoa huduma katika sekta hiyo ambapo lengo lake kubwa ni kuhakikisha kuwa fursa za mradi huo zinatumika ipasavyo kwa manufaa ya muda mfupo na mrefu ya watanzania.

ATOGS, kama taasisi nyingine zitakazoelezwa baadae, imeonesha mfano wa utayari kwa kuwa na mpango mkakati wake ambao unalenga kuwawezesha watoa huduma wa humu nchini wanapata fursa hizo kwa kuwasaidia kwa namna mbali mbali tangu hatua za awali za kuwania fursa hizo hadi utekelezaji wake.

Makamu Mwenyekiti wa Taasisi hiyo Abdulsamad Abdulrahim katika moja ya mikutano na waandishi wa habari alisema taasisi yake imejipanga kuwajengea uwezo watoa huduma na kutoa wito watoa huduma hao kwa waliokuwa bado hawajajiunga wajiunge na taasisi hii kwa minajili ya kufaidika na uwezeshaji wao.

Halikadhalika, Baraza la Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi (NEEC) nalo linaeleza kuwa limejidhatiti kuhakikisha kuwa watanzania watakaobahatika kupata fursa za kutoa huduma katika mradi huo hawashindwi kwa kukosa fedha za kutekeleza kandarasi zao.

“Hatutaki kusikia mtanzania amekosa fursa hii kwa sababu ya kukosa fedha …ukibahatika njoo kwenye Baraza tutakushauri… Serikali ina mifuko 17 yenye fedha za kutosha kukuwezesha” anaeleza Mkurugnezi wa uwezeshaji wa NEEC Bwana Edwin Chrisant.

Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Sekta Binafsi nchini (TPSF) Bwana Godfrey Simbeye aliwaambia waandishi wa habari kuwa taasisi yake imejipanga kuhakikisha kuwa mikataba ya kandarasi itakayofikiwa inazingatia maslahi ya pande zote na utekelezaji wake unafanyika kulingana na vipengele vya mikataba.

Dhamira hizi zilizoelezwa na taasisi hizi muhimu nchini, hapana shaka yoyote kuwa ni habari njema inayoashiria matumaini makubwa na kuonesha sasa watanzania wameamka na wamedhamiria kujenga Tanzania mpya kwa kila mmoja kwa nafasi yake kuyatumia mazingira yaliyopo kujenga uchumi wa taifa.

Kama kweli taasisi hizi zitatekeleza yale ziliyojipangia ikiwemo kuwapatia watoa huduma msaada wa kitaalamu, huduma za kisheria, kifedha, viwango na vigezo katika manunuzi, utaalamu, kuwaunganisha na wabia, kuwajengea uwezo vijana wasomi ili waweze kushika nafasi zitakuwa zimetoa msaada mkubwa kwa nchi.

Kwa hakika mradi huu kama ilivyoelezwa awali utakuwa kigezo muhimu kupima utayari, umakini na uwezo wa sekta binafsi kuchangamkia fursa zinapotokea na mafanikio ya ushiriki wa sekta hiyo huenda ukawa mwanzo mzuri wa kuupa mgongo utamaduni ulizoeleka wa watanzania kulalamika hususan kuilalamikia Serikali kuwa haiwapi fursa kama hizi.

Wahenga walisema “shike shike na mwenyewe nyuma” kwa hili Serikali zimefanya wajibu wake sasa mpira uko kwa wadau katika sekta binafsi kuucheza kwa zitumia fursa na ni vyema kukumbuka kuwa “mso matendo hula uvundo” hivyo watanzania wachangamkie fursa wasije wakajikuta karamu imekwisha ‘wakaramba vyungu.

 Ni vyema pia kutanabahisha kuwa fursa za mradi huu haziko kwa watoa huduma kama hao pekee ambao wao ni wafanyabiashara na wataalamu ambao tayari wanajielewa, wana uwezo na wako katika sekta hiyo hivyo tunaweza kusema wana angalau uzoefu.

Lakini ukweli hi kuwa fursa za mradi huu zimetapakaa kila mahala katika ngazi mbali mbali kuanzia wakulima wa jembe la mkono, wafugaji wadogo wadogo, mafundi mchundo, hadi vibarua wa ujenzi. Hivyo taasisi zinazohusika zinapaswa pia kuliangalia kundi hili kubwa na kuhakikisha linashiriki vyema.

Hii ni kwa sababu, inapozungumziwa ajira elfu kumi na ajira nyingine zaidi ya elfu thelathini nyingi zinawagusa watanzania wa kundi hili. Ikumbukwe kuwa kundi hili ambalo ndilo litakalokuwa karibu na mradi ndilo litakalokuwa la kwanza kulalamika pindi litakapokosa fursa na kujikuta halina namna ya kushiriki na kufaidika.

Utekelezaji mzuri na wenye ufanisi wa mradi huu kwa kushirikisha sekta binafsi nchini utakuwa kigezo cha kufungua milango kwa miradi mingine mikubwa ya aina hii humu nchini.



Watanzania hawana budi kumpongeza Rais Magufuli kwa jitihada zake za kujenga Tanzania Mpya yenye matumaini mapya. Hakika Tanzania yenye uchumi wa kati na ya viwanda inawezekana, kama kila mmoja atatimiza wajibu wake.

Zimbabwe

Rais Mugabe na mkewe GraceHaki miliki ya pichaREUTERS
Image captionRais Mugabe na mkewe Grace
Rais wa Zimbabwe Robert Mugabe ameambia umati wakati wa sherehe za siku ya mashujaa kwenye mji mkuu wa Harare, kuwa watu ambao waliwaua wakulima wazungu wakati wa mabadiliko ya mifumo ya ardhi nchini humo hawatashtakiwa.
"Ndio tuna wale waliouwawa wakati walipinga. Hatuwezi kuwashtaki wale waliowaua. Ninauliza mbona tunawashtaki?" alisema Mugabe.
Wakati wa ukoloni, ardhi nzuri ilitengewa wazungu na mwaka 2000, bwana Mugabe aliongoza kutwaliwa kwa ardhi hiyo kutoka kwa wakulima 4000.
Rais Mugabe awali alikiri kuwa mifumo ya ardhi ya nchi hiyo ilifeli na mwaka 2015 alisema:
"Nafikiri mashamba tuliyowapa watu ni makubwa, hawawezi kuyasimami.
Kutaliwa ghafla mashamba kutoka kwa wakulima wazungu, inaonekana kuwa sababu kuu ya kuporomoka kwa uchumi wa Zimbabwe tangu mwaka 2000.

Kamishna wa tume ya uchaguzi Kenya azuiwa Uwanja wa ndege

Kamishna wa IEBC Roselyn AkombeHaki miliki ya pichaIEBC TWITTER
Image captionKamishna wa IEBC Roselyn Akombe
Kamishna wa tume ya uchaguzi nchini Kenya IEBC Jumanne jioni alizuiwa kusafiri kuelekea nchini Marekani na kutolewa katika ndege aliyokuwa amepanda.
Roselyn Akombe alikuwa akielekea nchini Marekani kwa ziara rasmi ya kikazi wakati maafisa wa uwanja wa ndege wa JKIA walipomkamata kwa kukosa kibali cha kumruhusu kutoka nchini kutoka kwa mkuu wa maafisa wa umma.
Alizuiwa katika kituo cha polisi cha uwanja wa ndege kabla ya ubalozi wa Marekani kuingilia kati na kulazimu apalekwe katika anga ya serikali katika uwanja huo.
IEBC ilithibitisha kisa hicho ikisema kuwa Akombe alikuwa akielekea Marekani kwa ziara rasmi na alitarajiwa kurudi siku ya Jumapili Agosti 20.
Baadaye aliruhusiwa kuondoka baada ya mkuu wa maafisa wa umma Joseph Kinyua kuingilia kati.
Aliondoka nchini Kenya alfajiri ya siku ya Jumatano tarehe 16.
Akombe ni mmoja wa makamishna waliosimamia uchaguzi mkuu nchini Kenya ambapo rais Uhuru Kenyatta aliihifadhi kiti chake.
Upinzani nchini humo Nasa umepinga matokeo hayo na unatarajiwa kutoa mwelekeo kwa wafuasi wake siku ya Jumatano, Agosti 16.
Baadhi ya wafuasi wa muungano huo wamekabiliana na maafisa wa polisi wakipinga matokeo hayo.
Hatua hiyo imesababisha mauaji ya raia huku wengine wengi wakijeruhiwa.

UN yakataa ombi la Odinga kukagua matokeo ya uchaguzi Kenya

Kiongozi wa upinzani nchini Kenya Raila Odinga
Image captionKiongozi wa upinzani nchini Kenya Raila Odinga
Umoja wa Mataifa umekataa ombi la kiongozi wa upinzani nchini Kenya Raila Odinga kukagua matokeo ya uchaguzi wa tarehe 8 mwezi Agosti.
Msemaji wa umoja huo alikataa ombi hilo akisisitiza taarifa ya katibu mkuu wa Umoja huo Antonio Gutierrez ambapo amewataka viongozi wa Kenya kusuluhisho mgogoro wowote wa uchaguzi huo katika taasisi zinazofaa kikatiba.
Umoja huo umesema kuwa utatazama mpango mpya wa Raila Odinga ambao anapanga kutangaza siku ya Jumatano.
Wiki iliopita kiongozi huyo wa Nasa alitoa wito kwa Umoja wa Mataifa kukagua matokeo hayo ya uchaguzi uliokamilika.
Akizungumza na gazeti la Financial Times bwana Odinga alisema kuwa ana ushahidi wa kuthibitisha kwamba uchaguzi huo wa urais ulifanyiwa udanganyifu.
''Tutaonyesha ulimwengo ule mchezo uliochezwa, Kile tunachotaka ni Umoja wa Mataifa kubuni jopo la wataalam ambalo litatusaidia kutathmini matokeo hayo''.
Kiongozi huyo wa upinzani alisema kuwa tume ya uchaguzi nchini IEBC ilikuwa chini ya shinikizo kali kutoka kwa maafisa wa serikali inayoongozwa na rais Kenyatta.
Image captionAntonio Gutterres
''Kufuatia mauji ya mtaalam wa maswala ya kiteknolojia katika tume hiyo Chris Msando, wafanyikazi wengine waliogopa''.
''Kile kilichotokea kimeshinikizwa na serikali. Sio kuhusu mimi, Sio Kuhusu Raila Odinga sitokuwa mgombea tena. Tunataka Wakenya kujua kilichofanyika, kile ambacho dunia nzima haielewi kinafanyika''.
''Hakuna haja ya watu kwenda kupanga milolongo mirefu ya kupiga kura kwa saa kadhaa ama kufanya kampeni na huku kompyuta moja katika tume ya IEBC inatumiwa kuchakachua matokeo hayo''.

AfriCOG: Shirika la kutetea haki lavamiwa na maafisa wa serikali Kenya

Wakili wa AfriCOG Haroun Ndubi na mwanaharakati John Githongo wameshutumu uvamizi uliofanywa na maafisa hao mtaa wa Lavington
Image captionWakili wa AfriCOG Haroun Ndubi na mwanaharakati John Githongo wameshutumu uvamizi uliofanywa na maafisa hao mtaa wa Lavington
Polisi na maafisa wa mamlaka ya mapato nchini Kenya (KRA) leo walifanya jaribio la kuvamia afisi za shirika moja la kutetea haki ambalo lilikuwa limefutiwa usajili Jumanne.
Maafisa hao waliokuwa wamevalia mavazi ya kiraia walifika katika afisi za shirika la Africa Centre for Open Governance (AfriCOG) katika mtaa wa Lavington, Nairobi mapema asubuhi.
Walikuwa kwenye magari wawili wakiwa na agizo walilosema lilitoka kwa mahakama kuwapa idhini ya kufanya uchunguzi katika afizi hizo, wakisema lengo lao lilikuwa kufanya uchunguzi kuhusu tuhuma za ukwepaji kodi.
Maafisa hao hata hivyo walizuiwa kuingia na viongozi wa mashirika ya kutetea haki za kibinadamu.
Wakili Haron Ndubi amesema walitilia shaka uhalali wa agizo la mahakama ambalo maafisa hao walikuwa nalo.
odi ya kusimamia mashirika yasiyo ya kiserikali ilikuwa imetoa agizo la kutaka shirika hilo lifunge ikisema limekuwa likiendesha shughuli zake kinyume cha sheria.
Mkuu wa bodi ya kusimamia mashirika yasiyo ya kiserikali Fazul Mohammed, pamoja na kufutia usajili shirika hilo, alikuwa amependekeza wakurugenzi wake wakamatwe.
Shirika la AfriCOG liligonga vichwa vya habari mwaka 2013 baada ya kuwasilisha kesi ya kupinga kuchaguliwa kwa Rais Uhuru Kenyatta kwenye uchaguzi uliokuwa umefanyika mwezi Machi.
Taarifa kwenye vyombo vya habari zimekuwa zikidokeza kwamba huenda shirika hilo linapanga kuwasilisha kesi ya kupinga matokeo ya uchaguzi ambayo yalitangazwa Ijumaa ambapo Bw Kenyatta alitangazwa kuwa mshindi.
Maafisa hao walizuiwa kuingia afisi za AfriCOG
Image captionMaafisa hao walizuiwa kuingia afisi za AfriCOG
Hatua ya kufunga shirika hilo ilitangazwa Jumanne siku moja baada ya serikali kufutia usajili shirika jingine la haki za binadamu, Tume ya Haki za Kibinadamu Kenya (KHRC).
Umoja wa Mataifa na shirika la Amnesty International wameshutumu hatua ya kuyafunga mashirika hayo mawili na kuitaka serikali kuruhusu mashirika ya kutetea haki pamoja na wanahabari kuruhusiwa kufanya kazi bila kuhangaishwa.
Mkurugenzi wa Amnesty International katika kanda ya Afrika mashariki Muthoni Wanyeki amesema njia iliyotumiwa na maafisa hao kuvamia afisi za AfriCOG ni kinyume cha sheria.
Amesema ana wasiwasi sana kwamba serikali ya Bw Kenyatta imeanza kuandama mashirika ya kutetea haki za kibinadamu.

Mkapa miongoni mwa waathiriwa wa upanuzi wa barabara

Rais wa zamani wa Tanzania Benjamin MkapaHaki miliki ya pichaGETTY IMAGES
Image captionRais wa zamani wa Tanzania Benjamin Mkapa
Nyumba inayoaminika kumilikiwa na mke wa aliyekuwa rais wa zamani wa Tanzania Benjamini Mkapa itavunjwa ili kuruhusu upanuzi wa barabara ya Morogoro .
Nyumba hiuyo ya Anne Mkapa itakuwa miongoni mwa maelfu ya nyumba ambazo zinatarajiwa kuvunjwa , shughuli itakayowaathiri zaidi ya watu 10,000.
Gazeti la Th Citizen lilitembelea nyumba hiyo inayodaiwa kumilikiwa na bi Anne na mwanamke mmoja aliyepatikana katika eneo hilo alithibitisha kwamba ni nyumba ya Mkapa.
Natoka familia ya Mkapa, lakini siwezi kusema mengi kuhusu swalka hili.iwapo munataka maelezo zaidi ni muhimu kuwasiliana naye, alisema mwanamke huyo.

Watatu wazama Ziwa Victoria


Kuna ripoti kuwa wavuvi watatu wamepoteza maisha baada ya boti waliyokuwa wakitumia kuzama maji katika Ziwa Victoria.
Watu hao ambao majina yao bado hayajajulikana, walikuwa wakivua samaki katika eneo la Kyagalanyi lililopo kusini mwa Uganda upande wa Ziwa Victoria.
Mmoja wa watu aliyekuwa karibu na tukio, Ivan Ssendijjo alilimbia gazeti la Monitor la nchini humo kuwa wavuvi hao walikuwa wamekwenda kufuata nyavu walizozitega ziwani na ndipo walipopigwa na upepo mkali na kusababisha boti yao kupotea.
“Tulijaribu kwa kadri ya uwezo wetu ili kuwaokoa, lakini hatukuweza kufanikiwa kutambua sehemu waliyopotelea,” amesema.
Ofisa wa polisi katika eneo hilo, Ivan Tenywa amewaambia waandishi wa habari kuwa wamefanikiwa kupata miili ya wavuvi wawili, huku mwingine akiwa bado hajaonekana.
Tukio hilo limetokea siku chache baada ya watu wengine sita kuokolewa na mashua ya polisi wakati boti yao ilipozama katika ziwa hilo

Migogoro ya ardhi yapungua Morogoro


Wakazi wa Kata ya Mngazi, Wilaya ya Morogoro wamesema migogoro ya ardhi iliyokuwa imekithiri katika maeneo yao imepungua kutokana na ushirikiano wao, ambapo awali shughuli za maendeleo ndani ya jamii zilikwama.
Wananchi hao wamesema hayo wakati wakizungumza na mwandishi wa Mwananchi aliyekuwa katika kata hiyo kwa nia ya kufahamu namna migogoro ya ardhi inavyotatuliwa maeneo ya vijijini.
“Migogoro ya ardhi imepungua kutokana na wananchi kutambua njia sahihi ya kutatua migogoro na namna ya kuepuka isitokee tena katika maeneo yetu kwani watu wengi wameuawa na wengine kujeruhiwa,” amesema Asha Ally.
Amesema migogoro ya ardhi iliyokuwa inasumbua katika eneo lao ni pamoja na mipaka, mashamba ya urithi na baadhi ya viongozi wa vijiji kuuza maeneo bila ya kuwashirikisha wananchi, lakini hivi sasa haipo tena kutokana na wengi kupata uelewa, kujua nia sahihi ya kutatua na madhara ya migogoro ya ardhi.
Amesema kwa sasa wananchi wengi wamebadilika baada ya kupata elimu ya umiliki wa ardhi kutoka Kituo cha Wasaidizi wa Kisheria (MPLC) kupitia mradi wa kulinda haki za mwanamke katika kumiliki ardhi unaofadhiliwa na shirika lisilokuwa la kiserikali la Foundation for Civil Society.
Mkazi mwingine, Athuman Seif amesema mradi huo umesadia jamii yao kupatiwa hatimiliki za kimila za ardhi wanayotumia, hivyo kila mmoja kujua mipaka ya eneo lake baada ya kupimiwa na kuepuka muingiliano ambao unaweza kuzua mgogoro.
“Maeneo mengi ya kwetu migogoro ya ardhi ilikuwa inatufanya tushindwe kufanya shughuli nyingine za maendeleo, hivi sasa muda mwingi tuko shambani kulima na sio kushinda baraza la ardhi kusikiliza kesi kama hapo awali,”amesema Seif.
Ofisa Mtendaji wa Kijiji cha Vigolegole, Octavian Kobelo amesema hivi sasa kesi za ardhi katika baraza la ardhi kata zimepungua na kuwa, kabla ya mradi huo walikuwa wanapokea kesi 10 kwa mwezi, lakini kwa sasa kesi moja inapokelewa na kufanyiwa kazi.

Kairuki wa Kenya ashtakiwa kwa udanganyifu wa mamilioni

Mkurugenzi wa Kampuni ya Candy& Candy, Josiah Kiman Kairuki (38), Mkazi wa Mikocheni Jijini Dar es Salaam juzi alipandishwa tena kizimbani katika Mahakama ya Hakimu Mfawidhi Wilaya ya Longido mkoani Arusha, kujibu tuhuma za kujipatia Sh336 milioni   kwa njia ya udanganyifu.
Kairuki anatuhumiwa kujipatia fedha hizo baada ya kudai  kuwa ana kontena  la simu za I- Phone 7 ambalo limezuiwa katika bandari ya Dar es Salaam.
Kairuki ambaye ni raia wa Kenya, Julai 26 mwaka huu  mahakama hiyo ilimwachia huru katika shtaka hilo la kujipatia fedha hizo kwa njia ya  udanganyifu, kutoka kwa  Yusuph Mohamed  kutokana na maombi ya Jamhuri yaliyowasilishwa mahakamani na Mwendesha Mashtaka, Mkaguzi wa polisi Anastazia  Mutatina.
Hata hivyo, baada ya kuachiwa huru na Hakimu Mfawidhi wa mahakama hiyo, Aziza Temu alikamatwa na polisi akiwa nje ya mlango wa mahakamani na kurejeshwa kituo cha polisi cha wilaya ya Longido kwa mahojiano zaidi.
Juzi, mkurugenzi huyo aliunganishwa na Abdinasiri Adamnuru na mbele wa Hakimu Mfawidhi wa wilaya, Aziza Temu na walisomewa mashtaka mawili ya kujipatia fedha hizo kwa njia ya udanganyifu na kosa la pili lilimhusu Adamnuru kujifanya ofisa forodha kutoka Tanzania.
Mwendesha Mashtaka Mkaguzi wa Polisi, Anastazia Mutatina alisema watuhumiwa hao walifanya makosa hayo  kati ya Januari 23 na Juni 10, 2017 na upelelezi wa shtaka hilo bado haujakamilika.
Hata hivyo, aliomba watuhumiwa hao wasipewe dhamana kutokana na kiasi kikubwa cha fedha wanachotuhumiwa na pia wote kutokuwa na makazi wa kudumu hapa nchini.
Hakimu alikubali maombi ya upande wa mashtaka na watuhumiwa hao walirejeshwa katika mahabusu ya Kisongo mjini Arusha hadi Agosti 23 kesi yao itakapotajwa tena. 

Ridhiwani amkumbuka Ndesamburo


Mbunge wa Chalinze mkoani Pwani, Ridhiwani Kikwete amekutana na  familia ya marehemu Philemon Ndesamburo na kuelezea namna mzee huyo alivyokuwa karibu naye.
Ridhiwani amesema kuwa aliwahi kuambiwa na  mzee huyo kuwa anatamani kumuona anakua kijana mwenye mapenzi kwa vijana wenzake.
Ndesamburo aliwahi kuwa mbunge wa Moshi mjini kwa tiketi ya Chadema na pia mwenyekiti wa chama hicho hadi alipofariki dunia dunia miezi michache iliyopita.
Ridhiwani amesema hayo baada ya kwenda kuhani msiba nyumbani kwa marehemu mjini Moshi.
Akizungunza na baadhi ya ndugu na jamaa marehemu Ndesamburo, Ridhiwani amesema alikutana mara ya kwanza ana kwa ana na kuzungumza na mzee huyo miaka kadhaa iliyopita alipokwenda Moshi kumuona babu yake aitwaye Mzee Semindu na pia alikutana naye tena kipindi cha Bunge la Katiba.
"Namkumbuka sana, aliwapenda sana wabunge vijana na hata akiwaona wamekuwa kimya sana aliwauliza kuwa vipi mbona uko mpole leo?” amesema

Mahakama yataka kujua upelelezi kesi ya Aveva, Kaburu


Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu imeutaka upande wa mashtaka katika kesi inayomkabili   Rais wa Klabu ya Simba, Evans Aveva na makamu wake, Godfrey Nyange maarufu kama Kaburu kueleza upelelezi umefikia wapi.
Hakimu Mkazi Mkuu, Victoria Nongwa alieleza hayo baada ya Mwendesha Mashtaka Mwandamizi wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru), Leonard Swai kudai upelelezi bado haujakamilika.
Swai aliomba apewe siku 14 kwa ajili ya kukamilisha ripoti ya polisi ya upelelezi ambayo wanasubiri.
Kwa upande wa eakili wa utetezi, Mutakyamirwa Philemon  aliomba mahakama itoe siku saba, lakini Swai alisisitiza kuomba siku 14 kama ilivyo kwenye kesi nyingine.
Kesi hiyo imeahirishwa hadi Agosti 30, 2017 kwa ajili ya kutajwa ili kuangalia kama upelelezi umekamilika ama la.
 Aveva na Kaburu wanakabiliwa na mashtaka matano ya kughushi, kuwasilisha nyaraka ya uongo na kutakatisha fedha za kigeni Dola300,000 za Marekani.

Mashirika yasiyo ya kiserikali kusomesha elimu ya juu


Zaidi ya wanafunzi 50,000 ambao wamekosa ufadhili wa masomo kutoka kwenye vyanzo mbalimbali vya ufadhili wawapo vyuoni, watanufaika na mikopo  kutoka mashirika yasiyokuwa ya kiserikali.
Mkopo huo utalipwa na shirika lisilokuwa la kiserikali la Tanzania Social Support Foundation (TSSF) kwa kushirikiana na shirika lisilokuwa la kifaida la kimaitaifa la Cosmopolitan Development Foundation (CDF International) .
Kwa pamoja, mashirika hayo yamezindua mpango kabambe wa ufadhili wa masomo kwa wanafunzi wa elimu ya juu hapa nchini ambao wanatokea katika mazingira duni.
Taarifa iliyotolewa na Mkurugenzi Mkuu wa TSSF, Donati Salla imeeleza kwamba mpango huo utatumia zaidi ya Dola1 milioni za Marekani na kutoa fursa kwa zaidi ya wanafunzi 50,000 ambao watanufaika kuanzia mwaka huu.
Mpango huo ambao ni mpya na pekee kwa hapa nchini na una utaratibu ambao unaelekeana na Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa ELimu ya Juu (HELSB) umelenga kutoa fursa sawa kwa wanafunzi wa elimu ya juu ambao wana uhitaji hasa wale ambao wamekosa ufadhili wa masomo kutoka kwenye vyanzo mbalimbali.
Akibainisha malengo ya mpango huo, Salla alisema  mpango huo utafungua madawati ya huduma kwa wanafunzi hao katika taasisi ambazo zinatoa elimu ya juu ambapo kwa mwaka huu taasisi za elimu ya juu 98 ndizo zilizoidhinishwa kutoa elimu hiyo kwa ngazi ya shahada.
Pia, alieleza kwamba wanufaika wa mpango huo watakuwa ni wanafunzi wa Kitanzania ambao wanasoma kwenye taasisi za elimu ya juu zilizopo ndani ya mipaka ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Zaidi ya wanafunzi 59,378 wa elimu ya juu hukosa mikopo kutoka serikalini kila mwaka, jambo ambalo limesababisha mpango huo uanzishwe ili kuwapa fursa.
Katika kuhakikisha kwamba malengo yanatekelezwa kikamilifu, mashirika hayo mawili yameanzisha mfuko wa elimu ya juu unaoitwa Tanzania Social Support Foundation ambao utajikita kutelekeza malengo ya mpango huo.
Salla aliwaomba wanafunzi, taasisi na wadau wote wa elimu ya juu kushirikiana pamoja ili malengo ya mpango huo yaweze kufanikiwa.

Wananchi waandamana kudai ‘chao’ mgodi wa Acacia





Picha na Maktaba
Picha na Maktaba 
Wananchi wanaoudai mgodi wa Acacia North Mara fidia ya maeneo yao kwa kukaa muda mrefu bila kuwalipa, wameandamana kwenda mgodini kushinikiza malipo yao.
Alipoulizwa kuhusu suala hilo, Kamanda wa Mkoa wa Kipolisi wa Tarime/Rorya, Henry Mwaibambe amesema maandamano hayo yanafanyika mara kwa mara kutokana na baadhi ya  majina kuondolewa kwenye orodha ya waliohakikiwa.
Kamanda Mwaibambe amesema kuwa majina ya watu hao yaliondolewa kwenye orodha hiyo na mgodi huo baada ya kukutwa yameongezeka wakati wa kuwasilishwa mgodi hapo kwa malipo yaliyotakiwa kutolewa na kufanya shughuli ya ufidiaji kukwama.
Hata hivyo, kundi hilo la wananchi limetawanywa na polisi waliokuwa na gari la maji ya kuwasha ambalo limesimama kwenye lango mkuu la kuingia mgodi .
"Nina taarifa ya kuwepo kwa maandamano hayo siku za nyuma, lakini kwa siku ya Leo sina hiyo taarifa labda nifuatilie utanicheki baadaye," amesema Kamanda Mwaibambe.
Ameongeza kuwa baada ya mgodi huo kubaina kuwepo kwa ongezeko la idadi ya wanaodai wafidiwe maeneo yao, waliandika barua kwa Mkuu wa Wilaya ya Tarime, Glorious Luoga ili kulishughukikia.
"Mkuu wa wilaya ndiye anayeweza kulisemea hilo vizuri maana nijuaavyo mimi alikabidhiwa orodha hiyo kwa ajili ya kuishughulikia," amesema.
Hata hivyo, simu ya mkononi ya Mkuu wa Wilaya, Luoga ilipopigwa kujua hatua iliyofikiwa kwa wananchi hao kupata haki yao, haikuwa hewani.
Hivi karibuni kundi la wananchi lilivamia kwa siku mbili mfululizo mgodi huo likitaka kuokota mawe ya dhahabu ambapo watu zaidi ya 60 walikamatwa na kufunguliwa mashtaka ya uvamizi na hadi sasa wapo rumande.