Wednesday, August 16

UN yakataa ombi la Odinga kukagua matokeo ya uchaguzi Kenya

Kiongozi wa upinzani nchini Kenya Raila Odinga
Image captionKiongozi wa upinzani nchini Kenya Raila Odinga
Umoja wa Mataifa umekataa ombi la kiongozi wa upinzani nchini Kenya Raila Odinga kukagua matokeo ya uchaguzi wa tarehe 8 mwezi Agosti.
Msemaji wa umoja huo alikataa ombi hilo akisisitiza taarifa ya katibu mkuu wa Umoja huo Antonio Gutierrez ambapo amewataka viongozi wa Kenya kusuluhisho mgogoro wowote wa uchaguzi huo katika taasisi zinazofaa kikatiba.
Umoja huo umesema kuwa utatazama mpango mpya wa Raila Odinga ambao anapanga kutangaza siku ya Jumatano.
Wiki iliopita kiongozi huyo wa Nasa alitoa wito kwa Umoja wa Mataifa kukagua matokeo hayo ya uchaguzi uliokamilika.
Akizungumza na gazeti la Financial Times bwana Odinga alisema kuwa ana ushahidi wa kuthibitisha kwamba uchaguzi huo wa urais ulifanyiwa udanganyifu.
''Tutaonyesha ulimwengo ule mchezo uliochezwa, Kile tunachotaka ni Umoja wa Mataifa kubuni jopo la wataalam ambalo litatusaidia kutathmini matokeo hayo''.
Kiongozi huyo wa upinzani alisema kuwa tume ya uchaguzi nchini IEBC ilikuwa chini ya shinikizo kali kutoka kwa maafisa wa serikali inayoongozwa na rais Kenyatta.
Image captionAntonio Gutterres
''Kufuatia mauji ya mtaalam wa maswala ya kiteknolojia katika tume hiyo Chris Msando, wafanyikazi wengine waliogopa''.
''Kile kilichotokea kimeshinikizwa na serikali. Sio kuhusu mimi, Sio Kuhusu Raila Odinga sitokuwa mgombea tena. Tunataka Wakenya kujua kilichofanyika, kile ambacho dunia nzima haielewi kinafanyika''.
''Hakuna haja ya watu kwenda kupanga milolongo mirefu ya kupiga kura kwa saa kadhaa ama kufanya kampeni na huku kompyuta moja katika tume ya IEBC inatumiwa kuchakachua matokeo hayo''.

No comments:

Post a Comment