Sunday, August 27

HALI YA ESTER BULAYA INAENDELEA VIZURI BAADA YA KUPATIWA MATIBABU


Mjumbe wa Kamati Kuu ya CHADEMA, Mh. Edward Lowassa amefika Hospitali ya Taifa Muhimbili Dar kumjulia hali Mbunge Ester Amos Bulaya.


Dar es Salaam
. Hali ya Mbunge wa Bunda Ester Bulaya aliyelazwa katika Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH ) inaendelea vizuri baada ya kuanza kupatiwa matibabu jana.

Bulaya ambaye alipata tatizo la kupumua baada ya kuzidiwa akiwa mahabusu ya Kituo cha Kati cha Polisi mjini Tarime, alifikishwa hospitalini hapo juzi usiku na kulazwa katika wodi namba 18 Sewahaji.

Akizungumza Ofisa Uhusiano wa Muhimbili, John Stephen alisema leo Bulaya amepata ahueni kiafya na anaendelea vizuri na matibabu.

"Sasa ameanza kujihudumia mwenyewe, anakula vizuri na bado anaendelea na matibabu," amesema Stephen huku akisisitiza kuwa mgonjwa bado anahitaji utulivu kwa kipindi hiki.

Bulaya amesota rumande tangu akamatwe Ijumaa ya Agosti 18 kwa madai ya kuingia jimbo la Tarime na kufanya shughuli za kisiasa kwa kutoa msaada wa mifuko 50 ya saruji kwa ajili ya ujenzi wa miundombinu katika shule za msingi jimboni humo baada ya kualikwa na mbunge mwenzake Ester Matiko

TAMKO LA BAVICHA KUHUSU HALI INAYOENDELEA NCHINI YA KUTOFUATA UTAWALA UNAOZINGATIA SHERIA ZA NCHI


Jeshi la Polisi Arusha lazuia mikutano ya Lema


Arusha. Jeshi la polisi mkoani Arusha, limepiga marufuku mikutano ya mbunge wa jimbo la Arusha mjini (Chadema), Godbless Lema iliyokuwa inaendelea katika jiji la Arusha ili kupisha maandalizi ya mtihani wa darasa la saba na mbio za Mwenge.
Katika barua ya Mkuu wa polisi wilaya ya Arusha, Mrakibu mwandamizi wa polisi (SSP),E.Tille ambayo imethibitisha na Kamanda wa polisi mkoa wa Arusha,(SACP) Charles Mkumbo imeeleza kuwa, Lema amezuiwa kufanya mkutano kuanzia kesho Agosti 27 hadi Septembaa mosi.
"Ofisi ya Mkuu wa polisi wilaya ya Arusha, inakutaarifu kuwa imezuia mikutano yako yeye ratiba kuanzia Agosti27 hadi Septema mosi kwa ajili ya kupisha maandalizi ya kuhitimisha mtihani wa darasa la saba na mwenge wa uhuru" ilisomeka barua hiyo na kushauri Lema kupanga mikutano kuanzia Septemba 8 mwaka huu.
Kamanda Mkumbo amesema, sababu kubwa ya kuzuiwa mikutano hiyo ni kwa kuwa wanahitajika polisi wa ulinzi na hivyo haiwezekani kupata polisi wa kulinda mikutano na pia kushiriki katika masuala ya mitihani na mwenge.
"Haya ni mambo ya kitaifa hivyo ndio sababu OCD amesitisha mikutano ya mbunge na mambo haya yakimalizika ataendelea na mikutano yake"alisema.
Akizungumza na mwananchi jana, Lema alisema anapinga polisi kuzuia mikutano yake, kwani ni ukiukwaji wa sheria na haki za mbunge.
Lema amesema sheria ya bunge kifungu cha  nne fasihi ya  kwanza, kinazungumzia uhuru wa mbunge kufanya mikutano jimboni kwake na kifungu cha 4(1) na (2) vinaelezea uhuru huo wa mbunge kufanya mikutano na pia ni ukiukwaji wa sheria kuzuia mikutano ya mbunge kwenye jimbo lake.
Lema amesema anaamini, kuzuiwa mikutano yake ni njama baada ya kubainika katika mikutano zaidi ya  10 ambayo amefanya katika jimbo la Arusha imekuwa na mafanikio makubwa na wananchi wa Arusha wamepata fursa ya kujua ukweli wa mambo mbali mbali.
"Hizi ni njama najua walipanga kuvuruga mikutano na kuharibu vyombo vyangu wakashindwa, wakanitakama kwa kuzidisha dakika 7 kwenye mkutano wangu mmoja nikawashinda kwa hoja sasa wameona wazuie kabisa na ikiwezekana watumie nguvu"alisema
Amesema sasa anashauriana na wanasheria wake kuona kama akubali barua ya polisi ama aendelee na mikutano kwani kimsingi, maeneo ambayo mikutano imepangwa kufanyika sio ya shule .
"Sasa kesho Jumapili nipo nje ya mji eneo la Olmoti kuna maandalizi yapi ya mwenge na darasa la saba , ntakuwa na mkutano eneo la soko la Shuma kuna mkusanyiko kila siku wa watu, nitaathiri nini huo mwenge ambao utafika kuanzia Septemba 6"amesema
Hata hivyo amesema, baada ya barua hiyo na  kushauriana na mawaziri kadhaa na viongozi wa serikali, atalifikisha pia bungeni, kwani ni jambo la ajabu mbunge kuzuiwa kufanya mikutano kwasababu za mwenge na mitihani ya darasa la saba.
Amesema muda ambao umetakiwa na polisi afanye mikutano, anapaswa kuwa katika shughuli za kibunge jambo ambalo anaamini litaathiri ratiba za utendaji wa kazi zake.

''Je, Dembele anaweza kufikia kiwango cha Neymar?''

Dembele akifiungia France bao la ushindi dhidi ya UingerezaHaki miliki ya pichaGETTY IMAGES
Image captionDembele akifiungia France bao la ushindi dhidi ya Uingereza
Ousmane Dembele ana uwezo wa kuwa kama Neymar na huenda akawa mshindi wa taji la mchezaji bora dunia Ballon d'Or, kulingana na mchezaji wa zamani wa Uingereza na Bayern Munich Owen Hagreaves.
Dembele anatarajiwa kujiunga na Barcelona kwa kitita cha pauni milioni 135.5 kutoka klabu ya Ujerumani ya Borussia Dortmund.
Kiticha hicho cha uhamisho ni cha pili kwa thamani baada ya kile cha pauni milioni 200 ambazo Barca walipokea walipomuuuza Neymar kwa PSG.
Akizungumza kuhusu Dembele, Hagreaves aliambia BBC ni mchezaji bora mwenye umri wa miaka 20 duniani.
Mchezaji huyo wa zamani wa Manchester United aliongezea: Amekuwa akisakwa lakini mtu yeyote ambaye amemuona akicheza nchini Ufaransa na katika ligi ya Bundesliga msimu uliopita atajua kwamba ni mchezaji mzuri sana.
''Atakuwa ndoto dhidi ya mabeki wengi''.
''Kimaumbile ana nguvu na anaweza kucheza kwa kutumia miguu yote miwili.Anaweza kupiga mipira ya adhabu kwa kutumia miguu yote miwili''.

Majaliwa aishukuru Cuba kutambua mchango wa Nyerere


Cuba.Waziri Mkuu Kassim Majaliwa ameishukuru Serikali ya Cuba kwa kutambua na kuthamini mchango mkubwa uliotolewa na mashujaa wa ukombozi wa Bara la Afrika, akiwemo Baba wa Taifa Mwalimi  Julius Nyerere kwa kuwajengea mnara wa kumbukumbu.
Mnara huo umejengwa katika Manispaa ya Playa jijini Havana kwenye eneo maalumu la makumbusho ya mashujaa hao walioshiriki katika ukombozi wa Afrika, ambapo  zimewekwa sanamu zao pamoja na maelezo mafupi ya historia zao na nchi wanazotoka.
Waziri Mkuu amefanya ziara katika eneo hilo Ijumaa, Agosti 25, 2017 na kuweka shada la maua katika mnara huo uliozungukwa na sanamu za mashajuaa wa Bara la Afrika na kuonyeshwa sehemu itakayowekwa sanamu ya  Nyerere.
Akiwa katika eneo hilo, Waziri Mkuu aliishukuru Serikali ya Cuba kwa kujenga makumbusho ya mashujaa hao na kwamba Serikali ya Tanzania itashirikiana na Cuba kuhakikisha kuwa sanamu ya Mwl. Nyerere inawekwa katika sehemu iliyotengwa.
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Instuto Cubano De Amistad Con El Pueblo (Taasisi ya Ushirikiano wa Cuba na Nchi Marafiki),  Jose’ Prieto Cintado amesema mnara huo umejengwa kwa lengo la kutambua thamani na umuhimu wa viongozi hao.
Mkurugenzi huyo amesema Serikali ya Cuba inathamini mchango mkubwa uliotolewa na mashujaa hao katika vita ya ukombozi wa Bara la Afrika, ambapo iliamua kujenga mnara wa kumbukumbu katika nchi yao.
 Amesema wananchi wa Cuba pamoja na watu kutoka mataifa mbalimbali ndani na nje ya Bara la Afrika wanakwenda katika eneo hilo la makumbusho na kujifunza historia za viongozi hao. Pia eneo hilo linatumiwa na watafiti wa masuala ya kihistoria.
Mashujaa ambao tayari sanamu zao zimekwishawekwa kwenye eneo la kuzunguka mnara huo ni pamoja na Jomo Kenyatta (Rais wa kwanza wa Kenya), Modibo Keita (Rais wa Mali), Amilcar Cabral (Rais wa kwanza wa Guinea Bissau).
Wengine ni  Dk Kwame Nkrumah (Rais wa kwanza Ghana), Oliver Thambo (Kiongozi Mwandamizi wa Chama cha Ukombozi cha ANC cha Afrika Kusini), Eduardo Chivambo Mondlane (Kiongozi wa ukombozi nchini Msumbuji).
Wengine ni Samora Moises Machel (Rais wa kwanza wa Msumbuji), Sekou Toure (Rais wa kwanza wa Senegal), Seretse Khama (Rais wa kwanza wa Botswana), Alhaji Aboubakar Tafawa Balewa na Obafemi Jeremiah Awolowo (Mawaziri Wakuu wa zamani wa Nigeria) na Chifu Jeremia Azikiwe (Rais wa zamani wa Nigeria)  .

Samia ataka wanawake wamrithi


Dar es Salaam. Makamu wa Rais, Samia Suluhu Hassan amesema anatamani atakapomaliza muda wake wa uongozi nafasi yake ichukuliwe na mwanamke na watokee wanawake wengi waliofikia mafanikio yake .
Ili kufikia mafanikio hayo Samia amesema ni muhimu kwa wanawake kuwa na umoja na mshikamano na kushirikishana fursa za kujikwamua katika nyanja mbalimbali.
“Mimi siamini kwenye msemo wa adui wa mwanamke ni mwanamke kwani mpaka kufikia hapa kuna mchango mkubwa wa wanawake wenzangu walionilea na kuniamini naweza,”.
Mama Samia amesema hayo leo wakati akizindua jukwaa la uwezeshaji wanawake kiuchumi mkoa wa Dar es Salaam hafla iliyoambatana na uzinduzi wa huduma ya Sim Account ya benki ya CRDB.
Amesema hata sheria zote zikibadilishwa na kuwapendelea wanawake haitaleta tija kama wanawake wenyewe hawatajituma na kuamua kujikwamua.
Amesema muda umefika sasa kwa wanawake kujipanga ni namna gani wataweza kujikomboa kiuchumi na kuhakikisha wanashiriki kikamilifu kuijenga Tanzania mpya.
“Niwasihi wanawake hebu tuache mambo ya umbea, majungu na fitina, tushirikishane fursa, tusaidiane kujikwamua kiuchumi ili kutimiza malengo yetu. Nguvu tunazotumia kwenye kurushana rojo na kupigana majungu tuzitumie kuinuana,”
“Ule wakati wa kutambulika kama mwanamke ‘jiko’ pekee umeisha sasa ni mwanamke ‘viwanda’. Hapa  namaanisha kuwa ni mwanamke mwenye maamuzi yake kiuchumi, kielimu, kibiashara, kisiasa na mwenye uwezo wa kushika nyadhifa za juu katika sekta binafsi na umma na kuwa wawekezaji katika viwanda,”.
Mama Samia amesema ni anategemea kuanzishwa kwa jukwaa hilo ni chachu ya wanawake waliofanikiwa kuwainua wenzao ili kuhakikisha kila mwanamke ananufaika na keki ya watanzania.
Alisema, “Nafahamu miongoni mwetu kuna wabobezi wa masuala mengi tusinyimane ujuzi, tufundishane, tushirikishane fursa.
Aidha alizitaka taasisi za fedha kubuni huduma zitakazowavuta wanawake ikiwa pamoja na kuwawekea riba ndogo kwenye mikopo hasa wanaojihusisha na shughuli za ujasiriamali.
“Kupitia jukwaa la wanawake sasa tunategemea taasisi za fedha zitashindana kututafuta ili zifanye biashara, tutumie fursa hiyo kwa lengo la kuleta maendeleo,” alisema Mama Samia
Akizungumzia huduma ya Sim Account Mkurugenzi Mtendaji wa benki ya CRDB, Dk Charles Kimei alisema inalenga kuwarahisishia wanawake kufungua akaunti kupitia simu ya mkononi.
Amesema  benki hiyo imeona  fursa kubwa ya utekelezaji wa mkakati  kwa kuwakutanisha wanawake katika nyanja ya kiuchumi hivyo ikawaletea huduma hiyo.
"Ni asilimia 17 ya watanzania kati ya 50 milioni ndiyo wanatumia huduma rasmi za kibenki.Katika takwimu hizo wanawake ni milioni 25 pekee. Hii inaashiria kuwa upatikanaji wa huduma hizi bado ni changamoto”.
Kupitia Simu Account mtumiaji anaweza kuhamisha na kupokea fedha kwenda kwenye mitandao ya simu, kulipa ada, kulipia huduma, kuweka fedha kwenye kaunti ya CRDB, kufanya manunuzi ya bidhaa na huduma nyingine nyingi.

CUF watoa salamu za pole


Dar es Salaam. Chama Cha Wananchi (Cuf) kimetoa pole baada ya ofisi  Mawakili wa Kampuni ya Ishengoma Karume Masha and Magai (IMMMA ADVOCATES) yenye makao makuu yake kando ya barabara ya Umoja wa Mataifa, Upanga, Dar es Salaam kuteketea kwa moto.
Chama hicho  kimedai kupokea kwa  masikitiko ya taarifa ya kutokea kwa moto ulioteketeza ofisi hizo leo asubuhi.
Pole hiyo imetolewa kupitia  taarifa iliyotolewa na Naibu Mkurugenzi wa Habari uenezi na Mahusiano ya Umma Mbarala Maharagande kwa madi kwamba  kwamba kinatambua mchango wao katika kupigania haki.
“Tunatoa pole na kuungana na Mawakili na wafanyakazi wote katika kipindi hiki kigumu cha uharibfu wa mali na vitendea kazi mbalimbali vyenye thamani kubwa. Tunatambua mchango mkubwa wa Kampuni ya IMMMA na mawakili wake katika kutetea na kupigania haki, usawa, demokrasia na utawala bora katika nchi yetu,” amesema Maharagande.
Chama hicho kililitaka Jeshi la Polisi kuchukua hatua za haraka katika kufanyia uchunguzi tukio hilo na kutoa taarifa kwa umma ili ujue nini chanzo cha moto huo.
“Nchi yetu hivi sasa  imekumbwa na matukio makubwa ya ukiukwaji wa haki za binaadamu na vitendo vya uhalifu vinavyoonekana wazi kuwa vinaratibiwa makhsusi na kikundi cha watu wenye nia ovu dhidi ya watetezi wa haki, uhuru na demokrasia kwa lengo la kuogofya,” anasema.
Amesema ni wajibu na jukumu la kila Mtanzania kupinga na kulaani vitendo na mwenendo mbaya wa muelekeo wa Taifa letu katika hali hii.