Sunday, August 27

CUF watoa salamu za pole


Dar es Salaam. Chama Cha Wananchi (Cuf) kimetoa pole baada ya ofisi  Mawakili wa Kampuni ya Ishengoma Karume Masha and Magai (IMMMA ADVOCATES) yenye makao makuu yake kando ya barabara ya Umoja wa Mataifa, Upanga, Dar es Salaam kuteketea kwa moto.
Chama hicho  kimedai kupokea kwa  masikitiko ya taarifa ya kutokea kwa moto ulioteketeza ofisi hizo leo asubuhi.
Pole hiyo imetolewa kupitia  taarifa iliyotolewa na Naibu Mkurugenzi wa Habari uenezi na Mahusiano ya Umma Mbarala Maharagande kwa madi kwamba  kwamba kinatambua mchango wao katika kupigania haki.
“Tunatoa pole na kuungana na Mawakili na wafanyakazi wote katika kipindi hiki kigumu cha uharibfu wa mali na vitendea kazi mbalimbali vyenye thamani kubwa. Tunatambua mchango mkubwa wa Kampuni ya IMMMA na mawakili wake katika kutetea na kupigania haki, usawa, demokrasia na utawala bora katika nchi yetu,” amesema Maharagande.
Chama hicho kililitaka Jeshi la Polisi kuchukua hatua za haraka katika kufanyia uchunguzi tukio hilo na kutoa taarifa kwa umma ili ujue nini chanzo cha moto huo.
“Nchi yetu hivi sasa  imekumbwa na matukio makubwa ya ukiukwaji wa haki za binaadamu na vitendo vya uhalifu vinavyoonekana wazi kuwa vinaratibiwa makhsusi na kikundi cha watu wenye nia ovu dhidi ya watetezi wa haki, uhuru na demokrasia kwa lengo la kuogofya,” anasema.
Amesema ni wajibu na jukumu la kila Mtanzania kupinga na kulaani vitendo na mwenendo mbaya wa muelekeo wa Taifa letu katika hali hii.

No comments:

Post a Comment