Sunday, August 27

Samia ataka wanawake wamrithi


Dar es Salaam. Makamu wa Rais, Samia Suluhu Hassan amesema anatamani atakapomaliza muda wake wa uongozi nafasi yake ichukuliwe na mwanamke na watokee wanawake wengi waliofikia mafanikio yake .
Ili kufikia mafanikio hayo Samia amesema ni muhimu kwa wanawake kuwa na umoja na mshikamano na kushirikishana fursa za kujikwamua katika nyanja mbalimbali.
“Mimi siamini kwenye msemo wa adui wa mwanamke ni mwanamke kwani mpaka kufikia hapa kuna mchango mkubwa wa wanawake wenzangu walionilea na kuniamini naweza,”.
Mama Samia amesema hayo leo wakati akizindua jukwaa la uwezeshaji wanawake kiuchumi mkoa wa Dar es Salaam hafla iliyoambatana na uzinduzi wa huduma ya Sim Account ya benki ya CRDB.
Amesema hata sheria zote zikibadilishwa na kuwapendelea wanawake haitaleta tija kama wanawake wenyewe hawatajituma na kuamua kujikwamua.
Amesema muda umefika sasa kwa wanawake kujipanga ni namna gani wataweza kujikomboa kiuchumi na kuhakikisha wanashiriki kikamilifu kuijenga Tanzania mpya.
“Niwasihi wanawake hebu tuache mambo ya umbea, majungu na fitina, tushirikishane fursa, tusaidiane kujikwamua kiuchumi ili kutimiza malengo yetu. Nguvu tunazotumia kwenye kurushana rojo na kupigana majungu tuzitumie kuinuana,”
“Ule wakati wa kutambulika kama mwanamke ‘jiko’ pekee umeisha sasa ni mwanamke ‘viwanda’. Hapa  namaanisha kuwa ni mwanamke mwenye maamuzi yake kiuchumi, kielimu, kibiashara, kisiasa na mwenye uwezo wa kushika nyadhifa za juu katika sekta binafsi na umma na kuwa wawekezaji katika viwanda,”.
Mama Samia amesema ni anategemea kuanzishwa kwa jukwaa hilo ni chachu ya wanawake waliofanikiwa kuwainua wenzao ili kuhakikisha kila mwanamke ananufaika na keki ya watanzania.
Alisema, “Nafahamu miongoni mwetu kuna wabobezi wa masuala mengi tusinyimane ujuzi, tufundishane, tushirikishane fursa.
Aidha alizitaka taasisi za fedha kubuni huduma zitakazowavuta wanawake ikiwa pamoja na kuwawekea riba ndogo kwenye mikopo hasa wanaojihusisha na shughuli za ujasiriamali.
“Kupitia jukwaa la wanawake sasa tunategemea taasisi za fedha zitashindana kututafuta ili zifanye biashara, tutumie fursa hiyo kwa lengo la kuleta maendeleo,” alisema Mama Samia
Akizungumzia huduma ya Sim Account Mkurugenzi Mtendaji wa benki ya CRDB, Dk Charles Kimei alisema inalenga kuwarahisishia wanawake kufungua akaunti kupitia simu ya mkononi.
Amesema  benki hiyo imeona  fursa kubwa ya utekelezaji wa mkakati  kwa kuwakutanisha wanawake katika nyanja ya kiuchumi hivyo ikawaletea huduma hiyo.
"Ni asilimia 17 ya watanzania kati ya 50 milioni ndiyo wanatumia huduma rasmi za kibenki.Katika takwimu hizo wanawake ni milioni 25 pekee. Hii inaashiria kuwa upatikanaji wa huduma hizi bado ni changamoto”.
Kupitia Simu Account mtumiaji anaweza kuhamisha na kupokea fedha kwenda kwenye mitandao ya simu, kulipa ada, kulipia huduma, kuweka fedha kwenye kaunti ya CRDB, kufanya manunuzi ya bidhaa na huduma nyingine nyingi.

No comments:

Post a Comment