Saturday, February 23

Serikali ya Awamu ya Nne yaongoza kukopa


TAASISI isiyo ya kiserikali ina yojishughulisha na masuala ya Madeni ya Taifa na Maendeleo (TCDD), imesema Serikali ya Tanzania ndiyo inaongoza kwa kukopa zaidi, ikieleza kuwa kati ya mwaka 2008 hadi mwaka 2011, imekopa kiasi cha Sh15trilioni na kufanya deni la taifa kufikia Sh21trilioni.
Rais Kikwete aliingia madarakani mwaka 2005, baada ya rais aliye mtangulia, Benjamin Mkapa kumaliza kipindi chake cha uongozi wa miaka 10 kilichoanzia mwaka 1995 hadi mwaka 2005.
TCDD imebainisha kuwa Serikali inakopa fedha hizo kutoka Benki Kuu (BoT), Benki za Biashara, Kampuni za Bima na Mashirika ya Hifadhi za Jamii. Pia inakopa katika taasisi za kimataifa ikiwamo, Benki ya Dunia (WB), Benki ya Maendeleo Afrika (ADB) na Shirika la Fedha Duniani (IMF).
Katika maelezo yake, Mkurugenzi Mtendaji wa taasisi hiyo Hebron Mwakagenda, alisema kuwa kite ndo cha Serikali kukopa fedha kwa ajili ya matumizi yasiyo muhimu pamoja na kuwalipa watumishi wake mishahara, ndiyo sababu ya kukua kwa deni hilo la taifa.
“Serikali ya awamu ya nne imekopa kwa kiwango kikubwa, kwani tangu iingie madarakani imeshakopa Sh15trilioni, sasa sijui mpaka inamaliza muda wake itakuwa imekopa kiasi gani?” alisema Mwakagenda akihoji na kuongeza;
“Hata kama kukopa ni kuzuri basi tukope na fedha tuzifanyie mambo ya maana hasa katika maendeleo, tukope tu pale inapokuwa lazima kufanya hivyo.”
TCDD imeeleza kwamba hali hiyo ni hatari, hasa ikizingatiwa kuwa miaka kadhaa iliyopita, Tanzania kupitia Mpango wa Nchi Maskini zenye Madeni Makubwa (HIPC), ilifutiwa kiasi kikubwa cha madeni, lakini sasa imeanza kukopa tena na deni kukua kwa kasi.
Taasisi hiyo pia imesema kitendo hicho kimechangia kuporomoka kwa uchumi wa taifa kunakosababishwa na riba kubwa za mikopo hiyo, ambapo kulingana na idadi ya Watanzania ukigawanya deni hilo kwa wote, inaonyesha kuwa kila Mtanzania anadaiwa wastani wa Sh450,000.
Mwakagenda, ambaye taasisi yake inafanya kazi ya kuishauri Serikali katika suala zima la deni la taifa na maendeleo, alisema hadi kufikia Oktoba mwaka jana, deni la nje lilikuwa Sh15.9 trilioni.
Kwa mujibu wa taarifa ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), aliyoitoa bungeni mjini Dodoma mwaka jana, taifa linapoteza Sh3 trilioni katika ukwepaji wa kodi na ubadhirifu, huku akishauri kuwa mambo mawili yakifanyiwa kazi deni hilo litapungua au kumalizika kabisa.
“Deni linakuwa kwa kiasi kikubwa na tunakopa katika mabenki ya biashara, ambayo riba yake ni kubwa, fedha nyingi zinazokopwa hutumika kulipa mishahara,” alisema Mwakagenda.
Alifafanua kwamba mwaka 2007 hadi 2008 deni la taifa lilikuwa Sh6.4 trilioni na kwamba, kuanzia mwaka 2007 hadi 2011 deni hilo limeongezeka hadi Sh21 trilioni.
Alisema deni ni utumwa na fedheha na kwamba nchi inatakiwa kukopa kwa ajili ya ujenzi wa miundombinu, kwamba ifanye hivyo kama itashindwa kabisa kupata namna nyingine ya kugharimia maendeleo.
“Ukopaji katika benki za biashara zinazotoa riba kubwa kwa ajili ya kulipia matumizi ya kawaida ni hatari kwa taifa na kwa vizazi vya sasa na baadaye,” alifafanua.
Nini kifanyike
“Kama taifa, tukijipanga zaidi katika kuboresha usimamizi katika sekta mbalimbali sambamba na kusimamia mapato na ulipaji kodi, hatutakopa tena katika mabenki ya biashara,” alisema na kuongeza:
“Hata ukitazama ongezeko la deni hili la taifa, ni sawa na Sh3 trilioni kila mwaka, fedha ambazo kwa mujibu wa taarifa ya CAG zinapotea kila mwaka.”
Alifafanua kwamba hilo li nawezekana iwapo Serikali itaongeza wigo wa kudhibiti misamaha ya kodi, kuziba mianya ya ukwepaji kodi na kuangalia kwa makini sekta mpya kama za madini, gesi na utalii kuliko kukazana kukopa kama njia pekee ya kuendesha shughuli za maendeleo.
“Tunataka Serikali ifungue macho na kuona fursa mpya za kupata mapato ya ndani badala ya kugeuza mikopo kuwa ndiyo suluhisho la kudumu la mipa ngo yetu ya maendeleo,” alisema Mwakagenda.
Alisema jambo walilofanya kama TCDD ni kutoa mapendekezo kwamba Katiba ijayo iwe na kipengele kitakachoeleza kiwango cha ukomo wa kukopa (debt ceiling).
Januari 4 mwaka huu Mwakagenda aliliambia gazeti hili kwamba deni hilo ni kiwango cha juu kabisa kwa nchi kuweza kukopa kutoka kwenye masoko ya kimataifa. Deni limeongezeka kwa dola 456.1 milioni katika ki pindi cha mwaka mmoja tu tangu Oktoba 2011.
Alisema taarifa za Benki Kuu ya Tanzania zinaonyesha kuwa deni la ndani limefikia Sh5.1 trilioni hadi kufikia Oktoba mwaka jana na kwamba kiasi hicho ni sawa na ongezeko la Sh513 bilioni tangu mwaka 2011.
Alisema zipo fedha zinazotumika kujenga barabara, madaraja, majengo mbalimbali ya shule na vyuo, lakini kinachotakiwa ni Serikali kufikiri mara mbili kabla ya kuamua kukopa na kuzitumia fedha hizo za mkopo.
Katika mapendekezo yao, Mwakagenda alisema wameitaka Serikali kuwa na nidhamu katika kukopa kwa kuwa deni hilo limevuka kiwango cha kimataifa.
Katika ufafanuzi wake, Mwakagenda alisema baada ya kuwasilisha kwa Serikali kiwango hicho cha deni la taifa, Gavana wa Benki Kuu (BOT), Profesa Beno Ndulu alitoa takwimu kwamba hali ya deni siyo mbaya na kwamba imefikia asilimia 19, kiwango ambacho kinakubalika kimataifa kukopa tena.
“Waziri wa Fedha na Uchumi, Dk William Mgimwa yeye alitueleza kuwa bado tunakopesheka, lakini pamoja na hayo hatukubaliani na kauli ya Serikali kwa kuwa katika kipindi cha miaka mitano, deni limekuwa kwa kiwango kikubwa” alisema Mwakagenda.