Wednesday, June 12

"NIKIFA ASHA BARAKA ASIJE KWENYE MSIBA WANGU, NA KAMA ATAKUFA YEYE BASI SITAENDA".....ALLY CHOKI

MKURUGENZI wa Extra Bongo Ally Chocky ametoa kauli nzito kuhusu waajiri wake wa zamani, Asha Baraka na Baraka Msilwa.

Katika maongezi yake Chocky alisema katika watu asiowapenda duniani ni Asha Baraka (Mkurugenzi wa ASET) na Baraka Msilwa (Mwenyekiti wa ASET). Asha Baraka na Baraka Msilwa ni mtu na kaka yake.

Kiongozi huyo wa Extra Bongo akaenda mbali zaidi kwa kusema: “Nikifa leo hii Asha Baraka na Baraka Msilwa wasije kwenye mazishi yangu, na kama watanitangulia wao na mimi sitakwenda kwenye mazishi yao.

“Nina uhakika leo hii nikipata matatizo au nikifa Asha na Msilwa watafurahi, sasa kuna haja gani ya watu kama hao kuja kwenye mazishi yangu.

“ASET ni kama simba wako tayari kukutafuna hadi macho, nimetafakari kwa muda mrefu sana nimevumilia mengi sana lakini nimeshindwa na sasa natamka rasmi, Nikifa wasinizike.”

Chocky ameorodhesha sababu nyingi sana za kufikia hatua hiyo lakini miongoni mwa sababu zake ni hizi tatu:

Kwanza kitendo cha Aset kumpeleka mahakamani kumdai gari, pili Aset kukataa kurudisha pesa za Miraji Shakashia na tatu ni ASET kutothamini michango ya wasanii walioizalishia pesa nyingi.

Chocky ansema kitendo cha Aset kumpeleka mahakamani kumdai gari ambalo walimpa mwenyewe kilimkera sana.

“Mtu anapokupeleka mahakamani maana yake ni kwamba yupo tayari hata ufungwe, ukifungwa maana yake ni kila kitu kwenye maisha yako kinaharibika.

“Gari walinipa wenyewe na maandishi yapo kwamba nikimaliza mkataba wangu gari litakuwa la kwangu.

Lakini badala yake wakanigeuzia kibao na kwenda kunidai mahakamani kwamba nimeiba gari.

Kuhusu Shakashia, Chocky amesema mwanamuziki huyo alichukua shilingi milioni tano za Extra Bongo ili ajiunge nayo na akasaini mkataba wake.

“Lakini badala yake Shakashia akaingia mitini na pesa zetu, Aset wakasema watazirudisha wao na sasa wanakuja na hadithi mpya.

“Wanasema hawawezi kurudisha hizo pesa eti kwa vile wananidai, wanasahau kuwa mkataba wa Shakashia ni kati yeke na Extra Bongo na sio Ally Chocky.

“Hata kama kipo wanachonidai hiyo ni kati ya Chocky na Aset na haiingii akilini kuliingiza suala la Shakashia ndani yake.

“Huu ni utapeli na inatoa picha kuwa Aset walimtumia Shakashia kufanya utapeli huu, lakini wajue kuwa mwisho wa siku atakayeathirika ni Shakashia mwenyewe,” alisema Chocky.

Kuhusu kutothamini wasanii waliozalishia pesa nyingi kampuni, Chocky anasema wasanii walipota ASET na kuizalishia pesa hawana chochote walichopewa kulingana na thamani ya kile walichokizalisha. “Sio pesa tu bali hata heshima pia hakuna,” alifafanua Chocky.

Chocky akazama zaidi na kuwataja wakongwe kama Shem Karenga na Kasongo Mpinda ambao waliwahi kufanya kazi katika familia ya kina Asha Baraka kupitia bendi za MK Group na MK Beats.

“Wako wapi Kasongo Mpinda na Shem Karenga, Kasongo aliwatengenezea pesa nyingi kupitia MK Group “Ngoma za Magorofani” huku Shem Karenga akiwatengenezea utajiri katika MK Beats “Tukunyema”.

“Lakini hebu tujiulize wako wapi hawa wazee na wana kipi cha kujivunia?” alihoji Chocky.

Haikuishia hapo, tuliamua kumpigia Asha Baraka ambaye naye alikuwa na yake ya kujibu kuhusu mapigo ya Chocky.

Asha Baraka amesema hayo ni mambo ya kike na kwamba kuzikana si tija.

Asha Baraka akasema: “Hata mimi sina mpango wa kwenda kwenye mazishi yake na yeye pia asije kwenye mazishi yangu.

“Hivi kuzikana ni nini? Wazazi wangu walifariki na Chocky hakuja kuzika, kilipungua nini? Halafu mi nikifa sitaona na yeye akifa sitaona kwahiyo hiyo siyo ishu, wamanyema wenzangu watatosha kunizika hata wasanii wote wasipokuja achilia mbali huyo Chocky.

“Nilimzikia wazazi wake na hakuliona hilo kwahiyo hata tusipozikana hakipungui kitu.

“Chokcy tunamdai gari na pesa shilingi milioni 13, kwenda mahakamani ni sehemu ya kudai haki na yeye kama anaona amedhulumiwa kuhusu pesa za Shakashia basi aende mahakamani.”

Asha Baraka alimtaka Chocky aelewe kuwa baadhi ya wasanii wa Twanga ni virusi na watammalizia pesa zake bure.

“Wako wasanii wamelelewa vizuri, wamefanyiwa mengi na Twanga na wanaelewa utu kwahiyo akijipendekeza kwao atapoteza pesa zake bure.

“Hao ni virusi wetu, wanatuletea taarifa zote za kila mtu anapotaka kuwachukua.
Asha Baraka amesema kama ni roho mbaya Chocky ndio anaoongoza kwa roho mbaya.

“Alikaa yeye na kamati yake yenye wakiwemo mpaka wafanyakazi wa umma na kuzoa wanamuziki wa Twanga”

Anawataja wasanii wa Twanga waliowahi kuchukuliwa na Extra Bongo ni pamoja na Ferguson, Rogart Hegga, Hosea, Otilya, Nyamwela, Danger Boy, Aisha Madinda, Maria Soloma, Subrina pamoja na Kanuti ambaye baadae alirudisha pesa zao na kubakia Twanga.

Asha Baraka anawataja wasanii wengine wenye damu ya Aset ambao wako Extra Bongo ni Ephraim Joshua, Martin Kibosho, Athanas, Banza Stone na yeye mwenyewe Chocky.

“Kwa mfumo huo utaona wazi kuwa Extra Bongo inapumua kwa nguvu ya Aset lakini sisi hatujasema kitu, kama ni kutoa kauli ya kutozikana basi sisi ndio tulipaswa kuwa wa kwanza,” alifafanua Asha.

“Tunajua pia kuwa Chocky alihusika kushawishi usajili wa Chaz Baba Mashujaa Band akiamini kuwa kwa kuondoka Chaz Twanga itakufa,” aliongeza

Asha Baraka amemtaka Chocky aonyeshe mfano wa namna ya kulea wasanii kwa kuwapa maisha mazuri wanamuziki waandamizi kama Banza na Rogart.

“Asiangalie mambo ya Aset, ajitazame yeye anaishi vipi na Banza anaishi vipi, badala ya kutoa milioni tano kumnunua Shakashia, angemnunulia japo Corola Banza au Rogart.

“Chocky aitishe mkutano wa waandishi wa habari halafu mimi na yeye twende na mikataba ya wasanii inayoonyesha mishahara na marupurupu tuone nani analea vizuri wasanii.

“Mimi nilifanya kazi Bima na sijajengewa nyumba wala kununuliwa gari, silalamiki kwa kuwa haikuwa sehemu ya makubaliano yetu.

“Kama Chocky anadhani muziki unalipa kiasi cha kumnunulia kila mtu gari na nyumba basi atuonyeshe mfano kupitia Extra Bongo.

“Kila baya linalomfika basi mchawi ni Aset, mbona mimi naumwa mguu na sijawahi kusema ni Chocky?

“Chocky akapime afya yake apate ukweli, tunajua rekodi ya sehemu alizopita, sasa asije akadondoka akasema ni Aset …akapime kwanza” alimaliza Asha Baraka.

ALIANZISHA JAYDEE SASA IMEKUWA FASION AMA? HEBU TUELEZANE.

CCM YAPINGA UWEPO WA SERIKALI TATU....

Chama Cha Mapinduzi (CCM), kimepinga muundo wa Muungano wa Serikali tatu unaopendekezwa katika rasimu ya Katiba Mpya iliyotolewa na Tume ya Mabadiliko ya Katiba mwanzoni mwa wiki iliyopita. Chama hicho tawala kimesema bado kinaamini katika muundo wa Serikali mbili.


Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM, Nape Nnauye aliwaambia waandishi wa habari mjini Dodoma jana kwamba mapendekezo yaliyowasilishwa mbele ya Tume hiyo yanabaki kama yalivyo, hivyo msimamo wao ni kuwapo kwa muungano wenye muundo wa Serikali mbili.

“Mapendekezo ambayo ndiyo msimamo wa chama tulishayawasilisha kwenye Tume kuwa sisi tunapendekeza mfumo wa Serikali mbili na siyo tatu wala moja,” alisema Nape alipokuwa akitoa taarifa ya uamuzi wa Kamati Kuu (CC) ya CCM iliyokutana usiku wa kuamkia jana kujadili suala hilo.

Kauli ya Nape inafanana na matamshi ambayo yamewahi kutolewa na baadhi ya wanasiasa wakongwe ambao ni makada wa CCM wakiwamo, mawaziri wakuu wastaafu, Frederick Sumaye na John Malecela, Waziri wa Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Samuel Sitta na baadhi ya wabunge ambao mara kadhaa wamekaririwa wakipinga pendekezo la Serikali tatu.


Hata hivyo, Nape alisema matamshi ya viongozi hao yalikuwa ni maoni yao binafsi na kauli yake ndiyo rasmi ya chama hicho... “Mimi ndiye msemaji wa chama hiki. Ndiye ninayeeleza msimamo wa chama chetu, yanayozungumzwa na watu wengine hata kama ni viongozi siyo msimamo wa chama ni maoni yao binafsi.”


Habari ambazo gazeti hili ilizipata zinasema katika kikao hicho cha CC kulijitokeza hofu ya suala la wananchi kuwa na mamlaka ya kuwang’oa wabunge ikiwa hawatatekeleza masilahi yao na kwamba pendekezo hilo lina upungufu kwani halitafsiri masilahi hayo ni yapi.

Waunda kamati
Nape alisema rasimu iliyotolewa na Tume siyo waraka wa mwisho kwani bado unatoa fursa kwa Watanzania kuijadili na kutoa maoni yao na kwamba CCM kitatumia nafasi hiyo kuwasilisha maoni yake kuhusu jambo hilo.


Alisema chama hicho kitawasiliana na wanachama wake zaidi ya 6,000 nchini ili waendelee kutoa maoni yao kuhusu suala hilo. “Wengi wanadhani rasimu hii ndiyo ya mwisho… hii ni ya mwanzo tu, itajadiliwa italetwa ya pili na ya tatu, kwa hiyo hatuwezi kusema kilichoelezwa kwenye tume ndiyo msimamo.


Ndiyo maana tumeamua kurejesha suala hili kwa wanachama wetu liendelee kujadiliwa,” alisema na kuongeza:
“Kama wanachama wetu wakiamua kuwepo kwa Serikali tatu, hatutachakachua, tutayachukua na kuyapeleka kama msimamo wetu, lakini tutakubaliana ikiwa uamuzi utakuwa umewahusisha wanachama wetu katika ngazi zote.

“Hatuangalii kipengele kimoja tu. Tutapitia vipengele vyote hadi kuzimaliza kurasa zote zaidi ya 70 zinazoainisha mapendekezo ya Tume ya Jaji (Joseph) Warioba.”

Alisema wanachama wake wanapaswa kuipitia na kuijadili rasimu hiyo kwa kuzingatia mapendekezo kilichoyatoa awali wakati wa mchakato wa kukusanya maoni ya Katiba Mpya. “Tulitoa maoni yetu na sasa tunaijadili Rasimu ya Katiba Mpya kwa kuzingatia maoni yetu yale, CCM tunakwenda kwa mujibu wa sheria,” alisema.


Habari kutoka ndani ya CC ya CCM zinasema chama hicho kimeipa kazi kamati ambayo ilitumika kuandaa mapendekezo yake awali, kupitia rasimu hiyo na kufanya ulinganisho wa yale ambayo chama hicho kilipendekeza dhidi ya yale yaliyozingatiwa katika Rasimu ya Katiba hiyo.


“Kamati itafanya ulinganisho na baada ya hapo tutakwenda kwa wanachama kuwaeleza ni yapi tulipendekeza kama chama na ni yapi ambayo Tume imeyazingatia na hapo tutapata mawazo yao ambayo tutayatumia katika ngazi ya mabaraza ya Katiba,” kilisema chanzo chetu

PICHA ZA WAKENYA WALIVYOANDAMANA JUNE 11 NA KINYAGO CHA NGURUWE NA DAMU WAKIPINGA MISHAHARA YA WABUNGE

Miungano ya kijamii ikiongozwa na Bunge la mwananchi,Muhuri na pawa 254 miongoni mwa mengine yameandaa maandamano ya pili kupinga juhudi za wabunge kuhujumu tume ya kuratibu mishahara nchini kenya SRC ili kujiongezea mishahara ya hadi laki nane kinyume na ilivyopendekezwa na SRC.


Tofauti na wiki kadhaa zilizo pita ambapo waandamanaji waliwaelekeza nguruwe walioandikwa majina ya wabunge walio unga mkono mswada huo, hii leo waandamanaji walibeba kinyago wa nguruwe na damu walio ashiria mwisho wawabunge kukandamiza wakenya. huku wakijimwagilia damu kama ishara ya kuumizwa na kodi ya kuwalipa wabunge.
Waandamanaji pia walibeba mfano wa noti za shillingi alfu moja pesa za kenya zilizo chorwa Nguruwe mkubwa kwa upande mmoja na wanawe kwa upande wa pili, huku wakiwarushia wabunge noti hizo kuashiria kujitakia makuu kwa wabunge hao.


Viongozi wa waandamanaji wameahidi kuendeleza maandamano hadi pale wabunge watakapo sitisha hujuma dhidi ya tume ya bi sara serem ama SRC.
Tume ya SRC imependekeza wabunge kulipwa mshahara wa kati ya shillingi laki Nne hadi laki saba.Ilihali wabunge walipendekeza mshahara wa hadi shillingi millioni moja.

kwamujibu wa freebongo.blogspot.com