Wafanyakazi wa mizani nchini wametakiwa kufanya kazi kwa weledi, uadilifu na kuachana na vitendo vya rushwa ili kuleta tija na ufanisi wa kazi zao
katika usimamiaji na ulinzi wa barabara ambazo Serikali imekuwa ikitumia gharama kubwa katika ujenzi wake.
Hayo yamesemwa na Naibu Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano (Sekta ya Ujenzi), Mheshimiwa Elias Kwandikwa, leo mkoani Shinyanga, alipokuwa akikagua mzani wa Tinde (Shinyanga), na Mwendakulima (Kahama), ambapo amesisitiza ushirikiano kati ya wafanyakazi hao na madereva ili kutatua changamoto zinazojitokeza katika vituo vya mizani.
"Watumishi na madereva shirikianeni kutokomeza vitendo vya rushwa, kamwe msijihusishe kutoa wala kupokea rushwa ili kupata huduma za haraka, tukikubaini tutakuchukulia hatua kali za kisheria", amesema Naibu Waziri Kwandikwa.
Aidha, ametoa wito kwa madereva wa magari ya mizigo wanaotakiwa kuwa na stika maalum za usafirishaji wa mizigo yao kufuata utaratibu wa kuchukua stika hizo mahali husika ili kuepusha usumbufu na msongamano wa magari katika vituo vya mizani.
Akiwa katika eneo la sehemu ya maegesho na kulaza magari mjini Kahama Naibu Waziri Kwandikwa, ametoa wito kwa viongozi wa Halmashauri hiyo kuchukua hatua kali kwa madereva wanaopaki nje ya eneo hilo, ili kudhibiti uchafuzi wa mazingira unaoweza kufanywa na baadhi ya madereva hao.
Ameshauri kwa uongozi wa Halmashauri hiyo kuona namna ya kujenga maegesho mengine kama hayo ili kupata chanzo cha mapato na kusaidia kuujenga mji kuwa na Taswira nzuri.
Kwa upande wake, Meneja wa Wakala wa Barabara (TANROADS), mkoani Shinyanga, Mhandisi Mibala Ndilindi, amethibitisha kuwepo kwa vitendo vya rushwa kwa baadhi ya wafanyakazi wa mizani nchini ambapo amefafanua katika kupambana na suala hilo kwa watumishi wa mkoa wake tayari mwezi uliopita amewachukulia hatua za kinidhamu watumishi watatu wa mzani wa Mwendakulima.
Naye, Msimamizi wa shughuli za mzani wa Mwendakulima kutoka TANROADS Shinyanga, Bi Herieth Monjesa, amesema kuwa changamoto za msongamano wa magari katika mizani zinasabaishwa na baadhi ya madereva wa magari ya mizigo wanaotakiwa kuwa na stika maalum za usafirishaji wa mizigo yao kushindwa kufuata utaratibu, hivyo kupelekea usumbufu kwa wahudumu na watumiaji wengine wa mizani.
Katika hatua nyingine, Naibu Waziri Kwandikwa, amekagua barabara ya Uyovu- Bwanga (KM 45), ambapo ujenzi wake kwa sasa umefika asilimia 98 na mkandarasi amebakisha kazi za ujenzi wa mifereji na uwekaji wa alama za barabarani.
Imetolewa na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini, Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano.
Naibu Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano (Sekta ya Ujenzi), Mheshimiwa Elias Kwandikwa (Mwenye suti), akiangalia namna shughuli za upimaji wa magari zinavyoendeshwa katika mzani wa Tinde, mkoani Shinyanga. Kushoto kwake ni Meneja wa Wakala wa Barabara (TANROADS), wa mkoa huo, Mhandisi Mibala Ndilindi.
Msimamizi wa shughuli za mzani wa Tinde kutoka Wakala wa Barabara (TANROADS), mkoani Shinyanga, Bw. Lugembe Vicent (kushoto), akitoa taarifa ya kiutendaji ya mzani huo kwa Naibu Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano (Sekta ya Ujenzi), Mheshimiwa Elias Kwandikwa. Mzani huo unapima magari 300 kwa siku.
Naibu Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano (Sekta ya Ujenzi), Mheshimiwa Elias Kwandikwa, akiangalia namna watumishi wa mzani wa Tinde, mkoani Shinyanga wanavyopima na kurekodi taarifa za magari yanaoingia kupima uzito kwenye mzani huo.
Magari yakiwa katika foleni kusubiri huduma za upimaji uzito ili kuendelea na safari kwenye mzani wa Tinde, mkoani Shinyanga.
Muonekano wa barabara ya Uyovu- Bwanga (KM 45) kwa kiwango cha lami iliyopo mkoani Geita, ikiwa imekamilika kwa asilimia 98.