Friday, October 20

Finland ,Tanzania kushirikiana kuitunza


Dar es Salaam. Balozi wa Finland nchini, Pekka Hukka amesema Serikali yake itaendelea kushirikiana na Tanzania katika utunzaji wa misitu na mazingira kwa kuwezesha miradi mbalimbali inayohusiana na sekta hiyo.
Balozi Hukka ameyasema hayo leo jijini Dar es Salaam, muda mfupi baada ya kupanda mti kuadhimisha miaka 100 ya uhuru wa Finland na miaka 50 ya nchi hiyo kujihusisha na sekta ya misitu.
Balozi Hukka amesema nchi yake inaamini miti na misitu ina thamani kubwa kwa uchumi na maisha ya watu hivyo ina wajibu wa kuitunza.
Kupitia program na miradi mbalimbali ya mazingira na maliasili nchi hiyo imekuwa ikitoa fedha kuhakikisha miti na misitu inaendelea kuwepo na kuoteshwa kwa wingi.
Amesema kwa sasa tayari nchi yake imetenga Euro 10 milioni ambazo ni zaidi ya Sh26 bilioni kwa ajili ya mradi utakaoviwezesha vijiji kushiriki katika utunzaji na uhifadhi wa misitu.
“Tumeshazungumza na kukubaliana na Wizara ya Maliasili na Utalii kuhusu huu mradi kila kitu kipo sawa tunasubiri maelekezo madogo kutoka wizara ya fedha ili utekelezaji uanze,”amesema Hukka
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Jumuiko la Maliasili Tanzania (TNRF), Dk Suma Kaare ameiomba serikali kuendelea kushirikiana na wadau kuweka mikakati mbalimbali itakayohakikisha misitu inawanufaisha wananchi.
Amesema hilo likizingatiwa wananchi nao watashiriki kikamilifu katika utunzaji na usimamizi wa misitu hiyo.
“Wenzetu wa Finland wamekuwa wakitufadhili kwa muda mrefu katika masuala ya misitu, tuna kila sababu ya kushukuru kwa hilo. Kwa upande wa serikali tunaona ni muhimu kwa wananchi kuendelea kushirikishwa na wakajiona ni sehemu ya maliasili hii,”amesema
Amesema ni muhimu kuwa na mipango ya uvunaji endelevu wa misitu kwa kila halmashauri ambayo pia itahusisha wananchi wa eneo husika.

No comments:

Post a Comment