Wednesday, September 4

‘Mvua za Lowassa’ zagonganisha mawaziri

Dodoma.Suala la mvua za kutengeneza kutoka nchi ya Thailand maarufu kwa jina la ‘Mvua za Lowassa’ liliwagonganisha mawaziri wawili wa Serikali bungeni jana.

Ubishi mkali ulizuka baina ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais, Mazingira, Dk Terezya Huvisa na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Uratibu na Bunge), William Lukuvi waliokuwa wakivutana juu ya ukweli kuhusu teknolojia hiyo.

Wakati Waziri Huvisa akisema kwamba hakuna utaalamu wa aina hiyo, Lukuvi alisimamia kumpinga na kusisitiza kuwa jambo hilo lipo.

Suala la mvua hizo lililetwa nchini na aliyekuwa Waziri Mkuu Edward Lowassa mwaka 2007, baada ya kufanya ziara Thailand ambako alivutiwa na utaalamu wa kutengeneza mvua na kuahidi kuuleta nchini.

Kutokana na mvutano wa mawaziri hao, Lowassa ambaye pia ni Mbunge wa Monduli (CCM), alipewa dakika moja na Mwenyekiti wa Bunge, Jenister Mhagama kutoa ufafanuzi ambapo aliunga mkono hoja ya Lukuvi.

Malumbano hayo yalisababishwa na swali la nyongeza la Mbunge wa Viti Maalumu (Chadema), Susan Lyimo ambaye alihoji mpango wa kutengeneza mvua ulipoishia kwa kuwa Serikali imekuwa kimya.

“Sasa ni miaka takriban sita au saba tangu Serikali ilipokuja na mpango wa kutengeneza mvua ambao iliuchukua kutoka nchi za wenzetu, mpango huo umefikia wapi?” aliuliza.

Akijibu swali hilo, Waziri Huvisa alisema: “Mimi ni Rais wa Mazingira wa Afrika, nasema hakuna kitu kama hicho, si Marekani wala Malaysia ambao wanaweza kutengeneza mvua, hayo ni mabadiliko ya tabianchi tu.”

Waziri Lukuvi alionyesha kutokuridhishwa majibu hayo, ndipo aliposimama kutoa ufafanuzi na kusema Lowassa alikwenda Thailand ambako kuna utaalamu huo na kusisitiza kwamba upo na bado unaendelea kutumika hata Ujerumani wanakotumia mitambo ya kijeshi kusambaratisha mawingu.

Alisema kilichokwamisha mpango huo nchini ni ufinyu wa bajeti ya Serikali.

Baada ya majibu hayo, Lowassa alisimama akitaka kutetea wazo lake. Hata hivyo, kabla ya kumruhusu, Mhagama alimwomba akae chini kwanza ili atoe maelekezo.

“Mheshimiwa Lowassa, yeye siyo waziri na hivyo hastahili kutoa majibu ya Serikali, lakini kwa kutumia kanuni zetu bungeni kuhusu kutengeneza utaratibu mzuri wa kuongoza Bunge, naomba Lowassa usimame sasa walau kwa dakika moja au mbili utoe ufafanuzi,” alisema Mhagama.

Aliposimama Lowassa alizungumza kwa ufupi; “Nakushukuru Mheshimiwa Mwenyekiti, nilitaka kukazia tu kuwa jibu lililotolewa na Mheshimiwa Lukuvi ndilo jibu sahihi.”

Majibu hayo yalisababisha Bunge kulipuka kwa shangwe.

Mara baada ya majibu ya Lowassa, Waziri wa Kilimo, Chakula na Ushirika, Christopher Chiza naye alisimama akitaka kutoa maelezo. Hata hivyo, Mhagama alisema inatosha na kuwaagiza mawaziri hao kukutana kuliangalia jambo hilo badala ya kuwa na majibu kinzani.

Awali, katika swali la msingi, Mbunge wa Viti Maalumu (Chadema), Rachel Mashishanga alitaka kujua ni kwa nini Serikali isirasimishe utaalamu wa kuleta mvua kutoka kwa waganga wa jadi walioko Mikoa ya Katavi na Rukwa ili maeneo yanayokabiliwa na ukame yapate mvua?

Waziri wa Kilimo, Chakula na Ushirika, Christopher Chiza, alipinga mpango huo na kusema hakuna kitu kama hicho isipokuwa wapo watu wenye utaalamu wa kuangalia mawingu yanayoendana na mvua.

Alisema watu wote wanaosema kuwa wanaweza kutengeneza mvua kwa imani za kishirikina ni waongo na hivyo hawapaswi kuaminiwa.

Alisema siyo wakati mwafaka kwa Serikali kushinikizwa kurasimisha utaalamu huo wa kuleta mvua kwa kuwa hakuna tafiti zozote zilizofanyika na kuthibitisha kuwapo kwake.

Wabunge Z’bar wakwamisha Muswada wa kura za Maoni - mwananchi

Dodoma. Muswada wa Sheria ya Kura ya Maoni wa mwaka 2013 uliokuwa ujadiliwe katika mkutano wa 12 wa Bunge unaoendelea mjini Dodoma, umeondolewa na sasa utajadiliwa Bunge lijalo.

Habari za uhakika zilizopatikana jana, zilisema kwamba kuahirishwa huko kumetokana na wajumbe wa Kamati ya Katiba, Sheria na Utawala ya Bunge wanaotoka Zanzibar kupinga vikali kura ya maoni kupigwa visiwani humo kwa kuwa tayari huko kuna sheria hiyo.

Muswada huo ulikuwa ujadiliwe na wabunge katika kikao cha Bunge kinachoendelea ukitanguliwa na Muswada wa Sheria ya Marekebisho ya Sheria ya mabadiliko ya Katiba wa mwaka 2013.

“Ukisoma huu Muswada unasema kura hiyo itapigwa Tanzania Bara na Zanzibar sasa sheria hii ina apply vipi (inatumikaje) Zanzibar wakati kule tuna sheria yetu tayari?” alihoji Mbunge mmoja wa Zanzibar.

Kaimu Katibu wa Bunge, John Joel alipoulizwa jana, alithibitisha kuondolewa kwa muswada huo wa kura ya maoni kusema na utakaojadiliwa ni ule wa Sheria ya Mabadiliko ya Katiba pekee.

“Bunge litaahirishwa Ijumaa (keshokutwa) na ni kweli huo Muswada wa Kura ya Maoni umeondolewa kwa sababu bado uko kwenye ngazi ya kamati,” alisema Joel.

Alipoulizwa sababu za kuondolewa kwa muswada ambao ulishaingizwa kwenye ratiba ya Bunge, alitaka swali hilo aulizwe Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Uratibu na Bunge), William Lukuvi.

Waziri Lukuvi alithibitisha kuondolewa kwa muswada huo na kusema utajadiliwa katika Mkutano wa Bunge wa Oktoba.

“Ni kweli muswada huu hautajadiliwa na Bunge hili bado kuna mashauriano yanaendelea kati ya SMZ (Serikali ya Mapinduzi Zanzibar) na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,” alisema.

Kwa upande wake, Mnadhimu Mkuu wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni, Tundu Lissu alisema wabunge wa Zanzibar ndiyo waliokwamisha muswada huo kutokana na mgongano wa sheria.

“Wao wanasema masuala ya kura ya maoni siyo ya Muungano kwa sababu wao tayari wana sheria yao ya kura ya maoni. Sasa wanahoji inakuwaje sheria hii itumike tena hadi Zanzibar? Huu ni mgongano,” alisema.

Lissu ambaye pia ni Mbunge wa Singida Mashariki (Chadema), alisema tangu mwanzo aliliona suala hilo na kuitahadharisha Kamati ya Bunge kwamba mapendekezo hayo yana upungufu.

Muswada pekee uliobaki wa Marekebisho ya Sheria ya Mabadiliko ya Katiba unatarajiwa kuwasilishwa leo huku ukitarajiwa kuibua mjadala mzito kutokana na misimamo ya baadhi ya wabunge.

Muswada huo unawasilishwa wakati CCM kikiwa kimeweka msimamo wa kupinga baadhi ya mambo katika Rasimu ya Katiba.



Yanayotarajiwa kuzua mjadala

Waziri wa Katiba na Sheria, Mathias Chikawe amekiri kupokea mapendekezo kutoka kwa wabunge na hasa kwenye Sheria ya Marekebisho ya Mabadiliko ya Katiba akisema wametaka kuangaliwa upya kwa kipengele cha Kamati ya Uteuzi ya viongozi wa Bunge la Katiba. Alisema sasa wataweka sifa za mwombaji wa nafasi hizo na wasiokuwa nazo hawatagombea.

Muswada wa Sheria ya Mabadiliko ya Katiba unataka wawakilishi kutoka makundi ya jamii kuwa 166 katika Bunge la Katiba, lakini wabunge wanataka idadi iwe 200.

Mbunge wa Muhambwe, Felix Mkosamali (NCCR-Mageuzi) alisema uzoefu katika nchi nyingine unaonyesha kuwa mabunge ya Katiba hushirikisha watu wengi ili kupata uwakilishi mpana tofauti na mapendekezo yaliyotolewa.

Mkosamali ambaye pia ni mjumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Katiba, Sheria na Utawala, alisema ni vyema sheria ikasema wajumbe wa Bunge hilo watatoka katika taasisi zipi.

Kifungu kingine ni kile kinachohusu Kamati ya Uteuzi wa Mwenyekiti na Makamu wake ambao kwa mujibu wa muswada itaundwa na Spika wa Bunge la Jamhuri na Spika wa Baraza la Wawakilishi, Mwanasheria Mkuu wa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania (AG) na yule wa SMZ, Waziri wa Katiba na Sheria Tanzania Bara na Waziri wa Katiba na Sheria wa Zanzibar na Kiongozi Rasmi wa Kambi ya Upinzani Bungeni.

Mkosamali alisema muswada huo wa Mabadiliko ya Katiba unasema mwenyekiti wa muda atakuwa Spika wa Bunge lakini akataka: “Mwenyekiti wa muda atokane na Chama cha Majaji wastaafu maana wao hawafungamani na upande wowote.”

KASHFA YALIKUMBA JESHI LA POLISI TENA-CCTV ZAZIMWA KURUHUSU UJAMBAZI

SIKU chache baada ya tukio la wizi mkubwa wa fedha katika Benki ya Habibu mjini Dar es Salaam, siri nzito zimeanza kuvuja kuwa polisi wanadaiwa kuhusika katika tukio hilo kwa kuhujumu kamera za usalama za CCTV zinazomilikiwa na jeshi hilo.

Katika tukio hilo, watu wanaodaiwa kuwa majambazi walipora dola za Marekani 20,000 ambazo ni sawa na Sh milioni 32 za Tanzania.

Katika tukio hilo, Polisi Mkoa wa Ilala inamshikilia askari mmoja kwa kosa la kuhusika katika tukio hilo kutokana na kushindwa kuchukua hatua za haraka wakati tukio linatokea.

Habari za uhakika kutokana ndani ya jeshi hilo, zinasema siku ya tukio polisi waliokuwa zamu kuongoza mitambo hiyo, kwa namna moja au nyingine wanadaiwa kufanya hujuma hiyo, kwa lengo la kupoteza mawasiliano na maeneo mengi ya polisi.

Chanzo chetu hicho, kiliongeza kuwa siku ya tukio eneo lote la mzunguko wa barabara ya Uhuru na maeneo ya jirani na Kiwanda cha Bia Tanzania (TBL), sehemu zote hazikuwa na huduma ya kamera za usalama, jambo ambalo si la kawaida kutokea.

“Hatua iliyofikia sasa ni mbaya, huwezi amini siku ya tukio kamera za CCTV zinazotumiwa na polisi zilizimwa kabisa, kitendo hiki kilisababisha polisi makao makuu wasijue nini kinachoendelea pale.

“Ndiyo maana utaona kuna askari mmoja anashikiliwa katika tukio lile, haiwezekani kituo kikuu kishindwe kubaini uwapo wa tukio hili, wakati kuna mawasiliano ya kutosha, umefika muda wa kulisafisha jeshi letu kwa kasi,” kilisema chanzo chetu.

Chanzo hicho, kilisema mitambo ya kamera hizo, ilizinduliwa na Rais mstaafu Benjamin Mkapa mwaka 2004 na imekuwa ikifanya kazi bila matatizo yoyote.

“Nimekuwapo hapa tangu mwaka 2004, kamera hizi zilipozinduliwa rasmi na hazijawahi kuharibika hata siku moja, iwe siku ya tukio zisifanye kazi,” kilihoji chanzo chetu.

Askari aliyekamatwa katika tukio hilo, anadaiwa anafanya kazi katika kituo cha Oysterbay Mkoa wa Kipolisi wa Kinondoni.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Ilala, Marietha Minangi, alithibitisha kukamatwa kwa askari huyo.

Kamishna wa Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam, Suleiman Kova alipoulizwa na MTANZANIA jana, alisema ameipokea taarifa hiyo na wanaifanyia kazi haraka iwezekanavyo.

“Taarifa hii tumeipokea, tunaifanyia kazi haraka sana ili kupata ukweli, naomba tuwe na subira,” alisema kwa kifupi Kamishna Kova.

Alisema bado polisi wanaendelea na uchunguzi wa tukio hilo na kwamba watu waliokamatwa watafikishwa mbele ya vyombo vya dola.